Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Ujumbe wa Kwaresima 2023: Utu Wema!
Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, - Dar es Salaam, Tanzania.
Utangulizi: Kwaresima ni kipindi cha kutafakari zaidi mateso ya Kristo aliye kielelezo cha utu wema. Katika Kwaresima ya mwaka huu tunaalikwa kutafakari sala ya Mtakatifu Paulo anapoiandikia jumuiya ya Waefeso, ambayo ilikuwa changa kiimani. Ni jumuiya iliyohitaji kuwa na elimu ya Mungu na ya Kanisa (rej. Efe 1:15-18; 3:14-19), iliyohitaji umoja hasa kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi (rej. Efe 2:11-22) na iliyohitaji kutiwa nguvu iii kuweza kushinda kila aina ya udhaifu (rej. Efe 4:17-5:18). Katika sala hii, ''[Mungu] awajalieni kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani" (Efe 3:16), Mt. Paulo anawaombea watu wa Efeso ili Mungu awajalie utu ambao kwa huo Kristo Yesu ataweza kuingia katika mioyo yao. Anatambua jinsi gani jumuiya hiyo inavyohitaji msaada wa sala iii kuendelea kuimarika katika ukristo wao, na hekima ya Mwenyezi Mungu ambaye anaimarisha taifa lake kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Anapoandika juu ya utu wa ndani wa mtu, Mt. Paulo anamaanisha roho ya mtu. Hii ni sehemu ya mtu inayoweza kuimairishwa na Roho Mtakatifu. Utajiri wa utukufu huo wa Mwenyezi Mungu unazidi kuonekana katika kutunza na kuimarisha viumbe wake akiwemo binadamu. Tunaalikwa sisi sote kupiga magoti na kujiombea, tukianza kwa kutambua ukuu na utajiri wa utukufu wa Mwenyezi Mungu. Ufanisi wa sala zetu unapatikana tunapojikita katika kumtanguliza Mungu mwenyewe. Tunaalikwa kutambua kwamba roho zetu zinaweza kutaka kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa njia mbali mbali lakini zikalemewa na udhaifu wa mwili (rej. Mt 26:41) kama vile: uchovu, ugonjwa, msongo wa mawazo, uvivu, woga, hali zetu za kifamilia, kiuchumi, kisiasa na kijamii. Roho Mtakatifu atuimarishe iii tuweze kutumia vizuri zaidi nyenzo za kiroho hasa sala, maisha ya sakramenti, mazoezi mengine ya kiroho kama kufunga na matendo ya huruma (rej. 2 Tim 1:7) kuishi maisha yampendezayo Mungu. Kwa kifupi ujumbe huu unatualika tutafakari juu ya thamani ya utu wetu sisi wanadamu. Tunamwomba Roho Mtakatifu kuimarisha utu wa ndani ili tuweze kufanya mapenzi ya Mungu.
SURA YA KWANZA: MAANDIKO MATAKATIFU NA MAFUNDISHO YA KANISA JUU YA UTU
A. MAANDIKO MATAKATIFU
1. Utu ni hali ya binadamu ya kuwa na kutenda kadiri ya hadhi yake kama alivyoumbwa na Mungu. Katika Maandiko Matakatifu, Mt. Paulo anatualika kuvaa utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli (rej. Efe 4:24). Mwanadamu ana utu wa nje na utu wa ndani, utu wa kimwili na utu wa kiroho. Kwa maneno mengine mwanadamu anaweza kuwa na utu wa kale na utu mpya.
2. Utu wa kale ni utu wa asili yaani utu ambao mtu anaurithi kutoka kwa wazazi wake (dhambi ya asili). Aidha, ni utu ambao mtu alijifunza au alifundishwa lakini ukiwa ni utaratibu ulio kinyume na wokovu wa Mungu katika Kristo Yesu. Tunachotakiwa kufanya juu ya utu wa kale ni kuusulubisha. iii utu huo ubatilike (rej. Rum 6:5-14). Kibiblia, Utu mpya ni matokeo ya mabadiliko ya utu wa kale.
Kuvaa utu mpya
3. Utu mpya ni ule tulioupokea kwa ubatizo wakati tunampokea Yesu Kristo kama Mwokozi wetu. Utu huo unatakaswa na Neno la Mungu (rej. Yn 17:17). Aidha, utu mpya ni mabadiliko ya rohoni (rej. Kol 3:8-10) yanayofanywa na Roho Mtakatifu kwa njia ya Neno la Mungu ndani ya mtu. "Mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya!" (2 Kor 5:17). Kwa msaada wa Neno la Mungu ambalo ni "taa ya miguu
..." (Zab 119:105), mtu atafanya yampendezayo Mungu. Ndivyo anavyotuambia Yoshua, "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana." (Yos 1:8). Kila Mkristo anahimizwa kuwa mtu wa ibada na mwenye uchaji wa Mungu.
4. Kuvaa utu mpya ni kukubali kuongozwa na Reho Mtakatifu, "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Reho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu" (Rum 8:14). Ni kujitenga na ubaya wa kila namna iii Mungu wa amani mwenyewe atutakase kabisa; nafsi zetu na roho zetu na miili yetu ihifadhiwe tuwe kamili, bila lawama mpaka wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo (rej. 1 Thes 5:22-24). Tukizingatia sana maelekezo hayo tutakuwa na utu mpya ulio safi, unaopatikana tu katika Kristo Yesu Mwokozi.
Matokeo ya kuvaa utu mpya
5. Tunda la utu mpya ni kufanana na Kristo - kumvaa Kristo. Wakristo wanapaswa kumwiga Kristo katika upendo, msamaha, utu wema, amani, huruma, upole na haki (rej. Mt 5:1-12). Kwa jinsi hiyo wanakuwa kweli watoto wa Mungu (rej. Mt 5:45).
6. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunapotafakari juu ya tunda la utu mpya, pamoja na mengine, tunaalikwa kumwangalia Kristo, aliye mfano wetu halisi wa kusamehe na kutenda mema. Wakristo tunaalikwa kuishi maisha ya kusamehe na kuwaombea baraka watu wote.
7. Msamaha ni uamuzi wa Mungu au mtu wa kutofuatilia makosa ambayo ametendewa. Ni kutambua kosa kwa jinsi lilivyo, na halafu kuliacha kwa upendo, kulisahau na kujenga uhusiano mpya na mtu aliyemkosea (Ebr 10:17-18). Mungu ndiye asili ya msamaha. Mwanadamu alipomkosea Mungu kwa dhambi, Mungu ndiye aliyechukua hatua ya kumsamehe kwa kumtuma Mwanae ulimwenguni (rej. Yn 3:16-17). Kristo alipokuwa msalabani alisamehe watesi wake (rej. Lk 23:34).
8. Kwa kumwiga Kristo yatupasa kuwasamehe na kuwaombea baraka hata maadui zetu na kuwatendea mema kama Maandiko Matakatifu yanavyotuasa, "Lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi" (Mt 5:44). Tena yanasema "Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani" (Rum 12:14; rej. 1 Pet 3:9; Rum 12:17, 20-21).
9. Utu wema ni hali ya kujali wengine na kuguswa na yale wanayoyapitia. Ni hali ya kuona kuwa jirani yako ni sawa na wewe (rej. Mwa 1:27). Hivyo anapopitia magumu kuwa tayari kushiriki pamoja naye kwa upendo. Kujenga msingi imara wa utu wema yakupasa kuwapenda wengine kama unavyojipenda, kujali furaha zao, kuwaona wao kuwa ni bora zaidi na kuachana kabisa na majivuno (rej. Flp 2:3-5).
10. Utu wema unaonekana katika kujali, kumuwazia mwingine mema, kuona hitaji la mtu na kumsaidia pasipo kuombwa au kuambiwa. Ni kutoa msaada kwa kutambua uhitaji wa watu. Kimsingi ni ngumu sana kumtendea wema mtu aliyekutendea mabaya, ila kwa msaada wa Mungu tunaweza yote.
11. Mtu anapotenda wema si vema kujionyesha au kutangaza iii watu wafahamu. "Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye wa mbinguni" (Mt 6:1). Kutokana na andiko hili tunajifunza ya kwamba mema tuyatendayo ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, Yeye pekee ndiye anayestahili kutukuzwa.
