Tafuta

Sherehe ya Ekaristi iwe ni fursa kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu. Sherehe ya Ekaristi iwe ni fursa kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu.  (Vatican Media)

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Uwepo Halisi wa Kristo Kwa Mwili na Damu Yake Azizi

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha uwepo wa Kristo Yesu kwa nguvu ya Neno lake na Roho wake Mtakatifu. Kwa mageuzo ya mkate na divai hufanya mabadiliko ya uwamo wote wa mkate na divai kuwa ni Mwili na Damu yake Azizi. Kanisa Katoliki kwa haki na usawa limeyaita mabadiliko haya kuwa ni "Mageuzo-uwamo" (transsub-stantiatio). Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu ya upendo ambao kwao aliwapenda waja wake upeo hadi kutoa uzima wake, juu ya Msalaba.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi iwe ni fursa kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu; tayari kutoka kimasomaso kuinjilisha kwa njia utakatifu wa maisha; kwa kujikita katika ari na mwamko wa kimisionari, kwani Ekaristi Takatifu ni mkate wa uzima wa milele hata kwa walimwengu. Wakristo watambulikane katika kuumega mkate, changamoto ya kuadhimisha, kuabudu na kulitafakari Fumbo hili kubwa katika maisha na utume wa Kanisa; kielelezo cha huduma na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi, yalete chachu ya huruma, mapendo, uadilifu na utakatifu wa maisha! Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News dominika hii, Kanisa linaadhimisha sherehe ya Ekaristi Takatifu yaani Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni adhimisho ambalo ndani yake Kanisa linakiri, linatangaza na kuadhimisha uwepo halisi na hai wa Bwana wetu Yesu Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Masomo kwa ufupi: Tukianza moja kwa moja na somo la Injili (Yoh 6:51-58), Yesu anasema Yeye ndiye chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni na kwamba mtu akila chakula hicho ataishi milele. Yesu anazungumza maneno haya kwa watu ambao katika historia yao wanakumbuka kipindi ambacho chakula kweli kilitoka mbinguni kikawalisha babu zao waliokuwa jangwani wakisafiri toka utumwani Misri kwenda katika nchi ya ahadi. Simulizi la chakula hicho walichokiita mana tunalisikia katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Chakula hicho, au mikate hiyo, ililetwa na Mungu mwenyewe kuwashibisha na kuwapa nguvu watu wake waliokuwa safarini. Kitendo hicho ambacho Mungu alikifanya kwa taifa lake teule ni kitendo ambacho tunaweza kukiita kitendo-alama kwa sababu kilikuwa na maana inayovuka tendo hilo lenyewe la kula mkate kutoka mbinguni.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Alama ya kwanza ndiyo hiyo aliyoilezea Musa, kuwafundisha kuwa mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila litokalo katika kinywa cha Mungu. Ni fundisho kwa mwanadamu kumtegemea Mungu na si kutegemea nguvu zake pekee. Wayahudi kupata chakula hicho hawakukifanyia kazi wala hawakulima bali kilishuka kutoka katika wema wa Mungu. Ndilo hilo fundisho la kutegemea maongozi ya Mungu, fundisho kuwa maisha ya mwanadamu na uzima wake vimo mikononi mwa Mungu. Alama ya pili ndiyo hiyo ambayo Yesu ameionesha katika somo la Injili. Yesu anasema “mimi ndio hicho chakula kilichoshuka kutoka mbinguni.” Kwa maneno haya Yesu anaonesha kuwa kitendo cha Mungu kuwapa Waisraeli mana jangwani kilikuwa ni kiashirio cha ule mkate wa uzima ambao atakuja kuutoa kwa njia ya Kristo, mkate ambao utawashibisha walio safarini hapa duniani kuelekea ile nchi ya ahadi ambayo ni mbinguni aliko Mungu mwenyewe. Hapo Yesu anaongeza kusema kuwa ule mkate ambao anautoa yeye, mkate ambao ni mwili wake ni lazima watu waule. Kwa maana anasema “msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna uzima ndani yenu.” Yesu alilitekeleza hilo siku ile ya Alhamisi Kuu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi alipowaambia wanafunzi wake twaeni mle nyote huu ndio mwili wangu, kisha twaeni mnywe wote hii ndiyo damu yangu. Kisha kulikamilisha tendo hilo kwa kifo chake msalabani, mitume wanaendeleza hadi leo kitendo hicho ambacho kwa njia yake mkate na divai hugeuzwa kuwa mwili na damu ya Yesu. Hiki ndicho anachokieleza Mtume Paulo katika somo la pili la dominika hii. Katika waraka wa kwanza anaowaandikia Wakorintho anawahakikishia kuwa kile kikombe cha baraka kinachobarikiwa katika adhimisho la Misa Takatifu, ni damu ya Yesu. Na tena ule mkate unaomegwa katika Misa Takatifu ni mwili wa Yesu. Kwa njia yake, wote wanaoshiriki wanaunganishwa kuwa mwili mmoja katika Kanisa na wanaunganishwa kuwa mwili mmoja na yule wanayempokea, yaani Yesu Kristo mwenyewe.

