Tafuta

Dk. Ungunmerr Baumann,mama wa Asilia wa Australia akiwa na Balozi wa Australia anayewakilisha nchi yake mjini Vatican wakati wa uzinduzi wa kazi yake ya Kisanii Dk. Ungunmerr Baumann,mama wa Asilia wa Australia akiwa na Balozi wa Australia anayewakilisha nchi yake mjini Vatican wakati wa uzinduzi wa kazi yake ya Kisanii 

Mzee wa asilia atembelea Vatican kwa Juma la Upatanisho la Australia!

Huyu ni Dr Miriam-Rose Ungunmerr Baumann,ambaye wakati wa kukaa kwake mjini Vatican,pamoja na kukutana na Papa atakutana na maafisa wakuu wa Vatica ili kujadili imani,ikolojiana upatanisho na watu wa kiasilia.Kwa hakika ni mama wa asilia kutoka Australia,mwalimu na msanii,ambaye amenza ziara yake tangu tarehe 29 Mei na atahitimisha tarehe 3 Juni 2023.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Dk. Miriam-Rose Ungunmerr Baumann, mzee wa asili wa Australia, mwalimu na msanii,yuko mjini Vatican kuanzia tarehe 29 Mei 2023  hadi tarehe 3 Juni 2023. Wakati wa ziara yake ya Juma nzima, atazungumza juu ya mada za kiroho, kikolojia, na upatanisho kati ya Kanisa na wenyenyeji wa asili wa Australia. Hata hivyo Dk. Ungunmerr Baumann amekutana na Papa Francisko tarehe 31 Mei na kuhudhuria hafla kadhaa na viongozi wakuu huko Vatican. Balozi wa Australia anayewakilisha nchi yake Vatican, Chiara Porro, wakati wa kutoa hotuba yake kwenye afla iliyoandaliwa kwenye Jumba la Makumbusho  tarehe 30 Mei,  jioni alisema safari yake imehamasishwa na mmoja wa viongozi wa asili wanaoheshimika zaidi wa nchi yao.  Historia yake ni kwamba Dk. Miriam - Rose Ungunmerr Baumann alizaliwa mnamo mwaka wa 1950 katika Wilaya ya Kaskazini ya Australia, na amefanya kazi kama mwalimu, msanii, na mtetezi wa haki za Watu wa Asilia. Mnamo 1975, alikuwa mwalimu wa kwanza wa asili aliyehitimu kikamilifu katika nchi nzima. Mnamo 1993, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule ya Mtakatifu  Francis  Xavier huko  Mto Daly. Mnamo 1986, wakati huo huo, alianzisha Kituo cha Sanaa cha Merrepen, ambacho kinalenga kukuza ukuaji wa kiroho kupitia sanaa ya kuona. Amefanya kazi sana na watoto wa asili, akiwasaidia kutumia sanaa kuchunguza uhusiano wao na ulimwengu wa asili. Uongozi wake umemletea Agizo la Medali ya Australia na tuzo ya Mwaustralia Mkuu wa Mwaka wa 2021.

Dr Miriam-Rose  U. Baumann
Dr Miriam-Rose U. Baumann

Ziara ya Dk. Ungunmerr Baumann mjini Vatican ni katika fursa ya Juma la Upatanisho wa Australia, ambayo ni maadhimisho ya kila mwaka ya historia na utamaduni wa Watu wa Asilia.  Katika tukio kuu la  ziara yake tarehe 30 Mei 2023 jioni kwenye Makumbusho ya Vatican Dk. Ungunmerr Baumann aliwakilisha kazi yake mpya maalum ya kisanii inayochota kutoka katika mila na Utamaduni wa Watu wa Asili na Ukristo ambapo kazi ya uumbaji na pia uharibifu wake inaoneshwa.  Tarehe 31 Mei 2023  baada ya kukutana na Papa Francisko wakati wa katekesi, alishiriki katika majadiliano ya hadhara na Askofu Paul Tighe, Katibu wa Baraza la Kipapa la Elimu na Utamaduni, vile vile Kadinali Arthur Roche Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa ataongoza Misa ya Takatifu katika kuadhimisha miaka 50 tangu idadi kubwa ya Watu wa Asili  walipo kusanyika huko Melbourne kwa ajili ya Misa ya kwanza iliyojumuisha vipengele vya lugha na utamaduni wa Watu wa Asilia.

