Tanzania,Tamko la TEC kuhusu Mkataba wa bandari:Raia wasikilizwe na Serikali!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Ijumaa tarehe 18 Agosti 2023, Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini Tanzania (TEC) limetoa tamko la kupinga mkataba wa usimamizi na uendelezaji wa bandari za Nchi uliosainiwa kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Nchi za Falme za Uarabuni huko Dubai na kuridhiwa kupitia azimo la Bunge mnamo tarehe 10 Juni 2023, huku wakifafanua kwa kina jinsi ambavyo mkataba huo haukubaliki kwa watanzania wengi, tangu kuanza kwa mjadala. Tamko hilo limesainiwa na Maaskofu wakuu na maaskofu wote 37 wa Majimbo Katoliki Tanzania ambapo kabla ya kukabidhiwa kwa Mkataba huo kwa waandishi wa Habari, imetangazwa kwa umma na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mheshimiwa Padre Charles Kitima kwa vyombo vya Habari
Kwa upande wake Padre Kitima amesema Maaskofu hawaungi mkono bandari kuwekwa chini ya mwekezaji mmoja na kwamba tamko hilo la Maaskofu lina kauli moja ambayo ni kwamba “kama wananchi hawautaki mkataba, serikali iwasikilize wananchi. Serikali iachane na Mkataba wa Bandari kwa sababu wananchi wamegawanyika kuhusu mkataba huo na zaidi ni kutokana na vifungu flani fulani ambavyo haviendani na Katiba ya Nchi na matakwa ya raia”. Hata hivyo hii siyo kwa mara ya kwanza sauti ya Viongozi wa kidini kusikika, hata siku zilizopita waliweza kutoa maoni yao na sio viongozi wakatoliki tu, lakini hata wa makanisa mengine na madhehebu mbali mbali kupitia mijadala.
Mjadala juu wa uwekezaji unaotarajiwa katika usimamizi wa bandari za Tanzania umedumu tangu mwanzoni mwa mwezi Juni 2023 huku kukiwa na mitazamo tofauti kati ya wanaounga mkono na wanaopinga. Na hii ilisababishwa na kukosekana muda wa wanachi wote kupewa fursa zaidi ya kuadili. Na siku za hivi karibuni, baadhi ya wanasheria, walipeleka hata mashtaka, katika mahakama ili kutaka haki za wananchi, lakini hatimaye wakaishia kuwekwa ndani, ambapo wameachiliwa huru tarehe 18 Agosti 2023. Katika muktadha wa haki za binadamu (Amnesty International), hivi karibuni lilinaomba: “waachilie mara moja Wakosoaji waliozuiliwa wa mkataba wa bandari nchini Tanzania.
Hawa ni Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Boniface Mwabukusi, mwanasheria na mwanaharakati, na Mdude Nyagali, mwanaharakati wa kisiasa, ambao wote walikamatwa kati ya 12 na 13 Agosti 2023, kwa kosa la kukosoa makubaliano kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kuhusu bandari”. Hayo yalisemwa na Shirika la Amnesty International mnamo tarehe 14 Agosti 2023, kupitia kwa msemaji wake Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda ya Amnesty International ya Afrika Mashariki na Kusini.
Kwa mujibu wake alisema “ Makubaliano hayo yanaweka mfumo wa kisheria kwa UAE kushirikiana na Tanzania katika maendeleo, usimamizi na uendeshaji wa bandari za Tanzania, kanda maalum za kiuchumi, mbuga za usafirishaji, korido za biashara na miundombinu mingine inayohusiana nayo. Ukandamizaji wa mamlaka ya Tanzania dhidi ya wakosoaji wa mpango wa bandari ya UAE unaonesha kuongezeka kwa kutovumilia kwao upinzani. Kwa hiyo Mamlaka lazima ziache kuwashikilia wanaharakati kiholela kwa sababu tu ya kutoa maoni yao kwa amani na kuwaachilia mara moja na bila masharti wanaharakati hawa ili kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki ya uhuru wa kujieleza.” Alisisisitiza Tigere Chagutah.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, inakutleta Hati nzima ya Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania iliyopchapishwa tarehe 18 Agosti 2023: Ni katika audio: