Tafuta

Fumbo la mateso na kifo linapata mwanga wake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; alfa na omega; mwanzo na mwisho. Fumbo la mateso na kifo linapata mwanga wake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; alfa na omega; mwanzo na mwisho.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika V ya Kipindi cha Kwaresima: Kifo, Ufufuko na Uzima wa Milele

Injili inasimulia kufufuliwa kwa Lazaro ishara kuwa katika Ubatizo, Kristo anatufufua kutoka mauti ya dhambi na kutupatia uzima mpya wa Kiroho ndani mwetu na maisha mapya kama wana wa Mungu. Kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo ya dominika hii, ni vyema tujikumbushe haya; Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima, zinatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo mema na kuwahudumia wahitaji. Imani!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya tano ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Katika dominika hii kuna mambo makuu mawili ya kuzingatia. Kwanza, kadiri ya utamaduni na Mapokeo ya Kanisa, kuanzia Dominika hii misalaba inafunikwa, mpaka ijumaa kuu wakati wa kuadhimisha mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa, mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya Pasaka. Pili, kadiri ya mpangilio wa Injili za mwaka A wa kiliturjia kuanzia domenika ya 3A tulipoanza matakaso matatu ya wakatekumeni, dominika hii ya 5A ya Kwaresima linapoadhimishwa takaso la tatu na la mwisho, Injili inasimulia kufufuliwa kwa Lazaro ishara kuwa katika Ubatizo, Kristo anatufufua kutoka mauti ya dhambi na kutupatia uzima mpya wa Kiroho ndani mwetu na maisha mapya kama wana wa Mungu. Kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo ya dominika hii, ni vyema tujikumbushe haya; Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima, zinatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo mema na kuwahudumia wahitaji. Dominika ya 5 ni siku 33 ya kipindi hiki na zinabaki siku 7 kuingia juma kuu linalofunguliwa na jumapili ya matawi. Ni mda mwafaka kujitafakari na kujiuliza: Je, ile dhambi ninayoipenda nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu kwaresma ianze, ni nini nilichojinyima kwa ajili ya wahitaji kwa siku hizi 33 tangu kwaresma ianze? Katika wimbo wa mwanzo mzaburi anasali; “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe Mungu uliye nguvu zangu” (Zab.  43:1-2). Sala hii ina maana kwa yule ambaye siku hizi 33 zimemfanya awe karibu zaidi na Mungu kwa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo ya huruma.

Dominika 5 ya Kwaresima: Misalaba an Sanamu zinafunikwa.
Dominika 5 ya Kwaresima: Misalaba an Sanamu zinafunikwa.

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 37:12-14). Katika somo hili, Nabii Ezekieli anahusianisha uhamisho wa Babeli kwa waisraeli kama kifo cha Taifa teule na kwamba taifa zima lilizikwa. Mungu kwa huruma na upendo wake anaahidi kuwafufua Waisraeli, yaani kuwarudisha katika nchi takatifu. Ukombozi huo ni mfano wa ufufuko wa miili yetu siku ya mwisho. Waisraeli walipelekwa uhamishoni Babeli kwa dhambi zao. Walipotambua makosa yao na kuyatubu, walimlilia Mungu kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyoimba; “Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia, Bwana, usikie sauti yangu. Masikio yako yaisikilize sauti ya dua zangu” (Zab. 130). Walitambua kuwa; “Kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi” (Zab. 130:7). Mungu kwa huruma yake akasikia kilio chao, hakuyahesabu maovu, akawasamehe. Ndipo akamtuma Ezekieli kuwapa habari hii ya matumaini ya kutolewa katika makaburi yao, kutolewa utumwani na kurudishwa tena katika nchi yao. Ndivyo inavyokuwa kwetu tunapotenda dhambi, tunakuwa kama wafu ndani ya makaburi, kwani dhamiri na nafsi zetu zinakuwa chafu mfano wa uchafu ulio ndani ya kaburi. Kutubu dhambi zetu ni sawa na kufufuliwa na kuvalishwa utu mpya. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:8-11). Katika somo hili mtume Paulo anatukumbusha kuwa, shauku ya dhambi hutokana na mwili. Matendo mema yanayompendeza Mungu hutokana na Roho Mtakatifu tuliyempokea katika Ubatizo. Basi tumfuate Roho huyo ili tumpendeze Mungu, naye Roho Mtakatifu atatufufua siku ya mwisho na kutufanya tuwe watu wapya. Wakati wa mwisho ni upi na unakuja lini? Hakuna anayejua siku wala saa basi tuwe tayari mda wote. Tumrudie Mungu mapema iwezekanavyo, kila tunapomkosea na kumwomba msamaha.

