Tafuta

2023.09.15 Waamini Jimboni Kayanga Tanzania wafanya Siku Kuu ya Kutuka kwa Msalaba katika kituo cha Hija huko Kayungu. 2023.09.15 Waamini Jimboni Kayanga Tanzania wafanya Siku Kuu ya Kutuka kwa Msalaba katika kituo cha Hija huko Kayungu. 

Ask.Rweyongeza:Imarisheni imani,upendo,ufuasi&ushuhuda

Askofu Rweyongea wa jimbo katoliki la Kayanga nchini Tanzania Septemba 14 aliwaongoza Maelfu ya mahujaji katika misa Takatifu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu katika kituo cha hija cha Kalivario Kayungu huku akiwataka kusameheana na kuwapenda maadui zao kwani kusamehe ni kutakasa kumbukumbu.

Na Padre Sylivanus Mugisha; - Jimbo Kayanga, Tanzania.

Msalaba ni alama muhimu sana kwa ukombozi wa mwanadamu. Ni mahali ambapo ukombozi wetu umetambulika. Na hatuna shaka juu ya hilo kwa sababu ya Kristo na kifo chake msalabani. Ni katika muktadha huu ambapo  Askofu Almachiusi Vicent Rweyongea wa jimbo katoliki la Kayanga nchini Tanzania aliwaongoza Maelfu ya  mahujaji katika misa Takatifu ya Kutukuka kwa  Msalaba Mtakatifu katika kituo cha hija  cha Kalivario Kayungu  huku akiwataka kusameheana na kuwapenda maadui zao kwani kusamehe ni kutakasa kumbukumbu. Hija hiyo ilifanyika tarehe 14  Septemba 2023 katika siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha  kumbukizi hii tukufu ya Kutuka kwa Msalaba. Katika fursa hiyo Askofu alianza  kwa kubariki vituo vipya 15 vya njia ya msalaba vilivyojengwa upya katika mlima wa Kalvario uliopo katika parokia ya kimkakati ya Kayungu.

SIKU KUU YA KUTUKUKA KWA MSALABA MTAKATIFU
SIKU KUU YA KUTUKUKA KWA MSALABA MTAKATIFU

Akiongoza Misa katika hija ya 13 ya kijimbo,  Askofu Rweyongeza alisema lengo la hija na ziara ya msalaba ni kuimarisha imani, upendo, ufuasi, ushuhuda na mshikamano na Yesu pamoja kutubu na kumuomba Yesu wa msalaba. Katika mahubiri yake Askofu Rweyongeza alisisitiza kuwa Yesu kristo akiwa msalabani kati ya maneno aliyosisitiza ni pamoja na msamaha akimsihi Mungu kuwasamehe hata walio msurubisha,hivyo waamini hawana budi kusamehe ili kutakasa kumbukumbu ya mambo yaliyopita. Askofu wa Jimbo la Kayanga aidha alisema kuwa kuna makundi matatu ya kusamehe ikiwemo kujisamehe mwenyewe, kumsamehe mwenzako na kumsamehe Mungu na kufafanua kwa undani zaidi kuwa kujisamehe mwenyewe ni kuisamehe nafisi yako kutokana na mambo mabayo unayotendea nafsi kwa uzembe.

MSALABA MTAKATIFU
MSALABA MTAKATIFU

Kuhusiana na vituo vipya vilivyokarabatiwa, Mkurgenzi wa hija jimbo Katoliki la  Kayanga,  Padre Nicodemus Byakatonda alisema kuwa kuna faida nyingi katika vituo hivyo na kuongeza kuwa kuna shuhuda nyingi za watu ambapo wengi wanaokwenda kwa imani na kusali katika kituo hicho wengi wamepona magonjwa, pamoja kutatuliwa shida zao kutokana na imani kwa msalaba. Naye Katibu wa Askofu Padre Castor Tindyebwa akisoma salaamu za Askofu wa jimbo la Kayanga aliwasihi waamini na watu wote  wenye mapenzi mema kutumia vituo hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kusali na kuomba na akawasihi kuacha hata matumizi mabaya ya vituo hivyo. Kwa upande wa Laurent Laurean ambaye  ni katekista katika Parokia ya Kayanga alisema  kwamba wakristo wanapokutana kwa pamoja katika Hija wanapa nafasi ya kusali pamoja na kupata Baraka kutokana na kutafakari matendo mema ya Mungu. 