12. Tukiongozwa na utu wema tunaalikwa kutenda matendo ya huruma na huduma iii tuweze kuurithi ufalme wa Mungu. Matendo mema ni pamoja na kuwapa chakula wenye njaa, kuwavika wasio na nguo, kuwatembelea wagonjwa, kuwatembelea wafungwa ... (rej. Mt 25:31-46).
13. Utu wema unatupelekea kuwa na uhai mpya rohoni mwetu. Ni kufufuka parrioja na Kristo, yaani: kuua chochote kilicho cha kidunia, mfano uasherati, matendo machafu, mawazo mabaya na tamaa mbaya, kujilimbikizia mali ambako ni sawa na kuabudu miungu ya uongo, kuacha hasira, ukorofi, chuki, uongo, mazungumzo yenye matusi na yasiyofaa (rej. Kol 3:1-11).
B. MAFUNDISHO YA KANISA JUU YA UTU WA KALE NA MPYA
14. Vyanzo vya ufunuo (mafundisho) katika Kanisa ni Biblia Takatifu na Mapokeo Matakatifu. Baada ya kuona Biblia inasema nini juu ya "Utu" tunageukia mafundisho ya baadhi ya Mababa wa Kanisa, Watakatifu na Mababa Watakatifu.
Maandiko ya Mt. Yohane Krisostom (347-407)
15. Mt. Yohane Krisostom alisema kuwa iii mtu aweze kuondoa utu wa zamani na kuvaa utu mpya, safari ya mtu huyo ya wokovu, inayojumuisha kutubu, kusali, kusamehe, kufanya matendo ya huruma (sadaka) na kuwa na unyenyekevu, inabidi iwe endelevu.
16. Njia ya kwanza ya kutubu ni mtu kuondokana na dhambi zake mwenyewe. Akiri dhambi zake na atasamehewa (rej. Yer 14:20-22). Kwa hiyo mtu akiziacha dhambi zake mwenyewe, itakuwa sababu ya kutosha Mungu kumsamehe dhambi maana mtu anajiwekea malengo ya kutorudia kutenda dhambi tena. Mtu anashauriwa asutwe na dhamiri yake kabla hajafika mbele ya kiti cha hukumu cha mwenyezi Mungu.
17. Njia ya pili ya kutubu dhambi ni kusamehe. Mt. Yohane Chrysostom anasema kuwa katika hatua hii mtu anaondoa fikra ya kulipa kisasi katika kichwa chake kwa sababu ya yale aliyotendewa. Anatawala hasira zake na anasamehe ndugu zake dhambi walizomtendea. Ikiwa mtu anasamehe wadeni wake hata Mungu atamsamehe dhambi zake.
18. Njia ya tatu ni sala hai zinazosaliwa kwa uangalifu na kutafakari, ambazo zinatoka moyoni mwa mtu.
19. Njia ya nne ni kufanya matendo ya huruma ambayo yana faida kubwa katika maisha ya kiroho, bila kushurutishwa au kupangiwa.
20. Njia ya tano ni kuishi maisha ya unyenyekevu. Kati ya njia zilizotajwa hapo juu, hii ni njia kubwa ya kuondoa dhambi. Mfano mzuri unaoeleza njia hii ni ule wa mtoza ushuru na Farisayo (Lk 18: 9-14). Mtoza ushuru hakuwa na matendo mazuri ya kutoa mbele ya Mungu lakini unyenyekevu wake mbele ya Mungu ulimwondolea mzigo wa dhambi zake zote alizokuwa nazo.
Maandiko ya Mt. Agustino wa Hippo (354-430)
21. Mt. Augustino wa Hippo anasema kuwa, anguko la kwanza la wanadamu (dhambi ya asili) lina sura ya ulimwengu huu wa watu wanaoitwa "watu wenye utu wa zamani". Wale wenye sura ya mtu wa mbinguni wanaitwa "watu wenye utu mpya". Watu wenye utu wa zamani wapo mbali na Mungu. Wale wenye utu mpya wanasimama mbele ya Mungu na wanakaa katika mwanga wa kimungu.
22. Mwanzoni mtu aliumbwa mzuri lakini baada ya anguko la Adamu, ufalme wa shetani ulijengwa na huu haukuwa na uwezo kumfikisha mbinguni. Ni kwa kupitia fumbo la ukombozi wa Bwana wetu Yesu Kristo utu mpya umezaliwa. Watu waliopata neema za Kristo walifanya sadaka ya Kristo ijidhihirishe katika njia ya wokovu.
23. Anaendelea kusema kuwa mtu anayetaka kuacha utu wa zamani na kupyaisha maisha yake (utu mpya) hana budi kufanya juhudi iii kuacha maisha ya kidunia. Mtu huyo pia inabidi afanye bidii kukuza maisha yake ya kiroho kwani kila mara kuna mvuto wa dhambi ya asili aliyorithi kutoka kwa wazazi wake na udhaifu wake. Hivyo, anapoweka juhudi kukuza maisha yake ya kiroho, taratibu kwa kupitia nguvu ya neema ya Mungu, maisha mapya yanazaliwa ndani yake na kumfanya mtu mpya.
24. Mtakatifu Agustino anaamini kuwa, yapo mabadiliko ya kimaendeleo ya kiroho kwa kupitia hatua zifuatazo:
1. Mtu anaiga watu wenye mifano mizuri ya maisha ya watu wa zamani (Watakatifu) na wa sasa.
2. Mtu anaanza kuvutiwa na ukweli wa kimungu kuliko mambo ya dunia yanayopita. Badala ya kukumbatia tu sheria za kidunia zinazopita, anaanza kuelewa sheria au ukweli ambao haubadiliki unaotoka kwa Mungu, unaohusu misingi ya ulimwengu.
3. Mtu anaruhusu vionjo vya mwili wake (carnal appetitive) vitawaliwe na akili yenye busara na hekima. Mwili na roho vinakuwa kitu kimoja hivyo mtu hatendi dhambi tena.
4. Mtu anaanza utendaji, akisukumwa na ujasiri ambao unamwezesha kustahimili na kushinda madhulumu na mahangaiko ya maisha ya kiroho.
5. Mtu anafikia amani na utulivu ambao unatokana na hekima isiyobadilika ya kimungu.
6. Mtu anabadilika kabisa, havutiwi tena na mambo geugeu ya ulimwengu huu, anaishi amekamilika akionyesha sura ya Mungu.
7. Kwa kuwa mtu ameishi maisha hayo anakuwa mpya kabla ya kifo na baada ya kifo anafikia hatua ya mwisho ya kufikia ukamilifu, yaani kufurahia uzima na furaha ya milele akiwa ameunganika na Mungu.
25. Baada ya kusoma na kuthamini ukweli wa Biblia Takatifu, Mt. Augustina aliona ndani yake nguvu mbili zinazovutana, yaani maisha ya utu wa kale na utu wa mpya. Anakiri kuwa utu mpya ulishinda utu wa zamani. Alisema alisaidiwa na neema ya Mungu kushinda utu wa zamani. Kwa maneno yake mwenyewe alisema "Nimekuwa nikitafuta nafasi kwa nguvu zangu zote kuwa na ibada kwa Mungu lakini nimekuwa nikirudishwa nyuma na minyororo na udhaifu wa utashi wangu lakini neema ya Mungu itaendelea kunisaidia kushinda". (Hii ni nukuu toka kwa Mt. Ireneus: "Adversus Haereses, IV, c. 34, n. 1: PG 7, pars prior, 1083: "Omnem novitatem attulit, semetipsum afferens'.)
