Tafakari Dominika ya Tano ya Kipindi cha Pasaka: Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kuwa Yesu ni njia Ukweli na Uzima. Wimbo wa mwanzo ni mwaliko wa kumwimbia Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya (Zab 98:1-2). Maajabu hayo ni ukombozi na kujaliwa uzima wa kweli kwa njia ya Yesu kama sala ya mwanzo inavyoashiria ikisema; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 6:1-7). Somo hili linatukumbusha jinsi shida zilivyoanza kujitokeza kwa mara ya kwanza kati ya wakristo wa kwanza na jinsi walivyozitatua kwa kwa kuwapa madaraka mashemasi wa kwanza saba waliowachagua kushughulika na watu fukara ili mitume waendelee kuhubiri na kusali. Nasi tukitaka kutimiza wajibu wetu vizuri, ni lazima tushirikiane katika kazi mbalimbali za kanisa kuliko kuwaachia watu wachache au kujilimbikizia mamlaka na majukumu kana kwamba hakuna wengine wanaoweza kufanya au kwamba mmoja ndiye muweza wa yote.
Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 2:4-9). Katika somo hili Petro aliyepewa jina la mwamba yaani jiwe na Yesu naye anamfananisha Yesu na jiwe lililo hai lililokataliwa na waashi yaani Wayahudi hata kumtoa asulubiwe na kuuwawa kifo cha msalabani. Wakristo ambao ni taifa jipya la Mungu, wanashiriki uhai wa Kristo ambao wanazirithi fadhili za taifa la Mungu katika Agano la Kale. Na wale wanaokataa kumsadiki wataangamizwa na jiwe hilo yaani Bwana wetu Yesu Kristo katika hukumu ya mwisho (Mt. 28: 31-46). Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yoh.14:1-12). Injili hii ni sehemu ya hotuba aliyoitoa Yesu siku ile ya karamu ya mwisho. Katika sehemu hii ya Injili Yesu anawaimarisha mitume katika imani kwani walifadhaishwa na utabiri wa usaliti wa Yuda, mkano wa Petro na kuaga kwake Yesu. Sisi twaimarishwa pia tukijua kuwa Yesu ni njia yetu sababu ametufunulia njia ya kumfikia Baba; Yesu ni Ukweli sababu anatufundisha kuishi dini ya kweli; Yesu ni Uzima wetu sababu anatugawia uzima wa Baba. Ni maelekeo ya kibinadamu kutafuta na kutamani kuishi vizuri katika nukta ya sasa na hata katika maisha ya baadaye. Kutokana na maelekeo haya tunahangaika kutafuta ni namna gani tutaweza kuyapata maisha mazuri na ya furaha, sasa na hata baadaye. Ndipo tunapofikia kuogopa mateso na kuona kama ni dalili ya wazi ya maisha mabaya ya sasa na ya baadaye, kinyume na maelekeo yetu ya kutamani maisha mazuri. Na hivi tunajaribu kutafuta njia mbalimbali ambazo zinatupa tumaini la maisha mazuri na ya furaha. Yesu akijua mahangaiko na maelekeo hayo, anasema “Mimi ndimi njia, ukweli na Uzima."
Mungu alimtoa mwanaye wa pekee kuja ulimwenguni ili awe kielelezo cha maisha yetu hapa duniani na mwisho kuupata ufufuko na kufurahi naye huko Mbinguni. Sisi tulio wafuasi wa Kristo tunapopambana na ugumu tunakuwa na wasiwasi ya kupata furaha ya kweli tunayoiendea. Yesu kama kielelezo cha maisha yetu anatupa nguvu na kututia moyo kwamba tusitishwe na magumu tunayopambana nayo, magumu na mateso ni sehemu ya njia hii ya kumfuata yeye. Tukijikabidhi kwake yeye aliye kielelezo cha maisha yetu hapa duniani na kuwa tayari kutumikiana tutamwona Mungu katika nafsi tatu kati yetu. Na hivyo woga na mashaka havitatutawala tena katika maisha yetu kwani tutakuwa tunaishi katika yeye aliye njia, ukweli na uzima. Baada ya Yesu kuwapa wanafunzi wake fundisho kuu katika karamu ya mwisho la kutumikiana kwa upendo na kuwaambia yatakayompata yaani mmoja wao atamsaliti, habari ya kuondoka kwake na utabiri wake kuwa Petro atamkana, wanafunzi wake wanajawa na wasiwasi na kujiuliza maswali mengi. Ili kuwaondoa wasiwasi na kuwaimariaha katika imani Yesu anawaambia wasifadhaike kwasababu wanamwamini Mungu lakini pia kwasababu nyumbani mwa Baba mna nafasi kubwa ya kumuishi yeye kwa njia ya kutumikiana na kuhudumiana kwa upendo. Tomaso anapata mashaka juu ya njia ya kufika huko aendako Bwana, akisema kama hawajui aendako watajuaje njia. Ndipo Yesu anasema; “mimi ndimi njia, ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”. Hii ndiyo habari njema na ya furaha inayotupa amani na utulivu katika mioyo yetu na pia inatupa nguvu na ujasiri wa kuendelea kukabiliana na changamoto na magumu katika kumfuata Kristo aliye njia, ukweli na uzima.
