Pd.Tibangayuka:Ubichi wa mwanadamu unatokana na kuwa na amani Rohoni!
Na Patrick Tibanga, -Bukoba, Tanzania & Angella Rwezaula, - Vatican.
Kila mwaka, Juma Kuu Takatifu linafunguliwa na Dominika ya Matawi, ikiwa ndiyo mwanzo wa Mafumbo makuu ya Wokovu wa ubinadamu wote, ambaye katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu katika wafu, binadamu huyo anakombolewa pia, kwa sababu Bwana anashinda mauti kwa kishindo kikubwa kwa kumwaga damu yake Takatifu. Ni katika muktadha huo ambapo Vijana Wakatoliki Wafanyakazi nchini Tanzania(VIWAWA), wametakiwa kumtanguliza Mungu kwa sala na kuendelea kuwa imara kama tawi la mtende na kuutunza ubichi wa kiroho katika maisha. Wito huo ulitolewa na Padre Patrick Tibangayuka, Gambera wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Anthony wa Padua Ntungamo Jimbo la Bukoba, Tanzania wakati wa homilia yake katika Dominika ya Matawi mnamo tarehe 2 Aprili 2023 katika Seminari Kuu ya Ntungamo Jimboni Bukoba.
Ubichi wa mwanadamu unatokana na sala na ibada mbali mbali
Katika tafakari yake Padre Tibangayuka alisema kuwa, kupitia sala na Ibada mbali mbali, kijana anautunza ubichi wa Kiroho kwa kuongea na Mungu na kumueleza yanoyomsibu kwa kupitia masifu na kusali Rozari Takatifu na kumtanguliza Mungu katika changamoto wanazopitia na kumhoji Mungu kwa imani. “Ubichi wa mwanadamu unatokana na kuwa na amani Rohoni, kijana kubaki katika Ubichi kunatokana na kuwa mtiifu kwa Mungu, kuzishika amri zake, kusali rozari na kutafakari na kuongea na Mungu ikiwemo kumhoji kwa imani, hivyo ninawaomba vijana mjenge imani kwa kuwa watu wa Mungu na kuzishika amri zake kikamilifu, kama wewe ni Frateli, fuata kiapo chako cha ufrateli, wewe ni Padre fuata kiapo chako, wewe uliye kwenye ndoa takatifu fuata kiapo chako kikamilifu na tufuate kwa yale yote tunayoelekeza”,alisema Padre Patrick.
Mtende ukinyauka unabaki umenyoka:vijana walishe neno la Mungu
Gambera wa Seminari Kuu Ntungamo aidha akiendelea na tafakari hiyo kwa kutumia ishara za mwanzo wa Juma Takatifu ambalo Liturujia imeweka kusheherekea siku hiyo ya Matawi, aliwataka vijana katika jamii kuiga mfano wa jani la mti wa mtende ambalo halipukutiki matawi yake linapokauka na linabaki limenyoka, kwa hiyo aliwasihi vijana kupokea maelekezo na kulishika neno la Mungu wakati huo huo wakijiombea wenyewe, viongozi wa Kanisa, Taifa na wazazi na kuwa kijana akipoteza ubichi angali kijana atajuta akiwa mzee.
Kamwe usikubali kutembea bila Rosari mfuko mwako
Padre Patriki alisema: “Tunawaomba vijana, mnapopokea maelekezo mkingali wabichi, mkipokea maelekezo ya wakubwa na kushika amri za Mungu na kulishika neno lake kwa wakati huu mkiwa bado wabichi, pamoja na kujiandaa vyema katika sala na ibada za kila siku kwa nia maalum na mkiwaombea wazazi wenu na taifa zima hata mkikua na kuzeeka, hamtapukutika kamwe, tenga muda wako usali Rozari takatifu, masifu pamoja na kutafakari makuu ya Mungu na aliongeza Padre Tibangayuka: “kamwe usikubali kutembea bila Rozari mfukoni mwako” Kwa kuhitimisha Padre Patrick alisema kuwa: “Formula ya kijana katika maisha ni moja, ukipoteza ubichi ungali kijana usitegemee uimara ukiwa mzee, kwani uimara wa uzeeni ni matokeo ya ubichi uliotunzwa wakati wa ujana, ndio maana tunawaomba vijana tunzeni ubichi wa kiroho kwa kuntegemea Mungu kwa kila jambo”, alihitimisha.
Juma Kuu Takatifu katika kutafakari mafumbo ya ukombozi
Katika mantiki ya Juma Kuu Takatifu, Mama Kanisa anaadhimisha: kuanzia Dominika ya Matawi, Alhamisi Kuu ya ambayo ni kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu la Upadre na huduma ya upendo kwa watu wote wa Mungu. Ijumaa Kuu, ni ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi Kuu, Kanisa zima, linakaa kimya kwa kutafakari mateso hayo, wakati likiwa na matumaini ya Kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Na hatimaye, Dominika ambayo ni Pasaka, siku ya Ufufuko wa Bwana.