Mtakatifu Paul VI, Papa
26. Baba Mtakatifu Paulo VI anasema kuwa "kueneza injili kunamaanisha kuleta Habari Njema katika tabaka zote za wanadamu, na kwa njia ya mvuto wake kuwabadilisha wanadamu kutoka ndani na kuufanya kuwa mpya, hili ndilo linafanya uumbaji wote kuwa mpya. Lakini hakuna ubinadamu mpya ikiwa kwanza hakuna watu wapya wanaofanywa upya kwa Ubatizo na kwa maisha yanayoishi kulingana na Injili. Kusudi la uinjilishaji kwa hiyo hasa ni mabadiliko ya ndani, na kama ingepasa kuonyeshwa katika sentensi moja njia bora zaidi ya kusema ingekuwa kusema kwamba "Kanisa linaeneza injili ya kuongoka pekee kwa njia ya uwezo wa Kimungu wa ujumbe anaotangaza, dhamiri za kibinafsi na za pamoja za watu, shughuli wanazozifanya, na maisha na mazingira halisi ambayo ni yao".2
Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa
27. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua ya kichungaji mwanzoni mwa "Milenia ya Tatu" "Novo Mil/enio Ineunte anatualika kutubu kwa kusema "ninaomba pia ujasiri mpya wa kichungaji iii kuhakikisha kwamba mafundisho ya kila siku ya jumuiya za Kikristo yanawasilisha kwa ushawishi na kwa ufanisi utendaji wa Sakramenti ya Upatanisho'13• Watu wahimizwe kuthamini na kupokea Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara. Hapo ndipo watafanywa viumbe vya Mungu, kutafuta utakatifu hapa duniani na kufikia uzima wa milele. Hii ndiyo dhana nzima ya utu mpya.
Baba Mtakatifu Francisko
28. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake Kichungaji ya "Furaha ya Injili" anafundisha juu ya Maisha mapya katika Kristo anaposema kuwa upya wa kuhubiri unaweza kuwapa waamini pamoja na wale walio vuguvugu na wasiotenda, furaha mpya katika imani na kuzaa matunda katika kazi ya uinjilishaji. Moya wa ujumbe wake daima utakuwa sawa... Mungu huwafanya upya waaminifu wake bila kujali umri wao: "Watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia" (Isa 40:31). Kristo ndiye "Injili ya milele" (Ufu 14:6); yeye "ni yeye yule jana na lea na hata milele" (Ebr 13:8), lakini utajiri wake na uzuri wake havikomi. Yeye ni mchanga milele na chanzo cha mara kwa mara cha upyaisho".4
Hitimisho
29. Ni dhahiri kwamba utu huu unadai sadaka kubwa kwa upande wetu, lakini ni makosa kuuona kama ni kazi ya kishujaa ya mtu binafsi; kwani hii ni kazi ya Bwana, inayopita kitu chochote ambacho tunaweza kuona na kuelewa. Upya halisi ni upya ambao Mungu mwenyewe anauleta kwa siri, kuuongoza na kuusindikiza kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yeye "alitupenda sisi kwanza" (1 Yoh 4:19) na kwamba yeye peke yake hukuza (rej. 1 Kor 3:7). Mungu anauliza kila kitu kutoka kwetu, lakini wakati huo huo yeye hutoa kila kitu kwetu.
30. Katika nyakati hizi upya huu wa maisha utadhihirishwa kwa kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, yaani: msamaha, utu wema, upendo katika familia, amani katika jumuiya, moyo wa sala, maisha ya Sakramenti, hasa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu.
31. Wakati huu wa Kwaresima tunajifunza namna ya kutibu majeraha yetu ya dhambi. Tufanyie kazi mafundisho haya iii tuwe na afya ya kiroho, na tuwe tayari kwenda mezani kwa Bwana kwa kujiamini, tukutane na utukufu wa Kristo, Mfalme wa Utukufu iii baadaye tupate baraka ambazo zitatupatia neema, huruma na wema wa Kristo, ambao utatufikisha katika wokovu wa milele.
SURA YA PILI: UTU UNAUNDWAJE?
Utangulizi
32. Utu ni hali ya binadamu ya kuwa na kutenda kadiri ya hadhi yake kama alivyoumbwa na Mungu. Ni hali inayomtambulisha mtu katika tabia na mienendo, hususani katika maweza yake, namna ya kufikiri, mtazamo, mwelekeo, na kutenda kwake. Ni ile hali ya ndani inayomfanya awe tofauti kabisa na viumbe wengine wote; yaani kinachomfanya afikiri, atende tofauti na wanyama wengine. Kwa maneno mengine twaweza kusema utu ni hadhi ya mwanadamu.
33. Tabia zinazotambulisha utu huweza kuwa za kuzaliwa nazo (inherent) au za kutokana na malezi/makuzi (acquired) na hujionesha kwa jinsi mtu anavyohusiana na watu wengine na mazingira yanayomzunguka. Tumewahi kusikia watu wakisema "fulani sio mtu kabisa!!" au "fulani hana utu kabisa!!" Kwa kusema hivyo hawamaanishi kuwa mtu huyo hana uhai au kwamba amegeuka mnyama wa miguu minne bali wanamaanisha mtu huyo amepoteza sura ya Mungu ndani yake. Dhamiri yake imejeruhiwa kiasi cha kuona mabaya kama mema na mema kama mabaya. Mtu huyo anakuwa amefifisha hali yake ya kuwa "mfano na sura ya Mungu" (Mwa 1:26).
34. Katika ulimwengu wa lea wengi wetu tunaelekea kuthamini mali na vitu zaidi kuliko utu. Utu wa mtu huweza kupimwa katika nyanja mbalimbali. Katika sura hii, tunapojifunza muundo wa utu wa mtu tutaangazia utu wa mtu kimwili, kiroho, kiakili, kisaikolojia kichungaji na kiutume - jinsi tunavyoweza kulelewa katika hali hizo.
Malezi ya kimwili
35. Malezi ya kimwili huanza katika umri wa awali kabisa wa uhai wa mtoto. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao kukua katika mapendo na imani wakiwa katika umri mdogo; na kwa kufanya hivyo hutengenezwa taifa la baadaye lenye kuheshimu utu wa binadamu. Wazazi wanapaswa daima kuwafuatilia watoto wao iii kuwaepusha na hatari ya kuiga tabia kutoka katika makundi wanayokutana nayo katika umri wao wa awali, kwa kuwa katika umri huo siyo rahisi kwao kutofautisha tabia iliyo nzuri na ile iliyo ya hatari kwa maisha ya baadaye. Hivyo, wazazi yawapasa kukumbuka kwamba ikiwa watawalea watoto wao katika njia nzuri (lishe bora, mavazi yanayostahili, malazi bora, n.k) kamwe (watoto) hawataiacha hata watakapokuwa wazee (rej. Mit 22:6).
36. Wazazi watambue ukweli kuwa Bwana wetu Yesu Kristo amekuwa mfano hai na wa kuigwa katika kukua na kukomaa kimwili (rej. Lk 2:40). Utu wetu ni wa pekee na ni zawadi ambayo tunapaswa kuipokea kwa mapendo. Wazazi wanatakiwa kutambua kwamba, familia zetu ndio shule ya kwanza kufundisha maana ya ubinadamu wetu, utu wetu na tofauti ya jinsi. Watoto huzaliwa na kulelewa ndani ya familia. Kila jambo linalofanyika ndani ya familia: maongezi na matendo ya kila siku kati ya wazazi na watoto na chakula cha pamoja yote haya huchangia kwa mtoto kukua kimwili au kiutu na hapo mtoto huweza kujifunza namna ya kuhusiana vema na wenzake.
37. Tunawasihi familia kuishi kwa upendo, iii watoto waweze kutambua vipaji na karama zao za kweli ndani ya familia. Kwa kupitia kuishi kwa upendo ndani ya familia na kuwajibika katika kuwafunza watoto, tutapata watoto wanaopokea sifa katika mazuri na walio tayari kukosolewa pale wanapokosea.
Malezi ya kiroho
38. Malezi ya kiroho ni uhusiano unaojengwa siku kwa siku baina ya binadamu na Mungu wake katika kila nyanja ya maisha. Kusudi kuu la malezi ya kiroho ni kuwasaidia waamini kujenga na kuboresha mahusiano yao na Mungu. Kupitia mahubiri ya kiroho utu wa mtu utajengwa katika mahusiano mema na Mungu, na hatimaye kwa kumtambua Mungu mwanadamu atajenga uhusiano mwema na jirani ambaye ni "sura na mfano wa Mungu" (rej. Mwa 1:26-27). Wachungaji na walezi katika ngazi zote za kidini na za kiserikali wanahitajika kuwalea wanaowazunguka kwa kuwa mfano bora kwa matendo iii kuimarisha thamani ya binadamu na imani yake (rej. KKK 2252-2253.)
