Kuanzia Agosti14-17,Katibu wa Vatican atakuwa ziara nchini Sudan Kusini
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Juba, Kardinali mteule Stephen Ameyu Martin Mulla, katika Mkutano na waandishi wa Habari kupitia ukurasa wa Facebook wa Radio Bakhita, Jumamosi jioni tarehe 12 Agosti 2023, alibainisha juu ya ziara ya Kardinali Parolin, Katibu wa Vatican kwa mara ya pili kuanzia Jumatatu tarehe 14-17 Agosti 2023; na kwamba lengo lake ni mwendelezo wa ziara ya hivi karibuni ya Papa Francisko nchini Sudan Kusini, na ambapo atakutana na Rais Salva Kiir na naibu wake kwa kutaka kutekelezwa kwa makubaliano ya amani. Kardinali Parolin pia anatarajiwa kutembelea majimbo katoliki ya Malakal na Rumbek.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ameyu, alisema: “Anakuja kufuatilia baadhi ya kazi ambazo alipewa na kazi hizo ziko wazi katika akili zetu kama serikali na Kanisa. Tuko hapa tukisisitiza suala la amani ya kina miongoni mwa watu, amani ambayo ilitiwa saini mjini Addis Ababa, Mkataba Uliohuishwa wa Amani. Kufikia sasa bado haujatekelezwa kwa utaratibu na kuna dosari kuhusu mkataba huu na kwa hivyo lazima ufuatwe,” alisisitiza Askofu Mkuu Ameyu. Kwa kuongezea: “Baba Mtakatifu alipokuja, alituambia, hasa serikali kwamba watu wa Sudan Kusini wanapaswa kuwa pamoja, wafanye kazi pamoja. Na alisisitiza kuwa: “Umoja ndio utakaoweza kutuletea amani na Papa alirudia neno ‘pamoja’ mara tatu kwa sababu ameongeza Ameyu "umoja maana yake ni umoja, umoja maana yake tunaweza kupata amani kati yetu na umoja maana yake kuna aina ya mazingira ya kirafiki miongoni mwetu,” alisisitiza Askofu Mkuu Ameyu
Kulingana na ratiba ya Kardinali, baada ya kukutana na Rais Kiir na viongozi wakuu wa serikali, Kardinali Parolin atawatembelea baadhi ya viongozi wakuu akiwemo Kadinali Gabriel Zubeir, na kupanda miti katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresa. Askofu Mkuu Ameyu alisema kuwa Katibu wa Vatican alitaka ziara yake ishughulikiwe kwa faragha na mapadre, watawa na waamin wachache sana wa kumpokea katika uwanja wa ndege siku ya Jumatatu karibu saa 4.00 asubuhi. Kwa mujibu wa Kardinali Ameyu alisema: “Kadinali Parolin angependa ziara hii ishughulikiwe zaidi faraghani na hapendi mapokezi makubwa. Hata hivyo, kutakuwa na baadhi ya viongozi wa dini, watawa wachache na ndugu wa kwenda kumlaki katika uwanja wa ndege akifika, kisha atapelekwa Ubalozi wa Vatican na taratibu nyingine zitafuata." Aidha alisema kuwa "Ziara hii ni maalum kwa Jimbo la Malakal ambapo amealikwa na Askofu Stephen Nyodo Ador wa Malakal, kwenda kujionea hali ya Malakal. Sisi sote tunaifahamu hali ya Malakal, mikasa ya asili, mafuriko na mambo mengine mengi na mikasa inayosababishwa na wanadamu,” Alikiri Askofu Mkuu Ameyu. “Pia, kuna fursa ya amani kwa hivyo atapenda kwenda kuona Malakal na kutoka hapo ataelekea Rumbek na atarudi hapa na kuruka mara moja tarehe 17 Agosti hadi Roma, "alihitimisha maelezo yake Askofu Mkuu Ameyu.