Padre Agapito Mhando alikuwa na juhudi ya kichungaji!
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Askofu Andrea Migliavacca wa Jimbo katoliki la Arezzo-Cortona-Sansepolcro, nchini Italia aliongoza misa ya mazishi ya Padre Agapito Batholomeo Mhando aliyeaga dunia tarehe 18 Februari 2023 katika Parokia ya Mtakatifu Egidio, huko Orciolaia, Arezzo, Italia. Misa hiyo iliudhuriwa na waamini wa parokia, makuhani wa jimbo hilo na wengine waafrika kutoka sehemu mbali mbali za majimbo, wakiwemo baadhi ya wawakilishi wa Jumuiya ya Watanzania Roma. Baada ya misa mwili ulipelekwa kwenye makuburi ya mji wa Arezzo. Kwa wengi wasiojua ni kwa nini hakurudishwa Tanzania, ikumbukwe tayari Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo la Morogoro, tarehe tarehe 21 Februari 2023 katika taarifa iliyotolewa aliandika kuwa “Nimefanya jitihada kubwa za kuurudisha mwili wake hapa Tanzania kwa ajili ya mazishi lakini imeshindikana kwa sababau alijiunga na Jimbo la Arezzo (Incardinated in Arezzo Diocese)…”. Kwa hiyo basi ndugu msomaji wa makala hii kwa mujibu wa kipengele cha usajili au inkadinisheni ya waklero kuanzia (n.265-272) kutoka katika kitabu cha Mkusanyo wa Sheria za Kanoni, kinafafanua wazi juu ya Mklero/watawa wa mashirika/ ambaye anahama kutoka Kanisa mahalia kwenda jingine kwa mujibu wa sheria halali, na katika suala la Padre Agapito alikuwa tayari ni mwanajimbo halali la Arezzo.
Katika mahubiri yake Askofu Migliavacca, kwa kuongozwa na Injili iliyosomwa kuhusu kifo cha Yesu, Msalabani alisema: “Daima kuna hali ya maswali mengi ya huzuni na kujiuliza kwa kina, sababu gani ya kifo, aina fulani za kifo, mbele ya kifo, maana ya kifo, maana ya maisha, maana ya kuteseka, na maana ya uhusiano na kile ambacho kimefanyika au labda kile ambacho hakikufanyika”. Tuhisi wote, kuwa karibu na Msalaba wa Yesu kama Injili ilivyosema, kwamba walikuwa karibu na chini ya msalaba Mama yake Yesu, dada yake, mama wa Kleofa na Maria Magdalena. Injili inasema kuwa, Yesu aliinamisha kichwa akakabidhi roho. Mbele ya kifo, sisi sote tuko mbele ya Msalaba. Hali halisi inakuwa kama ile ya uchungu wa kuondokewa, lakini katika sura ya Injili kwenye janga kama hili, inatukabidhi zawadi ya neno, matumaini na mwanga; na katika kifo hicho cha Yesu juu ya msalaba, ndimo yatazaliwa maisha, utazaliwa upendo kama Yesu anavyoelekeza kwa Maria na mwanafunzi mpendwa kwamba: “Mama tazama mwanao” na kwa Mwanafunzi: “tazama huyo ni mama yako”.