Ibada ya kwanza ya Watu wa Asili

Tarehe Mosi Juni, Dk. Ungunmerr Baumann atazungumza juu ya mada ya “Mtazamo wa watu asilia kuhusu ikolojia fungamani: dhana ya Dadirri. Tukio la mwisho la juma litakuwa mkutano na  Padre Frank Brennan SJ, wakili wa Watu Asilia  wa Australia, kuhusu  uamuzi wa 'Mabo' wa 1992, ushindi muhimu wa kisheria kwa haki za watu wa Asilia. Ilikuwa wakati mzuri sana katika moja ya maeneo ya makumbusho ya kiasili  iitwayo: “ Anima mundi". Historia kwa ufupi ni ilikuwa ni mnamo 1925, ambapo  Papa Pio XI aliandaa tukio kubwa la Maonesho ya Vatican, ambayo kupitia kwake angeweza kujulisha mila ya kiutamaduni, kisanii na kiroho kwa watu wote. Mafanikio makubwa ya Maonesho hayo, ambayo yalionesha zaidi ya vitu 100,000 na kazi za sanaa kutoka ulimwenguni kote hadi wageni zaidi ya milioni moja, yalimshawishi Papa kubadilisha tukio la muda kuwa maonesho ya kudumu. Hivyo ilizaliwa Makumbusho ya Wamisionari wa makabila ya kiutamaduni iitwayo (Anima Mundi)ambayo kwanza iliwekwa katika Jumba la  Laterano hadi uhamisho wake, ambao ulifanyika mapema miaka ya sabini, hadi mahali ilipo sasa ndani ya Makumbusho ya Vatican.

Kazi ya kisanii ya watu wa Asili iliyomo katika Jumba la makumbusho eneo la Anima Mundi
Kazi ya kisanii ya watu wa Asili iliyomo katika Jumba la makumbusho eneo la Anima Mundi

Kwa hiyo katika mkutano uliofanyika katika Jumba la makumbusho baada ya salamu za Dk, Barbara Jatta, mwanahistoria wa sanaa wa Italia ambaye amekuwa mkurugenzi wa Makumbusho ya Vatican tangu Juni 2016 ilifuatia hotuba ya Balozi wa Australia anayewakilisha Nchi yake mjini Vatican Dr. Chiara Porro na  kuhitimisha kwa kumkaribisha Dr. Miriam -Rose Ungunmerr Baumann, atoe historia yake ya kusisimua sana kuhusu Maisha yake na  ikolojia, elimu, na masuala ya Watu wa asilia, ambapo aliweza kubadilishana mitazamo mbali mbali kuhusu masuala mengi ya kipaumbele kwa Australia na Vatican.

Kazi ya kisanii ya Dr Miriam - Rose Baumann

Kwanza kabisa katika mchoro  kwenye kadi unaonesha,  Mama Maria akishika Mwili wa Mwanaye Yesu, ambapo ni (Ni kituo cha 13 / 14 cha njia ya Msalaba). Dr Rose anaeleza kuwa  “Mama mzazi (Mama wa asili) ndiye tu pekee anaweza kumfariji  Mwanae hata kama ni mtu mzima, ambaye yuko katika hali ya huzuni  kwa kumgusa kwa mkono wake, lakini pia mara tu akisha kufa, anaweza kuuchukua mwili wake kwa mikono yake ikiwa ni kwa mara ya mwisho. Mwili wa Maria na mwanae huunganika na kuwa kitu kimoja. Machozi ya Maria ni ishara ya huzuni yake, kama ilivyo katika Kituo cha Nne,  lakini wakati huo  mng'ao wa moja kwa moja katika Maisha yetu yote hutokea  kutokana na machozi ya Maria kama ishara ya maisha mapya kutoka kwa mtoto wake  mfufuka. Kristo aliyekufa mikononi mwake yuko hai ndani yake. Yeye hubeba, naye atamzaa tena, kama Mkristo wa kwanza na kama Mama wa Kanisa. Ufufuko, ni kama vile Umwilisho wenyewe,  ambao tayari unatokea ndani ya Maria kwa njia ya Imani kabla ya kutokea kweli kwa Kristo mwenyewe.” Dr. Miriam - Rose Ungunmerr Baummann anahitimisha: “Mwili wa Maria na Mwili wako ni mmoja, Yesu. Uhai wako huko ndani ya mwili wake.  Yeye abeba maisha yake ndani yake.”

