Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Yesu Akasema "Naenda Kuwaandalia Mahali"
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia
Utangulizi: Kutokana na Maandiko Matakatifu, Mama Kanisa anafundisha kuwa “Kristo alipaa mbinguni mwili na roho na ameketi mkono wa kuume wa Baba.” Kolekta ya Sherehe ya Kupaa Bwana inatueleza maana hasa ya tukio la Kupaa Bwana: “Kwani kupaa kwake Kristo Mwanao ni kuinuliwa kwetu.” Kwa kupaa kwake, Kristo anatangulia kwa Baba kutuandalia makao kama alivyotuahidi: “Naenda kuwaandalia mahali.” Nasi tulio mwili wa Kristo twatumaini kufika huko aliko Kristo aliye kichwa cha Kanisa. Kiliturujia Sherehe ya Kupaa Bwana huadhimishwa Alhamisi inayotimiza siku arobaini baada ya Ufufuko wa Bwana. Lakini kwa sababu za kichungaji inaadhimishwa Jumapili ili waamini wengi washiriki. Tukio la Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni linatendeka katika Mlima wa Mizeituni (rejea Mdo. 1:12). Tuangalie kwa undani ufafanuzi wa masomo yetu. SOMO LA KWANZA (Mdo. 1:1-11). Luka, katika somo letu la kwanza, anasimulia tukio la Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni. Kwa Luka hili ni simulizi lake la pili juu ya kupaa Bwana. Simulizi lake la kwanza linapatikana katika Injili yake (Lk. 24:50-51). Luka anaanza kitabu chake cha Matendo ya Mitume kwa simulizi la Kupaa Bwana. Nini sababu ya kufanya hivyo? Luka anataka kuonesha kuwa kwa Kupaa kwake Yesu anahitimisha utume wake hapa duniani na wakati huo huo kupaa kwake ni mwanzo wa utume wa mitume wake kueneza Injili kwa mataifa yote. Katika simulizi la Kupaa Bwana kwenye somo letu la kwanza kuna mambo matatu: (i) Ahadi ya Roho Mtakatifu, (ii) jukumu wanalopewa mitume na (iii) ushuhuda wa malaika (watu wawili). Kwanza, Yesu anawaahidi Roho Mtakatifu ambaye atawapa mitume nguvu ya kuwa mashahidi wa yote aliyoyatenda Kristo na wa mateso, kifo na ufufuko. Yesu anatambua wazi kuwa bila nguvu ya Roho Mtakatifu mitume hawawezi kuwa mashuhuda wa Injili. Pili, Yesu anawapa jukumu la kuwa “mashahidi wake”. Shahidi ni mtu anayetoa uthibitisho wa neno analolijua au tukio aliloliona na ya kwamba yeye mwenyewe ameguswa au kuliona lile analolitolea ushahidi. Hivyo Yesu anawapa mitume jukumu la kushuhudia mambo yote aliyofundisha na kutenda na kwa namna ya pekee kutoa ushuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wake. Malaika (watu wawili wenye nguo nyeupe) kwa upande wao wanawahikishia mitume kuwa Kristo atarudi tena (parousia, yaani ujio wa pili wa Bwana Wetu Yesu Kristo).
Tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwenye somo letu la kwanza: (1) Roho Mtakatifu ndiye anatuimarisha katika ushuhuda wetu wa Kikristo. Ni kwa nguvu na msaaada wa Roho Mtakatifu ndipo tunaweza kuwa mashuhuda thabiti wa Injili ya Kristo: Roho Mtakatifu ndiye anayetupa ujasiri wa kushuhudia ukweli; ni Roho Mtakatifu ndiye anayetupa nguvu za kuishuhudia imani yetu katikati ya mateso, mahangaiko na magumu ya maisha; ni Roho Mtakatifu ndiye anatufariji nyakati za magumu na huzuni; ni Roho Mtakatifu ndiye anatuwezesha kufanikiwa. Tukumbuke kuwa ndani ya Kanisa Katoliki kuna hazina ya sala nyingi za kumwomba Roho Mtakatifu, hivyo tuzitumie. (2) Utume wetu ni kuwa “mashahidi wa Kristo.” Kwa kuwa sisi nasi ni mitume wa Kristo kwa njia ya ubatizo wetu, tunao wajibu wa kuwa mashahidi wa Kristo kwa mwenendo wetu wa maisha, kwa maneno yetu, kwa mawazo yetu na kwa namna ya mahusiano yetu na Mungu. Tunapaswa kutoa ushahidi wa yale tunayofundishwa na yale tunayotendewa na Kristo na kwa namna ya pekee ushuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wake. Je, mwenendo wa maisha yako unakutambulisha mbele za watu kuwa wewe ni Mkristo? Je, maneno na maandishi yako yanamshuhudia Kristo? Je, namna yako ya kupokea mateso na magumu inaonesha kuwa wewe ni Mkristo? Je, upo tayari kuifia imani yako kwa Kristo? Je, kazi yako na imani yako vinaambatana pamoja au vinatengana? Kwa bahati mbaya wengi wetu maisha yetu hayamshuhudii Kristo: wengi wetu tunatenda kinyume kabisa na kile anachofundisha Kristo (tumetawaliwa na dhuluma, visasi na ukatili); wengi wetu tunaikana imani yetu kwa sababu ya vitisho na maslahi binafsi; wengi wetu tunaweka kando imani yetu tuwapo kazini (tunashiriki kutoa mimba tukijidai kuwa tunatimiza jukumu la kuokoa maisha ya mama), wengi wetu tunaendekeza imani za nguvu za giza; wengi wetu ni waoga wa kuitetea imani yetu hadharani. Tafakari, chukua hatua.