Chini ya Msalaba, huo husiano mpya ni upendo, upendo wenye uwezo wa kuzaa maisha milele. Upendo unaohifadhi maisha, kwa hiyo mbele ya kifo cha Padre Agapito, mshangao wetu wote unafanana kama ule wa “wote walikuwa chini ya Msalaba wa Yesu”. Lakini Neno lake alilotamka akiwa msalabani, hata kwa sisi na kwa Padre Agapito ni Neno la Uzima, ni neno la upendo. Yesu akiwa msalabani anatuelekeza njia ya kusoma matukio yote hata tusiyopenda ya maisha, hata kifo cha Padre Agapito katika mtazamo wa upendo, wa Mungu anayependa ambaye haachi wakati wa kifo, hata kile cha ajabu ambacho kinaweza kutokea, Mungu hamwachi mtu. Kila kifo kilicho kumbatiwa na Msalaba wa Yesu, kimekumbatiwa na upendo, na hakiwezi kisizalishe maisha. Kifo cha Padre Agapito kinakutana kwa hiyo na mkumbatio wa Msulubiwa, wa yule ambaye ni mwenye utajiri wa huruma, na mkumbatio huo, unapokea moyo wake nyumbani mwake, katika ufalme wa maisha wa mpendwa wetu Padre Agapito. Chini ya Msalaba kwa hiyo tupo sisi na kuna hata Jumuiya nzima ya Parokia ya Orciolaia, “Ninajua mateso yenu ninyi nyote, ninaweza kuwa sauti tu ya kutangaza kwamba kutoka katika msalaba, kwetu sisi, kwenu ninyi wa Orciolaia, kuna mkumbatio ule wa faraja na zawadi ya matumaini, ya mwanga ambao unapaswa kuwasindikiza katika uhakika, jimbo, hata mimi, nitawasindikiza”.
Chini ya Msalaba, karibu na msalaba, kuna ukleri wote wa Jimbo, makuhani wa jimbo, na wengi waliwakupo, na aliwashukuru Askofu. Akiendelea alisema: “Sisi sote katika mkumbo kwa kina na maombolezo haya, lakini wote kwa kuhifadhiwa na imani na matumaini, Yesu Msulibiwa anatualiki sote, anabariki ukweli mzima na kutufariji na manukato yake ya upendo. Chini ya Msalaba kuna familia yake Padre Agapito hata Jumuiya nzima ya kikuhani ya Watanzania ambao siku hiyo walikuwa hai, “walinitafuta kwa ajili ya rambi rambi zao. Kwao wote, tunawaonesha ukaribu wetu,sala zetu ambao misa hii hiko live wanafuatilia, na tunasali pamoja nao”. Baba Askofu akigeukia, somo kutoka kitabu cha Yeremiah, alisema anayesimulia wito wa nabii ni simulizi ya kijana aliyeitwa na Mungu na yeye akatumwa, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni mwa mama yako, nalikutakasa. Mtu huyo Nabii ana hofu kubwa, anayo maswali mengi na udhaifu mwingi, hadi kufikia Mungu anamsihi na kumwambia asiogope, kwa sababu “mimi niko pamoja nawe, ili kukulinda”. Neno la Mungu linaendelea kueleza kuwa “ Mimi ninakuweka maneno yangu katika kichwa chako”. Kwa hiyo kurasa za Yeremiah, kuhusu wito wake, zinatualika kutazama maisha kama uzoefu mkubwa ambao kuna kujipyaisha na kuitwa kwa Mungu. Na kuitwa kwa upande wa Mungu tangu kuzaliwa kwetu kutoka umbu la mama, hata maisha ya Padre Agapito ni ya kujieleza kama miito mingi ya Mungu.
Akiendelea Baba Askofu Migliavacca, alitoa wasifu wake kwamba, Padre Agapito alizaliwa mnamo tarehe 15 Desemba 1972 katika Jamhuri ya Muungano Tanzania. Alipewa daraja la ukuhani mnamo tarehe 17 Septemba 2003, baada ya mafunzo yake Jijini Roma na kupata digree ya Taalimungu ya Kichungaji, wakati huo huo akitoa hata huduma yake katika kipindi kimoja cha idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. Alipokelewa katika Jimbo la Arezzo 2015. Katika Kanisa mahalia, Padre Agapito alianza huduma yake katika Umoja wa Kichungaji wa Mashariki ya Casentino hadi 2017, na baadaye 2018 baada ya muda mfupi katika Kanisa la huko Sansepolcro, alikuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Msalaba Mtakatifu huko Arezzo. Na hatimaye mnamo mwezi Juni 2021 alikuwa ameteuliwa kuwa msimamizi wa Parokia ya Mtakatifu Egidio huko Orciolaia, akisaidiwa na Padre Silvano Paggini. Kifo chake kimeacha bila maneno na uchungu mkubwa kwa waamini wa Orciolaia ambapo kama alivyosisitiza Askofu wa Jimbo hilo kwamba walimpokea vizuri kwa wema na walipata kumpongeza kwa ukarimu wake, tabasamu lake, na hata jumuiya mbali mbali za Jimbo mahali ambapo Padre Agapito alihudumia shughuli zake cha kichungaji, ikiwa ni pamoja na makleri wote wa Jimbo.
