Washiriki wa Sinodi ya Kiafrika Wahimizwa Kufahamu Hati ya Kitendea Kazi ya Sinodi
Na Padre Andrew Kaufa SMM; - Nairobi, Kenya.
Kabla ya Sinodi ya Oktoba mwaka huu, washiriki wa Kiafrika katika Sinodi wamekusanyika jijini Nairobi , Nchini Kenya kwa ajili ya mkutano wa siku mbili ya tarehe 16 na 17 Agosti 2023 wenye lengo la kutaka kujuana wao kwa wao na kufahamiana na zaidi katika kujikita kwenye hati ya kibara na Hati ya kitendea Kazi ya Sinodi (Instrumentum Laboris.) ya Sinodi inayokaribia. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM) Kardinali Fridolin Ambongo na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Kinshasa Congo (DRC) aliwaalika washiriki kufanya kazi pamoja kama familia ya Mungu na kuingia katika mienendo ya Sinodi. “Tuna bahati ya kualikwa kushiriki katika sinodi. Sinodi ya kisinodi ni wakati wa kihistoria na wa pekee kuhusu mada yake, sifa yake maalum ya kusafiri pamoja na kusikilizana sisi kwa sisi na Roho Mtakatifu, na mtindo wake wa kipekee unaoifanya kuwa tofauti na sinodi zote zilizopita,” alisema Kardinali Ambongo.
Kikao cha maandalizi kutazama hati ya kitendea Kazi ya Sinodi ijayo
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa SECAM, Padre Rafael Simbine Jr, alisisitiza kuwa mkutano huo uchukuliwe kama kikao cha awali ambapo washiriki watafanya shughuli kuu mbili, ambazo ni kuangalia tena hati ya sinodi ya Afrika na Hati ya Kitendea Kazi (Instrumentum Laboris). “Malengo makuu ya semina hii kimsingi ni manne: kwa washiriki wa Sinodi kutoka Afrika ili kujuana na kutambuana; kujitambulisha na Hati ya Kitendea Kazi( Instrumentum laboris) na kuuliza maswali kwa ufafanuzi; kuongeza uelewa wetu wa mbinu ya Maongezi ya Kiroho; na kushiriki matarajio yetu binafsi ya mkutano ujao wa Sinodi ya Sinodi huko Roma,” alisema Padre Simbine.
Madhumuni ya waraka wa Bara la Afrika wa 6 Machi 2023
Akianzisha mkutano huo, Padre Vitalis Anaheobi alichukua zamu yake kuwakumbusha washiriki kwa ufupi maudhui ya waraka wa Bara la Afrika kama ilivyoidhinishwa na wajumbe wa mkutano wa wajumbe wa Afrika wa mnamo tarehe 6 Machi 2023 mjini Addis Ababa, Ethiopia. Waraka huu umesisitiza vipaumbele katika muktadha wa Kanisa Barani Afrika ambavyo pamoja na mambo mengine, ni kukuza moyo wa masinodi katika muktadha wa Kanisa Barani Afrika; kuoanisha kanuni za sinodi na Injili na tunu za Kiafrika; Kanisa linalojizatiti katika kuendeleza amani na haki katika mazingira ya Kiafrika ambayo yanatambulika kwa unyonyaji wa rasilimali na migogoro ya kijamii; kukuza ushirika katika muktadha wa ufadhili na uwajibikaji pamoja wa washiriki wote waliobatizwa wa Kanisa; huduma ya kichungaji kwa familia; na Kanisa lililojitolea kushughulikia haki na uwakili wa ikolojia.
Askofu Muandula: Zingatia matunda yaliyo tayari tangu kuanza mchakato wa Sinodi
Katika Hati ya Kitendea Kazi (Instrumentum Laboris), Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, Msumbiji na ambaye tangu tarehe 15 Machi 2023, Kardinali Mario Grech, katibu mkuu wa Sinodi ya Maaskofu, alimteua kuwa mjumbe wa tume ya maandalizi ya utekelezaji wa Mkutano Mkuu wa XVI wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 ikiongozwa na kauli mbiu: “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Ushirika, Ushiriki na Utume; aliwakumbusha washiriki wa sehemu mbili katika waraka wa kitendea kazi hasa kwa wito wa kuzingatia matunda ambayo tayari yamekusanywa tangu kuanza mchakato wa safari ya sinodi na maswali mawili muhimu ambayo yatatoa matokeo ya kutambuliwa kwa hatua zinazohitajika za kiutendaji ambazo lazima zichukuliwe na Kanisa kuanzia sasa na kuendelea.
Roho Mtakatifu ndiye anayekuza utume wa Kanisa
“Pamoja na Roho Mtakatifu kama mhusika mkuu, mchakato wa safari ya sinodi imekuwa fursa kwa Kanisa Barani Afrika,” alisema kuwa “Instrumentum Laboris" inashughulikia Kanisa la Sinodi lililoanzishwa kwa utambuzi wa hadhi ya pamoja ya kila mbatizwa kama mshiriki wa Kanisa, akiongozwa na Roho Mtakatifu na kutumwa kutimiza utume.” Kwa njia hiyo, Askofu Lucio alijikita na misingi ya kuwahimiza washiriki ili kuangalia maswali muhimu yaliyotolewa katika Hati ya kitendea kazi na kwamba katika hatua hiyo, ujuzi na mbinu ya Mazungumzo ya Kiroho inakuwa muhimu katika kutambua hatua muhimu kwa ajili ya kukuza utume wa Kanisa. "Kanisa katika roho ya sinodi ambayo inasisitiza ushirika, uwajibikaji pamoja na mtazamo shirikishi wa utawala na utekelezaji wa mamlaka."
Shukrani kwa Baba Mtakatifu kwa uteuzi wa washiriki wa Sinodi
Kwa upande wake Kardinali Ambongo vile vile alisema kuwa Kanisa Barani Afrika linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewateua kutoka Barani humo, Makardinali 5, Maaskofu 48, Mapadre 6, Watawa 6 na Waamini walei 2 kushiriki katika Sinodi hiyo. Katika mkutano huo, zaidi ya washiriki 47 wamekusanyika kutoka Kanda nne za SECAM.