Ukweli wa Mungu umefunuliwa kwetu sisi wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo na kilele cha ufunuo huo ni fumbo kuu la imani yetu yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alikuja ili kutuonesha njia ya kwenda kwa Mungu. Njia hiyo ni yeye mwenyewe kwa maisha yake na maagizo yote aliyotoa kwetu tuyatekeleze. Tusitafute njia ya mkato katika kwenda kwa Mungu kama Filipo alivyoomba; “Bwana tuonyeshe Baba nasi yatutosha”. Yesu mwenyewe ametuhakikishia yeye yumo ndani ya Baba na Baba ndani yake. Binadamu tumekuwa katika mahangaiko ya kutafuta njia sahihi ya kumjua na kumfikia Mungu. Mahangaiko haya yanatupelekea kukosa msimamo katika mwenendo wetu wa maisha ya imani. Yesu anatufumbua kuwa kuishi kama yeye alivyoishi na kadiri ya maagizo yake ndio njia sahihi na ya ukweli kuelekea uzima wa milele. Mitume walipata shida namna ya kuyaelewa mafundisho haya kwani fumbo kuu la kifo na ufufuko wake lilikuwa halijatimia. Sisi hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi ilimradi tunaishi kulingana na mapenzi na maagizo yake. Tiketi ya kumfikia Mungu na kumwona kama alivyo tumepewa na Yesu Kristo. Kila moja anayo nafasi ya kumuishi Yesu katika maisha yake na katika mazingira yake kwa kutumikiana na kuhudumiana kwa upendo.
Tukumbuke kuwa magumu, matatizo, shida na mateso ni sehemu ya maisha yetu ya kikristo kwani yeye aliye njia, ukweli na uzima alipambana nayo hata akakubali kufa msalabani ili mapenzi ya Baba yatimie. Lakini tusiyasababishe wala kuyatafuta hapo tutakuwa kinyume na mapenzi yake. Tusiwe na mashaka wala wasiwasi tunapopata magumu au mateso hayo na kuona kana kwamba tumepotea njia bali tujitahidi kuyaweka yote katika Kristo na kujiaminisha kwake Yeye aliye Njia, Ukweli na Uzima. Binadamu ana hamu ya kuishi mda mrefu. Matamanio haya ya kuishi muda mrefu yana mizizi ndani mwetu na chanzo chake ni Mungu mwenyewe. Sisi tunapenda kuishi maisha marefu lakini Mungu anapenda tuishi milele. Mungu alipomwumba Adamu alimpulizia pumzi ya uhai, Adamu akawa nafsi hai. Mungu aliweka ndani ya Adamu sehemu ya uhai wake, Adamu akawa na uhai wa milele. Lakini Adamu alipoteza uzima huu wa milele kwa dhambi. Mungu hakumwacha mwanadamu katika hali ya dhambi, aliahidi kumkomboa. Mungu alitekeleza ahadi hiyo alipomtuma mwanae Yesu Kristo ulimwenguni aje kutukomboa na akaturudishia uhai wa milele. Yesu alikamilisha kazi hiyo kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Baada ya ufufuko wake, kabla ya kupaa mbinguni Yesu aliwatokea wafuasi wake akiwaimarisha katika imani juu ya maisha ya milele. Sala ya kuombea dhabihu inaweka msisitizo; “Ee Mungu, umetushirikisha umungu wako mkuu katika kuishiriki sadaka hii takatifu. Tunakuomba utujalie tuufuate kwa mwenendo mwema ule ukweli wako kama tunavyoujua”. Na baada ya Komunyo Padre anahitimisha sala kwa sala akisema; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utufikishe kwenye uzima, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya”. Hili ndilo tumaini letu tunalolisherehekea katika kipindi hiki cha ufufuko wa Bwana. Tumsifu Yesu Kristo.