SOMO LA PILI (Efe. 1:17-23): Somo letu la pili ni sala ya Mtume Paulo akiwaombea Wakristo wa Waefeso wapate “kuelewa mafumbo ya imani yaliyotendwa na Mungu kwa njia ya Kristo.” Mtume Paulo anawaombea Waefeso mambo makubwa mawili: Kwanza, roho ya hekima na Ufunuo ili wazidi kumjua Mungu. Bila hekima na ufunuo wa Mungu hatuwezi kumwelewa Mungu. Hekima ya kimungu ndiyo inatusaidia kutofautisha kati ya ufunuo wa kimungu na wa kibinadamu. Hata sisi tunahitaji hekima ya Mungu kwani kuna nyakati hekima yetu ya kibinadamu inatusukuma kuhangaikia mambo ya kibinadamu zaidi ambayo hayana tija kwa wongofu wa roho zetu kama vile madaraka, umaarufu, pesa na anasa. Kwa kukosa hekima na ufunuo wa kimungu hata Wachungaji wameanza kupotosha mafundisho ya kimungu na kuanza kufundisha mafundisho ya kishetani wakipotosha Maandiko Matakatifu. Pili, mioyo yao itiwe nuru. Hata sisi tunahitaji Mungu aiangaze mioyo yetu. Mioyo yetu ikiangazwa itaweza kutambua kuwa Mungu ameonesha upendo mkubwa kwetu kwa kifo cha Mwanae. Na hivyo, mrejesho pekee kwa upendo huo wa Mungu ni kumpenda Mungu Baba na Kristo mwanae ambaye amepewa mamlaka na nguvu zote. Tumaini letu liwe kwa Kristo aliye ukamilifu wa vyote.
SOMO LA INJILI: Mt. 28:16-20: Katika somo letu la Injili tunasikia juu ya “agizo la Yesu kwa wafuasi wake kabla ya kupaa mbinguni- agizo linalowataka wafuasi wake kuendeleza kazi ya Kuhubiri Injili, kazi ambayo Yeye Mwenyewe ameifanya kwa miaka mitatu akiwa nao.” Hata hivyo, Yesu anafahamu wazi kuwa utekelezaji wa agizo analolitoa kwa wanafunzi wake si suala lelemama bali utekelezaji wake utakumbana na changamato na magumu mengi na ndiyo maana anaahidi kuwa atakuwa pamoja nao hadi ukamilifu wa dahari (mwisho wa nyakati) ili kuwatia nguvu na kufanikisha utume wao. Tunapolitazama agizo la Yesu tunafunuliwa kuwa: (1) “Injili ni kwa ajili ya watu wa mataifa yote.” Yesu alihubiri Injili miongoni mwa Wayahudi wenzake ambao daima walijiona kuwa wao ni bora kuliko wengine. Wayahudi hawa pia walijona kuwa wao ndiyo wenye hatimiliki ya wokovu, yaani habari ya wokovu ni kwa ajili yao tu- watu wa mataifa mengine hawahusiki. Leo Yesu anawataka mitume wake kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa yote na siyo kwa Wayahudi wenzao tu. Injili haifungwi na mipaka ya kijiografia, kikanda au kikabila. Injili ni haki ya watu wa mataifa yote: Injili ni ya wote. Kwa bahati mbaya hata leo wapo watu wanaofikiri wokovu ni amana yao wao tu. Lakini wapo pia miongoni mwetu ambao wanafikiri Injili ni kwa ajili ya waliobatizwa tu na hivyo wapagani hawana nafasi ya kuhubiriwa Injili.