Mchoro unaonesha Maria akimkumbatia mwanae Yesu
Mchoro unaonesha Maria akimkumbatia mwanae Yesu

Katika kadi nyingine iliyochorwa inawakilishwa na : Yesu anakutana na Mama yake njiani (Kituo cha 4/14 cha Njia ya Msalaba).ambapo  Dr. Miriam - Rose Ungunmerr Baummann anabainisha kuwa: “ Wakati Mama Mzazi wa kiasilia anataka kumfariji mwanae ambaye yuko katika hali ya uchungu, anamgusa kwa mkono wake. Maria anashika mkono wake mwingine mbele ya macho yake kwa hofu, na uchungu wote unabaki ndani mwake, yaani rohoni mwake. Mtazamo uliopo ndani ya  kichwa cha Yesu unaonesha wazi ufahamu wake wa kile kinachoendelea ndani yake na mistari ya uchungu inayong'aa ni neema ya kimungu na msaada wa kibinadamu ambao anamtumia. Kwa hiyo ugusaji wake wa mikono unapelekea ujumbe kati yao. Anahitimisha: “Ni kwa Jinsi gani wewe Yesu na Maria Mlivyoteseka mlipokutana na kupata uchungu pamoja! Tunashukuru uchungu wenu na maumivu mliyoteseka kwa ajili yetu. Tunasikitika Yesu.”

Mchoro Mwingine Yesu anakutana na Mama yake njiani
Mchoro Mwingine Yesu anakutana na Mama yake njiani

Na katika mchoro mwingine  ambao umewekwa kama alama ya maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanza mahusiano ya kidiplomasia ya Vatican na Australia, mnamo 1973 -2 023, Dr Miriam-Rose, Ungunmerr Baumann alichora kwa ajili ya  Kanisa la Mtakatifu Francis wa Xavier huko Nauiyu Nambiyu Mto Daly, wenye kichwa: Mungu Pamoja Nasi katika mto Daly.  Mchoro hupo pia katika kasula.

Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanza uhusiano wa kidiplomasia wa Vatican na Australia
Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanza uhusiano wa kidiplomasia wa Vatican na Australia

Kwa njia  hiyo maelezo ya mchoro huo ni kwamba: Muundo wa msingi ni ule wa kikombe, juu yake na nyuma yake kuna msalaba na katikati ya sehemu hizo mbili, mkono ulionyooshwa ukisaidia kushika hostia takatifu. Juu ya Msalaba kuna njiwa, Roho ya Mungu, ambapo chini ya mabawa zake zilizofunguliwa(tandazwa) kuna Amri Kumi za Agano la Kale zinazoungana na kuwa sheria au Amri moja ya Agano Jipya iliyotolewa kwetu kupitia mkono wa Kristo, yaani ni Amri  ya upendo. Amri hii na amani na umoja unaokuja kutokana na kuitii, inatangazwa kwa watu wote wa mataifa na rangi mbalimbali kupitia kuitangaza Injili iliyowakilishwa hapo na vidole vinne vya mkono. Kidole cha katikati kimeoneshwa kwa umuhimu wake ili kuonesha kwamba kupitia Kristo, ambaye ndiye Njia, Roho Mtakatifu anatuongoza katika ukamilifu mdogo lakini kamili (uliooneshwa na umbo dogo lenye mviringo mwishoni mwa kidole). Umoja huu, utakamilishwa tu katika Umungu Utatu au Utatu Mtakatifu (uliooneshwa na pembetatu inayounda msingi wa kikombe).

Mchoro wa Dr Miriam- Rose Baumann wa Australia
Mchoro wa Dr Miriam- Rose Baumann wa Australia

Umoja wetu kwa pamoja na umoja wetu na Mungu hutokea kwa sababu ya upendo wa Mungu mwenyewe unaomiminwa mioyoni mwetu kupitia Roho ambaye ametolewa kwetu na  upendo uliowakilishwa hapo na madoa meupe yanayozunguka kila upande. Umoja huu kiukweli unafanywa kwa kujitoa sadaka ya Kristo msalabani na kupyaishwa katika Ekaristi (hivyo kipande kitakatifu cha hostia kinachosaidiwa na mkono pia kinakuwa jeraha katika mkono wenyewe). Hii hutokea katika jumuiya isiyo na vizingiti yaani Kanisa (ambalo msingi wake ni Mitume kumi na wawili  ambao wanaisaidia  msingi wa kikombe.”

Dr Ungunmerr na Angella Rwezaula wakati wa kufurahi pamoja kwenye afla ya kuwakilisha kazi yake ya kisanii
Dr Ungunmerr na Angella Rwezaula wakati wa kufurahi pamoja kwenye afla ya kuwakilisha kazi yake ya kisanii
Historia ya mwanaasilia kutoka Australia Dk Miriam-Rose U. Baumann.
31 May 2023, 17:53