Zimbabwe wanapiga kura:ZCBC,wataka uchaguzi wa amani na usio na vurugu!
Na Paul Samasumo; - Vatican
Tarehe 23 Agosti 2023, Zimbabwe inaendesha Uchaguzi Mkuu huku duru ya pili ikitarajiwa kufanyika tarehe 2 Oktoba 2023 ikiwa hakuna mgombeaji wa Urais atafikia 50% katika duru ya kwanza. Katika taarifa ya kabla ya uchaguzi iliyotolewa katika mkesha wa uchaguzi, katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Harare, Askofu Rudolf Nyandoro wa Jimbo Katoliki la Gweruna, na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zimbabwe, alitoa ombi kwa ajili ya raia kufanya uchaguzi wa amani.
"Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zimbabwe (ZCBC), kupitia Tume yake ya kijamii ya haki na amani, ingependa kuchukua fursa hii kuhimiza kila mtu kwenda kupiga kura kwa amani. Kupiga kura, kwa maoni yetu, ni wajibu kwa wote kuchangia manufaa ya pamoja ya taifa letu tunalolipenda. Kama ZCBC, tunaamini kuwa upigaji kura ni fursa kwa kila mtu kushiriki moja kwa moja katika utawala wa nchi yetu,” alisema kiongozi huyo wa Jimbo Katoliki la Gweru.
Kulingana na waangalizi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, ghasia za baada ya matokeo hutegemea jinsi chama tawala kitakavyo ridhishwa na matokeo ya mwisho. Wakati huo huo, Maaskofu wa Zimbabwe watakuwa wakiomba kwa moyo wote ili maneno yao kwa ajili ya chaguzi tasiyo na vurugu yapate masikio ya kusikiliza, hasa miongoni mwa wanasiasa na makada wa vyama vya siasa.
“Tunaomba uchaguzi uwe wa amani. Kumbuka kwamba kuna maisha kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kwa hiyo, tunatoa wito kwa wapiga kura wote kuheshimu taratibu za uchaguzi. Ndugu Wazimbabwe, tunawaomba kwa unyenyekevu muendelee kuwa wastahimilivu, kuwa na heshima na amani wakati wa kupiga kura na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi,” alisema Askofu Nyandoro. Na kuongeza, “kwa Kanisa, tunaamini kuwa chaguzi za amani na zisizo na vurugu ndiyo njia pekee halali ya kutafuta kuungwa mkono na ofisi za umma. Tumepiga hatua katika kukua na kuwa nchi ya kidemokrasia, na tunahimiza sana mazingira ya amani kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu,” alisema Askofu huyo.
Mchuano ni kati ya ZANU-PF na CCC
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, (Citizens Coalition for Change- CCC), kinachoongozwa na Nelson Chamisa, kina kibarua kigumu cha kujaribu kumfukuza Rais aliyeko madarakani, Emmerson Mnangagwa wa chama cha ZANU-PF - madarakani kwa zaidi ya miaka arobaini. Uchaguzi wa Juma hili utakuwa wa pili baada ya Rais wa muda mrefu Robert Mugabe kulazimishwa kuondoka madarakani mwaka 2017.
Kulingana na matokeo ya uchaguzi wa 2018, Mnangagwa wa ZANU-PF alipata 52.3% ya kura zote zilizodumishwa hasa na kura katika maeneo ya vijijini. Chama cha upinzani cha Chamisa kilipata 44%. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zimbabwe linasema wametuma waangalizi 1,500 wa kusimamia uchaguzi nchini humo.