Dominika ya 21 Mwaka A:Umasiha wa Kristo na Ukulu wa Mtume Petro!
Na Padre Paschal Ighondo; – Radio Vatican,
Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanaweka wazi kuwa mamlaka yoyote halali, ya kisiasa au ya kidini yanatoka kwa Mungu. Lakini msisitizo ni fundisho juu ya Ukulu wa mtume Petro wa kumpewa mamlaka na Yesu ya kuliongoza na kulilinda Kanisa lake hapa duniani, kazi na mamlaka anayoyapokea kila Baba mtakatifu, ambaye ni Askofu wa Roma na Halifa wa Mtume Petro ya kuliongoza Kanisa lote ulimwenguni chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 22:19-23). Somo hili ni utabiri wa Nabii Isaya wa kunyang’anywa mamlaka kwa Shebna juu ya nyumba ya mfalme Hezekia na kuyapewa Eliakimu kwa ishara kuu mbili; kupewa funguo za kufunga na kufunga yote katika Israeli na mavazi atakayoyavaa. Hiki kilikuwa ni kipindi ambapo mji wa Yerusalemu ulitishiwa na maadui zake toka taifa la waashuru. Mfalme Hezekia aliomba ushauri kwa nabii Isaya nini cha kufanya. Nabii Isaya alimwambia asiogope, amtegemee Mungu, ndiye atakayeiokoa Yerusalemu. Shebna, msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme kwa majivuno ya utajiri wake na kwa mamlaka makubwa aliyokuwa nayo juu ya watu, alimshauri mfalme asifuate ushauri wa nabii Isaya wa kumtegemea Mungu. Ndipo sasa Nabii Isaya akamlaani Shebna kuwa atapelekwa uhamishoni na kufia huko n anafasi yake itachukuliwa na Eliakimu ambaye ni mwaminifu na mcha Mungu. Ni kweli Eliakimu alichaguliwa kushika nafasi ya Shebna baada ya yeye kupelekwa uhamishoni.
Eliakimu kwa nafasi hii alivaa mavazi maalum, kanzu nyeupe na mkanda kiunoni. Alipewa ufunguo mkubwa wa mbao ambao aliubeba begani mwake kuonesha mamlaka aliyokuwa ya kufungua au kufunga. Alikuwa na mamlaka juu ya mji mzima kufungua milango yake asubuhi na kuifunga jioni, mamlaka juu ya kinara walikokaa askari walinzi wa mji, mamlaka juu ya hazina ya mfalme kulikohifadhiwa vitu vya thamani katika chumba cha ndani karibu na hekalu na karibu na ngome. Huu ndio uwezo na mamlaka aliyopewa Eliakimu kwa maneno ya Isaya kuwa; “Akifunga, hakuna atakayefungua na akifungua, hakuna atakayefunga” (Isa. 22:22). Nabii Isya anamfananisha Eliakimu na ndoana ya mbao au chuma ambayo inaitumika kuchimba ardhini na kufungia kamba inayoshikilia hema ya wachungaji au askari walinzi kwa usalama nalo linaweza kuhimili dhoruba yoyote ile na hivyo walioko ndani wanakuwa salama. Huu ni usalama ambao Eliakimu angeuleta katika mji wa Yerusalemu aliokabidhiwa ausimamie.