39. Ni wajibu wa wazazi kuwapenda, kuwapa mafundisho msingi ya imani na kuwahimiza watoto wao kushiriki mafundisho mengineyo yakiwemo yale ya sakramenti, Misa Takatifu na ibada mbalimbali. Maaskofu, Mapadre, Mashemasi, Makatekista na waamini wote wahakikishe kuwa watoto wanapata malezi endelevu ya kiroho.
40. Sayansi na teknolojia vimesaidia sana watu wengi kutambua vipaji vyao na kukuza maendeleo katika jamii zetu. Kwa upande mwingine sayansi na teknolojia vimeleta athari ya watu kutokumfuata Mungu na hatimaye kupotea kwa thamani ya utakatifu wa maisha kwani utu hupewa thamani ndogo. Ni jambo la kusikitisha kwa jamii zetu kupoteza uwezo wa kujali utu wa mwanadamu: kwa mfano utengenezaji wa silaha za maangamizi, dawa na vifaa vya kudhoofisha afya na kuangamiza uhai wa mwanadamu, kubadili jinsia, wizi wa kimtandao na ukani Mungu (atheism). Kanisa daima linasimama kutetea utu na utakatifu wa maisha ya mwanadamu kama inavyokusudiwa na Mungu mwenyewe.
41. Malezi ya kiroho huzingatia pia uhusiano wa mtu na Mama Bikira Maria, kwani yeye anatufanya tuwe karibu na Mwanae - "Mama tazama Mwanao" (Yn 19:26). Hivyo basi Kanisa kwa mahubiri na mafundisho linalenga kuinua ibada kwa Mama Bikira Maria na kumfanya kuwa kioo na mfano bora kwa waamini iii kuishi maisha ya kweli ya kikristo. Waamini wanaalikwa kuthamini sana mazoezi na ibada kwake, kama inavyoelekezwa na Majisterio (rej. LG 58).
42. Iii kuujenga utu wa mwanadamu, wakati huu wa Kwaresima tunaalikwa kushiriki zaidi mazoezi mengine ya kiroho yakiwemo kusali Rozari, tafakari ya Neno la Mungu, kutafakari kimya mbele ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hija takatifu, tafiti ya moyo na mafungo; yote haya yatamfanya mwanadamu akue kiroho na kutambua uhusiano wake na Mungu na binadamu mwenzake.
Malezi ya kiakili
43. Tunarutubisha akili zetu kwa njia ya kufundishwa, kusoma/kujisomea, kwa njia ya mang'amuzi ya maisha, na kwa njia ya mifano ya maisha ya watu. Kwa kifupi mtu ni mwili, roho, akili na utashi [vyote kwa pamoja]. Akili inatusaidia kujua na kupembua jema na baya, wakati utashi ni nguvu ya ndani inayotusukuma kutenda: viwili hivi ni lazima vijengwe na vikuzwe. Kinachomtofautisha mtu na mnyama ni utashi. Utashi wetu ukikomaa akili na utu wetu hukomaa pia.
44. Maandiko Matakatifu yapo wazi kwamba mwanadamu anajijua yeye mwenyewe, watu wengine na Mungu (Rum 1:19-20), anajua juu ya uumbaji wa Mungu (Zab 8:6-7), anajua ukweli uliofunuliwa (Lk 8:10), anajua uzuri wa uumbaji na Mungu aliyeumba (Zab 8:1- 2), na anajua jema linalotakiwa kufanya na baya linalotakiwa kuachwa. Kumbe yote haya yanahitaji malezi sahihi ya kiakili ili mwanadamu aweze kutambua thamani ya maisha yakena kuyapokea kama zawadi kutoka kwa Mungu.
45. Malezi ya kiakili yanakuza fadhila za kibinadamu kwa nadharia na kwa vitendo pia. Kwa upande wa maadili husaidia kuweza kufanya maamuzi sahihi ya kipi kifanyike na kipi kisifanyike, kwani ndiyo sheria asili ya mwanadamu, yaani kufanya lililo jema na kuacha lililo baya. Zaidi ya hayo Kanisa linahimiza sana watoto na watu wazima walelewe katika kujua utamaduni mwema uliopo katika jamii yao na kuzuia tamaduni na mila zote potofu ambazo hukandamiza utu wa mwanadamu.
46. Iii kuweza kutoa malezi ya kiakili, wazazi na walezi wahimize katika kujua maana ya maisha ya mwanadamu iii kusudi watoto wakue wakiwa wanatambua thamani kubwa ya utu. Watoto wazuiliwe kuingia katika mazingira yenye makwazo, kama vile: kuangalia picha zenye kudhalilisha utu wa mwanadamu, kusoma au kusimuliwa hadithi zenye lengo la kudhalilisha utu, n.k, kwani hayo huweza kuleta mtazamo hasi katika kukua na kukomaa kiakili.
47. Katika kuhakikisha makuzi sahihi ya kiakili yanayopelekea kuthamini utu wa mwanadamu, waamini wanahimizwa kusoma Maandiko Matakatifu, kupokea mafundisho msingi ya Kanisa Katoliki hasa kuhusu utu wa mwanadamu, sheria za Kanisa, vitabu vya kiroho vyenye lengo la kukuza akili na utashi wa mwanadamu na kuzingatia mashauri ya kichungaji yanayotolewa na wachungaji wao. Hayo yatawasaidia wazazi kufanya uchaguzi sahihi wa shule zinazowafaa watoto wao sio tu kwa elimu dunia lakini hasa kwa ajili ya malezi ya kiakili na makuzi ya utu. Aidha, wazazi hawana budi kuzingatia umri sahihi wa kuwapeleka watoto wao shule za bweni.
Malezi ya kisaikolojia
48. Saikolojia ni elimu juu ya tabia ya mwanadamu. Tabia ni mjumuisho wa matendo, miitikio, au mienendo inayoweza kuonekana wazi, kupimwa na hata kuchunguzika kwa kufuata misingi ya kisayansi. Katika malezi haya ya kisaikolojia sambamba na malezi mengine, yafaa kuanza katika umri mdogo wa mwanadamu na kuendelea kulelewa kadiri anavyokua. Hili litasaidia kukuza tabia njema kwa mwanadamu na kuwa na uhusiano mwema na Mungu na wanadamu wenzake.
49. Katika saikolojia yafaa kutambua kwamba mtu ana m1s1ngi muhimu: uzuri, heshima, thamani na anatafuta ustawi wake mwenyewe na wa wengine. Heshima na utu havijali umri wa mtu; na uzuri na thamani ya mtu hutufanya tuweze kukua zaidi katika kuyathamini maisha ya binadamu na kuwa na maadili mema kwa viumbe vilivyoumbwa na Mungu. Katika kuthamini misingi hiyo, mwanadamu alelewe kutambua umuhimu wa misingi hiyo bila kumkosea Mungu na kumuathiri mwanadamu mwenzake. Mathalani, kumpenda mno mali kiasi cha kuweza kumwangamiza mwanadamu mwingine; matumizi mabaya ya fedha ndani ya familia kiasi cha kuathiri mahitaji muhimu ya kifamilia. Hivyo, wanadamu katika nyanja zote walelewe katika kuthamini utu wa mwanadamu.
50. Katika maisha yake mwanadamu anakutana na magumu ya kila namna: mateso, mahangaiko, wasiwasi na huzuni, kutojitosheleza mwenyewe na wengine. Pia huumizwa na kujeruhiwa na wengine au na mambo yanayotokea duniani. Mambo kama: magonjwa, vifo, kusalitiana na majanga ya asili visiwe sababu ya kukata tamaa, kututenganisha na wenzetu na kumwasi Mungu (rej. Rum 8:35-39). Kazi ya Kanisa na jamii ni kumlea mtu kisaikolojia iii atambue kwamba changamoto na matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.
51. Malezi ya kisaikolojia yamsaidie mtu kutambua utashi wa mwanadamu na uhuru wa kuchagua. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hivyo katika utashi wake mwanadamu anatakiwa kuwa huru katika lile analolifanya, yaani aweze kusema kwa uhuru, atimize wajibu wake kwa uhuru. Lakini uhuru wa kweli kwa mkristo ni kuwa na mahusiano mema na Mungu - kufuata yale anayotaka Mungu.
