Tafuta

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu  (ANSA)

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni adhimisho mojawapo ya mafumbo makuu ya imani; siku 40 baada ya kufufuka, Kristo alipaa mbinguni na huko amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Katika dominika hii pia Kanisa linaadhimisha kwa ngazi ya kiulimwengu, siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika siku hii unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuongea kutoka moyoni, ‘kadiri ya ukweli na upendo’."

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News dominika hii Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana. Sherehe hii ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu; siku 40 baada ya kufufuka, Kristo alipaa mbinguni na huko amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Katika dominika hii pia Kanisa linaadhimisha kwa ngazi ya kiulimwengu, siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika siku hii unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuongea kutoka moyoni, ‘kadiri ya ukweli na upendo’” (Efe. 4:15). Ndani ya ujumbe wake huu, Baba Mtakatifu anasisitiza kuzingatia upendo wa kindugu na umuhimu wa kukuza msamiati wa amani katika tasnia ya habari na mawasiliano kati yetu. Upendo wa kindugu ndio msingi wa kutoa Habari Njema zinazojenga na msamiati wa amani, anaongeza Baba Mtakatifu, hukuzwa pale ambapo tutaondoa fikra za malumbano na ugomvi ndani mwetu. Masomo kwa ufupi: Injili ya dominika hii ya Kupaa Bwana, inatoka kwa Mwinjili Mathayo. Ni kifungu ambacho Yesu mfufuka anawapa mamlaka wanafunzi wake na anawatuma waende kuwafanya Mataifa yote kuwa wanafunzi wake wakiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Ni somo linalokuja kutuonesha uhusiano uliopo kati ya Kupaa Bwana na mwanzo wa utume wa wafuasi wa Kristo, ulio pia mwanzo wa utume wa Kanisa.

Kanisa linatumwa kwenda kufundisha watu wa Mataifa.
Kanisa linatumwa kwenda kufundisha watu wa Mataifa.

Tuyapitie kwanza kwa kifupi masomo mawili ya mwanzo, somo la kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11) na somo la pili kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef 1:17-23). Somo la kitabu cha Matendo ya Mitume ndilo linatupa picha ya tukio la Yesu kupaa mbinguni. Yesu mfufuka anainuliwa machoni pa wanafunzi wake na wingu linampokea. Neno wingu hapa halina maana ya mahala balli ni alama ya uwepo wa Mungu. Uchaji wa dini ya kiyahudi haukuruhusu kulitaja jina la Mungu. Ndiyo maana katika injili, hasa injili ya Mathayo ambayo ina mwelekeo wa kiyahudi haipendelei kutaja moja kwa moja jina la Mungu. Kwa mfano badala kutaja “ufalme wa Mungu” yenyewe hupendelea kusema “ufalme wa mbingu” n.k. Kumbe Yesu kupokelewa na wingu humaanisha kurudi katika ule umungu aliokuwa nao kabla ya umwilisho. Malaika wanawaambia wanafunzi: namna alivyoenda ndivyo atakavyorudi. Kwa neno hili, malaika anawakumbusha wanafunzi wajibu ambao Yesu amewaachia, wajibu ambao Yesu atakaporudi atawadai hesabu yake Ni kuhusu wajibu huu ambao Kristo ametuachia ndipo linapojijenga somo la pili. Mtume Paulo anasema “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.”

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma na mapendo

Wajibu Kristo aliowaachia wanafunzi wake na kutuachia sisi sote ndio wito aliomwitia kila mmoja wetu ndio utume ambao kila mmoja wetu amepangiwa na Mungu katika maisha yake, katika mazingira yake na katika wakati wake. Kristo anapopaa kurudi kwa Baba, kazi yake anaiacha mikononi mwako. Wito wako na utume wako wa kila siku, katika huduma unayoitiwa kutoa, katika malezi ndani ya familia, katika kazi, biashara n.k wewe mkristo unaendeleza kazi ya Kristo mfufuka. Ni katika hilo Mtume Paulo anaandika akiomba ili kila mkristo ajaliwe kujua uzito, thamani na umaana wa utume ambao Kristo amewitia. Katika somo hili, Paulo anagusia pia tunayoweza kuiita “Taalimungu ya kupaa Bwana.” Anafundisha kuwa kitendo cha Kristo kupaa mbinguni kinaonesha mamlaka, hadhi na ukuu wake juu ya ulimwengu na juu ya viumbe vyote. Hakuna mwingine aliyepaa mbinguni akaketi mkono wa kuume wa Mungu Baba. Ni Kristo pekee. Ni Yeye pekee anayestahili kuabudiwa na ni yeye tunayestahili kumfuata na kuweka kwake tumaini letu.

Kanisa linatumwa kuinjilishaji hadi miisho ya dunia
Kanisa linatumwa kuinjilishaji hadi miisho ya dunia

Tafakari ya Somo la Injili: Somo la injili ni somo linalotulea agizo na mamlaka Yesu Mfufuka anayowapa wanafunzi wake. Waende kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi na kuwabatiza. Injili hii inakuja kukazia fundisho la mtume Paulo tuliloliona katika somo la pili: kupaa Bwana ni mwanzo wa utume wa waamini wa Kristo na ni mwanzo wa utume wa Kanisa. Eneo la utume wa Kanisa ni pana sana na linajumuisha ndani yake mambo mengi. Kati ya hayo mengi, sherehe ya kupaa Bwana inakuja na msisitizo wa pekee juu ya tumaini la kwenda mbinguni ambalo ni tumaini la uzima wa milele. Kuliingia fundisho hili tunaweza kuanza kwa kujiuliza swali. Kwa nini Kristo anapopaa kwenda mbinguni anaamua kufanya hivyo mbele ya wanafunzi wake wote? Anafanya hivyo ili kuwaonesha, ili kuwadhihirishia wao na kwa njia yao kuwadhihirishia waamini wake wote kuwa kule anaokwenda ndiko anakowaita wote waende, yaani yeye amekuja duniani ili kutufanya sote twende mbinguni. Kwa maneno mengine, Sherehe ya kupaa Bwana ni adhimisho linalokuja kutukumbusha kuwa maisha yetu wanadamu hayakomei hapa duniani tu bali yameinuliwa hadhi ili yawe ya milele. Kulifahamu fundisho hili, kulipokea fundisho hili na hasa zaidi kulitangaza, ni mojawapo ya eneo muhimu katika utume wa Kanisa na wetu sote waamini. Tukiangalia namna dunia inavyoenda kwa sasa, tutaona kuwa iko juhudi ya makusudi kuondoa dhana ya uzima wa milele katika maisha ya mwanadamu. Iko juhudi ya kumfanya mwanadamu aamini kuwa kile anachokiishi hapa duniani mwisho wake ni hapa hapa na hakuna kilichopo mbele ya maisha ya duniani. Na kwa sababu hiyo misingi ya imani hai kwa Kristo inabezwa na mwanadamu hatua kwa hatua anatamani kujinasua kutoka katika maongozi ya Mungu na hata kuondoa fikra ya uwepo wa Mungu katika maisha yake. Kristo anapopaa mbinguni anatuonesha yaliko makao yetu ya kudumu na anatualika tuyaishi maisha ya hapa duniani kama maandalizi ya kufika huko yaliko makao yetu ya kudumu.

Liturujia Kupaa Bwana

 

19 May 2023, 15:24