Askofu Lagweni: Watu wa Mungu Mbulu Upokeeni Msiba wa Pd. Nada Kwa Imani
Na Sarah Pelaji, - Dar es Salaam, Tanzania.
Jimbo Katoliki la Mbulu na Kanisa lote limepata simanzi baada ya kifo cha Paroko wa Porokia ya Karatu Misheni na Dekano wa Dekania ya Karatu Padre Pamfili Nada aliyefariki dunia baada kushambuliwa kanisani na mtu ambaye ana ulemavu wa akili ambaye naye aliuawa na watu waliofika Kanisani kutoa msaada. Padri Pamfili Nada amefariki dunia tarehe 19 Julai 2023 katika Hospital ya Fem Karatu alikopelekwa kwa ajili ya matibabu. Taarifa ya kifo chake imetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Askofu Anton Lagweni ambaye alifika eneo la tukio na kutoa pole kwa waamini wa Parokia ya Karatu misheni. Amewasihi wakristo, kuwa watulivu wakati huu wa kipindi cha msiba na pia, wapokee kwa imani taarifa hizo za kusikitisha na za ghafla. “Hili ni jambo ambalo hatuwezi kulirudisha, kwamba limetokea tujipe moyo, tusimame imara katika imani na tulipokee kwa imani tena kwa imani thabiti, kwa maana hiyo nina wapa wote pole.” Amesema Askofu Lagweni. Mhashamu Askofu Lagweni ameeleza kuwa Padre Pamfili alikuwa ni mtu ambaye aliufanya utume wake bila kuogopa na hata kifo chake kimetokea akiwa anapambana kulilinda Kanisa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dady Horacy Kolimba amesema wao kama serikali wanalitegemea Kanisa na hivyo kifo cha Padri Pamfili Nada ni pigo kwa Kanisa na taifa kwa ujumla huku akiomba jamii kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama. ‘’Tumesikitishwa sana na msiba huu na hasa jinsi ambavyo tukio hili limetokea. Padri Pamfili alikuwa ni kiongozi na sisi watu wa serikali tunalitegemea Kanisa hivyo kwetu ni pigo hivyo tushirikiane katika ulinzi jamii tuchukue tahadhari kabla ya hadhari,” amesema mkuu wa wilaya ya Karatu. Marehemu Padri Pamfili Nada enzi za uhai wake alihimiza sana familia na jamii kutunza mazingira kwa kupanda miti ya matunda katika maeneo yao, jambo ambalo alifanikiwa hasa katika maeneo aliyofanya utume wake ikiwamo Karatu. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri mwaka 1997 na Mwaka 2022 aliadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Daraja Takatifu ya upadri. Taarifa zinaeleza kuwa kijana mwenye umri wa miaka 30 anayesadikika kuwa na ulemavu wa akili alifika kanisani hapo majira ya saa tisa usiku kwa lengo la kutaka kusali na baada ya kuingia kanisani ndipo alipofanya mauaji hayo. Marehemu Padri Pamfili Nada atazikwa tarehe 22 Julai 2023 katika makaburi ya mapadri yaliyopo Kanisa Kuu la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Sanu Jimbo Katoliki Mbulu. Raha ya milele umpe ee Bwana na Mwanga wa Milele umwangazie apumzike kwa amani amina.