Wamisionari wa kwanza wa Consolata kwenda Afrika Wamisionari wa kwanza wa Consolata kwenda Afrika 

Tanzania:Miaka 100 ya utume wa Wamisionari wa Consolata!

Ni kusheherekea Mungu wa Utume,katika miaka 100 ya uwepo wa utume wa kimisionari wa Shirika la Consolata huko Iringa Tanzania.Ndivyo wanasema wakuu wa shirika hilo,wakielezea umuhimu wa utume wao kuwa wanaadhimisha Mungu wa utume na hija kila wakati katika njia na kutoka nje ili kufikia kila kiumbe wake.

Na Angella Rwezaula; - Vatican.

Ni nini maana ya kusheherekea miaka 100 ya uwepo wa Shirika la Wamisionari wa Consolata nchini Tanzania? Je wanaadhimisha Nini? Na je wanaadhimisha na Nani? Ni maswali  ambayo yameelezwa na kujibiwa na Sr. Simona Brambilla, Mkuu wa Shirika la Consalata wa Kike na Sr. Maria Michela Astegiano, katika fursa ya Jubilei hiyo muhimu ambayo imewaona katika jitihada kubwa kwa muongo mmoja huku wakihudumia huko Iringa nchini Tanzania. Katika taarifa iliyotolewa na Shirika la habari za Kimisionari Fides, Mama wakuu hao wamejibu maswali hayo wakibainisha kwamba:  “Tunamsherehekea Mwenyezi Mungu wa Utume, Mungu ambaye yuko katika hija mara kwa mara, njiani, akitoka nje kutafuta na kuwafikia kila kiumbe chake na kuwafunika kwa  mkumbatio wa Upendo wake mwororo, wenye nguvu na huruma."

Maadhimisho ya miaka 100 ya wamisionari wa Consolata Tanzania
Maadhimisho ya miaka 100 ya wamisionari wa Consolata Tanzania

Kusheherekea Mungu chanzo cha utume

Masisita hao, katika maelezo yao wamesema kuwa “Katika miaka hii mia moja hatujisherehekei sisi wenyewe, Wamisionari wa Consolata, bali kwake Yeye, ambaye ni Chanzo cha Utume.” Katika mchakato wa maadhimisho ya Misa Takatifu ya kutoa shukrani, kubwa kwa Mungu iliyofanyika mnamo tarehe 30 Januari 2023 , katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu huko Iringa, pamoja na wengine wote wahusika wa shirika hilo walikumbukwa Mwenyeheri Sr Irene Stefani na Mwenyeheri Sr. Leonella Sgorbati, waliojitolea maisha yao Barani Afrika, na ambao walijulikana sana katika maeneo waliyotenda utume wao huko Kenya.

Miaka 100 ya utume wa Kimisionari wa Shirika la Consolata huko Iringa Tanzania
Miaka 100 ya utume wa Kimisionari wa Shirika la Consolata huko Iringa Tanzania

Mwenyeheri Allamano alianzisha shirika mnamo 1910

Mwanzilishi wa Shirika la Wokonsolata, Mwenyeheri Giuseppe Allamano, alianzisha Taasisi hiyo mjini Torino nchini Italia mnamo mwaka 1910. Na mnamo tarehe 8 Desemba 1922, Masista Wamisionari wa kwanza wa Consolata, (MC), waliondoka jijini Torino kuelekea Tanganyika ya wakati ule  ambapo mnamo tarehe 26 Aprili 1964, Tanganyika Bara na Zanzibar ziliungana pamoja na kuapata jina la  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwasisi wake ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania aliyezaliwa tarehe 13 Aprili1922 katika kijiji cha Butiama, Musoma.

