Ni miaka 18 tangu alipoaga dunia Mtakatifu Papa Yohane Paulo II mnamo 2 Aprili 2005
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Maneno ya shukrani kwa Mtakatifu Yohane Paulo II katika kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo chake. Yalikuwa ni maandamano mengi ambayo yalifanyika tarehe 2 Aprili 2023 katika miji mbalimbali ya Poland ili kutoa shukrani kwa Karol Wojtyla yaani kwa Papa thabiti katika mapambano ya kujibu mashambulizi ya baadhi ya sekta za kiutamaduni na kisiasa za nchi dhidi ya sura yake. Mamia ya maelfu ya watu walishiriki katika maandamano, ya kuvutia zaidi huko Warsaw, lakini ni wazi pia huko Krakow na nchini kote. Mikutano na mikesha ya maombi pia iliandaliwa, huku ikihudhuriwa na waamini wa vizazi vyote.
Katika barua iliyochapishwa kwenye tovuti ya Uaskofu wa Poland, msemaji Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini humo Padre Leszek Gęsiak, alisitiza jinsi ambavyo leo hii kuna majaribio si ya kudharau tu, lakini hata kupita kimya kimya au kudhihaki yale ambayo Papa Yohane Paulo wa Pili amefanya kwa Kanisa la Ulimwengu na kwa Poland yenyewe. Msemaji wa Uaskofu wa Poland, Padre Gęsiak alisema “Kwetu sisi ambao tumekua na kukomaa wakati wa upapa wake, ni jambo lisilowazika kudharau kwa njia hii kile ambacho Papa wa Poland ameifanyia nchi yetu katika nyakati ngumu za kihistoria tulizoshuhudia.
Kwa hiyo msemaji wa Baraza la Maaskofu Poland amesisitiza kwamba "Kumbukumbu ya yale aliyofanikisha kwa ajili ya Kanisa la Poland na ulimwenguni kote, pamoja na ufahamu wa urithi mkubwa ambao tumetoka humo na ambao kwa njia nyingi bado unabaki kugunduliwa, na unahakikisha kwamba kila tarehe 2 Aprili saa 3.37 za usiku zinabaki kuwa hai kwa maana wengi wetu na tuna wakati maalum wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya nafsi yake. Haiwezekani kukadiria mema ambayo mtu huyu amewapa ubinadamu na kuingiza katika mioyo ya mamilioni ya watu duniani kote. Kwa hiyo, hatutaruhusu wema huu uliotolewa kwa ubinadamu wa Yohane Paulo kuharibiwa au kufutwa”.
Maadhimisho ya leo pia yalitiwa alama na baadhi ya vitendo vya uharibifu kwa shutuma za madai ya kushindwa katika vita dhidi ya dhuluma katika Kanisa wakati Wojtyla alipokuwa Askofu mkuu wa Krakow. Kwa hiyo huko Krakow picha ya ukutani yenye sura ya Papa ilipakwa rangi nyekundu, wakati huko Łódź, katikati mwa Poland, mnara uliowekwa wakfu kwa ajili ya Yohane Paulo II, mbele ya Kanisa kuu liliharibiwa. Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Grzegorz Ryś wa Jimbo Kuu Katoliki la Łódź, alisema "Nilipowasili hapa asubuhi ya leo kusherehekea Misa Dominika ya Matawi nilijiuliza: Je Yohane Paulo II angefanya nini? Jibu ni dhahiri: angewaombea waliohusika". Kwa hiyo Askofu alitoa mwaliko kwa waamini wote. Vile vile tendo mashambulizi hayo ya kuharibu yamelaniwa na askofu mkuu Tadeusz Wojda wa Jimbo Kuu la Gdansk, ambaye alizungumzia kama jaribio lisilo la msingi la kupindua mamlaka na kuharibu utakatifu wa Yohane Paulo II. “Kwa kumvunjia heshima mtu wake kuna hatari ya kuvinyima vizazi vichanga nukta muhimu ya marejeo katika masuala ya imani na maadili. Habari njema ni kwamba katika utetezi wake, pamoja na mapadre na maaskofu, watu wengi zaidi waamini wanasimama kwa ujasiri", alisema.