Tanzania:Askofu Thomas Kiangio awekwa wakfu wa kiaskofu kwa Jimbo la Tanga
Na Patrick Tibanga - Radio Mbiu,Bukoba & Angella Rwezaula; -Vatican.
Mnamo tarehe 7 Juni 2023, Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa Mheshimiwa Padre Thomas John Kiangio, aliyekuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanga, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tanga. Askofu mteule Thomas John Kiangio alizaliwa tarehe 17 Machi 1965 huko Mazinde Ngua, Jimbo Katoliki la Tanga. Alipata malezi na majiundo yake ya Kipadre kutoka Seminari kuu ya Mtakatifu Antoni, Ntungamano Jimbo Katoliki la Bukoba na Karoli Lwanga, huko Segerea Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mnamo tarehe 16 Julai 1997 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga.
Katika muktadha huo, mnamo Dominika tarehe 3 Septemba 2023 Nchini Tanzania kulikuwa na tukio kubwa la kikanisa ambapo aliwekwa wakfu wa kiaskofu, Thomas John Kiangio wa Jimbo Katoliki la Tanga. Misa iliyowaona maaskofu katoliki wa Tanzania na nje yake, Balozi wa Vatican Nchini Tanzania, viongozi wa Serikali, wakristo wote, waamini wakatoliki na wenye mapenzi mema katika mji wa Tanga.
Katika mahubiri ya Askofu Mkuu Jude Thadaeus Ruwa'ichi, wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salam, alisema kuwa sisi wanadamu tunapewa fursa ya kuanza upya kwa kuendea kiti cha Huruma ya Mungu kwa kupitia Sakramenti ya Kitubio, ambayo ni sakramenti tunayopewa bila mastahili, inayotuunganisha wanadamu na Mungu. “Sisi wanadamu tunalo hitaji kama la Petro la kujikusanya, kujikarabati na kuanza upya na tunapewa fursa hiyo kila tunapoendea kiti cha huruma ya Mungu na kupokea Sakramenti ya kitubio, ambayo ni Sakramenti tunayopewa bila mastahili na Sakramenti inayotuganga katika magonjwa yetu.” Katika mahubiri hayo Askofu Mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa, Mungu hawaachi watu wake, bali anamuibua nabii mwingine anayewatangazia habari njema ya kukombolewa kuwekwa huru na kuishi kwa amani na ustawi.
Askofu Mkuu katika muktadha wa siku hiyo akiuwageukia waamini alisema: “Leo tunaungana na familia ya Mungu Jimboni Tanga kuadhimisha habari njema baada ya kifo cha Askofu Anthoni Banzi. Jimbo hili limebaki bila Askofu Kwa miaka miwili kilikuwa ni kipindi cha maswali, mahangaiko na kuhuzunisha, Mimi mwenyewe nimekuja hapa kwa miaka kadhaa na kila nilipokuja walikuwa wananiuliza tutakaa hivi mpaka lini Askofu? niliwajibu tuendelee kusali tumpate Askofu atakayewaongoza, atakayelifundisha na atakayelitakatifuza Jimbo la Tanga, na sasa tumshukuru Mungu”, Alisisitiza Askofu Mkuu Ruwa'ichi. Katika takakari hiyo alisema kuwa ukamilifu wa ahadi hautimiliki kwa kupatikana nabii bali utatimilika kwa kupatikana masiha mpakwa mafuta ambaye ni Bwana na mwokozi wetu.” AlisemaAskofu Mkuu Jude Thadaeus Ruwa'ichi.
Maneno ya Yesu yanatimiliki kwa uwepo wa Kristo anayewafundisha, kuwatakatifu na kuwaongoza watu katika njia za Bwana, kwa kuitia huruma na upendo wake Kristo. “Huyu Kristo ndiye anayeita, anayetuma, kutakatifuza na ndiye muhimili wa Kanisa na ninawasihi waamini kutambua kuwa Kristo amemteua Padre Thomas Kiangio na kupenda awe mchungaji katika shamba lake, Kristo ndiye amemteua na kutenda kazi kwa kuliongoza na kulilisha kundi kwani Kristo hamuiti mtu kutokana na mastahili ya huyo anayeitwa bali anamuita mtu aliongoze kundi na kulichunga kundi lake na kulilisha kundi lake, sasa huruma na mapendo yake na kwa misingi hiyo.” Kwa upande wa ushauri wake, pia Askofu Mkuu Ruwa'ichi alimsihi Askofu mteule Kihangio kuutelekeza wito wake kwa dhati na kulihudumia kundi la Mungu bila kujibakiza. “Askofu wetu huyu hana cha kujigamba na kujitutumua kwa kufanywa kuwa Askofu anatakiwa kuupokea wito wake kwa unyofu na kuutelekeza wito wake kwa dhati na kujitoa katika utume wake bila kujibakiza.” Alihitimisha.
Kwa Upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya alimpongeza Askofu Thomas Kihangio na kumshukuru kwa kukubali kuyapokea majukumu ya Uaskofu na kumtakia matashi mema katika utume wake Jimboni Tanga na kumkabidhi kanuni za utendaji tayari kuanza rasmi kazi ya Uchungaji Jimboni Tanga.
Akitoa Salam kutoka Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa, uteuzi wake Askofu Kihangio unadhirisha anafaa kuwa Askofu wa Tanga na anao wajibu wa kuyaishi matakatifu na wakati huo huo aliwasihi waamini kumpatia ushirikiano wa kutosha ili jukumu la usimamizi wa Kanisa uweze kuwa mwepesi na waamini kumpenda na kumtii. Akimgeukia hata Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Tanga nchini Tanzania Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema: “Niwajibu wako kuendelea kuuishi wito wako ili uendelee kuaminiwa na waamini na Kanisa lote, nanyi waamini ninawasihi muendelee kudumisha Amani na umoja katika Kanisa na Nchi yetu kwani ni nguzo muhimu katika nchi yetu.”