Hungaria:Kasula ya maadhimisho wakati wa tukio la Ziara ya Kitume ya Papa!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu katoliki nchini Hungeria Jumatano tarehe 5 Aprili 2023 limetoa alama za na maana ya mavazi ya maadhimisho ya Ziara ya Kipapa nchini humo kuwa "kati ya tarehe 28 na 30 Aprili 2023, Papa Francisko atatimiza ziara yake ya kitume nchini Hungeria". Tukio litahitimishwa kwa maadhimisho ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa katika uwanja wa Kossuth ambayo itaongozwa na Baba Mtakatifu Dominika tarehe 30 Aprili 2023.
Vifaa vya kiliturujia, vilivyozalishwa na Desta, vimebuniwa na Sista Fecske Orsolya mchoraji wa Shirika la Watawa wa Kijamii kwa kuombwa na Baraza la Maaskofu wa Hungeria. Rangi zinazotawala za Kasula ni nyeupe na dhahabu ambapo zinaendana na utamaduni na maelezo ya kilirurujia ambayo yanajikita katika muktadha wa kipindi cha Pasaka. Kuhusiana na mavazi ya kiliturujia zaidi ya kasula, stola na mitra ni pamoja na Pluviale’ ya Papa na dalmatiki za mashemasi.
Mchoro unachukua kauli mbiu inayoongoza tukio la Ziara ya Kitume ya Papa isemayo: "Kristo ni wakati wetu ujao" na kwa namna nyingine hata jinsi ilivyo pambwa kimsingi wa Kasula ni ishara iliyowakilisha Kristo Mfufuka ambayo inaonesha mwanga katika weupe. Vile vile Mito miwili inatiririka kutoka moyoni mwake, ambapo kuna alama za maji na damu, ambazo zinapanuka hadi kuungana pamoja na kuwa mto mmoja. Picha ya mto huo unaingia kwa upya katika mto Danube, moja ya alama muhimu zaidi za nchi hiyo ya Hungeria na historia yake.
Zaidi ya hayo, inakumbusha pia alama za Kongamano la 52 la Kimataifa la Ekaristi Takatifu lililofanyika huko Hungaria mnamo mwaka 2021. Na zaidi rangi ya bluu nyepesi au maji ya mto inafanana na rangi ya anga inayoonekana juu ya Kristo mfufuka. Kwa upande wa rangi ya samawati nyepesi ni kama daraja kati ya dunia na anga na wakati huo huo inaweza kukumbusha pia sura ya Bikira Maria.