Tafuta

Sherehe hii inaadhimishwa kila mwaka siku ya arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Sherehe hii inaadhimishwa kila mwaka siku ya arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.  

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wa Tunu Msingi za Kiinjili

Siku arobaini ni kipindi cha kutosha ambacho Kristo mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwapa katekesi ya kina kusuhu mateso, kifo na ufufuko wake kadiri ya mpango wa Mungu. Baada ya kipindi hicho aliwatokea rasmi katika upeo wa macho yao wasimuone tena, zaidi ya kumtokea Saulo katika barabara ya Dameski Kutoweka kwake na kutomwona tena kwa macho ya kibinadamu, lakini Yesu yupo pamoja nasi katika: Kanisa, Neno lake na katika Sakramenti zake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Kupaa Bwana. Kwa fumbo la Umwilisho Mungu alichukua hali ya kibinadamu katika Nafsi ya pili, akazaliwa na Bikira Maria, akakaa na kukua katika familia. Baada ya ubatizo wake akiwa na umri wa miaka 33 akaanza kazi ya kutangaza habari njema ya wokovu kwa mda wa miaka 3. Baadaye alikamata, akateswa, akasulibiwa na kufa kifo cha Msalabani. Baada ya siku tatu alifufuka na kurudia hali yake ya Kimungu na kupaa mbinguni mwili na roho. Nyimbo na masomo yanaashiria tukio hili muhimu katika historia ya wokovu wetu. Kiitikio cha wimbo wa katikati kinakazia kikisema; “Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu” (Zaburi 47:5). Sherehe hii inaadhimishwa kila mwaka siku ya arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Licha ya kuwa kupaa Mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunapaswa kuadhimisha siku ya arobani baada ya dominika ya ufufuko, lakini kwa sababu za kichungaji ili waamini wengi waweze kushiriki, sherehe hii inahamishiwa dominika ya karibu. Ifahamike kuwa siku hizi arobaini ni kipindi cha kutosha ambacho Kristo mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwapa katekesi ya kina kusuhu mateso, kifo na ufufuko wake kadiri ya mpango wa Mungu wa kumkomboa mwandamu. Baada ya kipindi hicho aliwatokea rasmi katika upeo wa macho yao wasimuone tena, zaidi ya kumtokea Saulo katika barabara ya Dameski (Mdo.9:1-9). Kutoweka kwake na kutomwona tena kwa macho ya kibinadamu haina maana kuwa Yesu hayupo nasi. Yesu yupo pamoja nasi katika Neno lake na katika Sakramenti.

Hii ni sherehe inayoadhimishwa baada ya siku arobaini za ufufuko
Hii ni sherehe inayoadhimishwa baada ya siku arobaini za ufufuko

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11). Somo hili ni wosia wa Yesu kwa Mitume kabla ya kupaa kwake. Katika wosia huu Yesu anawaambia Mitume kuwa wanapaswa kuhubiri habari njema duniani kote pia anawaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu atakayewakumbusha yote aliyowafundisha na kuwaongoza siku zote katika kuitangaza habari njema ya wokovu. Baada ya maagizo haya Yesu “aliyochukuliwa juu na wingu likampokea wasimwone tena katika upeo wa macho lakini akawa pamoja kwa njia ya Roho Mtakatifu akiwaimarisha katika kutangaza habari njema ya wokovu. Nasi kwa njia ya ubatizo na kipaimara tumempokea Roho Mtakatifu hivyo hatuna budi kuwa mashahidi wa Imani yetu kwa Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef. 1:17-23). Somo hili ni sala ya Mitume inayotupa fundisho juu ya uweza na utajiri wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo ikisema; “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwisho wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”

Kumbe Mungu alimfufua Yesu Kristo toka wafu akamweka kuwa Kichwa cha Kanisa na ulimwengu. Yesu akiwa kichwa cha Kanisa yu pamoja na Kanisa daima. Yeye yuko juu ya vyote vilivyoumbwa na Mungu. Nasi hatupaswi kuwa na wasiwasi wowote maana Kristo yupo pamoja nasi daima. Kuna nukuu nyingine nyingi katika biblia zinazodhihirisha kuwa Kristo baada ya ufufuko wake alipaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu akituombea. Hebu tusome baadhi ya nukuu hizi; “Kristo Yesu ndiye aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, ndiye aliyefufuka kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye ndiye anayetuombea” (Rm 8:34). “Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Kol 3:1). “Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, Yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele Yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Ebr. 12:2). “Maji ya gharika ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia, si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo, ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake” (1Pet 3:21-22). Nukuu hizi zinatupa ujumbe unaofanana kuwa; Yesu baada ya ufufuko wake, aliingia katika hali ya utukufu aliyokuwanayo tangu mwanzo pamoja na Mungu Baba na Mungu Roho Mtakatifu. Kumbe jambo lililo muhimu katika sherehi hii ni kwamba Yesu alirudi mbinguni kwa Baba katika utukufu wake na anaendelea kutuombea nasi tufike aliko.

Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 28:16-20). Sehemu hii ya aya za mwisho za Injili ya Matayo ni tokeo la mwisho la Yesu kwa wanafunzi wake katika mazingira ya kipasaka huko Galilaya na linaweka wazi mambo makuu matatu ndani ya Kanisa: uwepo wa Mungu, utume wa kimisionari na ahadi ya uwepo wa mfariji ndiye Roho Mtakatifu. Sehemu hii ya Injili inaonesha nguvu na mamlaka ya Yesu juu ya mbingu na nchi; “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Danieli 7:14). Utume alioliachia kanisa chini ya uongozi wa Mitume la kuyafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake kwa njia ya ubatizo; “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu”. Kutoa katekesi kuhusu yote aliyowaagiza; “kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”. Na kuwa yeye mwenyewe Yesu atakuwa na kanisa katika hali zote; “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari”. Kumbe kupaa kwake mbinguni hakumfanyi asiwepo nasi. Yesu yupo daima nasi. Labda swali la kujiuliza ni kuwa tunaposema Yesu amepaa mbinguni tunamaanisha nini hasa? Itakumbukwa kuwa Wayahudi waligawa ulimwengu katika ngazi tatu. Anga kama mahali anapoishi Mungu. Dunia mahali ambapo viumbe vyote na binadamu wanapoishi na kuzimu kama mahali ambapo wafu wanaishi, pia mahali pa shetani. Mtazamo huu anao binadamu wa nyakati zote na mahali popote hata sasa. Lakini mama kanisa anatufundisha kuwa mbingu siyo mahali fulani juu bali ni hali ya utukufu. Ndiyo maana katika tukio la kugeuka sura kwa Yesu, Petro aliposhuhudia japo kidogo tu utukufu wa Yesu, alifurahi sana na kusema; “Bwana ni vizuri sisi kuwa hapa. Petro alitamani ile hali ya utukufu iendelee kua nao. Kwa hiyo tunaposema ya kuwa Kristo amepaa mbinguni hatumaanishi kwamba ameenda mahali pa juu, bali ameingia katika hali ya Utukufu wa Mungu. Na hali hii ilitokea mara tu baada ya kufufuka kwake ndiyo maana aliweza kuingia katika chumba walichokuwepo mitume ijapokuwa milango ilikuwa imefungwa kwa kuwa alikuwa tayari katika hali ya utukufu. Kitendo cha kupaa kwenda juu ni suala tu la kutamadunisha namna yetu ya kufikiri na kuona mambo.

Yesu yuko katika Kanisa, Neno la Sakramenti zake
Yesu yuko katika Kanisa, Neno la Sakramenti zake

Tunapoadhimisha sherehe hii ya kupaa Bwana tunakumbushwa wajibu wetu wa kikristo tulioupokea kutoka kwa Mitume kwa njia ya Ubatizo. Wajibu huu ni kuyafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Kristo. Sisi kwa ubatizo tulifanywa kuwa wakristo na sehemu ya Kanisa. Familia ya kikristo ni kanisa dogo la nyumbani. Hili ni kanisa la mwanzo linaloundwa na baba, mama na watoto. Katika kanisa hili la mwanzo, wainjilishi wa kwanza ni wazazi - baba na mama kwa njia ya matendo yao mema. Kanisa hili ni muhimu sana kwa sababu ni chimbuko la miito ya upadre, utawa na ndoa. Wazazi wasipotimiza wajibu wao vyema katika kuwalea watoto wao kulingana na maadili ya kikristo, miito hii inanyauka. Wazazi ni viongozi wa kanisa la nyumbani, hivyo wanapaswa kuwa mfano kwa sala na tabia njema. Tabia mbaya kwa watoto ni matunda ya malezi mabaya. Kwa mfano hakuna mtoto anayezaliwa mwizi, mvuta bangi, mlevi, mhuni au kahaba. Tabia hizi mbaya ni ishara ya kukosekana malezi mazuri na bora yanayosimika katika tunu njema za kikristo na kugubikwa kwa binadamu na malimwengu zaidi na kuacha kushughulika na mambo ya mbinguni. Kumbe, kila mmoja akitimiza wajibu wake vizuri katika uinjilishaji, tunakuwa tunashughulika na mambo ya mbinguni kama sala baada ya komunyo inavyosisitiza; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe watujalia sisi tulio hapa duniani kushughulika na mambo ya mbinguni. Tunakuomba uelekeze moyo wetu wa ibada huko aliko Bwana wetu, Mungu-mtu”. Na hivyo kila tunaposhughulika na mambo ya mbinguni tungali bado tuko duniani tunayakaribia ya mbinguni kama sala ya kuombea dhabihu inavyotilia mkazo ikisema; “Ee Bwana, tunaleta sasa kwa unyenyekevu sadaka yetu kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba utujalie kila tunapoyapokea mafumbo haya matakatifu, tuzidi kuyajongea ya mbinguni."

Tunatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka
Tunatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka

Kumbe basi sherehe ya kupaa Bwana mbinguni inatupa faraja kuwa nasi siku moja tutafika aliko Mungu Baba yetu. Ndiyo maana katika sala ya mwanzo Padre kwa niaba ya waamini anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia yeye kishwa chetu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake”. Na hili ndilo tunalolitumaini, kufika mbinguni aliko Mungu Baba yetu na Yesu Kristo Mkombozi wetu.

Kupaa Bwana
18 May 2023, 11:29