Dominika ya Huruma ya Mungu: Miaka 25 ya Kardinali Pengo na Miaka 5 Kituo cha Kiabakari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kama sehemu ya Maadhimisho ya Sherehe ya Huruma ya Mungu, inayofikia kilele chake Dominika tarehe 16 Aprili 2023, Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma, kinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka mitano tangu kilipopandishwa hadhi na kuwa ni Kituo cha Hija Kitaifa. Ni katika muktadha huu, Kituo pia kinamshukuru Mungu kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alipoteuliwa na kusimikwa rasmi kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 21 Februari 1999, Tanzania ikaweka historia ya kupata Kardinali mpya katika kipindi cha miezi michache tu, tangu alipofariki dunia Kardinali Laurian Rugambwa. Katika kumbukizi hii, tutagusia kuhusu: Umuhimu wa madhabahu kama kitovu cha uinjilishaji mintarafu Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma. Kumbukizi ya Miaka 25 tangu Kardinali Polycarp Pengo aliposimikwa kuwa Kardinali sanjari na mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania katika ujumla wake. Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho: Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao!
Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana: huruma, upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao! Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima, tayari kujielekeza katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kuzidimisha upendo kwa Mungu na jirani!
Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa, unaoganga na kuponya! Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika mkutano wake wa tarehe 21 Juni 2018, liliridhia ombi lililowasilishwa na Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma na kukipandisha hadhi Kituo cha Huruma ya Mungu Kiabakari kuwa sasa ni Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwamba, Kituo hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania katika mchakato wa kuimarisha imani, malezi na majiundo makini, kwa wale wote wanaokimbilia na kuzama katika “Bahari ya huruma ya Mungu.” Ndoto hii, ilifikia hatima yake, hapo tarehe 3 Oktoba 2018, wakati Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania wakati wa ziara yake ya kichungaji Jimbo Katoliki Musoma alipozindua kituo, kwa kushirikiana na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma. Katika mahubiri yake, alimshukuru na kumpongeza sana PadreWojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, na muasisi wa Parokia na Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, chemchemi ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.
Huyu ni mmisionari kutoka Jimbo kuu la Krakow, Poland, mahali wanapotoka Mtakatifu Yohane Paulo II na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma; Mitume wakuu wa Huruma ya Mungu. Ibada hii imemsaidia sana katika maisha na utume wake kuweza kueneza Ibada ya huruma ya Mungu, leo hii Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma kimekuwa ni kitovu cha huruma ya Mungu nchini Tanzania. Askofu mkuu Marek Solczyn’ski alisema hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume kwenye mji mkuu wa Vilnius, nchini Lithuania, mahali ambako Sr. Faustina kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alisali Rozari Takatifu ya Huruma ya Mungu na kuchora Picha ya Yesu wa Huruma. Kumbe, wajibu, dhamana na utume wa Mama Kanisa ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumfungulia njia inayompeleka kwenye wokovu na maisha ya uzima wa milele. Haya ni matunda ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu. Kwa njia ya Kristo Yesu watu wamekombolewa kwa kuoshwa dhambi zao kwa Damu Azizi. Kumbe, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Upatanisho, Kanisa linawashirikisha watu matunda ya Sadaka iliyotolewa na Kristo Yesu pale Msalabani. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha na kwamba, huruma ndiyo sifa yake kuu. Damu Azizi ya Kristo Yesu iwaletee watu msamaha wa dhambi na hivyo kuwakirimia maisha ya uzima wa milele. Changamoto kubwa kwa waamini ni kuondokana na ubaridi wa maisha ya kiroho, unaoendelea kusababisha mateso makali kwa Kristo Yesu. Waamini wanashauriwa kukimbilia mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu kwa: imani, uchaji na ibada.
Amri za Mungu na mashauri ya Kiinjili yawe ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo ili Mwenyezi Mungu apewe sifa na mwanadamu aweze kutakatifuzwa na kukombolewa. Waamini waendelee kumtumainia Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma baada ya kukumbana na kashfa ya Msalaba, akabahatika kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu. Waamini wajenge moyo wa Ibada, Imani na Uchaji wa Mungu kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuondokana na ibada za mazoea. Kwa njia hii, wataweza kutakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo na kushirikishwa Mkate wa uzima wa milele. Kituo cha Hija cha Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, kiwe ni mahali pa sala na chimbuko la huruma ya Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Sista Faustina na Mtakatifu Yohane Paulo II, Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu, wawaombee wote ambao mahali hapa patakatifu watamsihi Mungu msamaha wa dhambi zao na kushika njia ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 huko Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Juni 1971 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Na kwa kipindi cha miaka miwili yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1973 aliteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1977 alitumwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa la Lateran, Kitivo cha Taalimungu Maadili cha Alfonsianum, kilichoko mjini Roma. Aliporejea nchini Tanzania baada ya kuhitimu masomo yake, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenda kufundisha taalimungu maadili Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.
Kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1983 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Gambera na muasisi wa Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika, Kanisa la Tanzania linajivunia Seminari ya Segerea, matunda ya jasho na ubunifu wa Kardinali Polycarp Pengo. Tarehe 11 Novemba 1983 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na kuwekwa wakfu wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 1984 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Mtakatifu Yohane Paulo II. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Nachingwea hapo tarehe 19 Februari 1984. Tarehe 17 Oktoba 1986, akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lengo likiwa ni kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini katika kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Akasimikwa rasmi tarehe 12 Februari 1987. Tarehe 22 Januari 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuingia Jimboni tarehe 24 Mei 1990. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 12 Februari 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na kumsimika rasmi tarehe 21 Februari 1999. Tanzania ikaweka historia ya kupata Kardinali mpya miezi michache tu baada ya kufariki dunia, Kardinali Laurian Rugambwa. Tarehe 2 Septemba 1990 wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Tanzania, Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu mwandamizi, ndiye aliyetoa hotuba, wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa anazungumza na wakleri pamoja na watawa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alikazia kwa namna ya pekee uaminifu na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ari na mwamko wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.
Tarehe 12 Aprili 1994, Kardinali Pengo alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika na kukazia umuhimu wa waamini kumwilisha imani yao kila siku ya maisha kama ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu! Kardinali Pengo alishiriki katika mkutano wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya kumchagua Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Machi 2013. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Kardinali Polycarp Pengo, akang’atuka kutoka shughuli za uongozi Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa ufupi, hii ndiyo historia ya Kardinali Polycarp Pengo ambayo imeandikwa kwa jasho, uvumilivu na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!