Tafakari ya Dominika ya Huruma ya Mungu: Kiri Kuu ya Imani: Bwana na Mungu Wangu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya Pili ya Pasaka Mdo. 2:42-47; 1Pet 1:3-9; Yn. 20:19-31. Itakumbukwa kuwa katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, dominika ya pili ya Kipindi cha Pasaka ilipewa jina la “Dominika ya huruma ya Mungu.” Hii ni kusisitiza juu ya huruma ya Mungu waliyoipokea waliobatizwa usiku wa Pasaka kama wimbo wa mwanzo unavyoashiri: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu, aleluya” (1 Pet. 2:2). “Pokeeni furaha ya utukufu wenu, mshukuruni Mungu aliyeita kwa ufalme wake wa mbinguni, aleluya” (Ezr. 2:36-37). Ndivyo sala ya Koleta inavyosisitiza ikisema; “Ee Mungu mwenye huruma ya milele, unawasha imani ya taifa lako katika Sherehe hii ya Pasaka. Uwazidishie hiyo neema uliyowajalia (wale waliobatizwa), wapate kuelewa vema kwamba wametakaswa kwa maji, wamepata uzima mpya kwa Roho, na kukombolewa kwa damu”. Itakumbukwa kuwa Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ndiye aliyeaminishwa kuidhihirisha huruma ya Mungu kwa maono aliyoyaona ya miali ya mwanga ya rangi nyekundu ikiwakilisha damu ya Kristo na rangi ya bluu hafifu ikiwakilisha maji ya ubatizo. Masomo ya dominika hii yamesheheni mafundisho msingi sana ya Kanisa - yanatuonesha jinsi nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, kiri kuu ya imani ya Mtume Tomaso kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, kuwekwa kwa sakramenti ya kitubio, ashirio la vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:42-47). Somo hili linatueleza jinsi jumuiya ya kwanza ya mitume walivyoishi maisha ya kikristo hivyo kuwa ni mfano bora kwa maisha yetu ya kijumiya. Kiujumla wakiwa chini ya uongozi wa mitume, wakristo wa mwanzo waliishi maisha ya ushirika: walipendana, walisaidiana, walisali na kushiriki Ekaristi Takatifu pamoja. Itakumbukwa kuwa ujumbe msingi wa kipindi chote cha Pasaka ni kuwa: Bwana mfufuka alijionyesha kwa jumuiya ya wakristo popote walipokusanyika kama familia moja, aliwaangazia, aliwalisha, aliwaongoza na kuwalinda kwani wao walikuwa ishara ya Kanisa lake. Ni uwepo huu wa Yesu mfufuka kati yetu unaofanya maisha yetu ya kikristo kuwa pasaka inayoendelea. Wakristo wa mwanzo walielewa jambo hili vyema kila wakati walipokutana kuadhimisho fumbo la ukombozi, yaani pasaka, dominika baada ya dominika kwa mwaka mzima ambapo uwepo wa Yesu ulijidhihirisha kwa ishara na alama mbali mbali (Mdo 1:3). Kumbe licha ya matatizo yaliyojitokeza katika maisha ya jumuiya ya kwanza ya wakristo, imani kwa Kristo mfufuka iliwapa nguvu ya kuyashinda. Nasi tunapaswa kuiga mfano wao ili tuweza kupata nguvu za kupambana na mwovu na matatizo yanayotusulubu katika maisha. Somo la pili ni la barua ya kwanza ya Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 1:3-9). Katika somo hili Mtume Petro anawatuliza wakristo waliokuwa wanadhulumiwa sababu ya Imani yao kwa Kristo. Anawasihi akiwaambia kuwa ufufuko wa Yesu ni msingi wa matumaini yao ya kupata heri ya mbinguni. Matatizo na madhulumu wanayoyapitia ni kama vile dhahabu inavyopitia katika moto makali ili ubora wake udhihirike. Hata sisi tunaaswa kuufurahia ufufuko wa Kristo hata ikibidi kuteseka, maana hakika mwishoni tutapata heri na utukufu kwa Mungu.
Injili ilivyoandikwa na Yohani (Yn 20:19-31) tunayoisoma katika dominika ya pili ya Pasaka imegawanyika sehemu kuu tatu: Katika sehemu ya kwanza (20:19-25) - Yesu mfufuka anawatokea wanafunzi wake wakati Tomaso hayupo na kuweka Sakramenti ya kitubio. Katika sehemu ya pili (20:26-29) – Yesu Mfufuka anawatokea wanafunzi wake na Tomaso akiwepo naye anakiri kiri kuu ya imani. Na sehemu ya mwisho ni 20:30-31 inadokeza vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa nje na Maandiko Matakatifu – Biblia. Yesu Mfufuka ni mjumbe wa Amani. Hii inajidhihirisha katika maneno yake ya kwanza kila alipowatokea wanafunzi wake akisema; “Amani iwe kwenu”. Kisha kuwasilimu anawatuma kwa kuwaambia; “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi”. Mwinjili Matayo anasema; “Enendeni ulimwenguni mwote mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba na la mwana na la Roho Mtakatifu” (Mt. 28:18-20). Marko anasisitiza; “Fundisheni kuyashika yote niliyowaamuru ninyi aaminiye na kubatizwa ataokolewa, asiyeamini atahukumiwa” (Mk. 16:15-16). Yohane anaendelea kusisitiza; “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yn.20:22-23). Huu ni udhibitisho wa kuwekwa kwa sakramenti ya upatanisho, sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya ondoleo la dhambi na mamlaka waliyopewa mitume ya kutuondolea dhambi. Hivyo hatunashaka juu ya mamlaka haya ambayo mapadre wamepokea kutoka kwa mitume. Mwenye mashaka na asiyeamini atahukumiwa, bali aaminiye ataokolewa.
