Tafuta

Waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. 

Ujumbe wa Pentekoste 2023: Wito wa walei Kwa Kazi za Kitume na Uongozi katika Kanisa

Walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili.

Na Kamati Tendaji ya Halmashauri Walei Taifa, - Dar es Salaam.

Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Dikrii juu ya Utume wa Walei (Apostolicam Actuositatem -AA) inaweka wazi kuwa kila Mwanakanisa, kutokana na Ubatizo wake, anao wajibu na haki ya kutenda Utume wake kadiri ya hali yake ya maisha (AA, 16). Na kwa msisitizo inasema kwamba “Utume wa Walei hauwezi kutoweka kamwe katika Kanisa” (AA 1). Barua ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo wa II juu ya Wito na Utume wa Walei inataja wazi kuwa “Walei siyo tu wamo ndani ya Kanisa bali vile vile wao ni Kanisa” (Christifidelis Laici-CL 9); Waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili. Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Mtume Paulo katika kueneza Injili (rej. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (rej. 1Kor 16:17-18).

Waamini walei tusimame imara kuilinda, kuitangaza na kushuhudia imani yetu
Waamini walei tusimame imara kuilinda, kuitangaza na kushuhudia imani yetu

Nyakati zetu zinadai bidii isiyopungua kutoka kwa Walei; mazingira ya siku hizi yanadai utume uwe umekua kweli katika nguvu na upana kulingana na ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kisayansi na ya kiteknolojia. Wakristo katika hali ya aina yoyote ya maisha wanaalikwa kuishi kikamilifu maisha ya Kikristo na ukamilifu wa upendo. Waamini wote wanapaswa na wanaalikwa kuwa watakatifu kwamba mawazo, matakwa na upendo wa mtu yote yaelekezwe kwa Bwana. Walei tuna fursa nyingi sana za kutimiza utume wa uinjilishaji na wa utakatifuzaji kwa kuwa tumezungukwa na malimwengu. Matendo mema na yanayotimizwa kwa roho ya Kimungu yana nguvu ya kuwavutia watu katika imani na kwa Mungu kama anavyosema Bwana “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mt 5:16). Walei tupende na kutamani kujitoa kwa bidii na kwa uwezo wa kila mmoja kadri alivyokirimiwa na Mungu tukianzia katika familia zetu, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Vigango, Parokia, Majimbo na Taifa. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unatuagiza walei tuzoee kufanya kazi bega kwa bega na Mapadre wetu. Waamini Walei yatupasa kujenga Mwili wa Kristo kutumia karama tulizopewa; tukisaidiana na wengine, kwa muda wetu na mali zetu. (rej. AA 10). Kwa kadri tunavyoshiriki katika mambo hayo, tuyafanye tukioongozwa na roho ya Injili ili kutumika vema katika kueneza Ufalme wa Mungu tukiinjilisha na kutakatifuza, huku tukikuza na kukamilisha mpango wa malimwengu kwa roho ya Injili. Mpango huo walei wamepewa na Mungu mwenyewe kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara. Kwa Ubatizo Mlei anakuwa mwana wa Mungu na mfuasi wa Kristo, kwa Kipaimara Mlei anaimarishwa kuwa askari hodari wa Kristo aweze kumtangaza Mungu na Yesu Kristo yaani, wanawekwa na kufanywa watendaji katika Taifa la Mungu wakimshuhudia Kristo mahali pote wakifanya Utume wa Kanisa uletao wokovu (rej. AA1, 2, 3).

Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa
Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa

Wapendwa waamini, nyakati hizi tunaposhuhudia changamoto nyingi za kiimani zinazozikumba jamii yetu, tunawasihi na kuwahimiza sana kuliko wakati wote kwamba, tuilinde imani yetu. Tunashuhudia wimbi la baadhi ya waamini Wakatoliki wakigeuka na kujiunga na madhehebu mengine yanayochipuka kana kwamba hawakuwa na misingi imara ya imani yao: Imani juu ya Mungu aliyeumba mbingu na dunia, anayekomboa kwa njia ya Mwana wake Yesu Kristo, juu ya Roho Mtakatifu na juu ya Kanisa moja Takatifu, Katoliki la Mitume, kama tulivyofundishwa katika mafundisho ya Komunyo ya kwanza na Kipaimara na kila siku kukiri kwenye Sala ya Kanuni ya Imani. Inasikitisha kuona ufahamu wa wakristo wakatoliki kuhusu imani yao unakosa dira na mwelekeo hata kufikia kupokea udanganyifu wa wahubiri wa madhehebu yanayoibuka na kuota kama uyoga. Yatupasa tuongeze uelewa wa imani ya Kikristo ya Kikatoliki, ipenye katika mawazo na moyo. Ili kukoleza imani yetu hatuna budi kuweka bidii katika sala, kusoma na kulitafakari neno la Mungu na kushiriki maisha ya Sakramenti za Kanisa, hususani Ekaristi Takatifu na Kitubio. Haya yote hayana budi kuonekana katika matendo yetu mema ya kila siku kwani Mt. Yakobo anasema “Imani bila matendo imekufa” (Yak 2:26).

Maaskofu Katoliki Tanzania na baadhi ya watawa, Kanisa kuu la Mt. Petro
Maaskofu Katoliki Tanzania na baadhi ya watawa, Kanisa kuu la Mt. Petro

Tunapoadhimisha Sherehe ya Pentekoste hatuna budi kumwomba Roho Mtakatifu atujaze na atugawie Mapaji yake Saba ili tujitoe kwa mwili na roho kwa kazi za kitume, tuweze kumtukuza Mungu, tukitambua kwamba sisi ni viungo wa Mwili wa Kristo. (rej. 1Kor 12:12-27). Roho Mtakatifu aifanye miguu yetu iwe mepesi kwa ajili ya kazi za kitume kwani “Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio Habari Njema” (Rum 10:15). Aidha, tunaalikwa kufumbua macho yetu ili tutazame maajabu ya Mungu. Mzaburi anasali akisema “Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako” (Zab 119:18). Kama waamini wa Kikatoliki tunaalikwa kutimiza wajibu wetu wa kikuhani na kinabii kwa kufungua vinywa vyetu ili kufundisha, kuonya na kukaripia pale ambapo imani na maadili katoliki yanatetereka. Mt. Paulo anatukumbusha sote kwa kusema “Lihubiri neno, uwe tayari, wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho” (2 Tim 4:2). Wapendwa waamini, kwa nyakati zetu hizi tunapopitia changamoto mbalimbali za kiimani na kimaadili zitokanazo na maendeleo ya sayansi na teknolojia na athari zake nyingi za utandawazi, tunaalikwa kumwomba Roho Mtakatifu atusaidie kujenga familia zetu kuwa shule za sala; mahali pa kusoma na kulitafakari neno la Mungu; mahali pa mafunzo bora ya maadili; sehemu imara pa kukiri na kuiishi imani Katoliki. Tumwombe Roho Mtakatifu atujalie mapaji yake saba ili tuache ulegevu wa imani na tumshuhudie Kristo aliyetuagiza kwa kusema “Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:8). Nuru yetu Iangaze……………… Ili Tutakatifuze Malimwengu. Tumsifu Yesu Kristo.

Ujumbe wa Pentekoste

 

 

 

27 May 2023, 08:41