Misa ya shukurani kwa utume wa kimisionari wa Consolata nchini Tanzania
Misa ya shukurani kwa utume wa kimisionari wa Consolata nchini Tanzania

Tarehe 10 Januari 1923 walifika Dar Es Salaam

Wakiwa huko Mombasa kwenye Meli waliungana na masisita wengine wawili kutoka kanda ya Kenya ambapo walifika Dar Es Salaam mnamo tarehe 10 Januari 1923, na siku tano baadaye, watawa hao waliendelea na safari yao kwa treni hadi Dodoma. Baada ya mwendo wa masaa manne walifika Bihawana mahali  ambapo, mnamo tarehe 22 Januari 1922, pamoja na baadhi ya Mapadre  Wamisionari wa Consolata, waliokuwa tayari wamekwisha fika huko wakiwasubiri walianza msafara wa  kilomita 300 kwa miguu, na ambao uliwafikisha hadi Tosamaganga, ambako waliwasili mnamo tarehe 30 Januari. 

Kutembelea vijiji vya karibu na kuenga uhusiano na familia

Mkuu wa kituo cha kimisonari cha Tosamaganga, Padre Gaudenzio Panelatti, MC, alifanya yote awezayo ili hao watawa wapya waliokuwa wamefika waweze kuzoea mazingira mapya na kuanzisha uhusiano mzuri na wenyeji. Kila alasiri yeye alifuatana na watawa wapya waliofika ili kutembelea vijiji vilivyo karibu na kituo cha kimisionari waweze kujua na kuwa na uhusiano na  familia mbali mbali za mahalia.

Shughuli za jiko, bustani, watoto na maarifa ya nyumbani

Kila asubuhi walihitumia kuwa jikoni na katika bustani ya mboga, shuleni na watoto, kufundisha maharifa ya nyumbani kwa wasichana, shule za wakati ule na  mafundisho kwa watoto na wanawake. Katika muda wao wa ziada walianza kujifunza Kiswahili, lugha ya Taifa. Jioni watawa hao walikusanyika pamoja ili kuelimishwa juu ya utamaduni wa mahali hapo na walisimuliana kila kitu ambacho kiliwatokea au walikuwa wameona wakati wa mchana na kupanga pamoja nini ambacho kingefanyika kwa siku inayofuata.

Wakati wa maadhimisho ya miaka 100 katika Kanisa Kuu la Iringa ,watawa wawili walifunga nadhiri za daima
Wakati wa maadhimisho ya miaka 100 katika Kanisa Kuu la Iringa ,watawa wawili walifunga nadhiri za daima

Kujifunza kupitia miaka 100 na kutoa shukrani nyingi kwa Mungu

Kwa hiyo kwa miaka mia moja, imepita tangu wakati huo. Na wanatambua kuwa wamepokea na kuendelea kupokea zawadi kubwa ya Utume bure kabisa, na hivyo kuna umuhimu wa kufuatilia na kujifunza tena kupitia miaka hiyo mia moja ya historia yao ya umisionari nchini Tanzania na moyo wao umejaa shukrani nyingi, kwa Mwenyezi Mungu, walihitimisha kufafanua Sr. Simona na Sr. Maria Michela.

Watawa wawili wa Consolata nchini Tanzania walifunga nadhiri za daima wakati wa tukio la Jubilei ya miaka 100
Watawa wawili wa Consolata nchini Tanzania walifunga nadhiri za daima wakati wa tukio la Jubilei ya miaka 100

Katika sherehe hiyo walianza na maandamano ambayo yanaonesha watawa na waamini wakiwa wameshikiria mabango mbali mbali kwa kauli mbiu: "Miaka 100 ya kushirikisha faraja ya Kristo Tanzania". Pia katika  kilele cha adhimisho la  misa Takatifu  ya Jubilei hiyo kulikuwa na fursa ya watawa wawili wa Consolata kufunga nadhiri za daima. 

