Mongolia:Mapenzi ya Mungu yatimie.Ushuhuda wa Mmisionari wa Fidei Donum
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika fursa ya Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Nchini Mongolia kuanzia tarehe 31 Agosti hadi 4 Septemba 2023, Padre Peter Hong anafafanua Nchi ya Mongolia katika mtazamo wa kuishi kiroho katika utumishi wake wa umisionari nchini humo. Kwa mujibu ake akizungumza na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides anasema “Kanisa la Kimongolia ni changa sana na dogo. Hili ni sharti la lazima kabisa ili Mungu aweze kufanya mapenzi yake. Ninaamini hii ni hali ambapo Mungu anaweza kuonesha kwa uwazi kabisa yaliyo katika mapenzi yake. Tukikariri Baba Yetu, tunasema, Mapenzi ya Baba yatimizwe duniani kama huko mbinguni, na tunaomba yafanyike huko Ulaan Baatar, Mongolia.”
Padre Peter Hong, mwenye umri wa miaka 40, padre wa Jimbo la Dajeon ya Korea alitumwa Mongolia miaka 5 iliyopita kama Mmisionari wa “ fidei donum, ikiwa ni sehemu ya historia ya ushirikiano la kimisionari kati ya Makanisa ya Mongolia na Korea Kusini ambayo imekuwa ikiendelea kwa takriban miaka 25. Ukaribu huo unaoneshwa kwa upande mmoja kwa kutumwa kwa mapadre wa “Fidei donum" (kwa sasa kuna wamisionari watatu kutoka jimbo la Daejon), kwa upande mwingine kukiwa na uwezekano wa waseminari wa Kimongolia kukamilisha masomo yao ya chuo kikuu nchini Korea Kusini.
Kwa mujibu wa Padre huko alisema: “Tunaishi neema ya kuwa wadogo na Ziara ya Kitume ya Papa Francisko ni fursa nzuri ya kuthibitisha hilo. Kanisa la Mongolia ni dogo sana, lakini Papa anakuja Mongolia hasa kwa sababu ya waamini 1,500 waliopo hapa. Hii inatukumbusha juu ya Umwilisho wa Yesu Kristo, ambaye alijivua nguo, akajifanya mdogo, akaja katika ulimwengu huu kuokoa ubinadamu, na hapa Mongolia, basi ni njia ya uhakika ya kumfuata Yesu,”alisema mmisionari huyo. Wamongolia na Wakorea ni watu wenye uhusiano wa kikabila kwani katika karne ya 13, Wamongolia walivamia China na peninsula ya Korea, na hii iliacha uhusiano wa lugha na kiutamaduni; urithi fulani uliohifadhiwa kwa karne nyingi unahusu makundi ya farasi-mwitu waliopo kwenye kisiwa cha Korea Kusini cha Cheju, ambacho bado kinaitwa ‘Mongols’leo hii.
Katika Nchi ya Mongolia leo hii utamaduni wa Kikorea umeenea kwa mfano (chakula, mila na utamaduni, muziki wa K-pop, na mfululizo wa televisheni); kwa kuzingatia sifa za kimaumbile zinazofanana, kwa kampeni za utangazaji nchini Mongolia, kampuni za Korea Kusini hazijisumbui kupiga tena picha za video au mabango yenye miundo ya ndani. Mnamo 2021, Ulaan Baatar na Seoul walianzisha ushirikiano ili kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, hasa katika nyanja za madini, utalii na maendeleo ya miji. Biashara, utalii, mabadilishano ya kiutamaduni na ushirikiano wa kielimu na Korea Kusini huingiliana na kuwa na ushawishi kwa jamii ya Kimongolia. Mikutano ya hivi karibuni ya kisiasa imepanga kuongeza uwekezaji na kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na elimu, kwa wazo kwamba hii itakuwa na matokeo chanya kwa mustakabali wa Mongolia.