“Bwana wangu na Mungu wangu” (Yn. 20:28) ni kiri ya Kuu ya Imani ya Mtume Tomaso aitwaye pacha kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli. Tomaso mwanzoni hakuamini kuwa Kristo amefufuka na amewatokea wenzake akisema; “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo” (Yn.20:25). Yesu alipowatokea mara ya pili naye akiwapo alimwambia; “Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye” (Yn.20:27). Tomaso akajibu, akamwambia; “Bwana wangu na Mungu wangu”! Yesu akamwambia, “Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yn. 20:29). Kumbe tunaona kuwa Imani haipatikani katika kile mtu anachoona kwa macho. Mtu hawezi kuthibitisha yale tunayoaamini kwa kutuletea vithibitisho vya kisayansi. Mtu anayetaka kuona, kugusa, kuonja na kuhisi hawezi kuwa mtu wa imani. Yesu anasema wamebarikiwa wale wasioona lakini wakaamini kwa sababu imani yao ni ya kweli, safi – isiyo na mashaka, tena ni ya kudumu. Kumbe, tunaona kuwa katika sehemu ya kwanza na ya pili katika injili hii na katika somo la kwanza linalohusu jumuiya ya kwanza ya wakristo, ni katika jumuiya tunakutana na Yesu mfufuka. Tomaso alipokuwa nje ya jumuiya hakumuona Yesu, na aliporudi ndani ya jumuiya alimuona na kukiri wazi “Bwana wangu na Mungu wangu”. Na ni katika jumuiya ya waamini wa Kanisa la kwanza nguvu za Yesu mfufuka zilijidhihirisha kwa njia ya mitume. Ni katika maadhimisho ya kiliturujia ndipo tunapokutana na Yesu kwa njia ya sakramenti na neno la Mungu.
Sakramenti na Neno la Mungu ni mali ya Kanisa – mwili wa Kristo. Hivyo tunalihitaji Kanisa ili tukutane na Yesu. Paulo anauliza: “Wataliitaje jina lake yeye ambaye hawamwamini? Na watamwaminije yeye ambaye hawajawahi kumsikia? Na watasikiaje kama hakuna mhubiri?” (Rom 10:14). Kwa hiyo, tunahitaji jumuiya ili kusikiliza mahubiri na mafundisho ya imani. Ni katika jumuiya Kristo anakutana nasi. Jumuiya ya Wakristo wa Kwanza ni mfano wa kuigwa kwa jumuiya zetu. Wajibu wetu ni kuzifanya jumuiya zetu ziwe kweli ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni. Watu wamtambue Kristo katika jumuiya zetu. Kama kuna shida yoyote katika jumuiya suluhisho si kujitenga na jumuiya bali ni kutatua matatizo hayo. Je, upo ndani ya jumuiya? Kama haupo ingia sasa, jiunge na jumuiya, jiunge na vyama vya kitume, shiriki katika shughuli za Kanisa ili ukutane na Yesu Mfufuka upate neema na baraka tele. Sehemu ya mwisho ya Injili ya dominika hii (Yn. 20:30-31) inatujulisha kuwa kuna vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa. Kanisa Katoliki lina vyanzo vikuu vinne vya mafundisho yake ambavyo ni Bibilia Takatifu, mapokeo kutoka kwa mitume, mababa wa imani na mitaguso ya Kanisa. Bibilia sio chanzo pekee cha mafundisho ya Kanisa maana sio yote aliyoyafanya Kristo yameandikwa katika Biblia – “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake” (Yn. 20:30-31).
Habari ambazo Yohane anasema hazijaandikwa katika Bibilia ni mafundisho mengine ya Kanisa ambayo tunayapata katika Mapokeo kutoka kwa Mitume, Mababa wa Imani na Mitaguso ya Kanisa. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho msingi ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Bibilia Takatifu kwani hayo tunayapata katika vyanzo hivyo vingine. Kumbe, basi maisha ya mkristo yanapaswa daima kuwa maisha ya pasaka. Bwana mfufuka anajifunua kwetu wakati wote. Kuwa na imani katika Bwana mfufuka inamaanisha kujikabidhi kwake na kwa mpango wake wa upendo kwetu katika kila hatua ya maisha yetu. Tukumbuke daima kuwa imani kwa Kristo inaleta msamaha, amani na furaha. Basi imani yetu kwa Bwana mfufuka itusaidie kujenga jumuiya za kikristo ambapo ndiyo Kristo ndiye kiongozi wake. Ziwe ni jumuiya zisiyo na ubinafsi, zinayojali maskini na ni jumuiya zinayozingatia sala. Ni katika jumuiya ya namna hii Bwana mfufuka anajifunua, ni katika jumuiya ya namna hii Bwana mfufuka anatukirimia baraka na neema zake. Tumsifu Yesu Kristo.