2023.07.26   Watawa 35 wa Shirika Jipya la Mtakatifu Karoli Lwanga,Jimboni Bukoba Tanzania limeona nadhiri za kwanza katika Parokia ya Mtakatifu Maria wa Mateso saba,Kashozi. 2023.07.26 Watawa 35 wa Shirika Jipya la Mtakatifu Karoli Lwanga,Jimboni Bukoba Tanzania limeona nadhiri za kwanza katika Parokia ya Mtakatifu Maria wa Mateso saba,Kashozi. 

Bukoba,Tanzania:kuanza Shirika Jipya&Nadhiri za kwanza kwa watawa 35 wa Mt.Karoli Lwanga!

Julai 25,limeanza rasimi Shirika la Mtakatifu Caroli Lwanga,Jimbo Katoliki la Bukoba,Tanzania kwa nadhiri za I za manovisi 35 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba,jimboni huo.Hili ni tukio kubwa kwa zaidi ya miaka 60 ya wahusika wakiishi udugu wa kijumuiya(Banyakaroli).Misa iliongozwa na Askofu Kilaini,Msimamizi wa Kitume wa Jimbo hilo.

Na Angella Rwezaula, - Vatican & Patriki Tibanga,-Radio Mbiu -Bukoba

Jumla ya Wanovisi 35 wameweka nadhiri kwa mara ya kwanza kwa miaka zaidi ya 60, tangu ulipoanzishwa Udugu wa Jumuiya  ya Mtakatifu Karoli Lwanga  ambapo kwa hivi karibuni limekuwa shirika  la Jimboni Bukoba linalotambulika. Misa Takatifu ilifanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba, Kashozi,  tarehe 25 Julai kwa kuadhimishwa na Askofu Method Kilaini .msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Bukoba,  akisaidiaiana na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo katoliki la Kayanga, Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo katoliki la Rulenge Ngara,  Askofu Augistino Shao wa Jimbo katoliki la  Zanzibar, na Askofu Desderius Rwoma Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Kwa upande wa Jimbo la Bukoba tukio hilo lilikuwa kubwa ambalo, idhaa ya kiswahili inapenda kukuletea mahubiri yake  Askofu Methodius Kilain, baada ya masomo ya tarehe 25 Julai 2023 ambayo Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Mtakatifu Yakobo Mtume  na  Somo la kwanza,  lilitoka 1 Sam. 3:1-10; 2 Kor. 4:7-15 na hatimaye Injili ya  Mt. 20:20-28.  

Maandamano ya kuingia kanisa la Bikira Maria wa Mateso Saba,Kashozi Bukoba Tanzania.
Maandamano ya kuingia kanisa la Bikira Maria wa Mateso Saba,Kashozi Bukoba Tanzania.

Askofu Kilaini akianza mahubiri hayo alisema “Sote tuko hapa kwa tukio kubwa sana la kihistoria, si kawaida kwamba askofu atoke Zanzibar kuja Bukoba hivi hivi au atoke Kayanga au Rulenge Ngara. Si kawaida Mama Mkuu wa shirika kubwa la Iringa asafiri na kukaa nasi wiki nzima na kamati nzima ya shirika na watawa wengine bila kuwataja wengine wengi ambao tunekuja kuwa kaishemboni, ikimaanisha mashuhuhuda wa neema kubwa ya Bwana.  Shirika jipya linazinduliwa leo kwa watawa wa kwanza kuweka nadhiri zao za utawa. Tumshukuru Mungu. Leo ni siku ya shahidi wa kwanza ambaye mwenye siku ni Mtume Yakobo. Mtakatifu Mtume Yakobo alikuwa kati ya wale wa kwanza kuitwa na Bwana wetu Yesu Kristu pamoja na mdogo wake Mtume Yohane. Walishuhudia sehemu zote muhimu za Bwana wetu Yesu Kristu pamoja na mtume Petro. Mama yao Salome alijaribu kuwatetea wapate nafasi maalum katika ufalme wa Bwana. Hii iliwafanya wenzao waone wivu lakini Bwana anatukumbumbusha kwamba kumtumikia Mungu siyo kupata faida binafsi bali ni kutumikia na kujitoa. Hilo ni somo kwetu sote. Mwishoni alikuwa ndiye mtume wa kwanza kufa shahidi akishuhudia Bwana wake aliyemwamini na kumtegemea.” Askofu Kilaini akiendelea na tafakari hiyo alisema “Sikukuu hiyo tunaiunganisha na Mtakatifu Kalori Lwanga na wenzake waliofia dini Uganda. Wengine kati yao walikuwa bado watoto kama Kizito lakini walihimiri maumivu yote kwa jina la Bwana.

