Tafuta

Injili linatueleza juu ya fundisho la kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambayo kwayo tunasamehewa dhambi. Injili linatueleza juu ya fundisho la kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambayo kwayo tunasamehewa dhambi. 

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu Anawashukia Mitume: Mwanzo wa Kanisa

Injili linatueleza juu ya fundisho la kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambayo kwayo tunasamehewa dhambi ambayo kimsingi ni kazi ya Roho Mtakatifu: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Kupitia Injili tunafunuliwa kuwa Roho Mtakatifu (Nafsi ya Tatu ya Mungu) ni Roho anayefanya kazi ya kutupatanisha na Mungu na kuturudishia uzima wa kiroho.

Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia.

Sherehe ya Pentekoste ndiyo inahitimisha Kipindi cha Pasaka. Sherehe ya Pentekoste kwa asili ilikuwa Sherehe ya Kiyahudi ambayo walisherehekea kufikia ukomo wa mavuno ya nafaka. Kwa asili ilikuwa ni sherehe ya mavuno. Licha ya kuitwa Sikukuu ya Mavuno (Kut. 23:16), pia iliitwa Sikukuu ya Mavuno ya Ngano (Kut. 34:22), na iliitwa pia Sikukuu ya Majuma (Hes. 28:26) kwa sababu ilikuwa inasherehekewa Majuma saba (7) baada ya kuanza mavuno ya shayiri. Kwa asili ilikuwa ni sherehe iliyohusiana na kilimo. Wakati wa Sikukuu ya Pentekoste Wayahudi walipaswa kumtolea Mungu mikate miwili iliyotengenezwa kutokana na ngano inayotokana na mavuno mapya ya mwaka huo. Kitendo cha kutumia ngano mpya kiliashiria kuwa Wayahudi wanaanza maisha upya. Baadaye Sherehe hii ilipata maana mpya miongoni mwa Wayahudi. Badala ya kubaki kama sikukuu ya mavuno, Wayahudi waliitumia Pentekoste kama Sherehe ya kukumbuka tukio la kupewa amri kumi mlimani Sinai kupitia mwakilishi wao Musa. Sherehe hii ya Pentekoste ilikuwa ni tukio la shangwe kubwa. Kwetu Wakristo Pentekoste ya Kiyahudi imepata maana mpya: Sherehe ya Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume- hii ndiyo Pentekoste tunayoiadhimisha leo.

Sherehe ya Pentekoste Mwanzo wa Kanisa
Sherehe ya Pentekoste Mwanzo wa Kanisa

SOMO LA KWANZA (Mdo. 2:1-11): Tukio la Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume linatukia wakati Wayahudi wanasherehekea Sikukuu ya mavuno ambayo pia ni sikukuu ya “kukumbuka tukio la Musa kupewa amri kumi na Mungu pale mlimani Sinai” wakiwa safarini kutoka utumwani Misri. Hivyo, kwao ni sikukuu ya kurudia agano lao na Mungu. Pentekoste ilikuwa ni siku ya furaha na nderemo. Katika siku hii ya furaha na nderemo, mitume wanashukiwa na Roho Mtakatifu ambaye anaelezwa kama: (i) uvumi wa upepo wa nguvu: upepo kwenye Maandiko Matakatifu unaashiria uwepo wa Mungu (rejea 2 Sam. 5:24 na 1Flm 19:11). Hivyo, Roho Mtakatifu ni Mungu Mwenyewe na (ii) ndimi za moto zilizogawanyika. Hapa Roho Mtakatifu anashuka katika mwonekano wa “ndimi za moto.” Kazi ya “moto” ni kutakasa vitu (kama vile dhahabu), kupasha moto/kuleta joto na pia kuleta mwanga (watu huwasha moto ili kupata mwanga). Hivyo Roho Mtakatifu anawashukia wafuasi ili kuwatakasa, kuwapasha moto kutokana na kuwa baridi kwa kuwahofia Wayahudi na pia kuitia nuru mioyo yao na imani yao ili wazidi kumtambua Mungu na kuishuhudia imani ya Kristo. Kwa nini ndimi zimegawanyika? Roho Mtakatifu ana “mapaji mengi yanayogawanywa” kwa kila mtu bila upendeleo. Matokeo ya kushukiwa na Roho Mtakatifu ni kusema kwa lugha mbalimbali.

Tunatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Tunatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Kusema kwa lugha za watu wa makabila na mataifa mbalimbali kunaashiria kuwa Roho Mtakatifu anawapa wafuasi uwezo wa “kuwahubiria watu wa makabila na mataifa yote.” Hapa agizo la Yesu la kuwataka mitume wake “wawafanye mataifa yote kuwa wanafuzi wake” linaanza kutimia (Mt. 28:19). Kuna jambo kubwa la kulibaini baada ya wafuasi kuanza kunena kwa lugha mbalimbali: watu waliowasikia wafuasi wakinena walielewa kilichokuwa kinazungumzwa na wafuasi. Tendo hili linaashiria kuwa kazi ya Roho Mtakatifu ni kuleta umoja na maelewano, na wala siyo kuleta utengano. Wale wanaomwamini Mungu na kuongozwa na Roho Mtakatifu huwa na umoja na maelewano. Wale wanaotegemea nguvu zao wenyewe, utajiri wao wenyewe na kutaka kuonesha majivuno na kiburi chao ni watu ambao hawana Roho Mtakatifu. Hao Mungu huwatawanya kama alivyowatawanya wajenzi wa mnara wa Babeli kwa kuwafanya washindwe kusikilizana (rejea Mwanz. 11:1-9). Sisi sote tumempokea Roho Mtakatifu wakati wa ubatizo na kupokea mapaji yake saba (7) katika Kipaimara. Je, baada ya kumpokea tumebaki wamoja? Je, tuna maelewano kati yetu? Tunapokuwa na migogoro tunamuomba aingilie kati? Je, tunatambua kwamba Yeye ndiye mgawaji wa mapaji au tunafikiri yametoka kwetu wenyewe? Je, katika maisha yetu Roho Mtakatifu ana nafasi? Je, Roho Mtakatifu ana nafasi kazi maisha yetu ya sala?

Pentekoste ni siku ya waamini walei
Pentekoste ni siku ya waamini walei

SOMO LA PILI (1 Kor. 12:3b-7, 12-13): Moja kati ya changamoto zilizowakabili Wakristo wa Korintho ilikuwa ni “mpasuko/mgawanyiko” miongoni mwao. Wapo Wakristo katika jamii ya Wakorintho ambao walijiona kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine kutokana na vipaji na karama zao, uwezo wao wa elimu, utajiri wao, ukaribu wao na mitume na hata kujihisi kuwa wao ni wacha-Mungu zaidi kuliko wengine. Hivyo, mtume Paulo anawakumbusha kuwa yote waliyonayo yametoka kwa Mungu- Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Karama walizonazo, kazi wanazozitenda na huduma wanazofanya hazitokani na uwezo wao, akili zao au utajiri wao bali ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mtume Paulo anawakumbusha kuwa wanapaswa kutumia karama walizopewa na Mungu kwa “kufaidiana” (yaani kwa faida ya wote) wala siyo kwa ajili ya maslahi binafsi. Karama tulizonazo, huduma tuzifanyazo na kazi tuzitendazo zafaa kutuletea umoja kama ambavyo viungo ni vingi lakini vyote ni vya mwili mmoja. Mungu mmoja katika Nafsi Tatu ametupatia karama na upendeleo mkubwa – uwezo wa kiakili, hekima, uwezo wa kujenga hoja, nguvu za mwili, afya njema, busara, karama ya uongozi, nguvu ya ushawishi, karama ya uhamasishaji, karama ya uandishi, karama ya kuhubiri na mengineyo. Je, hivi vyote tunavitumia kwa manufaa/faida ya wote? Kwa bahati mbaya wengi wetu tunavitumia kujinufaisha na kujikweza wenyewe. Katika ulimwengu wa sasa watu wengi wanatumia karama na kazi zao kutafuta maslahi binafsi. Baadhi ya waandishi wanatumia karama yao ya uandishi kutafuta maslahi binafsi kwa kuandika habari za uongo na za kudhalilisha wengine na hata kuandika habari za kuvuruga amani. Wengine wameacha kusali kwenye Jumuiya ati yeye ana akili sana na hivyo hawezi kuongozwa na viongozi ambao hawana elimu. Wengine wana kipaji cha uongozi lakini hawataki kuongoza ati kwa kuwa hawafaidiki na chochote. Wengine wana karama ya kuwa na nguvu ya ushawishi lakini wanaitumia vibaya kwa kuwashawishi wengine kuwapinga viongozi halali katika ngazi za kiserikali na kikanisa. Wengine wamepata madaraka wakajisahau na kufikiri kuwa wao wana akili na mawazo mazuri kuliko wengine na hivyo kujifanyia yale wanayotaka wao. Wengine tumetumia utajiri wetu kuwanyanyasa wanyonge. Wengine tumetumia karama zetu za kuhubiri kujitafutia fedha na umaarufu hadi kufikia hatua ya kupotosha Neno la Mungu. Wote tutumie karama, huduma na kazi zetu kwa faida ya watu wote tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Matokeo ya kweli ya karama/vipawa zetu ni kuwanufaisha wengi.