Askofu katika mahubiri hayo alisisitiza kuwa "Alijitoa bila kujibakiza katika shughuli zake za kichungaji. Padre Agapito alikuwa mpole, myenyekevu, wa kujenga urafiki, mwenye uwezo wa kusikiliza. Hadi kufikia siku hizi, wamemsimulia mengi kuhusu tabia yake ya tabasamu, la kukaribisha, la heshima, tabasamu la kushirikisha safari ya maisha. Yeye alikuwa hivyo kwa sababu, kwa miezi michache, walijifunza kumjua na kumpenda. Yeye alikuwa ni mwema, kuhani ambaye kila wakati alijibidhisha katika maisha ya jimbo, mtembeaji na tabasamu huku akisindikizwa na Jumuiya Padre Agapito kiukweli alikuwa kuhani wa huduma wa jimbo, akonekana na roho ya utii na sadaka, hata katika ugumu, lakini kwa kutembea yeye mwenyewe, uwezekano wake na upole wa roho yake ya mchungaji."
Simulizi hizi zilisindikizwa na shukrani kubwa na uchungu lakini wa kuondokewa naye. Yote haya lakini ya safari ya Padre Agapito yanaonekana sasa kufuatilia na kujipyaisha miito yote ya Mungu na mojawapo wa miito hiyo hata awamu za maisha yake ni Mungu anayeita akitoa imani, akisindikiza na kuingilia kati katika mchakato aliouanzisha. “Kwa hiyo hata kifo kinaishi wito wa Mungu. Tunaamini, kwamba hata kifo cha Padre Agapito kitakuwa kimekumbana kifumbo na Mungu ambaye kwa upya anaita daima, anaita wito kwa upendo”. Askofu amefikiria na kusema kuwa wakati wa mateso ya maisha ya kuhani wetu atakuwa alimwambia: “Padre Agapito usiwe na hofu kwa sababu mimi niko pamoja nawe ili kukulinda. Ni neno lililojaa huruma hata katika anguko la maisha, hata katika umaskini wetu, kwa sababu Mungu anatutazama tu kwa kutupenda, na ndivyo hivyo mtazamo wa Mungu kwa Padre Agapito, alimpenda yeye tu daima”. Kwa kuhitimisha Askofu Andrea: “Safari njema Padre Agapito, hacha ukumbatiwe na upendo usio na mwisho wa Mungu”.
Wakati wa kutangaza juu ya kifo chake kwa mapadre, mashemasi, na waamini, Askofu wa Jimbo hilo la Arezzo-Cortona-Sansepolcro, Andrea Migliavacca aliandika kuwa “katika sala zetu, tumsindikize sasa kwa upendo ule ule na kujitoa kule kule ambako alikaribishwa na kufuatia kwa miaka hii hadi siku zake za mwisho, katika jumuiya zetu, na za makuhani ambao walishirikiana naye, na kumkabidhi kwa imani katika mkumbatio wa huruma wa Bwana.” Askofu huyo alihakikishia ukaribu wake kwa familia ya padre aliyeaga dunia, kwa parokia ya Orciolaia, na Jumuiya nyingine na mapadre wote wa Jumuiya kwamba: “Niko karibu nanyi nyote, ninashirikisha masikitiko na rambirambi. Maombi na kumtumainia Mungu utusaidie”. Padre Agapito Mhando,umetuachia pengo kubwa, idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican na Kiingereza Afrika. Roho yako ipumzike kwa Amani. Amina.