Tafuta

2023.02.02 Mkuu wa Kiorthodox wa Pergamo Ioannis Zizioulas amefariki tarehe 3 Februari 2023 akiwa na umri wa miaka 92. 2023.02.02 Mkuu wa Kiorthodox wa Pergamo Ioannis Zizioulas amefariki tarehe 3 Februari 2023 akiwa na umri wa miaka 92.  (Υπουργείο Εξωτερικών)

Ioannis Zizioulas,mtaalimungu mkuu Kikristo,amefariki akiwa na umri wa miaka 92

Mauti yamemfikia kiongozi mkuu wa Kiorthodox wa mji wa Pergamo katika hospitali ya Athene,ambapo alilazwa akiwa na maambukizi ya Uviko.Aliheshimiwa sana na Papa Francisko hadi kumwita kuchangia katika Waraka wake wa Kitume wa 'Laudato si'.

Na Angella Rwezaula; - Vatican.

Askofu Mkuu wa Kiorthodox Ioannis Zizioulas, wa jiji la  Pergamo wa Upatriki wa Constantinople amefariki dunia Ijumaa  tarehe 3 Februari 2023  ambapo mnamo tarehe 10 Januari, alikuwa ametimiza miaka 92 ya kuzaliwa na ambaye alikuwa amelazwa katika hospitalini ya  Athene kwa sababu ya kuambukizwa Ugonjwa wa UVIKO. Alikuwa ni mhamasishaji mkuu wa uekumene,  ambaye tayari miaka arobaini iliyopita,  Padre Yves Congar alikuwa amemtaja kama mmoja wa wataalimungu wa asili na wa kina wa zama zetu. Miongoni mwa mada kuu katika ngazi ya Kikatoliki-Kiothodoksi, Zizioulas alikuwa amezungumzia mara kadhaa kuhusu ukuu wa Petro pia kwa kuzingatia kile kilichoibuka katika Mtaguso II wa Vatican. Akiunga mkono usawa kati ya kila Askofu wa kila Kanisa mahalia, alikuwa amethibitisha pamoja na mambo mengine katika mahojiano kwamba uwezekano wa kukubali ukuu wa ulimwengu wote wa Papa ungekubalika kwa ulimwengu wa Kiorthodoksi katika mwelekeo wa Sinodi ambapo Askofu wa Roma hasingeweza kufanya lolote bila maaskofu wengine. Kwa hiyo kama Askofu anapaswa kushauriana nao kila wakati, akiweka (depositum fidei)  amana ya imani katika ushirika tu na maaskofu wengine.

Mchango kwa Laudato Si'

Hata Papa Francisko  kwa hiyo pia alimheshimu sana kiongozi huyo Ioannis Zizioulas na alimwita kuchangia katika Waraka wake wa Kitume wa Laudato si' na kiongozi mkuu huyo wa Pergamo alikuwa miongoni mwa wale waliohudhuria, mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwasilisha hati ya kipapa mnamo tarehe 18 Juni 2015.  Waraka aliufafanua kama  tukio la kihistoria ambapo katika maoni yake alisema “hili ni tukio la furaha na kuridhika kwa Waorthodox, ambao tangu 1989 wamekuwa wakitoa wito wa uharaka wa mjadala juu ya kazi ya uumbaji. Athari za kiikolojia katika fundisho la Ukristo la uumbaji kwa maana hiyo alisisitiza kwamba mara nyingi zimepuuzwa, badala yake kazi ya uumbaji wote umejazwa na Mungu na mwanadamu ni kuhani wa uumbaji na sio mnyonyaji wake. Kisha alisema kuhusiana na uvujani wa uhusiano sahihi kati ya mwanadamu na ulimwengu, alibainisha  kama 'dhambi ya kiikolojia' kwa Mungu na jirani leo hii  na katika siku zijazo.

Mgogoro wa kiikolojia, fursa ya kiekumene

Kwa  upande wa Zizioulas shida ya kiikolojia ni shida ya kiroho. “Katika msingi wa dhambi hii ni utafutaji wa furaha ya mtu binafsi, uchoyo unaozalisha ukosefu wa haki wa kijamii. Hili lazima lilinganishwe na 'ustaarabu wa kiikolojia' ambao ni usikivu kwa viumbe vyote, ikizingatiwa kwamba sote tunategemeana”. Kwa kiongozi huyo wa kiorthodox,  mgogoro wa kiikolojia ni tukio la kiekumene, wito wa umoja katika sala kwa ajili ya mazingira, katika uongofu wa mioyo na mtindo wa maisha ili kila zawadi ya Mungu iheshimiwe: Kwa hilo tunaitikia 'Amina' kutoka kwa Mungu chini ya moyo wangu”. Na Papa Francisko mara nyingi alimnukuu Zizioulas, hata wakati alipenda kufanya mzaha kuhusu njia ya kiekumene na mjadala wa kitaalimungu na kusema kwamba wataalimungu watakubaliana siku baada ya hukumu ya mwisho.

Wasifu wake

Ioannis Zizioulas, alizaliwa  mnamo tarehe 10 Januari 1931, alisomea katika vyuo vikuu vya Thessaloniki na Athene, kisha katika Taasisi ya Kiekumene ya  Bossey. Alipata  shahada ya udaktari wake kwa tasnifu juu ya “Umoja wa Kanisa katika Ekaristi Takatifu na katika Askofu wakati wa karne tatu za kwanza”. Alimaliza masomo yake ya kitaalimungu katika Chuo Kikuu cha Harvard. Alikuwa profesa wa taalimungu ya kidogma katika Chuo Kikuu cha Edinburgh na taalimungu ya utaratibu katika vyuo vikuu vya Glasgow (1973-1987), Thessalonike (1984-1998), Chuo cha King's London, Chuo Kikuu cha Gregoriana Roma na Geneva. Mnamo 1986 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Waorthodox huko  Pergamo. Aliwakilisha Upatriaki wa Constantinople katika tume ya pamoja ya kimataifa ya mazungumzo ya kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox.

Kifo cha Askofu Mkuu wa Kiorthodox Ioannis Zizoulas huko Athene
03 February 2023, 16:21