Misa kwa ajili ya nadhiri za manovizi 35 wa Shirika Jipya la Mtakatifu Karoli Lwanga, Bukoba
Misa kwa ajili ya nadhiri za manovizi 35 wa Shirika Jipya la Mtakatifu Karoli Lwanga, Bukoba

'Shirika la Banyakalori' na kijana wa kwanza 'Bernardo Mutekanga'

Kwa upande wa shirika hilo ambalo lilikuwa ni tukio la siku, Askofu Kilaini alisema “Mwazilishi wa shirika, Ta Bernardo Mutekanga aliwakabidhi kwa ulinzi na mfano wa shahidi huyu shupavu Kalori Lwanga, na hivyo  nasi tunaendeleza mapokeo hayo kwa sababu ndiyo yametufikisha siku ya leo. Leo sitoi historia ya Banyakalori au ya Mpendwa wetu Mutekanga bali kuonesha tu hawa dada zetu wanaoweka nadhiri zao walitoka wapi. Mnamo tarehe 13 Januari 1942 Padre Heise wa shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) aliunda kikundi cha vijana wa kutetea Kanisa dhidi ya wachokozi na kukiita Catholic Young Men’s Association of Kashozi (CYMAC)” na kumchagua kijana Bernardo Mutekanga kuwa kiongozi wao na mwezi Juni 1942 akawaweka chini ya ulinzi wa Mtakatifu Kalori Lwanga. Kijana Mutekanga alikuwa shupavu na katika miaka ya 50 alitumwa sehemu mbali mbali za Tanzania kuendeleza utume wa uliojulikana kwa wengi kwa jina la Aksio Katoliki akiuunganisha na ujumbe wa Kalori Lwanga, huko  Songea, Mtwara, Iringa, Zanzibar na kwingineko.”

Manovisi 35 wa Shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga kabla ya kufunga Nadhiri za Kwanza
Manovisi 35 wa Shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga kabla ya kufunga Nadhiri za Kwanza

Askofu Kilaini kwa hiyo alisisitiza kwamba: “Mnamo tarehe 20 Machi 1959 ndipo mpendwa Ndugu na baba Bernardo Mutekanga aliunda kikundi cha wasichana wacha Mungu ambao walijitoa kumtumikia Mwenyezi Mungu. Toka wakati huo hadi anafariki aliwalea na kuwapa karama yake ya moyo wa kujitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa mfano wa Kalori Lwanga na mashahidi wa Uganda; kuwahudumia maskini na kutangaza Neno la Mungu bila kuchoka. Aliweka mbele yao mtakatifu Kalori Lwanga akiwaasa kuwa tayari kwa kila jambo na kuwa na uvumilivu, ustahimilivu na imani kama ya Kalori Lwanga. Kwa njia hiyo “Kuna wasichana wengi waliopitia mikononi mwake  na wakaingia mashirika mengine, kama vile ya Wakanosa, Binti wa Msaada wa daima, Masista wa Upendo Upeo wa  Jimbo la Kayanga na mashirika mengine walikokwenda moja mmoja. Lakini mzee Mutekanga, mtu mwenye Imani kubwa, hakuchoka akitumainia kwamba siku moja wasichana wake wataunda shirika la watawa”.

Manovisi wa Shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga katika Parokia ya Kashozi, Bukoba
Manovisi wa Shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga katika Parokia ya Kashozi, Bukoba

Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba vile vile alikiri kwamba “Wakati naandika historia ya jimbo la Bukoba tulipokuwa tunaadhimisha miaka 100 ya Ukristu, niliandika juu wa walei wachache sana na mmoja wao mwenye nafasi kubwa alikuwa ndugu Mutekanga, mmojawapo wa mashujaa  ambaye siyo tu wa Bukoba bali wa Kagera nzima. Mzee Bernardo Mutekanga alipofariki mnamo tarehe 7 Julai 2011, ilionekana kwamba sasa wamekuwa yatima bila mbele au nyuma kumbe alipokwenda kwa Baba aliweza kuwatetea na kufanya makubwa kuliko hata yale aliyoyafanya akiwa kati yenu. Ninakumbuka tulipopata hiyo habari nilikuwa na mneo somo wangu Metodia kule Ishozi aliniuliza swali moja tu sasa tutakuwa wa nani? Nilimjibu hatutawatupa kamwe; nikiungwa mkono na askofu Nestor Timanywa tuliahidi kwamba tutakuwa pamoja nanyi katika safari hii."