52. Basi kukiwa na malezi bora ya kisaikolojia kwa watu katika jamii yetu, watu wataweza kuthamini utu wa mwanadamu. Matukio mabaya ya ubakaji, ndoa za jinsia moja, unyanyasaji kwa watoto wadogo yatakosa nafasi katika jamii tunayoishi. Kanisa lihimize kufundisha elimu ya kisaikolojia katika ngazi zote za elimu iii kukuza dhana ya kumthamini mwanadamu. Iii utu wa kisaikolojia uwe sawa, vionjo na hisia zisitawale fikra na utendaji wa mtu.
Malezi ya kichungaji
53. Kristo ndiye Mchungaji Mwema (rej. Yn 10:11). Upendo wa kichungaji unadai kumwiga Kristo katika fadhila, ambazo ni: wema, upole, huruma, unyenyekevu, ukarimu, uvumilivu, kujali, busara, haki, subira, utulivu na moyo wa kuwajali watu wote.
54. Wazazi/walezi kama wachungaji wa awali wanaalikwa kuwalea watoto wao katika moyo wa sala, katekesi, maisha ya sakramenti na maisha ya fadhila. Matokeo yake watoto wataandaliwa kusikia sauti ya Mungu na kutambua miito yao.
55. Wajibu wa wachungaji (wenye Daraja Takatifu) na wanakanisa wote ni kutoa malezi ili kuhakikisha watoto na waamini wanakuwa katika tabia njema; kuhakikisha wanaweza kufanya kwa vitendo wema, upendo na fadhila zote za kimungu na za kibinadamu. Jamii ijenge hofu ya Mungu katika shughuli zake za kila siku, izitambue na kuziishi amri za Mungu na kujali utu wa mtu. Iii kutimiza wajibu wa kichungaji ni lazima mchungaji awe mwenye utu, yaani aweze kuthamini, kutambua na kujali mahitaji ya kondoo kwa kukumbuka kuwa yeye ni wakili aliyeaminishwa kundi la kondoo wa Kristo. Utume wa Kanisa unadai ushirika wa waamini wote: walei, watawa na waklero (Rej. KKK 849, 863 na 913).
56. Hivyo, katika mahubiri na malezi ya kuhakikisha imani ya watu inakua (kuanzia familia, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, Vyama vya Kitume/VMJ n.k) yafaa kutambua kwamba malezi ya kiutu, malezi ya kiroho na malezi ya kichungaji kamwe hayambagui mtu bali ni kwa ajili ya taifa late la Mungu. Hapa ni muhimu kutambua kwamba katika ubatizo wetu tunatumwa sate kumlea mtu katika kuujua ukweli kuhusu Mungu na uumbaji wake na kufahamu thamani ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (rej. Mwa 1:26).
Malezi ya Kitume
57. Malezi ya kitume yana msingi katika umisionari: kutumwa, kupewa ujumbe na kuondoka. Katika kuujenga utu wa mtu kimisionari, kila mbatizwa anatumwa na Kristo: "... Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe" (Mk 16:15); anapokea wito na kwenda kutumika na kutumikia. Utume huo ndio ule wajibu unaotafsiri na kutekeleza ahadi za ubatizo wetu. Katika hili twakuta jinsi Mwenyezi Mungu ametujalia karama mbalimbali na ambazo kwazo yatupasa kuzitumia katika kuwatumikia watu.
58. Waamini wanaitwa kuwa mitume, sio tu kuwa katika vyama vya kitume, bali pia kujenga mayo wa kizalendo katika utume wao. Upendo wa kikristo ndio utakaosaidia kutambua uhusiano wao na Kristo na jirani zao. Hapo ndipo ambapo waamini watajengewa mayo wa kuinjilisha na kuutangaza ufalme wa Mungu kwa watu wote na kumfanya Mungu atawale na kuongoza mioyo ya watu wote. Na hivyo kuwa wajumbe wema kwa maneno na matendo juu ya utu na thamani ya mtu.
59. Waamini wajenge moyo wa kushikamana na wengine, kufanya matendo ya huruma, wenye kuona mahitaji ya wenzake, kuishi kwa upendo na kila mtu pasipo kujali hali yake ya maisha pamoja na eneo la utume. Kwa kufanya hayo waamini wanapata fursa ya kuubadilisha ulimwengu kuanzia mahali pale walipo.
60. Kanisa linaweka wazi mbinu ambazo waamini wanatakiwa kuzitumia iii waweze kuwa mitume na wamisionari katika mazingira wanayoishi. Wawahudumie maskini, walemavu, wasiojiweza, wagonjwa na wazee ambao utu wao umedharauliwa katika ulimwengu wa leo. Wakemee bila kuchoka vitendo vya kikatili dhidi ya mwanadamu kama vile mauaji ya wazee/vikongwe katika baadhi ya maeneo, unyanyasaji kwa wafanyakazi, ajira ambazo hazilingani na umri wa mtoto na mila potofu. Waamini wahakikishe thamani ya utu inakua kati ya wanadamu na kueneza Injili ya uhai wa maisha ya mwanadamu.
61. Wakristo watambue na kufanya kama Bwana wao ambaye "hakuja kutumikiwa bali kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia kwa wengine" (Mk 10:45). Kumbe lazima kuachana na ubinafsi, chuki na mioyo migumu katika kutoa maisha yetu kwa ajili ya wengine. Kristo alikuja duniani si tu kuhubiri bali kutuonyesha njia ya kuufikia ufalme wa mbinguni, yaani ufalme ambao tayari tunauishi, wakati huu uliopo na utakaokuja. Na Yesu mwenyewe ndiye alama za nyakati (rej. Lk 12:54-56).
62. Waamini wawe tayari kutolea maisha yao kwa ajili ya wengine wakimfuata Kristo ambaye anajifunua kama mchungaji mwema na ambaye yupo tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake (rej. Yn 10:11). Utume unatudai kumfanya Kristo atambulikane kwa watu kwa njia ya ushuhuda wa imani yetu kwa matendo mema.
Hitimisho
64. Mwanadamu akumbuke kwamba ana thamani kubwa machoni pa Mungu aliyemuumba kwa sura na mfano wake. Kwa kukataa ufunuo wa Mungu, mwanadamu amejiingiza katika mahangaiko mbalimbali kiasi cha kupoteza sura na mfano wa Muumba wake, kulikopelekea kupoteza utu wake. Kwa njia ya Nena wake, Mungu anaendelea kumwita mwanadamu kurudia asili yake (rej. Ebr 1:1- 2). Ni jukumu la Kanisa kumsaidia mwanadamu kumtazama Mungu na kusikiliza ujumbe wake katika majiundo yanayopitia ngazi mbalimbali za maisha. Jamii yote kwa ujumla ina wajibu wa kushirikiana na Kanisa kuhakikisha kwamba majiundo haya yanatekelezwa kwa kufuata mpango wa Mungu.
SURA YA TATU "KUFANYWA IMARA KATIKA UTU ... "
Utangulizi
65. Utu ni hali ya kuwa na tabia nzuri iliyomo ndani ya mwanadamu inayomwezesha kutenda matendo yanayompendeza Mungu, bila kusahau wanadamu wenzake; ni zawadi ambayo Mungu amempatia mwanadamu tangu kuumbwa kwake. Ni dhahiri mwanadamu anahitaji sana neema ya Mungu iii aweze kutunza zawadi hiyo. Pasipo Mungu mwanadamu hukengeuka na kufuata akili, vionjo na hisia zake katika utendaji wake na kujikuta anapoteza hii zawadi adhimu. Matokeo yake chuki, wivu, kiburi, mauaji, na mambo mengine mengi maovu hutawala.
Kufanywa imara katika utu
66. Ni kuwa tayari kuingizwa katika Fumbo la Ukombozi wetu yaani, mateso, kifo na ufufuko wake Kristo. Tunapaswa kujifunza kila jambo kutoka kwa Yesu Kristo aliye mwalimu na kiongozi wetu iii kufanywa imara. Tunapaswa kuungana na Kristo kama tawi linavyoungana na mti kama Kristo mwenyewe anavyotualika, "Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote" (Yn 15:4-5).
67. Kristo Yesu anao uwezo wa kutufanya imara katika utu, yaani uwezo wa kuweza kuteseka au kujitoa bila ya kutazamia faida binafsi bali faida ya wengine (rej. Mk 10:45). Huu ni mwaliko ambao Bwana wetu Yesu Kristo anampa kila mbatizwa kuishi maisha yenye faida pia kwa wengine. Ni kipindi cha kujikatalia yote yanayotuweka mbali na Mungu, tukitafakari gharama aliyoingia Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu.