Ubatizo ni chemchemi ya maisha mapya
Ubatizo ni chemchemi ya maisha mapya

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn 11:1-45).  Sehemu hii ya injili inahusu simulizi la kufufuliwa kwa Lazaro. Katika tukio hili kuna mambo manne ya kuzingatia; Urafiki wa kweli wa Yesu na Lazaro pamoja na dada zake Martha na Maria, Imani thabiti ya Martha na Maria juu ya ufufuo na uzima wa milele, dhamani ya uhai wa mwanadamu uliodhihirishwa kwa uchungu mkubwa aliokuwa nao Yesu kwa kifo cha rafiki yake Lazaro hata kulia kwa huzuni kama binadamu wengine, na nguvu ya sala ya Yesu kwa Mungu Baba. Ni wazi kifo kinatisha na kuogopesha kwani kinakatisha furaha ya maisha ya sasa. Kifo kinatunyang’anya uhai, tunu aliyotujalia mwenyezi Mungu. Lakini kwa imani tunasaidiki kuwa kifo si mwisho wa maisha ila ni daraja la kuelekea uzima wa milele. Kifo na kuhuishwa au kurudishiwa uzima tena kwa Lazaro kunatuambia kuwa mtu hawezi kuishi milele isipokuwa kwa njia ya Kristo mwenyewe, kwani yeye mwenyewe anasema; “Mimi ndimi ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuamini hatakufa kabisa hata milele.” Ni hulka ya binadamu kupenda kuishi, na kuogopa kufa hata mzee mwenye zaidi ya miaka zaidi ya 100, bado angependa kuendelea kuishi. Hamu hii ya kutaka kuendele kuishi imepandwa na Mungu ndani mwetu kwanza wakati wa uumbaji wa Adamu na Eva na sasa siku ya kutungwa mimba kwa kila mmoja. Hii hamu haiwezi kamwe kukamilishwa kwa maisha ya hapa duniani mpaka pale tutakapomuona Mungu aliye asili ya maisha yetu. Ndiyo maana Mtakatifu Augustino wa Hippo aliweza kusema; “Ee Mungu umetuamba kwa ajili yako na Roho zetu hazitatulia kamwe mpaka pale zitakapo kuona wewe”. Lakini hata hivyo tunawajibika kama mama Kanisa anavyotufundisha katika nyaraka mbalimbali zinazohusu thamani ya uhai; kuuheshimu, kuulinda na kuutunza uhai ambayo ni tunu ya pekee aliyotujalia mwenyezi Mungu. Tunapaswa kujitunza kwa kujilisha na kujivika, kutafuta tiba tunapougua, kujihami na kujilinda panapotokea hatari yoyote ile kwa kutumia njia halali.

Ufufuko nwa Kristo Yesu ni chanzo cha matumaini
Ufufuko nwa Kristo Yesu ni chanzo cha matumaini

Tunu hii ya uhai ni ya milele. Kwa dhambi ya asili, dhambi ya Adamu na Eva kukosa utii kwa Mungu, kifo kiliingilia maisha kama adhabu. Lakini kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kifo chetu sio tena adhabu bali ni njia ya kuufikia uzima wa milele kama Yesu mwenyewe anavyosema; “Nalikuja ili muwe na uzima tena muwe nao tele”. Na kabla ya kumfufua Lazaro alisema; “Mimi ndimi ufufuo na uzima”. Lakini kuupata huo uzima wa milele, sharti ni moja, kumwamini Kristo Yesu; “Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi, naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa.” Basi tunapokaribia kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, tumruhusu Yesu aingie na tumpatie nafasi akae ndani mwetu kwa neno lake, na sakramenti zake, tujenge unafiki naye kama wa Lazaro, Maria na Martha sio tu kwa Yesu lakini pia kati yetu sisi kwa sisi katika raha na taabu. Tuwe na Imani dhabiti kama ya Martha na Maria, na tujivunie kuwa tukiwa karibu na Yesu hakuna litakaloshindikana. Tudhamini uhai wetu na wa wengine, tudhamini maisha yetu na ya wengine, tuone uchungu pale tunapoona mwenzetu ananyimwa haki ya kuishi kwa namna yoyote ile na kumtetea. Tuone uchungu kama Yesu alivyoona uchungu kwa kifo cha rafiki yake Lazaro na kumlilia. Kulia kwa Yesu kwa huzuni kubwa ni kutuonesha kuwa kifo kamwe siyo sehemu ya mpango wa Mungu, bali ni kwa sababu ya dhambi kifo kiliingia katika historia ya Maisha ya mwandamu. Kulia kwake ni kutuonyesha ushiriki wake katika huzuni ya dhambi ya mwanadamu. Basi tutumie vema muda huu mfupi uliobaki kabla ya Pasaka tumlilie Mungu kwa huzuni kuu, tuone uchungu wa dhambi zetu, tumshukuru Mungu kwa neema anazotujalia kisha tumwite naye atatuitikia ili siku ya Pasaka tuweze kufufuka pamoja Kristo na tutoke makaburini na kuingia katika uzima mpya. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Dominika 5 Kwaresima

 

25 March 2023, 08:25