Ni kweli masimuliza ynasema kuwa Eliakimu aliweza kuleta amani na usalama katika mji wa Yerusalemu kwa sababu alimcha Mungu na alikuwa mwaminifu kwa maongozi yake. Hapa tunaona sifa za kiongozi mzuri wa kisiasa au kidini anakuwa na hofu ya Mungu, anatii amri na maagizo yake Mungu, anamsikiliza Mungu na anatambua kuwa amewekwa na Mungu awaongoze watu kwa jina lake na kwa niaba yake awapeleke kwake akiweka mipango ya kuwaletea maendeleo ya kiroho na kimwili. Kinyume chake ni kweli kiongozi dhalimu na fisadi ana kiburi na majivuno hatasikilizi watu aliokabidhiwa na Mungu wala pia hamsikilizi Mungu mwenyewe, wala ushauri wa watu, na hivyo daima ataishia pabaya kama Shebna, uhamishoni na kufia katika nchi ya kigeni. Utabiri huu wa nabii Isaya licha ya kuwa yote aliyoyatabiri yalitukia katika historia ya wana wa Israeli katika Agano la Kale, ulikuwa pia ni utabiri wa yalikuja kutukia katika Agano Jipya kwa kusimikwa kwa Kanisa juu ya Mtume Petro Khalifa wa Yesu Kristo kwa “kupewa funguo”, ishara ya mamlaka anayokabidhiwa mwanadamu na Mungu kwa mambo yamhusuyo Mungu kama ilivyo katika Injili ya domenika hii inayohusu ukulu wa mtume Petro katika kukabidhiwa madaraka ya kuliongoza Kanisa.
Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 11:33-36). Katika somo hili mtume Paulo anaisifu na kuitukuza hekima ya Mungu inayopita ufahamu wa kibinadamu. Hekima hii inajionyesha kwa kuwaokoa watu wote, wayahudi na wasio wayahudi, kwa njia ya mwanae mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo. Paulo anatuambia kuwa hii; “Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangaliielewa hawangalimsulibisha Bwana wa utukufu” (1Kor 2:8). Hekima hii ndiyo inayowapa mamlaka wale anaowachagua Mungu wawe viongozi wa watu wake, ili wawaongoze vyema kwa kusikiliza na kufuata maongozi yake.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 16:13-20). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyompa Petro mamlaka ya kuliongoza Taifa Jipya teule la Mungu yaani Kanisa na kumkabidhi funguo kama alama ya ukuu, mamlaka na utumishi wake, baada ya kuungama kuwa Yesu ni Masiya, Mwana wa Mungu aliye hai. Mamalaka haya ndiyo anayokuwanayo kila Baba mtakatifu anayechagualiwa kuliongoza Kanisa kwani ni halifa wa Mtume Petro. Kiri hii ya imani ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu na sio kwamba Petro aliitambua kwa akili na uweza wake mwenyewe.
Tukio hili linatokea katika mji wa Kaisaria-Filipo nje kidogo ya Palestina kaskazini mwa Galilaya. Historia inaosimulia kuwa katika mji huu palikuwa na miungu mingi ya wagiriki na wa Syria. Katika mji huu Herode Mkuu alijenga hekalu akaweka sanamu ya Kaisari wa Roma aliyepaswa kuabudiwa kama mungu ishara ya shukrani kwake kwa kupewa eneo hilo alitawale. Filipo mtoto wake Herode aliongezea jina lake pakawa panaitwa Kaisaria-Filipo. Yesu akiwa katika eneo hili anawauliza wanafunzi wake swali la kutaka kujua watu wanasema yeye ni nani na wanafunzi wake wenyewe wanamchukulia kuwa ni nini? Swali hili ni la maana sana hata kwetu katika kumpenda, kumfuasa na kumwamini Kristo Yesu. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema; “Basi watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena watamwaminije kama hawajapata kumsikia wala kumjua?” (Rom 10:14).
Kujua ni msingi wa mahusiano. Jinsi tunavyofahamu mtu ndivyo tunavyohusiana naye. Kumbe tunavyomjua Yesu ndivyo tunavyohusiana naye. Wayahudi hawakumuelewa vizuri Yesu ni nani kwao. Mwanzoni walimuona kama mfalme na mkombozi wao kuwaokoa kutoka katika mikono ya maadui zao. Baadae wakamuona kama mwanaharakati, mwanamapinduzi na mpinzani wa kisiasa. Na mwisho wakamuona kama mhalifu na hivyo wakaamua auawe kwa kutundikwa msalabani. Kumbe hata katika maisha ya kawaida ukijua kuwa Yesu ni Mungu muweza wa yote, utamkabidhi maisha na mahangaiko yako. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu anayejua yote hutamdanganya. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu na Mungu ni upendo, basi nawe utampenda. Ukijua kuwa Yesu ameukomboa ulimwengu kwa msalaba, utakuwa tayari kuteseka kwa ajili ya imani yako kwake. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu na kwa Mungu siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja, hutakata tamaa hata ukiona anachelea kujibu sala zako maana unaelewa kuwa Bwana hakawii kuitimiza ahadi zake (2Pet 3:9). Lakini ukidhani kuwa utawala wa Kristo ni wa hapa duniani utamwomba ukae mkono wa kulia au wa kushoto katika utawala wake ili upate sifa na utajiri hapa hapa duniani bila kushughulikia maisha ya kiroho. Ndiyo maana Mtakatifu Augustino alisema; “nimechelewa mno kukujua wewe ee Bwana”.
