Ishara ya Mama wa Mbinguni ya Kanisa nchini Mongolia,katika video mpya kutoka Fides!
Vatican News.
Uwepo na shughuli za wamisionari wa Shirika la Wasalesian la Mtakatifu John Bosco huko Mongolia na historia ya kusisimua ya sanamu ya Mama iliyopatikana kwenye shimo la taka taka na ambayo imekuwa ishara ya Kanisa katika la nchi ya Asia inasimuliwa na Padre Leung Kon Chiu, Msalesian kutoka Hong Kong, kwa karibu miaka 18 yuko Mongolia, katika ripoti ya sita ya video iliyotolewa kwa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari na Teresa Tseng Kuang yi, kwa mtazamo wa Ziara ya Kitume ya Papa Francis kuanzia tarehe 31 Agosti hadi 4 Septemba 2023.
Kuwasili kwa Wasalesiani huko Mongolia, kwa maelezo ya mmisionari huyo, kulianza mnamo mwaka wa 2001 kwa mwaliko wa Askofu wa eneo hilo, Padilla, ambaye aliwaita wamsaidie katika uwanja wa elimu. Padre alieleza kazi zilizoanzishwa na kuendelezwa katika miaka ya hivi karibuni, katika sehemu mbalimbali, na wamisionari wa shirika lake kama vile shule za kitaaluma, pia zinazothaminiwa na mamlaka ya kiraia, kozi za Kiingereza na Computer (IT), parokia ya Darkhan iliyojitolea kwa Mtakatifu Mari Msaada wa Wakristo, shamba la kukuza mbinu za kisasa za uzalishaji wa kilimo katika nchi ambayo kilimo hakitumiki sana, hufanya kazi kusaidia watoto wa mitaani huko Ulaanbaatar.
Historia ya sanamu ya Maria, Mama wa Mbinguni
Padre Leung Kon Chiu kisha alisimulia historia inayohusishwa na sanamu ya Maria inayopendwa sana huko Mongolia: baada ya kuipata kwenye jaa la taka taka la Darkhan, mwanamke mmoja aliiweka katika sehemu nzuri zaidi ya nyumba yake ambapo mnamo 2013 iligunduliwa na mtawa wa Kisalesian. “Ikiwa alichosema Mama huyo ni kweli aliipata sanamu hii kabla ya sisi makasisi na watawa hatujafika katika sehemu hiyo ya nchi. Kwa hivyo Mama huyu ametuandalia mazingira. Na kusema ukweli kwamba tuko hapa ni neema yake.”Alisisitiza Padre huyo. Alipopata habari kuhusu kupatikana, Kardinali Giorgio Marengo, Balozi wa Kitume wa Ulaanbaatar, aliomba sanamu hiyo kuwekwa katika Kanisa Kuu na pia alizungumza juu yake na Papa Francisko ambaye alipendekeza kumpatia Mama aliyeoneshwa kwenye sanamu jina rasmi. Hilo la “Mama wa Mbinguni” liliamuliwa kufuatia na Kardinali Marengo ambaye aliteua kipindi cha kuanzia tarehe 8 Desemba mwaka 2022 hadi tarehe 8 Desemba mwaka 2023 kuwa Mwaka wa Mama Yetu wa Mongolia.
Mongolia ni Kanisa linalochanua katika ndoto ya Don Bosco
Hatimaye, katika maelezo kwa njia ya video hiyo, Padre Leung alikumbuka moja ya ndoto maarufu za Don Bosco ambayo inahusu Mongolia. “Ndoto za Don Bosco hazikuwa ndoto tu, lakini ufunuo halisi kutoka kwa Mungu”. Na katika mmoja wao, mtakatifu wa Piemonte alisema kwamba aliona maua ya utukufu wa Ukatoliki, hata zaidi ya huko Ulaya, katika nchi ya zamani sana na kubwa sana, shukrani pia kwa kazi ya wamisionari ambao walitoka Tartaria. Na Tartariani ni jina la kale la Mongolia, alifafanua Padre Leung. Siku chache kabla ya kuwasili kwa Baba Mtakatifu Francisko, Padre amesema: “Ninaamini kwamba kuwasili kwa Papa hapa ni ishara kutoka kwa Mungu. Siwezi kabisa kusema kwa sababu sijui. Lakini ninadhani historia itatuambia...” alihitimisha.