68. Maandiko Matakatifu yanatufundisha kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, hivyo tunapaswa kuwa na tabia za Kristo kwa kuwa sio sisi tunaoishi tena bali ni Kristo anaishi ndani yetu, "mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, iii mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena ..." (Rum 6:6-14).
69. Kufanywa imara katika utu ni kutafakari mapenzi ya Mungu ndani yetu. Mtume Paulo katika barua yake kwa Warumi juu ya kukubali kutoa maisha yetu kwa ajili ya wengine, anasisitiza tusifuate kawaida ya dunia hii, bali tugeuzwe na kufanywa upya nia zetu iii tupate kujua mapenzi ya Mungu. Kumbe, tusipojua mapenzi yake ni vigumu kumpendeza Mungu (rej. Rum 12:1-2). Kristo awe kipimo cha utu wetu
70. Kristo Yesu hakujali sana vinavyoonekana kwani alijua vinavyoonekana ni vya muda tu, bali visivyoonekana ni vya kudumu. Ndiyo maana hakujali pale ambapo utu wake wa nje ulipoharibiwa kwa kuwa alijua utu wake wa ndani ndio udumuo milele. Mt. Paulo anatualika kutafakari utu wetu wa ndani bila kujali utu wa nje uliochakaa, kwa kuwa utu wetu wa ndani hufanywa upya siku kwa siku (rej. 2Kor 4:16-18).
71. Kipimo cha utu si fedha au madaraka au elimu; bali ni ustaarabu. Kwa wakristo, kipimo chetu cha ustaarabu kipo katika kuyaangalia maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo, yaani namna alivyowatendea watu wa makundi mbalimbali kwa kuwajali, kuwathamini na kuwatendea kiutu. Mathalani, aliwakumbatia watoto na kusema "waacheni wadogo waje kwangu" (rej. Mt 19:13- 15), kwa wagonjwa na wenye dhambi aliwahurumia na kuwaponya (rej. Lk 5:1-20), kwa wenye njaa aliwalisha (Yn 6:1-15). Ustaarabu wake (utu wake) ulionekana katika maneno na matendo yake ya kila siku.
72. Nasi waamini tunaalikwa kuuonesha utu wetu katika maneno na matendo yetu ya kila siku. Tunahimizwa kuuvua utu wa kale, yaani moyo wa jiwe na kuvaa utu mpya, yaani, moyo wa nyama (rej. Eze 36:26-27). Utu huu mpya ni ule wenye kujali wengine, kusamehe, moyo wa kuchukia wivu na ukatili wa kila aina, wenye kuchukia uchu wa madaraka, usio na usaliti, wenye kuchukia ubinafsi, chuki za kisiasa, moyo wenye kujitoa kwa ajili ya Kanisa na wahitaji.
73. Licha ya matendo yetu ya kila siku, utu wetu hauna budi kuonekana pia katika maneno yetu. Familia zetu ziwe shule za kufundisha utu. Wanafamilia wajifunze kutumia maneno yanayojenga amani, furaha, upendo n.k. Mathalani: Asante: Kusema asante kwa Mungu na kwa wenzetu pale tunapotendewa jambo jema bila ya kujali cheo chako na kuona ni haki yako. Samahani: Kuwa tayari kuomba msamaha na kukiri kosa na kuahidi kujirekebisha, baada ya kutafakari madhara ya kosa ulilotenda. Hii humrejeshea mtu heshima na kumrejeshea amani na furaha moyoni. Tafadhali: Kusema tafadhali bila kujali umri au cheo, ni alama ya unyenyekevu na ni kipimo cha ukomavu kiutu (rej. Mt 11:28; Flp 2:8).
Imani thabiti ni chanzo cha "Utu" wema
74. Imani huleta ujasiri. "Ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana" (Ebr 11:1). Mt. Paulo anasema "Basi imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo" (Rum 10:17). Kristo Yesu aliye chanzo cha utu wema anamwalika kila Mkristo kulinda imani thabiti aliyotuachia.
75. Katika dunia ya leo zipo imani nyingi zilizoibuka na zimekanganya wengi na hasa walio wachanga wa imani ya kweli ya kumfuata Kristo Yesu na mafundisho yake. Watu wengi wameamua kuyapenda maisha ya mkato, wakidhani kuna njia fupi ya kupata furaha. Wanataka Pasaka bila Ijumaa Kuu, huu ni ulegevu wa wazi kabisa wa imani.
76. Wakatoliki wengi kwa kujua au bila kujua wamejikuta wakiamini vitu kama vile nywele, maji, kucha, mafuta, chumvi, udongo, nguo/sanda, na kumwacha Kristo Yesu aliye Mkombozi wa kweli. Wengi wamejikuta wakiweka imani yao katika kutegemea vitu badala ya kuweka imani kwa Mungu. Yoshua anatualika wote kuwa hodari na moyo wa ushujaa, tena tusiogope kwa kuwa Bwana Mungu wetu yupo pamoja nasi (rej. Yos 1:9). Haya yote huondoa utu wa mtu na kumfanya mtumwa wa vitu badala ya kumtumainia Mungu.
77. Ulegevu katika maisha ya kiroho na kukosa kuwa na vipaumbele katika imani yetu kunakosababishwa na uvivu wa kusoma Neno la Mungu, kusali, kuungama mara kwa mara, kuhudhuria Misa Takatifu na kushiriki maisha ya kisakramenti, hupelekea udhaifu unaoweza kumfanya mtu kujizamisha katika imani za kishirikina na ahadi potofu za kupata vitu bila ya kufanyia kazi. Hayo humfanya mtu kupoteza hadhi ya utu wake. Kupenda vitu vya dunia hii hutupelekea kukosa utu kwa kuwa tutakuwa tayari kufanya chochote hata ikiwa ni kuhatarisha maisha ya wengine kwa ajili ya manufaa yetu.
78. Katika kipindi cha Kwaresima kila mkristo anaalikwa kutafakari njia zake kwa kina, hasa kuepuka nafasi za dhambi, kuungama mara kwa mara na kujifunza kutenda mema. Mwanadamu anapaswa kutambua kuwa dhambi hupoteza neema ya Mungu ndani yake na neema ikiondoka anapungukiwa utukufu wa Mungu (rej. Rum 3:23). Hivyo, anapaswa kuilinda hii neema inayowekwa ndani yake na Mungu mwenyewe.
79. Hiki ni kipindi cha kuuvua "Utu" wa zamani na kuvaa Utu mpya. Ni kipindi cha kufanya badiliko la ndani kwa kupambana kuacha dhambi, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu kwamba "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili" (Mk 1:15; rej. Yoe 2:1-12; Ebr 12:4).
80. Ni kipindi cha kusali, kufunga na kufanya matendo mema. Kila muamini anapata wasaa wa kufanya mazoezi ya kiroho yenye lengo la kuuvua utu wa kale; yaani, kukataa dhambi, kujenga mazoea ya kuwa karibu na Mungu kwa njia ya sala, kujitoa kwa ajili ya wengine, kuwaombea wakosefu na kuwasaidia ambao wana mahitaji mbalimbali n.k. (rej. Isa 58:6-7).
81. Kwaresima ni kipindi cha kutafakari zaidi mateso ya Kristo aliye kielelezo cha utu wema. Pia ni kipindi cha kutafakari maisha ya watakatifu ambao ni mashuhuda wa imani yetu, kwani kupitia maisha yao tunajifunza mambo mengi yahusuyo imani yetu, huku tukimtazama Kristo aliye mwanzilishi wa safari yetu (rej. Ebr 12:1).
SURA YANNE TUNAUVUAJE UTU WA KALE?
Utangulizi
82. Ipo tofauti kubwa kati ya "utu wa kale" na "utu mpya." Kwa njia ya ubatizo tumefanywa watu wapya, viumbe vipya. Kuwa "mtu mpya" maana yake ni kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kuuvaa "utu mpya" ni kule kuenenda kadiri ya Roho wa Mungu, na hivyo ni kuishi na kuongozwa na Roho Mtakatifu; kunakomwezesha mtu kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo ni "mapendo, furaha, imani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi" (Gal 5:22-23).