Kadhalika, bado wapo watu wengi ambao hawajafikiwa na Injili na hivyo tunapaswa kuwafikia pia. (2) Majukumu ya mkristo ni (i) kuwafanya watu kuwa wafuasi wa Kristo, (ii)kubatiza na (iii) kufundisha yale aliyoamuru Kristo: Mosi, kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Kristo. Hapa Kristo anataka kila mmoja wetu awajibike kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Kristo ambaye aliteswa, kufa na kufufuka. Bado wapo watu wengi ambapo hawajawa wanafunzi wa Kristo kwa kuipokea imani ya Kikristo lakini wapo pia ambao ni wanafunzi wa Yesu kwa majina tu. Hawa wote wanahitaji bado kuinjilishwa ili wawe wanafunzi kweli wa Yesu. Pili, kubatiza. Ingawa jukumu hili kwa maana ya kwanza walipewa mitume, lakini ni wajibu wa kila mmoja wetu ambaye kwa ubatizo wake amefanyika kuwa mtume. Kwa njia ya ubatizo mbatizwa hufanyika kuwa “kiumbe kipya, mwana wa Mungu, mshirika wa tabia ya uungu, hekalu la Roho Mtakatifu na mshiriki wa kazi tatu za Kristo: ukuhani, unabii na kifalme.” Hivyo tunapopewa wajibu wa kubatiza tunakabidhiwa wajibu wa kuwafanya watu wote kuwa viumbe vipya, watoto wa Mungu, hekalu la Roho Mtakatifu na washiriki wa kazi za Kristo. Tunaweza tu kufikia malengo haya ikiwa tutatoa mfano mzuri wa maisha yetu, ikiwa tutakemea maovu, ikiwa tutahimiza wenzetu kuongoka (kuacha mwenendo mbaya), ikiwa tutafanya kazi ya kikuhani ya kuwatakatifuza wenzetu kwa maneno na mifano yetu. Kwa kutimiza haya tutakuwa tumebatiza wengine: tutakuwa tumewatakasa.
Tatu, kufundisha watu kuyashika yale aliyoamuru Kristo. Yale aliyoamuru Kristo (aliyofundisha na kutenda Kristo) yaweza kufupishwa kwa maneno sentensi tatu: Kristo alifundisha UPENDO, Kristo alifundisha HURUMA, Kristo alifundisha MSAMAHA. Hayo ndiyo tunaagizwa leo kuwafundisha wengine. Kufundisha ni suala la kutamka tu bali kuyaishi kwa matendo hayo tunayotamka. Kwa bahati mbaya hata sisi wabatizwa tunafundisha kinyume kabisa cha yale aliyoamuru Kristo: tunafundisha kulipiza visasi, tunafundisha kuwachukia adui, tunafundisha kutokuwa na huruma. Kadhalika sisi tulio mitume wa Yesu tunapaswa kufundisha wengine yale “aliyoamuru/aliyofundisha/aliyotenda Kristo.” Kwa bahati mbaya baadhi yetu sisi ambao ni mitume wa Yesu (mapadre, wachungaji, manabii) tumekengeuka na kuanza kufundisha waamini wetu “mambo yetu wenyewe” badala ya kuwafundisha waamini “yale aliyoamuru Kristo.” Kwa maneno mengine badala ya kuhubiri mafundisho ya Kristo tunahubiri mafundisho yetu wenyewe: tunajihubiri na kujitukuza wenyewe, tunatangaza biashara zetu, tunawaahidi watu utajiri wa haraka, tunawaahidi miujiza lukuki, tunawaahidi kutokomeza kabisa magonjwa na mikosi katika maisha. Je, hayo ndiyo aliyotuamuru Kristo? Mbona Kristo anafundisha kuwa kubeba msalaba (mateso, taabu na shida) ni sehemu ya masharti ya kuwa mfuasi wake? Mbona Kristo alifundisha kumpenda Mungu na jirani ilihali sisi tunawafundisha watu kutafuta na kupenda magari, pesa na fahari za dunia? Tujitafakari na kurudi njia kuu.