4 Julai 2018 tangazo la kusinduliwa mchakato wa Shirika la Mtakatifu Karoli

"Baba askofu Desiderius Rwoma alipofika aliwachukua kama binti wake na kuwahangaikia.  Mnamo Tarehe 4 Julai  2018, alitangaza na kuzindua rasmi mchakato wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Karoli Lwanga la jimbo Katoliki la Bukoba na kutuma maombi Roma ili likubaliwe. Baada ya kuhangaika sana katika kuomba mashirika mbali mbali, Roho Mtakatifu mnamo mwaka 2019 alileta zawadi kubwa kwa shirika tarajiwa la Masista wa Shirika la Wateresina wa Iringa chini ya Mhes. Sr. Teresia Kindole akiwa Mama Mkuu waliojitosa kulea shirika hili. Wamejitoa bila kujibakiza wakishiriki magumu yenu na kutoa siyo tu maisha yao lakini na nyenzo zote kwa hali na mali. Kwa kuongezea katika hilo, Askofu Kilaini alisisitiza kuwa: “Asante sana! Mama Kindole, Mama Alvina na masista wote kwa moyo wenu wa kimama na kikristu. Mungu tu ndiye anaweza kuwazawadi na zawadi kubwa ni siku ya leo.

Maisha ni safari ndefu, hatimaye  Banyakaroli wametambuliwa kuwa shirika
Maisha ni safari ndefu, hatimaye Banyakaroli wametambuliwa kuwa shirika

Kuanzia tarehe 15 Agosti 2019 walipitisha kikundi chote katika hatua ya Uaspiranti na upostulanti. Mnamo Mwaka 2021 kikundi cha kwanza kiliingia rasmi malezi ya miaka miwili ya unovisi ambayo sasa imekamilika. Baada ya Askofu Desiderius Rwoma kustaafu, ilibidi nichukue jukumu lote moja kwa moja. Muhimu ilikuwa ni mawasiliano na Roma ili shirika liende sambamba na matakwa ya Kanisa. Baada ya kupata kinachohitajika ilikuwa bahati nilipokwenda Roma kwa matembezi ya Ad Limina ya maaskofu aliweza kumwona uso kwa uso mhusika wa watawa katika Idara ya Uinjilishaji Roma, Monsi Padre Joseph Koonamparapil, C.M.F. Nilimkabidhi hati zilizohitajika zikiwemo katiba ya shirika, hati ya kusimikwa shirika, barua za kuunga mkono  shirika kutoka kwangu kama Msimamizi wa Kitume, Mama Mkuu na Mlezi Mkuu wa Shirika,  Sr. Teresia Kindole, maaskofu wenye watawa na wanaowafahamu, Askofu Severini Niwemugizi wa Rulenge Ngara, Askofu Agostino Shao wa Zanzibar na Askofu Almachius Rweyongeza wa Kayanga waliunga mkono kwa nguvu sana pamoja na kujibu maswali yaliyoulizwa”. Baada ya hayo alituhakishia kwamba sasa mchakato wa kufikia utambuzi kamili utaendelea kama mashirika mengine, na kwamba sasa manovisi waweke nadhiri zao na masista waishi maisha ya kawaida kama mashirika mengine na ripoti itumwe Roma mara kwa mara juu ya maendeleo ya shirika. Hapa ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Padre Gilbert Gosbert Ndyamukama ambaye anafanya kazi katika ofisi za idara ya uinjilishaji Roma aliyesaidia sana kutuunganisha na kitengo husika bila msaada wake kazi ingeliniwa ngumu sana. Mungu ni Mwema huyu ni mjukuu wa mwanzilishi wa shirika Baba Bernardo Mutekanga. Bahati nzuri mama yake Helenestina mtoto wa Mutekanga yuko pamoja nasi leo hii.

