Tanzania,Ask.Rweyongeza:Dhambi za dunia zinaendelea kumtesa Yesu!
Na Patrick Tibanga, -Bukoba, Tanzania & Angella Rwezaula, - Vatican.
Siku ya Ijumaa Kuu ni siku ambayo waamini wote wakristo wanatafakari mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ile ambayo inajieleza wazi ni nini maana ya msalaba. Msalaba ni bendera na bango la ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Msalaba ni alama ya ukombozi (Yn.12:13-33), msalaba ni alama ya upendo wa Kristo kwetu sisi wadhambi (Yn.3:14-18). Msalaba ni alama ya maisha ya kikristo (Mk.8:34). Msalaba ni alama ya umoja na Kristo. Msalaba ni alama ya ufuasi wa kweli wa Yesu Kristo (Mk 8: 34). Msalaba ni sadaka ya Yesu, ni zao la upendo (Yn 13:1; 15: 13). Ni kwa njia ya msalaba sisi sote tumekombolewa.
Ni katika muktadha huo ambapo wazazi waamini wa Mungu wameombwa kulea watoto katika maadili na kuwafundisha kazi za nyumbani pamoja na kukemea vitendo viovu vya ndoa za jinsia moja na kutoa sala zao mbele ya msalaba na kumuomba Mungu toba kutokana na maovu yanayoshamiri. Wito huo ulitolewa na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga wakati wa Homilia yake katika Ibada ya Ijumaa Kuu Takatifu, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu George Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Kayanga, tarehe 7 Aprili 2023.
Katika homilia yake Askofu Rweyongeza alisema, wakati wa mateso hadi kifo chake, Yesu alijinyenyekeza akafa msalabani na kumkomboa mwanadamu, na kupitia wokovu huo wakristu wanatakiwa kuonesha imani yao kwa Mungu na kuacha kufanya maovu kwani dhambi za ulimwengu huu zinaendelea kumtesa Yesu msulibiwa. “Mungu alitupatia baraka ya kuzaa na kuijaza dunia, sasa dunia imeanza kujishangaa, badala ya kuzaa na kuongezeka sasa wanyama ndio wanaongezeka kuliko binadamu na wameanza kututawala sasa, baadhi yenu hawapendi kuzaa wanatumia vidhibiti mimba, vijiti, wengine wamethubutu hata kufunga kizazi, wapo wengine wanaua mimba wakidai eti maisha yamekua magumu, wapo humu humu tunasali nao. Dhambi za dunia, bado zinaendelea kumtesa Yesu kutokana na maovu yote tunayoyafanya ikiwemo kutoa mimba.” Alisema Askofu Rweyongeza katika homilia yake.
Askofu Almachius Rweyongeza aidha aliwashauri wazazi ili walee watoto katika maadili na kuwafundisha kazi za nyumbani pamoja na kukemea vitendo viovu vya ndoa za jinsia moja na kutoa sala zao mbele ya msalaba na kumuomba Mungu toba kutokana na maovu yanayoshamiri: “Tendo lisilo adilifu linamtenga mwanadamu na Mungu, hivyo waamini mtumie siku Kuu hizi tatu za Pasaka, kutafakari matendo yenu, mbadilike na kuyaishi matendo ya unyenyekevu kama Yesu Kristo pale msalabani, naomba niulize hivi ndoa za jinsia moja ni agizo la Mungu kweli hilo? Hata wanyama bado hawajafikia hapo, ndoa za jinsia moja, ushoga na usagaji huo ni ushetani. Hapo kuna kuutawala ulimwengu kweli? “Aliuliza Askofu Rweyongeza.
Askofu katika tafakari yake ya Ijumaa Kuu aliwaomba waamini kusali sana na kumuomba Mungu ili aepusha na kuwasemehe wanaohusika na vitendo hivyo ili Mungu asije kutuadhibu kama miji ya Sodoma na Gomora na kuongeza kusema kuwa anashangazwa na mataifa yanayo tetea uovu huo na kudai haki kwa kupitisha sheria za kutetea haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Askofu: “Tunahitaji kusali sana, hapo kwenye ndoa za mume na mume, mke na mke kuna kuzaana hapo na kuongezeka kweli na kuutawala ulimwengu? na hii dhambi imekumba jamii yetu na ulimwengu mzima kuona nchi zilizoendelea zinapitisha sheria kulinda hawa watu eti ni haki, haki gani za mashoga na usagaji, tuendelee kumcha Mungu ili Mungu akiamua kutuadhib kama miji ya Sodoma na Gomora basi tupone kwa kusali, Mungu anachukizwa na madhambi hayo ya kutoheshimu ndoa,”alihitimisha Askofu Rweyongeza.