Tafuta

Kanisa Kuu la Westmister nchini Uingereza. tarehe 24 Januari 2023 sala ya kiekumene imefanyika kumuombea Papa Benedikto XVI. Kanisa Kuu la Westmister nchini Uingereza. tarehe 24 Januari 2023 sala ya kiekumene imefanyika kumuombea Papa Benedikto XVI. 

Uingereza:sala ya masifu kwa kukumbuka Hayati Papa Benedikto XVI

Tarehe 24 Januari 2023,masifu ya jioni kiekumene yalifanyika katika Kanisa Kuu la Westminster nchini Uingereza,ambalo ni Kanisa Mama la Wakatoliki lililoko jijini London ili kumkumbuka Hayati Papa Benedikito XVI ambaye alifanya ziara yake mnamo 2010.

Na Angella Rwezaula; - Vatican.

Katika sala ya kiekumene kwenye masifu ya jioni iliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu wa Uingereza na Walles jioni tarehe 24 Januari 2023 katika Kanisa Kuu la Westmister  aliyeongoza alikuwa ni Kardinali Vincent Nichols, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Uingereza na wakati mahubiri yaliongozwa na Askofu Mkuu wa Kianglikan, Lord Rowan Williams, ambaye aliwahi pia kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury. Ni katika muktadha wa kufanya kumbukumbu ya  kifo cha Hayari Papa mstaafu Benedikto XVI aliyeaga dunia mnamo tarehe 31 Desemba 2022. Hata hivyo viongozi hao wawili, pamoja na Malkia Elizabeth na mme wake Filippo wakati bado wanaishi, walimpokea, Hayati Papa Benedikto XVI wakati wa ziara yake ya kitume huko Uingereza mnamo mwaka 2010.

Walioshiriki masifu ya jioni, yaliyokwenda  sambamba na Juma la Kuombea Umoja wa Kikristo ni pamoja na maaskofu 14 wakatoliki wa Uingerezea na Scotland, ambamo miongoni mwake, kuna maaskofu wakuu wa Liverpool, Birmingham na Cardiff, Malcolm McMahon, Bernard Longley na  Mark O’Toole.  Waliowakilisha Kanisa la Kianglikani la  Uingereza zaidi ya Askofu Mkuu Lord Williams, alikuwapo  pia Askofu Mkuu Justin Welby wa Canterbury, ambaye ni mkuu wa Kanisa hilo na wa kule  York, Stephen Cottrell, pamoja na Askofu Sarah Mullally wa London; vile vile  walishiriki pia maaskofu wa wakuu wa kiorthodox nchini Uingereza Nikitas (Lulias) wa Thyateira na wawakilishi wa Kanisa la Wametodi, wa Kanisa la Jeshi la Wokovu, wa Kanisa huru na hatimaye Jumuiya ya Kiislamu na Kiyahudi.

Tukirudi katika kumbu kumbu ya ziara ya kitume ya  Papa Mstaafu Benedikito XVI mnamo 2010 iliyoanzia Scotland, ilikuwa ya kusisimua. Jambo msingi lilikuwa la kutangaza Mtumishi wa Mungu  John Henry Newman,  kuwa Mwenyeheri mnamo tarehe 19 Septemba. Katika mahubiri yake Papa Mstaafu alisema:  Injili iliyosomwa ilikuwa inaeleza  kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa mtumishi wa mabwana wawili (rej. Lk 16:13), na mafundisho ya Mwenyeheri John Henry juu ya sala yanaeleza jinsi Mkristo mwaminifu anavyojiweka kwa uhakika katika utumishi wa Bwana wa pekee wa kweli, ambaye peke yake kuna haki ya ibada yetu bila masharti (Mt 23:10). Kwa njia hiyo Newman alisaidia kuelewa inamaanisha nini katika maisha yetu ya kila siku: kwamba Bwana wetu amekabidhi kazi maalum kwa kila mmoja wetu, ile huduma iliyofafanuliwa vizuri, iliyokabidhiwa kwa kila mtu pekee kwa hiyo: “mimi nina utume, Mimi ni pete katika mnyororo, kifungo cha uhusiano kati ya watu. Yeye hakuniumba bure hata kidogo. Nitafanya mema, nitafanya kazi yake; Nitakuwa malaika wa amani, mhubiri wa ukweli katika nafasi yangu hasa… nikifanya hivyo nitatii amri zake na kumtumikia katika wito wangu” (Tafakari na ibada, 301-2).

Papa Benedikto XVI akiendelea katika mahubiri hayo kuhusiana na tamaduni ya kidini  pia alisema:  “Uingereza ina desturi kubwa ya watakatifu wafia dini, ambao ushuhuda wao wa kijasiri umedumisha na kutia moyo jumuiya ya Wakatoliki, wakazi  kwa karne nyingi. Na bado leo hii ni sawa wanafaa, kwani  tunatambua utakatifu wa muungamishi, mwana wa taifa hilo ambaye, ingawa hakuitwa kumwaga damu yake kwa ajili ya Bwana, lakini  alimtolea ushuhuda fasaha wakati wa maisha marefu yaliyowekwa wakfu kwa huduma ya ukuhani, hasa katika kuhubiri, kufundisha na kuandika. Kwa hiyo inastahili kuchukua nafasi yake katika safu ndefu ya Watakatifu na Walimu wa  visiwa hivyo, kwa mfano Mtakatifu Beda, Mtakatifu Hilda, Mtakatifu Aelred, Mwenyeheri Duns Scotus bila kutaja wote. Na katika  Mwenyeheri John Henry, mapokeo hayo ya neema ya kufundisha, ya hekima kuu ya kibinadamu na upendo mwingi kwa Bwana, yalizaa matunda mengi kama ishara ya kuendelea kuwapo kwa Roho Mtakatifu ndani ya mioyo ya watu wa Mungu, na kuleta karama nyingi za utakatifu.