Shirika kuanza rasmi 25 Julai 2023

Askofu Kilaini katika tafakari hili ndipo alitoa tamko rasmi kuhusu shirika kwamba:“ Leo ndiyo tarehe ambayo shirika linaanza rasmi kwa kuwapata masista wao wa kwanza “Shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga la jimbo Katoliki la Bukoba”. Tuchukue wakati huu kumshukuru Mungu, kufurahi na kujitayarisha kiroho na kimwili kwa ajili ya siku hiyo muhimu sana katika historia ya shirika letu. Pamoja na Sr. Teresia Kindole tunawashukuru walezi waliokuja hapa Bukoba wakiongozwa na Sr. Alvina Anjela Mbago ambao licha ya mapungufu na shida nyingi wamestahimili kwa furaha na kutufikisha katika matokeo haya chanya.  Sasa kazi inayobaki baada ya Mungu kutusafishia njia ni kwenda katika neema zake kwa juhudi na utauwa.” Askofu Kilaini akitafakari somo la Kwanza lililosomwa  alisema: “Katika somo la kwanza Samuel anaitwa kuwa nabii wa Bwana, mwanzoni hajui anadhani ni Heri ndiye anamwita lakini heri anapotambua anamwambia ukiitwa sema “Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.”

Watawa 35 baada ya kufunga nadhiri wamepewa katiba ya shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga
Watawa 35 baada ya kufunga nadhiri wamepewa katiba ya shirika la Mtakatifu Karoli Lwanga

Askofu kilaini alisema "Nanyi manovisi wetu leo Bwana anawaita na inabidi kuitikia. Leo nina furaha kubwa kwa sababu katika maisha yangu ya kushuhudia nadhiri sijashuhudia nadhiri za kwanza za watu ambao tayari wameshatoa maisha yao kwa Mungu kwa uaminifu mkubwa bila kusita hata wakati hali ilipoonekana ngumu walimtumainia Mungu. Jana nilipitia ili nami nifanye mazoezi kidogo nilijisikia nimenyenyekea sana Novizi Veronica alipokuja pole pole na kupiga magoti akifanya zoezi na kutia nadhiri zake. Novisi Veronika ana umri wa zaidi ya miaka 70 na aliingia akiwa msichana na alidumu kila mara akimtumainia Mungu amefanya kazi mbali mbali katika hospitali na pengine leo nadhiri za kwanza ni kuweka mhuri wa moto katika maisha aliyoyaishi. Na wako kadhaa kama yeye somo wangu Metodia, Bibiana na wengine. Tumshukuru Mungu kwa sababu sasa kama Anna wa fanueli wanamwona Bwana.” , Alisistiza kwa furaha kubwa na shukrani Askofu Kilaini.

Tazama mimi hapa nimekuja kuyafanya mapenzi yako
Tazama mimi hapa nimekuja kuyafanya mapenzi yako

Askofu Kilaini vile vile aliwageukia hata waamini washiriki  wa Ibada ya Misa hiyo na kusema kuwa: “Wapendwa mliokuja hapa kushuhudia makubwa ya Mungu, mwuujiza wa Mungu, kutumaini dhidi ya matumaini tuungane nao kumshukuru Mungu mwingi wa huruma na neema, kuwashukru wote ambao wamefanya mengi kufikisha siku ya furaha ya leo. Mwishowe tuwaombee kwamba sasa baada ya kufika hatua hii wadumu katika nadhiri zao. Anavyotuambia Mtakatifu  Paolo katika barua yake kwa wakorinto iliyosomwa leo: “Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. (Kor 4:7-9)” Kwa hiyo: “Tuwaombee na kaka zao mabrother nao siku moja wafikie hatua hii nzuri. Tuwashukuru wazazi wao Wanyakalori waendelee kuilea miito mingine ishamiri katika shirika hili jipya lakini kongwe.” Alihitimisha Askofu Methodius Kilain Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Bukoba Tanzania.

Kwa kukumbusha  tena ni kwamba hao walikuwa ni  jumla ya  Wanovisi 35 ambao waliweka nadhiri za kwanza katika Shirika hilo Jipya lakini Kongwe kama Askofu Kilaini alivyosimulia kwa zaidi ya miaka 60, tangu  walipaaanza kufanya uzoefu wa udugu. Na kama tulivyosikia wapo hata kaka zao, ambao bado hawajafikia idadi ya kuwawezesha kuwa shirika. Lakini kwa mpango wa Mungu nao, Roho Mtakatifu atawajalia kufika hatua hiyo, tuzidi kuwaombea. Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache alisema Bwana.

Shirika jipya la Mtakatifu Karoli Lwanga na watawa wake wa kwanza 35 Jimboni Bukoba,Tanzania

 

26 July 2023, 14:25