Maaskofu Kenya waingilia kati,wakihimiza mazungumzo na amani
Na Angella Rwezaula, - Vatican
Kwa siku hizi mji mkuu wa Nairobi, Mombasa na Kisumu, ndani mwake kumekuwa na maandamano makubwa na yenye vurugu ya kupinga msururu wa ushuru ulioletwa na serikali ya Rais William Ruto. Maandamano hayo yalianza tarehe 19 Julai 2023 baada ya Raila Odinga, kiongozi wa upinzani kutoa Azimio la Umoja (Tamko la Umoja), kuanzisha maandamano ya siku tatu. Shule na biashara zilifungwa, usafiri wa umma ulisimamishwa na polisi wakiwa na vifaa vya kutuliza ghasia.
Kutokana na kile kilichoibuka kutoka kwa vyombo vya habari vya humo nchini, muungano wa Azimio uliwaalika Wakenya kujitokeza barabarani wakiwa wamejihami kwa vyungu na miiko, kuiomba serikali kupitia upya sheria ya fedha na kulisha nchi. Tayari wiki iliyopita watu 13 walikuwa wamepoteza maisha katika makabiliano na polisi na zaidi ya 20 walijeruhiwa vibaya. Majibu ya maaskofu wa Kenya (KCCB) yalikuwa ya haraka na waliomba kwa sauti kubwa kwamba mazungumzo ya pande mbili yaliyoshindwa, ambayo yanahusisha viongozi wa kidini pamoja na watetezi wengine na vyombo vingine, yaanze tena katika muktadha tofauti.
Kwa mujibu wa Maaskofu wakenya wanabainisha kuwa:“Tunaamini kwamba hakuna tatizo, hata liwe gumu kiasi gani, ambalo haliwezi kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo. Ni lazima kwa gharama yoyote ile tuepuke kupoteza maisha ya binadamu. Hakuna damu zaidi inayopaswa kumwagika,” Maaskofu hao walisema katika wito wao wa dhati kwa Rais Ruto na Odinga. “Ni muhimu kwamba serikali isikilize Wakenya kikamilifu, kutoa maelezo wazi na ya ukweli kwa ahadi zilizovunjika na kuweka kipaumbele kwa sera zinazopunguza mzigo wa kijamii na kiuchumi,” walisisitiza. “Mambo mengi bado hayaeleweki kuhusu sera na mwelekeo wa serikali; kwa mfano, elimu, afya, hali ya maskini, mikakati ya kuboresha ajira, wanasema wakiangazia vipaumbele vya Kenya.
“Tunajua kuna wahalifu wanaojichanganya miongoni mwa waandamanaji kuharibu mali, kuwaibia watu, kujeruhi na hata kuua. Polisi wanapaswa kuwafungulia mashtaka ili kuhakikisha maandamano ya amani yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria,” walionya maaskofu. Kinachoongeza machafuko ambayo yanazidi kuzorota nchini ni wahanga wa kile kinachoitwa “madhehebu ya mfungo” ambao kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, wamefariki zaidi ya 400, baada ya polisi kuwafukua wafuasi zaidi kutoka kwenye makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakaola, katika ukanda wa pwani ya nchi hiyo.