Tafuta

2023.09.01 Padre Emilius Salema,SDB Mkuu wa  Kanda mpya ya Wasalesiani wa Don Bosco nchini Tanzania. 2023.09.01 Padre Emilius Salema,SDB Mkuu wa Kanda mpya ya Wasalesiani wa Don Bosco nchini Tanzania. 

Padre Salema,Mkuu Mpya wa Kanda ya Wasalesiani,Tanzania anasimikwa rasmi

Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco,Ijumaa Septemba 8,litaadhimisha misa katika Parokia ya Mtakatifu Petro,Dar es Salaam kuanzia saa 3.30 asubuhi na baadae afla fupi,katika fursa ya kutoa kiapo cha Padre Emilius Salema,SDB ambaye amekuwa Mkuu wa Kanda mpya ya Wasalesiani wa Don Bosco,Kanda ya Tanzania.

Padre Philemon Chacha, SDB- Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco

Ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani mnamo tarehe 25 Januari 2023, mkuu wa Shirika la wasalesiani ulimwenguni, Padre Ángel Fernández Artime, SDB pamoja na Halmashauri yake waliridhia kuteuliwa kwa Tanzania kuwa ‘Salesian Province of Tanzania’, yaani ‘Kanda mpya ya Wasalesiani’ na kuifanya kuwa chini ya msimamizi wa Mtakatifu Artemide Zatti, mmoja wa watakatifu wasalesiani, huku makao yake makuu kuwa katika nyumba ya Don Bosco, Oyster Bay – Dar es Salaam kwa muda na baadae kuhamia mjini Dodoma. Kanda hii mpya ni matokeo ya jitihada wanazozifanya wasalesiani nchini Tanzania hasa katika kuwapatia elimu na malezi bora vijana wote hasa wale wahitaji na kuwaongoza katika kuwa “Raia Wema na Wakristo Hodari”. Matokeo yake ni kuongezeka kwa miito pamoja na upendo wa Mtakatifu Yohane Bosco ambaye aliyatoa Maisha yake kwa vijana. Kabla ya kufanywa kanda mpya, Tanzania ilikuwa chini ya ‘East Africa Province (AFE)’ yaani ‘kanda ya Afrika Mashariki  iliyoundwa na nchi kama Kenya, Sudani, Sudani ya Kusini Pamoja na Tanzania.

Padre Salema, Mkuu Mpya wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco wa Kanda mpya ya Tanzania
Padre Salema, Mkuu Mpya wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco wa Kanda mpya ya Tanzania

Baada ya uteuzi wa kanda mpya ya Tanzania, swali lililokuwa likiwaumiza kichwa watu wengi ni nani atakayeenda kuwa kama mtumishi mkuu wa kanda hiyo yaani kiongozi wa kanda. Baada ya mazungumzo na majadiliano kati ya wasalesiani wenyewe katika kanda hiyo chini ya usimamizi wa Padre Alphonse Owoudu, Mkuu wa Shirika kwa kanda ya Afrika na Madagascar, hatimaye mnamo tarehe 19 Juni 2023 Mkuu wa Shirika Ulimwenguni pamoja na halmashauri yake alimtanganza Padre Emilius Salema kuwa mkuu wa kwanza wa kanda ya Tanzania kwa muda wa miaka sita (2023-2029).

Ikumbukwe kuwa Padre Emilius Salema alizaliwa mnamo tarehe 09 Julai 1968, Rombo-Mashati mkoani Kilimanjaro. Alianza malezi yake ya unovisi na kuweka nadhiri za kwanza katika Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco tarehe 15 Agosti 1995 huko Moshi, mkoani Kililmanjaro. Aliweka nadhiri za daima tarehe 16 Agosti 2001 na baada ya masomo yake ya TaaliMungu katika Chuo Kikuu cha Tangaza huko Nairobi nchini Kenya alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 12 Julai 2003 katika Parokia ya Kristo Mfalme Moshi-Kilimanjaro. Amewahi kufanya utume wake katika jumuiya mbali mbali za Don Bosco ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwa Mshauri wa Mkuu wa Kanda ya Afrika Mashariki kwa muda wa miaka mitatu (2012-2015).

Mtakatifu Don Bosco, Mwalimu  bora wa Vijana
Mtakatifu Don Bosco, Mwalimu bora wa Vijana

Anakumbukwa Sanaa katika kipindi cha miaka sita alipokuwa Gombera wa Seminari Ndogo ya Don Bosco Mafinga, Iringa kuanzia mwaka 2008-2013. “Mwongozo wako ulikuwa zaidi ya masomo; ulitufundisha somo la maisha lenye thamani, ukatufunza maadili ya uadilifu na unyenyekevu, na kutufanya kuwa watu bora zaidi. Imani yako isiyoyumba, bidii yako ya kazi na kujitolea kwa wito wako kumekuwa daima chanzo cha msukumo kwetu”. Haya ni maneno ya mmoja wa past pupils yaani mwanafunzi aliyewahi kupata malezi katika seminari hiyo Bw. Sylivester Mwageni, ambaye sasa ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam. Tunampongeza sana Padre Emilius Salema kwa utayari wake wa kuongoza kanda hii na tunamtakia matashi mema katika uongozi wake akisaidiwa na halmashauri yake inayoundwa na Padre Augustine Sellam (Makamu), Padre Bonifas Mchami (Mhazini), Padre Michael Muia (Mkuu wa Utume kwa Vijana), Padre Sebastian Chirayath (Mshauri), Padre Nhati Francesco (Mshauri).

Padre Salema SDB
Padre Salema SDB

Mwenyezi Mungu awajalie hekima na nguvu ya kujitoa bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Shirika na Kanisa katika ujumla wake, huku mkijitahidi kufuata nyayo za Kristo Yesu na muendelee kujitoa kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre wote, Watawa wa Kike na wa Kiume, Wasalesiani Washiriki, Vijana, Past pupils wote wa shule zetu za Don Bosco, Wazazi wetu wapendwa na Familia nzima ya Wasalesiani karibuni sana katika Misa ya Ufunguzi siku ya Ijumaa tarehe 8 Septemba 2023 katika Parokia ya Mtakatifu  Petro Oysterbay, Dar es Salaam kuanzia majira saa 3.30 asubuhi na baadae kutafuata tafrija fupi katika ukumbi wa Chuo cha Don Bosco Oysterbay.  Hii ni siku ya Historia ya kuapishwa kwa kiongozi wetu mpya wa Kanda mpya ya Wasalesiani wa Don Bosco nchini Tanzania Padre Emilius Salema, SDB. Tuungane sote katika kumuombea na kumtakia neema na baraka tele katika kuliongoza Shirika nchini Tanzania.

Kanda Mpya ya Wasalesiani wa Don Bosco na Mkuu Mpya wa kanda hiyo Padre Salema
01 Septemba 2023, 10:37