(3) Tunapotimiza jukumu letu la kutangaza na kuishi Injili hatuko peke yetu- Yesu Kristo yu pamoja nasi sikuzote hadi ukamilifu wa dahari. Yesu Kristo anapohitimisha rasmi utume wake hapa duniani anawaambia mitume, “na tazama mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari”. Kuna neno la faraja na matumaini analotumia Yesu: neno “sikuzote”. Kama lilivyokuwa neno la faraja kwa mitume, neno hili pia ni faraja kwetu sisi jamii ya Wakristo. Yesu yupo nasi sikuzote, siyo kwa baadhi ya siku tu wala siyo kwa muda mfupi tu bali sikuzote. Ukweli huu ni dhahiri hata sasa. Kristo ni pamoja nasi sikuzote: yupo pamoja nasi katika nafsi ya Roho Mtakatifu akitutia nguvu, akitutakasa, akitutakatifuza na kutufariji, yu pamoja nasi kila tunaposoma na kuishi Neno la Mungu, yu pamoja nasi katika Sakrameti, na kwa namna ya pekee anadhihirisha uwepo wake kati yetu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yupo nasi katika nafsi ya makasisi wake, yupo nasi katika matukio ya maisha na changamoto tunayopitia. Hakuna nyakati yoyote katika maisha ambapo Yesu/Mungu ametuacha. Hata wakati wa shida, magumu na taabu si kwamba Yesu anatembea pamoja nasi, bali ametubeba mgongoni mwake. Hii ni bahati kubwa. Kwa nini Yesu anapaa kwenda mbinguni? Zipo sababu kadhaa zinazojibu swali hili: (1) Yesu anapaa kuonesha kwamba amekamilisha kazi ya ukombozi wa mwanadamu hapa duniani na hivyo anarudi tena mbinguni katika utukufu wake wa kimungu ambao alikuwa nao tangu awali. (2) Kupaa kwa Yesu kunaonesha asili/chimbuko lake.
Kitendo cha Yesu kupaa mbinguni kinaonesha kuwa alitoka mbinguni na hivyo anarudi mbinguni alikotoka. Mwinjili Yohane mwanzoni kabisa mwa Injili yake anaonesha asili ya Yesu (anaonesha kuwa Yesu alitoka mbinguni): “Hapo mwanzo alikuwako Neno; naye Neno alikuwako kwa Mungu; naye Neno alikuwa Mungu” (Yn. 1:1). Hivyo, kitendo cha Yesu kupaa mbinguni kinaonesha asili yake ya kimungu. (3) Yesu anapaa mbinguni kwa Baba kwenda kuwaandalia wateule wake makao: “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali” (Yn. 14:2) (4) Yesu anapaa kwenda mbinguni kuendeleza kazi yake ya kikuhani. Yesu hapai kwenda mbinguni kwa lengo la kupumzika baada ya kazi ngumu ya ukombozi. Yesu ni Kuhani Mkuu wetu “aliyeingia mpaka mbinguni” na huko mbinguni anaendeleza kazi yake ya kikuhani ya kuwaombea watu wake (rejea Ebr. 4:14-15; 7:25; 1 Yn. 2:1). Hivyo, Yesu anapaa mbinguni ili kwenda kufanya kazi yake ya kikuhani ya kuwaombea watu wake. Tukio la Kupaa Bwana lina maana gani kwetu? Mtume Paulo anatuambia kuwa Kristo ni kichwa cha Kanisa (Ef. 5:23) na sisi tu mwili wa Kristo (Efe. 1:22). Kama Kristo aliye kichwa cha Kanisa amepaa, hata sisi ambao ni mwili wake tunapaswa “kupaa”. Kimsingi “tunapaswa kupaa mbinguni tukingali hapa duniani”. Kwa maneno mengine tunapaswa “tuishi maisha ya mbinguni tukingali hapa duniani”. Tutapaaje mbinguni wakati bado tupo duniani? Tutaweza “kupaa mbinguni tukingali hapa duniani” na tutaweza “kuishi mbinguni tukingali hapa duniani” kwa njia moja tu ya “kuyatafuta yaliyo juu… kuyafikiri yaliyo ya juu, siyo yaliyo ya chini” (yaani kutafuta na kuyafikiri mambo ya mbinguni) kama Mtume Paulo anavyotuasa katika Kol. 3:1-2. Mbinguni viumbe vyote vinamsifu Mungu- Je, maisha yako ya hapa duniani yanamsifu na kumtukuza Mungu? Mbinguni kuna furaha ya milele- Je, unahangaikia kupata furaha ya milele kwa mwenendo wa maisha yako ya hapa duniani? Je, unahangaika kumjua Mungu? Jitahidi kupaa na Kristo Yesu. Sherehe njema ya Kupaa Bwana