83. Kuvaa "utu mpya" ni kule kufikiri kama Kristo na kumwiga Kristo. Kipimo cha "utu mpya" ni Kristo; ni kuishi maisha mapya ndani ya Kristo; ni kule kumpokea Kristo na kukaa ndani yake.
84. Wakati "utu mpya" ni kumpokea Kristo, kumwiga na kuenenda kadiri ya matakwa yake; "utu wa kale" ni kule kuishi katika dhambi na ni matokeo ya dhambi. Ni kule kuongozwa na kutenda kadiri ya mwili. Mt. Paulo anataja baadhi ya mambo yanayomfanya mtu kuenenda kadiri ya mwili. Ndiyo: "uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mabishano, mafarakano, husuda, ulevi, ulafi, na mambo mengine kama hayo" (Gal 5:19-21).
Kuuvua "utu wa kale"
85. Hatuna budi kufahamu kwamba kazi inayohusisha kuvaa "utu mpya" haianzi na kuisha kwa tendo la ubatizo tu, bali ni tendo linalopaswa kuwa la kudumu maisha yote ya mkristo. Tunahitaji kuendelea kudumisha "utu mpya" siku zote ya maisha yetu. Yapo mambo kadhaa yanayoweza kutusaidia kuudumisha "utu mpya" ambayo ni:
Neno la Mungu
86. Kwa Neno lake Mungu aliumba kila kitu (rej. Mwa 1:1-31). Neno hilo ni taa katika maisha yetu ya kiroho. Tunapoangazwa na Neno la Mungu tunawezeshwa kuona maovu si tu yaliyo ndani mwetu, bali hata yale yanayotuzunguka. Mzaburi anatuambia "Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu" (Zab 119:105). Neno la Mungu hutuangaza iii tuweze kuuvua "utu wa kale" na kurudi tena katika "utu mpya," hutuwezesha kusema na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu.
87. Mtakatifu Yakobo anaandika akisema "Msijidanganye wenyewe, kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo. Yeyote anayelisikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo. Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo ..." (Yak 1:22-25). Kama kioo, Neno la Mungu linatusaidia kujitazama na kujichunguza na hivyo kutupatia nafasi ya kujirekebisha (kuuvua utu wa kale). Kazi ya Neno la Mungu ni kuwa kioo kwetu na kutusaidia kutazama ndani ya mioyo yetu (rej. Yak 1:23). Hata hivyo iii tuweze kuuvua "utu wa kale" hatuna budi kufanya maamuzi magumu; vinginevyo tutakuwa kile asemacho Mt. Yakobo kwamba mtu "Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, mara husahau jinsi alivyo" (Yak 1:24).
88. Neno la Mungu huumba na huunda. Kama vile Mungu alivyoumba ulimwengu na vyote vilivyo ndani yake kwa neno lake (rej. Ebr 11:3; Zab 33:9), hata sasa neno la Mungu lina nguvu ya 'kutuumba na kutuunda upya.' Ni Neno hilo ambalo baada ya kutuumba linaendelea kututakasa kama vile Kristo alivyomtakasa yule mkoma kwa kumwambia, " ... Nataka, takasika" (Mk 1:41). Neno la Mungu ni kama moto unaowaka moyoni mwa mtu (rej. Yer 20:19). Kama moto utakasavyo, neno la Mungu hutakasa mioyo yetu iii tuachane na maisha ya "utu wa kale" na hivyo tuweze "kuvaa utu mpya".
89. Aidha, Neno la Mungu linatualika kufanya toba iii kumrudia (rej. Mk 1: 15). Ni Neno hilo ambalo linafundisha, linaonya na linarekebisha (rej. 2 Tim 3:16-17). Ni kwa njia ya neno lake, Mungu azungumza na watu wake (rej. KKK 104).
90. Kwa kusoma Neno la Mungu, kusali, kulitafakari na kuliishi, tunasaidiwa kuuvua "utu wa kale." Kwa kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu tunaweza kumfahamu vyema Kristo. Kinyume chake ni kutomjua Kristo kama asemavyo Mt. Hieronimo (Jerome) kwamba kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo. Kwa kulisoma na kulitafakari neno la Mungu tunajenga urafiki na Kristo na hivyo kutoa nafasi ya kuundwa upya na kuvaa utu mpya.
Sala
91. Sala ni kielelezo cha uhusiano binafsi na Yesu; ni kisima tunapochota nguvu za kufanikisha mengi kuhusu maisha yetu ya kiroho. Kuzingatia sala ni sawa na kuchagua fungu lililo bora, mfano wa Maria aliyechagua fungu bora kwa kukaa na Yesu (rej. Lk 10:38-42). Sala ni kuungana na Mungu katika nia na moyo.
92. Katika sala tunamwalika Kristo iii akae kati yetu. Maandiko Matakatifu yanasema " ... walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo hapo hapo kati yao" (Mt 18:20). Uwepo wa Kristo kati yetu ni utakatifu; ni nafasi ya kufanywa wapya na kuutengeneza utu wetu upya. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaielezea sala kama "ni maisha ya moyo mpya" (KKK 2697). Mfano halisi wa sala ambayo hutuunda upya ndani ya Mungu ni ile "Sala ya Bwana" yaani sala ya "Baba Yetu." Katika maadhimisho ya Ubatizo na Kipaimara, Sala ya Bwana "Huashiria kuzaliwa upya katika uzima wa Mungu.... ambapo wale waliozaliwa upya kwa njia ya neno la Mungu lenye uzima, lidumulo milele, wanajifunza kumwita Baba yao kwa lile Nena moja ambalo analisikia siku zote. ... Kanisa linaposali Sala ya Bwana, daima kama taifa la 'waliozaliwa upya' linasali na kupata huruma" (KKK 2769). Kwa njia ya sala Mwenyezi Mungu anatenda mengi katika maisha yetu na hata kutujalia wongofu na kuvaa utu mpya kwa kuuvua utu wa kale.
Maisha ya Kisakramenti
93. Sakramenti zote saba ziliwekwa na Kristo na huadhimishwa na Kanisa iii zituletee neema na kutuunda upya kadiri ya sakramenti husika. Kati ya sakramenti saba, tatu kati ya hizo (Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi) hutuingiza na kutuzamisha kabisa/kikamilifu katika "utu mpya." Kwa njia ya Sakramenti hizi mmoja anapata hadhi mpya, yaani kuwa mtu mpya kwa kuzaliwa kwa maji na
Roho Mtakatifu.
94. Kwa Sakramenti ya Ubatizo tumefanywa "wapya" kwa kuuvua "utu wa kale", utu wa dhambi. Hivyo kila aliyebatizwa amefanywa kiumbe kipya (rej. Kol 3:5-11). Kwa Sakramenti ya Ubatizo tunapewa neema ya kuzaliwa upya katika Mungu Baba (rej. KKK 683); kwa Ubatizo tunaondolewa dhambi na kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu (rej. KKK 1262); kwa Ubatizo tunafanywa "kiumbe kipya" na kuwa wana wa Mungu, warithi pamoja na Kristo (rej. KKK 1265).
95. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaendelea kufundisha kwamba "Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru kutoka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki wa utume wake" (KKK 1213). Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tunashirikishwa fumbo la Pasaka la Kristo kwani "tulizikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo nasi tuenende katika utu wa uzima" (Rum 6:4). Huku ndiko kuzaliwa mara ya pili au kwa maji na Roho Mtakatifu ambako Kristo alimwambia Nikodemo kama njia pekee ya kuurithi ufalme wa mbinguni (rej. Yoh 3:1-7).
96. Kwa Sakramenti ya Kipaimara tumefanywa askari hodari wa kuyalinda matakatifu na hasa kuulinda na kuupigania "utu wetu mpya" usiharibiwe na yule mwovu. Kwa Sakramenti ya Upatanisho, Padre anapotamka "Nami nakuondolea dhambi zako..." anayeondolewa dhambi "anauvua utu wa kale," utu wa dhambi, na "kuvaa utu mpya," utu wa neema.