Miaka 100 ya shirika la Consolata nchini Tanzania (1923-2023)

Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, katika fursa ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 ya Shirika la Watawa wa Consolata huko Iringa Tanzania katika utume wa kimisionari ni vema kusikiliza Tafakari ujumbe wa Papa Francisko uliochapishwa hivi karibuni wa Siku ya 97 ya Kimisionari ulimwenguni ambayo itaadhimishwa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 ikiongozwa na kauli mbiu: “Mioyo inayowaka, miguu inayotembea”(Lk 24,13-35). Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo  anabainisha jinsi ambavyo tema hiyo inaelezea kuhusu mitume huko njiani Emmaus. Wanafunzi hao wawili walichanganyikiwa na kukatishwa tamaa, lakini kukutana na Kristo katika Neno na katika mkate uliomegwa uliwasha ndani yao shauku ya kuanza tena safari ya kuelekea Yerusalemu na kutangaza kwamba Bwana amefufuka kweli. Katika masimulizi ya Injili, tunaelewa jinsi gani wanafunzi hao walivyo badilika kutokana na picha fulani zenye kudokeza kama vile mioyo yenye bidii,  kwa ajili ya Maandiko yaliyofafanuliwa na Yesu, ambapo macho yaliyofunguka katika kumtambua na kama upendo wa mchakato wa kutembea kwa miguu. Kwa kutafakari mambo hayo matatu, yanayoonesha ratiba ya wanafunzi wamisionari, Papa anasema tunaweza kpyaisha bidii yetu ya kueneza Injili katika ulimwengu wa sasa.

Baba Mtakatifu Francisko akifafanua kipengele cha kwanza kuhusu Mioyo inayowaka kama Maandiko yanavyofafanua ina maana kwamba, Neno la Mungu hutia nuru na kubadilisha moyo katika utume. Wakiwa njiani kutoka Yerusalemu kwenda Emau, mioyo ya wanafunzi hao wawili ilikuwa na huzuni kama ilivyotokea kwenye nyuso zao kwa sababu ya kifo cha Yesu, ambaye walikuwa wamemwamini (Lk 24,17). Wakikabiliwa na kushindwa kwa Mwalimu aliyesulubiwa, tumaini lao kwamba Yeye ndiye Masiha liliporomoka (Lk 24,21). Na tazama, walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe alikaribia, akatembea pamoja nao” (Lk 24, 15). Kama vile mwanzoni mwa wito wa wanafunzi, hata sasa katika wakati wa kupotea kwao, Bwana alianzisha hatua ya kuwakaribia wanafunzi wake na kutembea pamoja nao.

Katika huruma yake kuu, hachoki kuwa pamoja nasi, licha ya kasoro, mashaka, udhaifu wetu, licha ya huzuni na kukata tamaa ambako  kunatuongoza kuwa tusiofahamu, na  wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii”, (Lk 24, 25), kwa hiyo kuwa watu wa imani haba. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo anasema kwamba  leo hii kama wakati huo ule,  Bwana mfufuka yuko karibu na wanafunzi wake wa kimisionari na anatembea kando yao, hasa wakati wanahisi kupotea, kuvunjika moyo, kuogopa fumbo la uovu linalowazunguka na kutaka kuwakandamiza. Kwa hiyo, alitoa mwaliko kuwa “tusikubali kunyang'anywa tumaini!” (Evangelii Gaudium, 86). Bwana ni mkuu kuliko shida zetu, hasa tunapokutana nazo katika kutangaza Injili katika ulimwengu, kwa sababu utume huo, hata hivyo, ni wake na sisi ni washirika wake wanyenyekevu, ‘watumishi wasio na faida’(Lk 17,10).

Baba Mtakatifu kwa hiyo alipenda kudhihirisha ukaribu wake katika Kristo kwa wamisionari wanaume na wanawake ulimwenguni, hasa kwa wale wanaopitia wakati mgumu: Kwa hiyo aliwaeleza kwamba “Bwana mfufuka, yuko pamoja nanyi daima na anaona ukarimu wenu na sadaka zenu kwa ajili ya utume wa uinjilishaji katika sehemu za mbali. Sio siku zote za maisha zimejaa mwanga wa jua, lakini tukumbuke daima maneno ya Bwana Yesu kwa marafiki zake kabla ya Mateso kuwa “Ulimwenguni mna dhiki, lakini muwe na ujasiri: Mimi nimeushinda ulimwengu!”(Yh 16:33 ).

