Tafuta

2023.08.04 Papa awakti wa WYD alitoa sakramenti ya kitubio kwa vijana 2023.08.04 Papa awakti wa WYD alitoa sakramenti ya kitubio kwa vijana  (Vatican Media)

Dominika ya 24 ya Mwaka A:Wajibu wa kusamehe waliotukosea

Upendo ndio nguvu ya kutuwezesha kusamehe.Msahama wa kweli hujengwa katika amri kuu ya Mapendo.Mtu akisema naomba unisamehe ni sawa na kusema naomba unipende.Mtoto akikosea akaomba wazazi wamsamehe ni sawa na kuwambia anaomba wamepende.Wakifanya hivyo ni sawa na kumwambia wanampenda.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 24 mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Domenika ya 23 A yalitukumbusha wajibu na namna ya kuwasahihisha ndugu zetu waliotukosea ili kuwasaidia waweze kumrudia Mungu. Masomo ya domnika hii ya 24 A yanatilia mkazo sio tu wajibu wetu kama wakristo katika kuwasahihisha waliotukosea, lakini pia kuwasamehe bila kipimo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa katika maisha yetu ya kila siku kama wanadamu tunakosea, tunakosewa na kukoseana na hivyo kunaharibu mahusiano mwema tunayopaswa kuwa nayo. Njia pekee ya kurudisha uhusiano huu mwema ni toba na msamaha wa kweli vilivyo chemichemi ya amani ya kweli itokayo kwa Mungu kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Ee Bwana, uwape amani wakungojao, ili watu wawasadiki manabii wako; usikilize sala ya mtumwa wako, na ya taifa lako Israeli” (YbS. 36:15). Ni kwa kusameheana sisi kwa sisi, ndipo tunapopata kibali cha kusamehewa na Mungu kama sala ya mwanzo inavyotilia mkazo kusema; “Ee Mungu uliye mwumba na mwongozi wa vitu vyote ututazame, utuwezeshe kukutumikia kwa moyo wote, ili tupate baraka ya huruma yako”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira (YbS. 27:30-28:1-7). Somo hili linatueleza kuwa tunapaswa kuwasamehe wengine kwa kuwa hata sisi tunahitaji kusamehewa maana hatuko wakamilifu, tu wadhambi. Yoshua bin Sira anauliza, mtu mwenye dhambi anawezaje kutumaini kusamehewa makosa yake na Mungu iwapo anatunza hasira, ghadhabu na kisirani moyoni mwake? Kwanza yampasa amsamehe jirani yake ili naye apate kusamehewa. Kumbe mwenye kujilimbikizia kisasi ataona kisasi kutoka kwa Bwana; hakika Yeye atamfungia dhambi zake. Kumsamehe jirani/mtu mwingine maovu aliyokufanyia ni sharti la kusamehewa dhambi zako wakati utakaposali na kuomba msamaha kwa Mungu. Anasisitiza Yoshua bin Sira; “Mwenye kujilipiza kisasi ataona kisasi kutoka kwa Bwana; hakika Yeye atamfungia dhambi zake.

Umsamehe jirani yako dhara alilokufanyia, hivyo nawe utasamehewa dhambi zako wakati utakaposali”. Anaendelea kuuliza maswa: “Mwanadamu kumkasirikia mwanadamu. Je! Atatafuta kuponywa na Bwana? Mwanadamu hamrehemu aliye mwanadamu mwenzake. Je! Atalalamika kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe? Aliye mwili na damu tu huilisha hasira yake. Je! Ni nani atakayempatanisha yeye kwa makosa yake?” Kisha nahitimisha kwa ushauri murwa kabisa akisema; “Basi kumbuka mwisho wako, uuache uadui; kumbuka uozi na mauti, ujiepushe na kutenda dhambi. Kumbuka zile amri, usikasirike na jirani yako; nawe ulikumbuke agano lake Aliye juu, umwachilie ujinga wake”.

Basi tujitahidi kuwasamehewe waliotukosea, ili nasi tupate kibali machoni pa Mungu na kusamehewa uovu wetu kama wimbo wa katikati unavyotusihi; “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, naam, vyote vilivyo ndani yangu, vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote. Ndiye anayekusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote. Akomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema.  Yeye hatateta siku zote, wala hatashika hasira yake milele. Hatutendei kadiri ya hatia zetu, wala halipi kwa kadiri ya maovu yetu. Maana vile mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi” (Zab. 103:1-3, 9-12).

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 14:7-9). Katika somo hili mtume Paulo anatueleza kuwa kwa vile sisi sote tumekombolewa kwa kifo na ufufuko wa Kristo, basi sote tu mali ya Mungu. Yeye peke yake ni Bwana wetu. Hivi lengo la matendo yetu yote liwe katika kumpendeza Mungu. Na ili kumpendeza Mungu lazima tuwe na upendo kwa wenzetu kama Mungu anavyowapenda na kuwasamehe pale wanapokosea. Mtume Paulo anasisitiza kuwa sisi sote tunadaiwa na Mungu. Deni letu ni kubwa sana kiasi kwamba hakuna mtu mwenye matumaini ya kuweza kulilipa. Tunadaiwa na Mungu kwa kuwa vyote tulivyonavyo ni vyake; maisha yetu ni yake, akili zetu ni zake, utashi wetu ni wake na karama tulizonazo ni zake. Kumbe hakuna tunachoweza kudai kuwa ni haki yetu mbele zake, isipokuwa dhambi zetu tu. Lakini Mungu kwa upendo na huruma yake anatusamehe dhambi zetu kila tunapomuomba msamaha. Kumbe nasi tunapaswa kuwasamehe ndugu zetu waliotukosea kwa sababu Bwana ametusamehe makosa yetu.