Hitimisho
97. Kwaresima ni kipindi mahsusi cha kujitafakari upya undani wa maisha yetu. Ni kipindi cha "Kuvua utu wa kale" na "kuvaa utu mpya." Ni kipindi cha kuishi ushauri wa Mt. Paulo asemaye "Basi, komesheni kabisa kila kitu kilicho ndani yenu ambacho chahusika na mambo ya kidunia: uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu ambao ni sawa na kuabudu sanamu" (Kol 3:5). Katika dhamira ya "kuvua utu wa kale" na "kuvaa utu mpya" Mt. Paulo anaendelea kushauri akisema "Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani utu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa za udanganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionyesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu" (Efe 4:22-24). Kwa lugha ya mwaliko wa Kwaresima, "kuvua utu wa kale" na "kuvaa utu mpya" ni kurarua mioyo na si mavazi.
HITIMISHO
98. Kama alivyofanya Mt. Paulo akiwajulisha wakristo wa Efeso kwamba wanahitaji maombezi, nasi pia Maaskofu wenu tunawaombea mjaliwe kufanywa imara katika utu. Kupitia maombi na sala zetu wakati wa Kwaresima, tunaendelea kuwaombea mjaliwe neema au mpate baraka, kutoka kwa Mungu; mtengenezwe kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, yaani mfinyangwe na Mungu mwenyewe, pasipo kutegemea juhudi zenu tu.
99. Waefeso walikuwa ni jamii ya mchanganyiko wa watu wenye tamaduni, tabia, falsafa, desturi na mila mbalimbali; vivyo hivyo maisha ya mkristo (mkatoliki) wa leo yanakabiliwa na changamoto ambazo zinaweza kuwadhoofisha waamini wetu wa sasa ambao wanahitaji kuwa imara.
100. Tunawaombea na kuwasihi muwe imara katika utu. Utu ni sifa ya kitabia au kihulka ya hadhi ya mwanadamu. Sifa hii hujidhihirisha kwa njia ya moyo, akili na utashi wa mwanadamu. Kumbe kuwa imara katika utu ni kuwa na moyo imara, akili imara na utashi imara; yaani kutotetereka kwa kutokata tamaa. Vile vile ni kutoyumbishwa na mawazo au mafundisho yasiyohusu imani ya kweli (akili nyepesi isiyo pima mambo na kufanya uamuzi tambuzi; yaani na kwa kutokuwa na msimamo (utashi wenye kigeugeu).
101. Wakristo, kwa ujumla, tunahitaji kukua na kuimarika katika ukristo wetu na hekima ya Mwenyezi Mungu tukifuata mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ndivyo anavyotuandikia hivi mwinjili Luka akisema: Naye Yesu akazidi kukua/kuongezeka katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu (rej. Lk 2:52). Kama Yeye aliyekuwa Mungu-mtu alihitaji kuongezeka katika hekima iweje sisi leo.
102. Wapendwa wana familia ya Mungu, leo tuko kama Waefeso: tunahitaji kuombeana kwani tunaishi katika mazingira kama yao: tamaduni mbali mbali zenye majaribu mengi, tabia binafsi zisizojali utu wa wengine, falsafa za utandawazi zisizokuwa na mipaka katika maadili, desturi zisizokuwa na taratibu na staha, na imani zinazotikisa ukatoliki. Kwaresima hii itukumbushe udhaifu wetu, na tuombeane tuwe imara: tusitetereke katika mioyo yetu; tusiyumbishwe na mafundisho potofu; na tuwe na msimamo usiokuwa na "ugeugeu" katika akili na utashi wetu.
Ni sisi Maaskofu wenu.
1. Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu, Mbeya
2. Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Geita.
3. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora
4. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa' ichi, Ofm Cap, Dar es Salaam.
5. Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap Dodoma
6. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu, Songea
7. Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, Arusha
8. Mhashamu Askofu Mkuu Renatus Nkwande, Mwanza
9. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa
10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
11. Mhashamu Askofu Augustina Shao, Zanzibar
12. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
13. Mhashamu Method Kilaini Msimamizi wa Kitume, Bukoba
14. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS, Moshi
15. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
16. Mhashamu Almachius Rweyongeza, Kayanga
17. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same
18. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
19. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Mpanda
20. Mhashamu Askofu Bernadine Mfumbusa, Kondoa
21. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
22. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Mtwara
23. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, Kigoma
24. Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi, Arusha)
25. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga
26. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida
27. Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Sumbawanga
28. Mhashamu Askofu Antony Lagwen, Mbulu
29. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, Tunduru-Masasi
30. Mhashamu Askofu Simon Masondole, Bunda
31. Mhashamu Askofu Lazarus Msimbe, S.D.S., Morogoro
32. Mhashamu Askofu Henry Mchamungu, (Askofu Msaidizi Dar es Salaam)
33. Mhashamu Askofu Stefano Musomba, (Askofu Msaidizi Dar es Salaam)
34. Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa, Lindi
35. Mhashamu Askofu Christopher Ndizeye, Kahama.
YALIYOMO
VIFUPISHO iv
UTANGULIZI (UJUMBE WA KWARESIMA 2023} 1
SURA YA KWANZA
MAANDIKO MATAKATIFU NA MAFUNDISHO YA KANISA JUU YA UTU
A. MAANDIKO MATAKATIFU 3
Kuvaa utu mpya 3
Matokeo ya kuvaa utu mpya 4
B. MAFUNDISHO YA KANISA JUU YA UTU WA KALE NA MPYA 6
Maandiko ya Mt. Yohane Krisostom (347-407) 6
Maandiko ya Mt. Agustino wa Hippo (354-430) 7
Mtakatifu Paul VI, Papa 9
Mtakatifu Yohane Paul II, Papa 10
Papa Fransisko 10
SURA YA PILI UTU UNAUNDWAJE?
Malezi ya kimwili 13
Malezi ya kiroho 14
Malezi ya kiakili 15
Malezi ya kisaikolojia 17
Malezi ya kichungaji 18
Malezi ya Kitume 19
SURA YA TATU "KUFANYWA IMARA KATIKA UTU..."
Kufanywa imara katika utu 22
Kristo awe kipimo cha utu wetu 23
Imani thabiti ni chanzo cha "Utu" wema 24
SURA YA NNE TUNAUVUAJE UTU WA KALE?
Kuuvua "utu wa kale" 27
Neno la Mungu 28
Sala 29
Maisha ya kisakramenti 30
HITIMISHO
[ Photo Embed: Imani thabiti ni chanzo cha utu wema]
VIFUPISHO
1. Ebr - Waebrania (Waraka kwa Waebrania)
2. Efe - Waefeso (Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Waefeso)
3. Eze - Ezekieli (Kitabu cha Nabii Ezekieli)
4. Flp - Wafilipi (Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wafilipi)
5. Gal - Wagalatia (Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia)
6. Isa - Isaya (Kitabu cha Nabii Isaya)
7. KKK - Katekisimu ya Kanisa Katoliki
8. Kol - Wakolosai (Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wakolosai)
9. lKor - Wakorintho wa Kwanza (Waraka wa Kwanza wa Mt. Paulo kwa Wakorintho)
10.2Kor - Wakorintho wa Pili (Waraka wa Pili wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho)
11. LG - Lumen gentium (Mwanga wa Mataifa-Hati ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican)
12. Lk - Luka (lnjili ya Mtakatifu Luka)
13. Mit - Mithali (Kitabu cha Mithali)
14. Mk - Marko (Injili ya Mtakatifu Marko)
15. Mt - Mathayo (Injili ya Mtakatifu Mathayo)
16. Mwa - Mwanzo (Kitabu cha Mwanzo)
17. Rej. - Rejea
18. Rum - Warumi (Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Warumi)
19. lTes- Wathesalonike wa Kwanza (Waraka wa Kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wathesalonike)
20. 2Tim - Timotheo wa Pili (Waraka wa Pili wa Mtakatifu Paulo kwa Timotheo)
21. Ufu - Ufunuo (Kitabu cha Ufunuo wa Yohane)
22. VMJ - Vyama vya Kitume
23. Yak - Yakobo (Waraka wa Mtakatifu Yakobo kwa watu wote)
24. Yer - Yeremia (Kitabu cha Nabii Yeremia)
25. Yn - Yohane (lnjili ya Mtakatifu Yohane)
26. Yoe - Yael (Kitabu cha Nabii Yael)
27. 1Yoh - Waraka wa Kwanza wa Mtakatifu Yohane kwa watu wote.
28. Yos - Yoshua (Kitabu cha Nabii Yoshua)
29. Zab - Zaburi