Maneno saba ya Yesu msalabani

Yesu akiwa msalabani alitoa maneno saba muhimu. Tukisoma  Injili ya Mathayo 27:46 inatuambia kwamba saa ya tisa Yesu alilia kwa sauti kuu, akisema, “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha? Yesu alikuwa akionesha hisia zake za kuachwa, vile Mungu alivyoweka dhambi za ulimwengu juu yake na kwa sababu hiyo, Mungu alipaswa  kumsaidia. Yesu wakati huo alihisi uzito wa dhambi na alikuwa anapitia hisia za kuachwa  Mungu kwa muda pekee. Hii ilikuwa ni kutimiza maneno ya kinabii katika  Zaburi 22: 1.

“Baba, uwasamehe, kwa maana hawajui walitendalo (Luka 23:34) ni neno la pili Yesu akiwa Msalabani. Wale waliomsulubisha Yesu hawakutambua upeo kamili wa yale waliyokuwa wakifanya kwa sababu hawakumtambua yeye kama Masiha. Ujinga wao wa kutojua  ukweli wa Mungu haukumaanisha kwamba walistahili msamaha, na sala ya Kristo kati ya dhihaka ni uonesho la huruma isiyo na kikomo ya neema ya Mungu.

ASKOFU A. RWEYONGEZA WA JIMBO KATOLIKI KAYANGA TANZANIA
ASKOFU A. RWEYONGEZA WA JIMBO KATOLIKI KAYANGA TANZANIA

Neno la tatu ni:  “Nakuambia ukweli, leo hii utakuwa pamoja nami katika mbingu” (rej. Luka 23:43). Katika maneno haya, Yesu anahakikishia mmoja wa wahalifu msalabani kwamba atakapokufa, atakuwa pamoja na Yesu mbinguni. Hii ilitolewa kwa sababu, hata wakati wa kifo chake, mhalifu ameonesha imani yake kwa Yesu, akimtambua jinsi gani alikuwa (Rej. Luka 23:42).

Neno la nne: “Baba, mikononi mwako ninaweka roho yangu” (rej. Luka 23:46). Yesu hapa anakabidhi roho yake kwa hiari ndani ya mikono ya Baba, akionesha kwamba alikuwa karibu kufa na kwamba Mungu alikuwa amekubali sadaka yake. Kwa hiyo: “Alijitolea Mwenyewe asiye na hatia kwa Mungu” (rej. Waebrania 9:14).

Neno la tano: “tazama hapo ni mtoto wako! Na hapo ni mama yako!”. Haya ni kuonesha kwamba  Yesu alipomwona mama yake amesimama karibu na msalaba pamoja na Mtume Yohane, ambaye alimpenda, aliweka huduma ya mama yake mikononi mwa Yohane yaani Mtume/ Mitume. Na tangu saa hiyo Yohane akamchukua nyumbani kwake (rej. Yohane 19: 26-27). Yesu anamkabidhi mama yake kwa mitume kwa hiyo na sisi leo hii. Mama anakuwa mama wa mitume  na pia Mama yetu. Katika sura hiyo tunamwona Yesu, mwingi wa huruma anahakikisha kuwa mama yake wa duniani anajaliwa, na hata baada ya kifo chake.

Neno la sita:  “Nina kiu"(Yh 19:28). Yesu anatimiza unabii wa Kimasiha kutoka Zaburi 69:21 ambayo ilisema kuwa “Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.” Tendo la kutamka kuwa a alikuwa na kiu, aliliwafanya walinzi wa Kirumi kumpatia siki, ambayo ilikuwa ya kawaida wakati wa watu waliokuwa wakisulubiwa msalabani  na hivyo kutimiza unabii.

Neno la mwisho la saba:  “Imekwisha! (rej. Yh 19:30). Maneno ya mwisho ya Yesu yalimaanisha kuwa mateso Yake yalikuwa ni kutimiza kazi yote ambayo Baba yake alikuwa amemkabidhi kufanya, ambayo ilikuwa ni kuhubiri Injili, kuwafungua wafungwa, kuwakomboa wenye shida, njaa na mateso na vifungo vya dhambi na kupata wokovu wa milele kwa watu wake, ambapo kazi hiyo ilitimizwa na deni la dhambi likalipwa. Je tunaweza sisi kumlipa nini kwa mateso hayo msalabani?

Jimbo Kayanga na hija ya Msalaba Kayungu
15 September 2023, 18:22