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 18:21-35). Sehemu hii ya Injili inajibu maswali haya; Je, tunapaswa kuwasamehe jirani na ndugu zetu mara ngapi? Jibu ni daima, bila kipimo! Sababu gani ni lazima tuwasamehe jirani na ndugu zetu? Kwa sababu sisi pia hutegemea daima msamaha wa Mungu na maadamu sisi tu watoto wa Mungu, hatuma budi kuiga mfano wa Mungu Baba yetu. Haya ni mafundisho ya Yesu baada ya Petro kumuuliza ni mara ngapi tunapaswa kuwasamehe ndugu au jirani zetu wanapotukosea. Kumbe tunapaswa kufahamu kuwa kusamehe ni sharti la sisi kusamehewa na Mungu. Yesu anasema; “Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, msiwe na neno lolote juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu” (Mk. 11:25, 26).

Licha ya kuwa kuwasamehe wengine ni sharti la sisi kusamehewa, lakini pia kusamehe kuna faida katika maisha yetu ya kila siku kuliko kutokusamehe. Mafundisho na mang’amuzi ya mababa wa Kanisa, watakatifu na wasomi mbalimbali yanatufundisha faida nyingi zinazopatikana pale msamaha unapotolea. Msamaha na upatanisho huleta mahusiano mema na kukata mzunguko wa chuki, hasira, fitina na kisasi. Hivyo kuufa msamaha kuwa mlango wa uponyaji wa ndani na wa nje unaotuletea afya ya kimwili, kiakili na kiroho kwani unapotolewa unamuweka mtu huru, na mawazo yanayosababisha magojwa yasiyotibika kwa dawa za hospitalini. Kumbe ukisamehe unajiponya, ukisamehe unajitakia mema. Zaidi sana kusamehe ni utu, kusamehe ni uungwana, kusamehe ni upendo, kusamehe ni ukomavu kwani ni kufanya maamuzi ya kiutu uzima. Kusamehe kunakufanya uwe na mwelekeo mzuri na mipangilio mizuri katika maisha yako. Kumbe tunaweza kusema kuwa msamaha maana yake ni kurudisha tena hali njema kati ya mtu na mtu, kati ya mtu na jamii, kati ya mtu na Mungu. Kusamehe ni kurudisha upendo, amani na urafiki uliopotea.

Lakini mara nyingi inakuwa ngumu kusamehe pengine ni kwasababu ya kutokukomaa katika imani, kukosa moyo wa sala na moyo wa upendo. Pale tunapoona ugumu wa kusamehe, tunapopata kigugumiza kutoa msamaha, tumtazama Yesu juu ya msalaba ili tuchote kutoka kwake neema na nguvu za kuweza kusamehe na kusema kama Yeye alipokuwa kufani msalabani: “Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo”. Upendo ndio nguvu ya kutuwezesha kusamehe. Kumbe msahama wa kweli hujengwa katika amri kuu ya Mapendo. Kumbe mtu akisema naomba unisamehe ni sawa na kusema naomba unipende. Mtoto akikosea halafu akamwambia mzazi wake – baba au mama naomba unisamehe ni sawa na kumwambia baba au mama yake naomba unipende. Na baba au mama akijibu nimekusamehe mwanangu ni sawa na kumwambia nakupenda mwanangu. Kumbe ukimwambia mtu aliyekosea nimekusamehe ni sawa na kumwambia nakupenda. Hivi ndivyo tunavyoweza kuiishi amri ya mapendo. Na hii ndiyo dhana ya kusamehe inayoleta furaha ya kweli katika maisha yetu.

Tukumbuke kuwa msamaha ni zawadi ambayo ikitolewa inakumbukwa na vizazi vyote. Ni zawadi ambayo Yesu aliwapa waliomtesa na kumtundika msalabani. Ni zawadi ambayo Stefano shemasi aliwapa waliomuua. Basi nasi tujifunze kutoa msamaha ili tuweke kumbukumbu duniani na mbinguni. Tukifanya hivyo sala ya kuombea dhabihu inayosema: “Ee Bwana, uridhike na dua zetu; uipokee kwa wema dhabihu yetu sisi watumishi wako, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa heshima ya jina lako, kitufae sote kwa wokovu”, itakuwa na maana na itasikilizwa. Nasi tutakuwa na ushirika na Kristo kama antifona ya komunyo inavyosema; “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Bwana?” (1Kor. 10:16). Hivyo tutakuwa na nguvu ya kuishi vyema kama sala baada ya komunyo inavyosema; “Ee Bwana, tunakuomba nguvu ya neema zako za mbinguni itujaze mwili na roho, ili tusitawaliwe na tamaa zetu, ila tu na nguvu hiyo”.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 24 ya Mwaka A:Msamaha
15 September 2023, 17:36