Nigeria:Wamisionari wa Afrika waliotekwa nyara kati ya Agosti 2 na 3,waachiwa huru!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Padre Paul Sanogo na Mseminari Melkiori Dominick Mahinini, waliotekwa nyara mnamo tarehe 3 Agosti 2023 wameachiliwa huru. Habari hizo zilichapishwa tarehe 24 Agosti 2023 na Shirika la kipapa la Habari za Kimisionari (FIDES). Padre Sanogo na Mseminari Melkiori ni wa wamisionari wa Afrika, Ahirika ambalo linajulikana sana zaidi kama Mababa Weupe(White Fathers. Utekaji nyara huo ulitokea katika shambulio la parokia ya Mtakatifu Luka huko Gyedna Jimbo Katoliki la Minna), Mkoa wa Niger kaskazini-kati mwa Nigeria.
Kuachiliwa kwao kulithibitishwa na Mkuu wa Shirika hil, Padre Stanley Lubungo, tarehe 24 Agosti 2023. Hata hivyo kufuatiwa na kuwachiwa huru naye Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, Kanda ya Ghana -Nigeria ameandika barua ya kushukuru ambayo inasomeka hivi: “Ni furaha tele kuwajulisha kuhusu uhuru uliorudishwa wa ndugu zangu wawili leo tarehe 23 Agosti 2023, Padre Paul Sanogo kutoka Mali na kaka Melchior Mahinini kutoka Tanzania, waliotekwa nyara Jumatano usiku wa tarehe 2 Agosti 2023 katika eneo letu la jumuiya ya Gyedna, Jimbo katoliki la Minna, Wilaya ya Niger, nchini Nigeria. Wote wawili wako salama, wako hai na wana afya njema licha ya hali ya kuhuzunisha waliyopitia mikononi mwa watekaji nyara wakati wa utekwa kwa majuma matatu yaliyopita”. Hili lilipotokea, tuliomba msaada wenu wa kimaadili na maombi. Kuachiliwa kwao ni uthibitisho wa maombi yenu ya dhati na msaada. Ndiyo maana ninarudi kwenu nyote kwa shukrani kwa kuwa pale kwa ajili yetu wakati huu wa giza, mgumu na wa majaribu. Mtakatifu Paulo aliandika katika barua yake ya pili kwa Wakorintho 4, 5-12: “Maana tunachohubiri si sisi wenyewe, bali Yesu Kristo kama Bwana,... Tumesongwa kila upande, lakini hatuandamizwi; tunashangaa, lakini hatukati tamaa; kuudhiwa, lakini wala kuachwa; kupigwa chini, lakini si kuharibiwa. Sikuzote twachukua katika miili yetu kifo cha Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai siku zote tunatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Kwa hiyo,kifo kinafanya kazi ndani yetu, lakini uzima unafanya kazi ndani yenu.”
Padre PAM katika barua hiyo anaendelea kusema kuwa: "Ninawashukuru nyote, wa mbali na karibu, kwa ushiriki wenu katika ukombozi wao. Ninawashukuru kwa namna ya pekee Jimbo la Minna, pamoja na watu wengine mashuhuri, kwa kutupatia ushauri, mikakati na vifaa sahihi vya jinsi ya kufanya mchakato mzima. Asanteni nyote kwa uvumilivu. Tunawaombea uongofu wale wanaoendelea kufikiri kwamba njia rahisi zaidi ya kupata pesa ni kuwaumiza wengine. Tuendelee kuwa watoa uhai popote pale tulipo na kwa lolote tufanyalo ili wale tuliotumwa wapate uzima tele. Wenu katika Kristo, Padre PAM Dennis,Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika Kanda ya Ghana– Nigeria “, Anahitimisha Barua yake.
Kwa njia hiyo Padre Paul Sanogo asili yake ni kutoka Mali, huku Melkiori Dominick Mahinini ni mseminari Mtanzania mwenye umri wa miaka 27 anatoka Jimbo la Kigoma na ambaye alikuwa nchini Nigeria kufanya uzoefu wa kimisionari na Mapadre hao kabla ya kuendelea na masomo ya kitaalimungu, na anatoka parokia ya Kabanga mkoani Kigoma. Kwa mujibu wa kilichochapishwa na Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari (Fides), Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Benson Bana, naye alithibitisha kuachiwa huru kwa mseminari huyo na mwenzake. Hata katika mitandao ya Kijamii kupitia Youtube, Balozi Bana, alithibitisha akisema kwamba: “baada ya kuachiwa huru waliwapelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu maana kwa siku hizi tangu kutekwa kwao wamepitia katika shida mbali mbali, na hatua nyingine zingefuata na wangetoa taarifa zaidi.”
Vipindi vya utekaji nyara wa watu, wakiwemo makasisi na watwa kwa bahati mbaya ni vya kawaida nchini Nigeria. Katika taarifa za utekaji nyara ya tarehe 3 Agosti 2023 na mara baada ya kusambaa Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma aliandika barua ili kuwaomba waamini wasali kwa ajili ya kuachiwa huru hao watawa na vile vile Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, alisisitiza "umuhimu wa kuheshimu misingi ya haki za binadamu, na kuthibitisha kuungwa mkono na Kanisa kwa juhudi za wanadiplomasia ili kuhakikisha kuwa watu waliotekwa nyara wanaachiliwa bila masharti."