Askofu mkuu Nyaisonga Azindua Parokia Mbili: Uinjilishaji wa Kina!
Na Padre Stan Rodrigues, Jimbo Kuu la Mbeya, Tanzania.
Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania pamoja na mambo mengine: Kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia.” Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa.
Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania amezindua Parokia mpya mbili ikiwemo Parokia ya Mtakatifu Magdalena, Ivwanga-Karasha, iliyofunguliwa Mei, 8, 2023 pamoja na Parokia ya Petro Mtume-Ndaga, liyofunguliwa Mei, 9, 2023 na hivyo kufanya jumla ya idadi ya Parokia za Jimbo kuu la Mbeya kufikia 61. Pia amewateua makaimu Paroko watakaozisimamia Parokia hizo kuwa ni Padre Denis Hulla Paroko wa Parokia ya Vwawa kuwa Kaimu Paroko wa Parokia ya Ivwanga-Karasha. Askofu mkuu Nyaisonga amemteua Padre Patrick Njau C. S. Sp., ambaye ni Paroko wa Parokia ya Igoma kuwa Kaimu Paroko wa Parokia mpya ya Ndaga ambapo pia Parokia Mama ya Igoma imetoa zawadi ya Gari na amewapongeza wanaparokia kwa nyakati tofauti wanaparokia zote mbili kwa zawadi na baraka kwa watu wote na shukrani kubwa kwa Mwenyezi Mungu kutokana na huduma za kiroho kuweza kusogea karibu zaidi. Katika mahubiri yake wakati akiongoza adhimisho la ibada ya Misa Takatifu, wakati akizindua Parokia mpya ya Mtakatifu Magdalena, Ivwanga-Karasha, Jimbo kuu la Mbeya, iliyoenda sambamba na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 306, Askofu Nyaisonga ametoa wito na mwaliko kwa wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Amesema, uinjilishaji utasaidia kwa kiasi kikubwa kuitibu na kuinusuru dunia ambayo imezidi kukengeuka kwa kuhalalisha vitendo vya ushoga, ndoa ya jinsia moja ikiwemo na kasi ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote.
Askofu mkuu Nyaisonga amewapongeza wakristo kwa zawadi ya Parokia ya Ivwanga yenye maana ya neno la kabila la kinyamwanga kuwa ni kusema’, hivyo wamini wa Parokia hiyo wanapaswa “kuvwanga” (kusema, kunena) Habari Njema kwa watu wote walio na wasio wakristo ili wapate kuokoka. “Dunia leo hii tunaongelea ushoga ni aibu!! maneno yanayoleta maudhikama imefikia Mwanadamu anaweza kubadilisha yale makusudi yake Mungu, anasema leo hii amegundua mengine siyo kwamba mume na mke wanafunga ndoa eti hata mwanaume na mwanaume wanaweza kufunga ndoa na mwanadamu akajenga hoja na watu wanamshangilia inaudhi!!,"amesema. Ameongeza, “yaani inataka kuonesha dunia inayo nguvu kubwa kumpinga Kristo kwa hiyo wale waliojaliwa kumpokea Kristo wasinyamaze, kama jina la Parokia linavyomaanisha ‘kuvwanga’ ni “kusema” na hivyo ‘wavwange’, kila mkristo awe ‘mvwangaji na hata asiye mkristo aseme atakacho Mungu na akemee hasichokitaka Mungu. Askofu mkuu Nyaisonga amesema kuwa Maandiko na hasa Agano la Kale yanaonesha jamii ilipomsahau Mungu, watu waliteseka na kupata pigo katika Miji kama vile Sodoma na Gomora na kwingineko na hivyo Wakristo wanapaswa kuendelea kumtagaza Mwenyezi Mungu ili watu wote waweze kuongoka. Amezungumzia baadhi ya masuala ambayo, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akiyakazia ikiwemo utunzaji na uhifadhi wa Mazingira bora nyumba ya wote, na kwamba endapo watu wanaharibu kwa makusudi ni mojawapo ya maovu ambayo adhabu yake ni kujitokeza kwa majanga yanayowakumba hata wasiohusika.
Askofu mkuu Nyaisonga amesema, Leo tunaanza Parokia hii inayotukumbusha wajibu wa kusema, kuhubiri habari njema, Roho Mtakatifu anatuimarisha kwa mapaji yake ambayo yatatusaidia kuhubiri injili ipasavyo… basi tushikamane, dunia iwe sehemu salama ya kuishi tuache hata kufanyiana ubaya sisi kwa sisi ili tuione dunia ni sehemu salama ya kuishi kwa kila Mtu, amesema Askofu Nyaisonga. “Wazo kuu la leo tunapoanza siku ya kwanza kama Parokia wakati huo huo tunawaimarisha waamini wetu kwa kipaimara kama ambavyo Mwinjili Luka anavyosema katika kitabu chake sura ya 12 aya ya 32 katika sentensi ya kwanza kabisa kuwa: Msiogope enyi kundi dogo kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwa ufalme amewapa heshima ya kuwa Parokia, neno hili linawafaa ninyi wanaparokia, mlijiona kundi dogo hata Kanisa la kwanza lilianza hivyo hivyo walipoanza Mitume kumi na mmoja Yuda alipoondoka na kumwongeza Mathias kuweka idadi ya thenashara, "amefafanua Askofu mkuu Nyaisonga. Wakati huo huo, Askofu mkuu Nyaisonga akizindua Parokia mpya ya Ndaga amewaalika waamini kuwa mstari wa mbele na kilelezo kama Mtume Petro alivyosema na watu wa amani na mapatano kwa familia ya Mungu. Suala la ushoga linakuja kwa nguvu, wakatoliki muwe wasemaji, muwe sauti ya kukemea maovu Mwanamke ajivunie uanamke wake alikadhalika kwa mwanaume, na waache kudhulumiwa utu wao muwe wa kwanza kusema tunao uzima tunayo chemichemi ya kweli, mliopo hapa muwe wa kwanza kupeperusha bendera ya Kristo, Msalaba wa Kristo, makanisa na misikiti tuendeleze mapambano dhidi ya uovu, amehitimisha Askofu mkuu Nyaisonga.