Petro kama kiongozi wa Kanisa alikabidhiwa funguo ishara ya mamlaka na majukumu aliyopewa. Lakini sisi nasi kwa ubatizo, tukiwa chini ya Baba Mtakatifu, tumeshirikishwa jukumu la kuwafunguliwa watu ufalme wa mbinguni yaani kuwapatia habari njema, kuwafundisha maisha ya kumfuasa Yesu kwa mifano mema ya maisha yetu. Ili tuweze kuwafundisha watu vizuri Yesu ni nani, lazima sisi wenyewe tumfahamu. Hatuwezi kuwafundisha watu za Yesu kama sisi hatumfahamu vizuri katika uhalisia. Tutambue tusipotimiza wajibu huu, ujumbe huu; “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawafungia watu mlango wa ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii ndani, wala hamuwaruhusu wanaotaka kuingia waingie” (Mt 23:13-14), unatuhusu.
Ili tuweze kumfahamu vyema Kristo lazima tuwe na moyo wa unyenyekevu na imani ya kupokea ufunuo wa Mungu unaotolewa kupitia maandiko matakatifu, mafundisho ya Mababa wa imani, sala na tafakari binafsi. Lakini pia utambuzi binafsi ni wa muhimu katika imani. Tusimfahamu Yesu kwa jinsi tu tunavyosikia au tunavyofundishwa au tunavyosoma katika maandiko matakatifu, bali pia kwa jinsi ya maisha yako. Ndiyo maana Yesu aliposikia majibu ya Mitume jinsi watu wanavyosema, aliwataka na wao wasema kwa nafsi zao binafsi jinsi wanavyomfahamu. Hata Pilato alipomuuliza Yesu: “Ati wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu: Je, hayo ni maneno yako mwenyewe, au wengine wamekuambia habari hiyo juu yangu?” (Yn 18:34). Tutambue kuwa kuwa mkristo sio tu kujua kuhusu Kristo bali kumjua Kristo na kumfanya sehemu ya maisha yako. Unaweza kusoma sana teolojia utaelewa vizuri kabisa lakini ukawa hujamtambua Kristo bado. Unaweza kufahamu mengi kuhusu Kristo lakini usimfahamu Kristo.
Tukumbuke daima kuwa kumfahamu Kristo kunahitaji unyenyekevu kama maneno ya shangilio yanavyotilia mkazo kusema; “Kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga” (Mt. 11 : 25). Naye mzaburi katika wimbo wa katikati alipotafakari moyoni mwake alisema; “Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu. Naye amjua mwenye kujivuna” (Zab. 137: 9). Kumbe Mungu kupitia kwa Kristo anawafunulia wanyenyekevu siri za mbingu ili waweze kutambua nguvu zake katika maisha yao na hivyo kuwa imara hata katika mateso. Basi tujitahidi siku zote kutafakari ukuu wa matendo ya Mungu katika maisha yetu. Tuwe watu wa sala na kumkabidhi Mungu njia zetu ili ajifunue yeye ni nani na atuongoze katika kila jambo tuweze kumpendeze Yeye siku zote kama sala baada ya kumunio inavyohitimisha ikisema; “Ee Bwana, tunakuomba dawa ya rehema yako ituponye kabisa. Utukamilishe kwa wema wako na kutuhifadhi hivi hata tuweze kukupendeza katika mambo yote”.
Tumsifu Yesu Kristo.