Tafuta

Picha inaonesha Maaskofu wa Tanzania wakati wa misa Takatifu katika Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Picha inaonesha Maaskofu wa Tanzania wakati wa misa Takatifu katika Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 

Tanzania,Pd.Tindyebwa:Toa hofu kwa kuwa mmepokea mapaji 7 ya Roho Mtakatifu!

Mkristo Mkatoliki aliyepokea mapaji 7 ya Roho Mtakatifu, tayari amempokea Kristo Yesu na anatakiwa kushiriki ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo kama mfuasi wake. Kwa kupitia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, Roho Mtakatifu anashuka kwa Kanisa zima. Amesema hayo Padre Tindyebwa aliyetoa Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George,Jimbo Katoliki la Kayanga,Tanzania.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunasoma  historia ya ujio wa Roho Mtakatifu kuwa Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizo. Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu.  Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.

Kushangaa na kutoelewa nini maana yake

Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya. Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia,  Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi,  Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu. Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?”  Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi.

Petro alizungumza na Watu

Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini.  Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika: “Mungu anasema: Katika siku za mwisho, nitaimimina Roho yangu kwa watu wote. Wana wenu na binti zenu watatabiri. Vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Katika siku hizo nitaimimina Roho yangu kwa watumishi wangu, wanaume na wanawake, nao watatabiri. Nitafanya maajabu juu angani. Nitasababisha ishara chini duniani. Kutakuwa damu, moto na moshi mzito. Jua litakuwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja. Na kila amwombaye Bwana ataokolewa.”

Padre Tindyebwa:Pentekoste ni ishara ya umoja na ushirika

Ni katika muktadha huu ambapo Katibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, Padre Castor Tindyebwa, aliwaambia vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kuwa wasiwe na hofu kwa maana wamejaliwa kumtangaza Kristo, kupitia mapaji 7 ya roho Mtakatifu waliyopokea. Alisema hayo wakati akitoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 74 wa Parokia ya Mtakatifu George, ambalo ni Kanisa Kuu, la Jimbo Katoliki Kayanga, Tanzania katika Madhimisho la Misa Takatifu Sherehe ya Pentekoste, Dominika tarehe 28 Mei 2023. Padre Castor akizungumzia juu ya Sherehe ya ujio wa Roho Mtakatifu (Pentekoste) baada ya siku 50 tangu kufufuka kwa Bwana, alisema kuwa ni sherehe ya waamini inayowaalika kumpokea roho Mtakatifu na kwenda kutangaza habari njema. Sherehe ya Pentekoste ni ishara ya umoja, ushirika na kuzaliwa kwa Kanisa ambapo Kanisa linakumbuka kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya watu.

Mkristo aliyepokea mapaji 7 ya Roho Mtakatifu amepokea Kristo

Padre Castor, katika mahubiri akiendelea alisema kuwa Mkristo Mkatoliki aliyepokea mapaji Saba ya Roho Mtakatifu, tayari amempokea Kristo, hivyo anatakiwa kushiriki ukuhani wa Kristo kama mfuasi wake. Kwa kupitia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, Roho Mtakatifu anashuka kwa Kanisa zima na anawajaza waamini ili kuwa na karama zinazowasaidia katika kutenda. Padre Castor aidha aliwataka waamini kuacha tabia kuungama kwa sababu ya mazoea ya kudhani kuwa wao ni wema, bali waungame huku wakitambua kuwa wanaye roho Mtakatifu. Kwa maana hiyo alisisitiza kwamba, waamini Wakatoliki wajitahidi kupokea Sakramenti ya Kitubio,na wawe tayari kutangaza habari njema.

 

29 May 2023, 15:11