Tafuta

Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu kuwashukia kwa pamoja Mitume na wafuasi wa Kristo. Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu kuwashukia kwa pamoja Mitume na wafuasi wa Kristo.   (Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste: Kumtangaza na Kumshuhudia Kristo Mfufuka

Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu anawashukia kama ndimi za moto anawaimarisha kwa mapaji yake nao wanaondokana na hofu yao wanatoka nje na kuanza kumshuhudia Kristo Mfufuka na kuhubiri Injili. Ni kwa sababu hii Pentekoste huitwa pia siku ambapo Kanisa lililazaliwa. Hii ilikuwa ni siku ambapo kwa mara ya kwanza Mitume walianza kumhubiri Kristo. Changamoto na mwaliko kwa waamini walei kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mfufuka!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Dominika hii, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu kuwashukia kwa pamoja Mitume na wafuasi wa Kristo. Baada ya kifo cha Yesu mitume na wafuasi waliingiwa hofu, walihofia wao pia kukamatwa na kusulubiwa kama alivyofanywa Yesu. Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu anawashukia kama ndimi za moto anawaimarisha kwa mapaji yake nao wanaondokana na hofu yao wanatoka nje na kuanza kumshuhudia Kristo Mfufuka na kuhubiri Injili. Ni kwa sababu hii Pentekoste huitwa pia siku ambapo Kanisa lililazaliwa. Hii ilikuwa ni siku ambapo kwa mara ya kwanza Mitume walianza kumhubiri Kristo. Katika Kanisa letu la Tanzania, Pentekoste ni Sherehe pia ya Halmashauri ya Walei. Ni sherehe inayolenga kuamsha katika kundi hili kubwa la familia ya Mungu ari ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika mazingira ya kila siku. Waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili. Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Mtume Paulo katika kueneza Injili (rej. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (rej. 1Kor 16:17-18).

Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa
Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa

Masomo kwa Ufupi: Somo la kwanza (Mdo. 2:1-11) kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume ndilo linalotoa kama simulizi, alivyoshuka Roho Mtakatifu. Somo linaanza kwa kusema “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.” Ni vizuri kujikumbusha kuwa wayahudi walikuwa na sikukuu yao ambayo pia iliitwa Pentekoste. Kwao, Pentekoste ilikuwa ni sherrehe ya shukrani ya mavuno. Iliitwa Pentekoste kwa sababu ilisherehekewa siku 50 baada ya Pasaka yao. Tunaelewa kuwa Pasaka ya wayahudi haikuwa sherehe ya ufufuko wa Kristo, Pasaka ya wayahudi ilikuwa ni sherehe ya kukumbuka namna Mungu alivyowakomboa kutoka utumwa wa Misri. Pentekoste hiyo ya wayahudi ilikuwa pia ni sherehe ya Hija, kwa maana kwamba Wayahudi wote waliofikia umri wa kuhiji walipaswa kwenda Yerusalem kuhiji. Na hii ndiyo maana siku hiyo walikuwapo watu wengi Yerusalemu. Katika siku hiyo, Roho Mtakatifu akashuka kama ndimi za moto na akawajaza mapaji yake wote waliokuwa wamekusanyika katika nyumba hiyo nao wakaanza kunena kwa lugha na wakaanza kuyatangaza matendo makuu ya Mungu bila hofu. Somo la pili (Kor 12:3b-7, 12-13) linafafanua kuwa Roho Mtakatifu ndio kiini cha utendaji wa Kanisa na ndio chemchemi ya karama, huduma na utume wote wa Kanisa. Pamoja na fundisho hilo, Paulo haachi kusisitiza kuwa karama mbalimbali ambazo Roho anawajalia waamini ni kwa ajili ya Kanisa na hasa zaidi kwa ajli ya kuujenga umoja wa Kanisa. Huu si umoja kama ule mwanadamu alioutafuta wakati wa mnara wa Babeli ili ajiimarishe yeye kinyume na mapenzi ya Mungu. Umoja huu wa Kanisa ni umoja unaolitambulisha Kanisa kama mwili wa Kristo ambao una viungo vingi na kila kiungo kinafanya kazi kwa ajili ya faida ya mwili mzima.

Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Somo hili linatualika kuzipokea karama mbalimbali ambazo Roho amezimwaga katika Kanisa na kuwa tayari kuzitumia kwa ajili ya Kanisa. Hii ni pamoja na kutambua karama mbalimbali walizonazo wenzetu na kuzipa nafasi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Katika Injili, kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 20:19-23), Kristo mfufuka anawatokea mitume wake na kuwavuvia Roho Mtakatifu. Mitume wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi Yesu anawatokea,  anawatoa hofu na hapo hapo anawapa Roho Mtakatifu ambaye alikuwa amewaahidia. Injili inaonesha wazi kuwa waliopokea Roho Mtakatifu katika siku hii ni mitume peke yao. Na Roho huyu waliyempokea ni Roho anayewapa nguvu na mamlaka ya kutenda yale ambayo Kristo mwenyewe aliyatenda. Kristo aliponya roho za watu kwa kuwaondolea dhambi. Uwezo huu, sasa anawapa pia mitume anapowaambia “wowote mtakaowaondolewa dhambi wataondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi watakuwa wamefungiwa”. Maneno haya huashiria nguvu ya kisakramenti ambayo Mitume wanapewa katika kuondolea dhambi. Kumbe, kwa njia ya Roho Mtakatifu nguvu na uwepo ule ule wa Kristo unaendelea kuwa hai katika Kanisa kwa njia ya Sakramenti ambazo Mitume wanaziadhimisha kwa jina lake.

Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Sherehe ya Pentekoste ambayo ni adhimisho la kushuka kwa Roho Mtakatifu, linafunua kwetu jambo muhimu sana kuhusu huyu Mungu tunayemwabudu. Jambo hili ni kuwa yeye ni Mungu anayeshuka daima kuwafikia watu wake na ni yeye anayewatafuta. Na hii ni mojawapo ya sifa kuu inayomtofautisha Mungu na miungu wengine. Taifa takatifu lilipoingia katika nchi ya ahadi liliwakuta wakazi wake wanaabudu miungu. Pamoja na amri ambayo Mungu alikuwa amewapa, amri ya kutokuabudu miungu hiyo, Mungu mwenyewe aliamua kujitofautisha na miungu hiyo ili awaoneshe kuwa ndiye Mungu wa kweli. Naye aliwakumbusha daima kwa vinywa vya manabii kuwa ndiye atakayewatafuta kondoo wake, ndiye atakayewachunga kondoo hao na ndiye atakayewapeleka katika malisho bora. Taifa takatifu la Mungu, pamoja na uasi wa hapa na pale kwa Mungu, waliitambua tofauti hii. Katika sala na tafakari zao kama tunavyosoma katika Zaburi, walikiri kuwa Mungu wao si kama miungu ya kigeni. Miungu ya kigeni imetengenezwa na watu bali Mungu wao ni Mungu aliyeumba mbingu na dunia na ndiye aliyewatengeneza watu, yaani aliwaumba. Na katika Zaburi hizo hizo walikiri kuwa miungu ya kigeni ina masikio lakini haisikii, ina macho lakini haioni, ina pua lakini haina pumzi, na kadhalika na kadhalika.

Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa
Pentekoste ni Siku kuu ya waamini walei na mwanzo wa Kanisa

Tafakari hii inatuambia nini katika maisha yetu ya leo? Mwanadamu ana kiu ya kumtafuta Mungu lakini wakati mwingine hayuko tayari kumpokea Mungu anayejifunua kwake, hayuko tayari kumpokea Mungu anayeshuka na kumfikia katika maisha yake badala yake ni yeye mwanadamu hutafuta kumtengeneza mungu anayemtaka. Tukiliangalia kwa undani jambo hili tutaona kuwa ndio lililo chimbuko la mwanadamu kumkana Mungu na ndilo chimbuko pia la ushirikina. Ni chimbuko la mwanadamu kumkana Mungu kwa sababu Mungu anayebisha daima hodi katika maisha ya mwanadamu huonekana kama kikwazo na kizuio cha mwanadamu anayetakata kuishi bila usufumbufu wa dhamiri yake kumshtaki kwa yale anayofanya. Mungu anayeshuka daima kumfikia mwanadamu ili amwongoze katika maisha yake anaonekana ni kizuio cha ustawi, maendeleo na uhuru wa mwanadamu. Suluhisho analolichukua linakuwa ni hilo la kumkana Mungu au wakati mwingine bila hata kumkana lakini anajiweka mbali inavyowezekana ili kuyafikia hayo anayoyataka. Pia ni chimbuko la ushirikina kwa sababu wakati mwingine mwanadamu hatosheki na namna Mungu anavyojifunua kwake, badala yake ni yeye sasa anayetafuta kumtengeneza mungu anayemtaka: anamtaka mungu anayelipiza kisasi, anamtaka mungu anayemwambia tu yale anayoyataka, anamtaka mungu asiyemkemea, anamtaka mungu anayekuja tu pale anapohitajika na si wakati mwingine n.k. Ujio wa Roho Mtakatifu katika Sherehe hii ya Pentekoste ni ujio ambao unatambulisha pia utendaji na asili ya Mungu wetu. Kumpokea Roho Mtakatifu kumaanishe katika maisha yetu utayari wa kumpokea Mungu anayetutafuta katika kila siku ya maisha yetu ili atujaze na uwepo wake. Roho Mtakatifu atupe unyenyekevu ili tusianguke katika dhambi ya kumkana Mungu na dhambi ya ushirikina pale tunapojaribu kumtengeneza mungu tunayemtaka.

Liturujia Pentekoste

 

27 May 2023, 12:37