Katika kipengele cha Pili ambacho Baba Mtakatifu anakizungumzia kati ya vitatu amebinisha juu ya Macho “yaliyofunguliwa na kumtambua” katika kuumega mkate. Yesu katika Ekaristi ndiye kilele na chanzo cha utume. Mioyo ikiwa inawaka kwa ajili ya Neno la Mungu iliwasukuma wanafunzi wa Emau kumwomba Msafiri yule wa ajabu kukaa nao jioni ile. Na, wakiwa mezani, macho yao yalifumbuka, wakamtambua alipoumega mkate. Kipengele cha uamuzi kinachofungua macho ya wanafunzi ni mlolongo wa vitendo vilivyofanywa na Yesu. Kwanza alichukua mkate, akaubariki, akaumega na kuwapa. Hizi ni ishara za kawaida za mwenye nyumba wa Kiyahudi, lakini, zilizofanywa na Yesu Kristo kwa neema ya Roho Mtakatifu, na zikapyaishwa kwa wageni wawili ishara ya kuzidisha mikate na zaidi ya yote ya Ekaristi, sakramenti ya Sadaka ya msalaba. Ili kuweza kuzaa matunda ni lazima tudumu katika kuungana naye ( Yn 15:4-9). Na muungano huo unapatikana kwa njia ya sala ya kila siku, hasa katika kuabudu, kwa kukaa kimya mbele za Bwana, anayebaki nasi katika Ekaristi. Kwa kusitawisha kwa upendo ushirika huo na Kristo, mfuasi mmisionari anaweza kuwa fumbo katika utendaji. Mioyo yetu na itamani daima ushirika wa Yesu, tukitamani ombi la bidii la wale mitume  wawili wa Emau, hasa inapofika saa za  jioni na kusema: “Kaa nasi, Bwana!” ( Lk 24:29).

Baba Mtakatifu Francisko katika ufafanuzi wa kipengele cha tatu ni kuhusu  Miguu katika mwendo au njiani, kwa furaha ya kumsimulia Kristo Mfufuka. Kanisa kijana  milele ambalo daima linatoka nje. Uharaka wa utendaji wa umisionari wa Kanisa kwa kawaida unahusisha ushirikiano wa karibu zaidi wa umisionari wa washiriki wake wote katika kila ngazi. Hili ni lengo muhimu la safari ya sinodi ambayo Kanisa linatekeleza kwa maneno muhimu yasemayo “ushirika, ushiriki na utume. Mchakato wa njia hiyo kwa hakika si kujikunja kwa Kanisa ndani yake yenyewe; sio mchakato wa upigaji kura wa watu wengi kuamua, kama ilivyo katika bunge, nini ambacho ni cha kuamini na kutekeleza au kutofuata matakwa ya kibinadamu.

Badala yake, Baba Mtakatifu anasahuri kuwa ni kwenda njiani kama wanafunzi wa Emau, tukimsikiliza Bwana Mfufuka ambaye anakuja daima kati yetu ili kutufafanulia maana ya Maandiko Matakatifu na kumega mkate kwa ajili yetu, ili tuweze kuendelea na utume wake. Na nguvu za Roho Mtakatifu katika ulimwengu. Kwa hiyo na tuondoke tena, tukiwa tumeangazwa na kukutana na Aliyefufuka na kuhuishwa na Roho wake. Kwa hiyo na tuondoke tena kwa upya, tukiwa tumeangazwa na kukutana na yule Mfufuka na kuhuishwa na Roho wake. Tuanze tena kwa mioyo inayowaka, macho yakiwa wazi, miguu njiani, ili kuifanyamioyo mingine iwake kwa Neno la Mungu, tufumbue macho ya wengine kwa  Yesu katika Ekaristi, na tuwaalike watu wote watembee pamoja katika njia ya amani na wokovu ambao  Mungu katika Kristo amewapatia wanadamu wote.

Ujumbe wa siku ya kimisionari Duniani 2023
09 February 2023, 16:08