Karama za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa
Karama za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa

SOMO LA INJILI (Yn. 20:19-23): Somo la Injili linatueleza juu ya fundisho la kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho ambayo kwayo tunasamehewa dhambi. Hata hivyo, tunafunuliwa kuwa kuondolewa dhambi na kupatanishwa na Mungu ni kazi ya Roho Mtakatifu: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Kupitia Injili tunafunuliwa kuwa Roho Mtakatifu (Nafsi ya Tatu ya Mungu) ni Roho anayefanya kazi ya kutupatanisha na Mungu na kuturudishia uzima wa kiroho tunapotengana na Mungu kwa njia ya dhambi. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu ambao “wanamkufuru Roho Mtakatifu” kwa kukataa kwa makusudi kuijongea Sakramenti ya Kitubio ambayo kwayo Roho Mtakatifu huondoa dhambi zetu. Watu wa namna hiyo dhambi zao “zitafungiwa” (yaani dhambi zao hazitaondolewa). Lakini dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi? Ni dhambi ya kuendelea kung’ang’ania dhambi (sin of obduracy) - yaani mtu hayuko tayari kwa makusudi kabisa kutubu dhambi zake. Basi kila mmoja anaalikwa kuitumia Sakramenti ya Kitubio. Tusitafute visingizio: Padre ni kijana sana siwezi kuungama kwake; Padre huyu ni rafiki yangu sitaki ajue dhambi zangu; sina muda wa kuungama; nikiungama dhambi hii nitaitenda tena, basi bora nisiungame; nina dhambi nyingi siwezi kusamehewa; nimetenda dhambi kubwa sana, Mungu hawezi kunisamehe. Mungu haitaji visingizio bali anahitaji moyo uliopondeka, ulio tayari kuomba toba. Tukimpokea Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Kitubio tutapata amani ya kweli ambayo leo Kristo anawapatia mitume wake: “Amani iwe kwenu.”

Amani kwenu!
Amani kwenu!

Kwa sherehe ya Pentekoste Kanisa linakumbuka kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini, Mwanzo wa Kanisa na mwanzo wa utume wake kwa watu wa lugha na mataifa yote. Kwa kuwa sisi sote ni Mitume, hebu tuone baadhi tu ya kazi za Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Maandiko Matakatifu, Nyimbo na sala mbalimbali kwa Roho Mtakatifu zinadokeza baadhi ya kazi za Roho Mtakatifu: Roho Mtakatifu ndiye anayetakatifuza vitu vyote; Roho Mtakatifu ndiye anayetutia nguvu sisi tuweze kuishuhudia imani yetu kwa uthabiti; Roho Mtakatifu ndiye anayetusaidia katika udhaifu wetu na kutusaidia kuomba/kusali vizuri maana hatujui kuomba ipasavyo (rejea Rum. 8:26); Roho Mtakatifu ni Mfariji wetu tuwapo katika mahangaiko ya maisha ya hapa duniani; Roho Mtakatifu ndiye anayetupatia vipaji na karama mbalimbali; Roho Mtakatifu ndiye anayelainisha mioyo mikaidi ili iache kukumbatia dhambi; Roho Mtakatifu ni Msaidizi/Mtetezi wetu; Roho Mtakatifu ndiye anayetia mioyo yetu nuru ili iweze kutambua yaliyo mema; Roho Mtakatifu ndiye anayetuponya majeraha yetu ya kiroho, n.k. Tumuombe Mungu Roho Mtakatifu atujalie kumjua na kumpenda ili tupate neema zake na kudumu katika imani. Sherehe njema ya Pentekoste.

 

 

27 May 2023, 15:04