Ujumbe wa Pasaka Kwa Mwaka 2023 Kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumkirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko kwa waamini kudumisha Injili ya upendo na matumaini. Mwenyezi Mungu kwa njia ya huruma na upendo wake usiokuwa na upeo, amemkirimia mwanadamu matumaini mapya. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka kwa njia ya uhalisia wa maisha yao. Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu ambayo waamini wa Kanisa la Mwanzo uliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; wakauendeleza kama msingi wa Mapokeo ya Kanisa na kuuthibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya, wakauhubiri na kuushuhudia kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka sanjari na Fumbo la Msalaba: Kristo amefufuka kwa wafu. Kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti; wafu wamepata uzima. Rej. KKK 636-658. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023 alikazia kwa namna ya pekee kuhusu: Fumbo la mateso ya Kristo Yesu: Kiroho na Kimwili: Kiini cha ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; na chemchemi ya matumaini, kwa wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?”
Mama Kanisa katika Liturujia ya Neno la Mungu, amewawezesha waamini kusikiliza tena Zaburi ya 22: 2 inayohusu mateso na matumaini ya mwadilifu kama kiini cha Fumbo la Mateso ya Kristo Yesu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Huu ndio ukweli unaotangazwa na Mama Kanisa katika Kipindi hiki cha Pasaka ya Bwana! Ni katika muktadha huu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., katika ujumbe wake kwa Sherehe ya Pasaka kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ameshinda dhambi na mauti na hivyo anayafanya yote kuwa mapya.” Huu ndio ujumbe wa matumaini na upya wa maisha unaotolewa na Mchungaji Prof. Dr. Jerry Pillay, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Anawaalika waamini kutafakari kilio cha Kristo Yesu pale Msalabani alipolia na kusema: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" Baraza la Makanisa linasema, hiki ni kilio cha Kristo Yesu kinachoendelea kusikika miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, njaa, umaskini pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna watoto wanaonyanyaswa na hivyo kusigina utu, heshima na haki zao msingi. Kuna walemavu wanaoteseka, wanaotengwa na kunyimwa haki zao msingi.
Bado kuna watu wanabauguliwa kutokana na rangi, jinsia na mahali anakotoka mtu. Yote haya hayawezi kuvumilika kiasi kwamba, mara nyingi watu hawa wanafikiri kwamba, serikali, ndugu, jamaa na marafiki na hata pengine Mungu mwenyewe amewageuzia kisogo. Matokeo yake ni watu kujikatia tamaa ya maisha! Kristo Yesu aliteswa sana na hatimaye, akakata roho pale Mlimani Kalvari. Hivi ndivyo hata watu wa Mungu wanavyojaribiwa katikati ya machungu, mateso na kifo kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, amewaacha na kuwageuzia kisogo, lakini wanapaswa kuwa na uhakika kwamba, kifo hakina nguvu wala neno la mwisho, baada ya kifo, Kristo Yesu alifufuka kwa wafu, Mwenyezi Mungu ameyafanya yote kuwa mapya. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja nao katika safari ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi! Uhakika wa uwepo wa Mungu kati pamoja nao, uwawezeshe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini na nuru kwa ulimwengu. Pasaka ya Bwana, iwajalie waamini kuwa na nguvu na hamu ya kuendelea kujikita katika kufanya kazi kwa misingi ya haki, amani na maridhiano na Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa viumbe vyote.