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Misa, Maandamano na Ibada ya Kuabudu
Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Misa, Maandamano na Ibada ya Kuabudu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza na kuyafafanua masomo ya sherehe ya Ekaristi Takatifu ninawaalika sasa tuingie katika undani wa fumbo hili na kuona tunachota nini cha kutusaidia kama tafakari ya maisha na imani. Binafsi ninaguswa na mambo matatu ambayo ninapenda kuyatafakari pamoja nawe. Jambo la kwanza ni kuwa Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu inatukumbusha na kutuimarisha katika uhakika kuwa Yesu yumo kweli katika Ekaristi Takatifu. Ile hostia na ile divai vinayotolewa wakati wa Misa, baada ya Mageuzo huwa kweli mwili na damu ya Yesu. Uwezo wa kufanya hivyo ni Yesu mwenyewe aliowapa mitume na huo ni uwezo ambao unaendelea kurithishwa kwa kuwekewa mikono katika urika usiokoma wa mitume unaoendelezwa na maaskofu. Katika Kanisa Katoliki, Ekaristi Takatifu siyo tu kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho wala sio tu meza ya Bwana kwa maana ya alama ya nje inayorudia kile alichokifanya Yesu bali Ekaristi Takatifu ni adhimisho la kitu kile kile ambacho Yesu alikifanya, ni yule yule Yesu anayeaidhimisha na Yesu huyo yumo kweli na mzima ndani yake. Ukweli huu utusaidie kuongeza uchaji katika Ekaristi Takatifu, lakini pia utusaidie kukuza imani yetu, matumaini yetu na mapendo yetu kwa Kristo anayetupa zawadi kubwa isiyopimika katika maisha yetu. Padre anayeadhimisha Ekaristi Takatifu anapewa uwezo kupita hata uwezo wa malaika, muumini anayepokea Ekaristi Takatifu anapokea chakula ambacho ni Mungu mwenyewe.

Sherehe ya Ekaristi Takatifu kielelezo cha uwepo wa Kristo Yesu
Sherehe ya Ekaristi Takatifu kielelezo cha uwepo wa Kristo Yesu

Jambo la pili ni kuwa Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu ichochee ndani yetu bidii ya kushiriki Misa Takatifu yaani adhimisho la Ekaristi Takatifu. Kwetu sote waamini tunaalikwa kutokukosa kwa makusudi Misa Takatifu hasa Misa ya dominika na sikukuu zilizoamriwa. Mkristo mkatoliki asione kama ni kitu cha kawaida kutokupokea Ekaristi. Tena mkristo mkatoliki asipuuzie umuhimu wa kupokea Ekaristi na kuona kuwa kupokea au kutokupokea ni sawa tu. Maneno ya Yesu kwamba “asiyekula mwili wangu na kuinywa damu yangu hana uzima ndani yake” si maneno ya kuyachukulia juu juu. Ni agizo. Na ni agizo ambalo linamuwajibisha mkristo kuendelea kuishi ameungana na Bwana wake kwa njia ya Sakramenti. Agizo hili ndilo linalomkumbusha kila mkristo kujitahidi asijitenge na maisha ya Sakramenti na pale anapojikuta amejitenga ajitahidi kwa msaada wa Kanisa kurudi katika maisha ya Sakramenti. Jambo la tatu na la mwisho ni mifano ya watakatifu na wakristo wenzetu ambao wameyajenga maisha yao juu ya msingi wa Ekaristi Takatifu. Wapo katika jumuiya na parokia zetu, wakristo ambao wanatupa mifano ya kuiga wanapotuonesha kwa vitendo umuhimu wa kuyasimika maisha katika msingi wa Ekaristi Takatifu. Ndio wale wanaoshiriki na kupokea Ekaristi Takatifu mara nyingi iwezekanavyo, ndio wale wanaojiandaa kuishiriki na kuipokea kwa toba na sakramenti ya upatananisho, ndio wale wanaoshiriki katika ibada za kuabudu Ekaristi Takatifu n.k. Wapo pia watakatifu wengi wanaoshuhudia kuwa wameufikia utakatifu kwa njia ya uchaji kwa Ekaristi Takatifu. Mojawapo ni mwenyeheri Carlo Acutis, kijana aliyezaliwa mwakaa 1991 na kufariki mwaka 2006 akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka 15. Katika udogo wake, Carlo Acutis aliyasimika maisha yake katika Ekaristi Takatifu na yeye mwenyewe aliita uchaji kwa Ekaristi kuwa ni njia ya moja kwa moja ya kufikia mbinguni. Pamoja na Carlo Acutis wapo wengi ambao leo tunaweza kuwaangalia na kuchochewa na mifano yao ili nasi kukuza uchaji kwa Ekaristi Takatifu. Nakutakia heri na baraka za Mungu kwa sherehe ya Ekaristi Takatifu.

Liturujia Ekaristi Takatifu
09 June 2023, 09:56