Papa Mstaafu Benedikto XVI katika mahubiri hayo kwa waingereza alisema: “Ingawa wosia wa kitaaluma wa John Henry Newman ndio uliochukua nafasi kubwa ya uangalifu zaidi katika fasihi pana juu ya maisha na kazi yake, lakini alipendelea katika  fursa hiyo kutafakari ufupi juu ya maisha yake kama kuhani na mchungaji wa kiroho. Uchangamfu na ubinadamu ulioweka msingi wa uthamini wake wa huduma ya kichungaji ulioneshwa kwa uzuri katika hotuba nyingine maarufu kwa mfano: “Kama malaika wangekuwa makuhani wenu, ndugu wapendwa, hawangeshiriki mateso yenu, wala kuteseka,  wala kuwahurumia na kutafuta sababu za kukuhalalisha, tuwezavyo; wasingeweza kuwa vielelezo na viongozi wao, na kuwaongoza kutoka katika hadhi zao za  zamani hadi kwenye maisha mapya, kama wale walio katika malezi yao hayo wanavyoweza (“Men, not Angels: the Priests of the Gospel,” Hotuba kwa mashirika  mchanganyiko, 3 )

Kwa hiyo Papa Benedikto XVI aliongeza kusema kwamba  Mwenyeheri huyo  aliishi maono yale ya kina ya kibinadamu ya huduma ya kikuhani katika huduma ya kujitoa kwa watu wa Birmingham katika miaka aliyotumikia huku akijikita katika kituo alichokianzisha, akiwatembelea wagonjwa na maskini, akiwafariji walio maskini na kuwajali waliofungwa. Haishangazi kwamba baada ya kifo chake maelfu ya watu walijipanga kwenye mitaa huku mwili wake ukichukuliwa kwenda kuzikwa umbali wa nusu maili kutoka hapo.  Miaka mia moja na ishirini baadaye, Papa Mstaafu Benedikito XVI alibainisha kuwa makutano makubwa yalikusanyika hapo tena ili kushangilia na Kanisa  katika kukiri kwa dhati utakatifu wa kipekee wa baba wa kiroho aliyependwa sana. Ni njia gani bora zaidi ya kueleza furaha ya wakati huu kuliko kuongea na Baba yetu wa Mbinguni kwa shukrani kutoka moyoni, kwa kuomba  kwa maneno yaliyowekwa na Mwenyeheri John Henry Newman kwenye midomo ya kwaya za malaika Mbinguni.

Na katika hotuba  kwa serikali ya  Westminster ambapo  wakati akihutubia alipigiwa makofu kwa muda mrefu, Papa Benedikto XVI alisema:  “Katika mchakato huu wa kihistoria, Uingereza imeibuka kama demokrasia ya vyama vingi, ikiweka thamani kubwa juu ya uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujiunga na siasa na kuheshimu utawala wa sheria, kwa hisia kali za haki na wajibu wa mtu binafsi, na usawa wa wote, wananchi mbele ya sheria. Mafundisho ya kijamii ya Kikatoliki, ingawa yametungwa katika lugha tofauti, yana mambo mengi yanayofanana na mtazamo huo, ikiwa mtu atazingatia hangaiko lake kuu la kulinda hadhi ya  kila mtu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na mkazo wake wa wajibu wa mamlaka za kiraia ili kukuza manufaa ya wote.“Dini, kwa maneno mengine, si tatizo la wabunge kutatua, bali ni mchangiaji muhimu wa mijadala ya umma katika taifa.

Papa Mstaafu Benedikito XVI aidha alisema “Katika muktadha huu, ninaweza tu kueleza wasiwasi wangu katika kukabiliana na kuongezeka kwa kutengwa kwa dini, hasa kwa Ukristo, ambako kunashika kasi katika baadhi ya sehemu mbali mbali, hata katika nchi ambazo zinathamini sana uvumilivu. Kuna wengine wanaobisha kwamba sauti ya dini inapaswa kunyamazishwa, au angalau ishushwe kwenye nyanja ya faragha. Kuna wengine wanaobisha kwamba sherehe za hadharani za sikukuu kama vile Noeli zinapaswa kukatishwa, kwa imani yenye kutiliwa shaka kwamba huenda zikawaudhi kwa njia fulani wale wa dini nyingine au zisiwaudhi. Na bado kuna wengine ambao  kwa utata kwa lengo la kuondoa ubaguzi, wanaamini kwamba Wakristo walio na ofisi ya umma wanapaswa, katika hali fulani, kutenda kinyume na dhamiri zao. Hizi ni dalili zinazotia wasiwasi za kushindwa kutilia maanani ipasavyo si tu haki za waamini kwa uhuru wa dhamiri na dini, bali pia jukumu halali la dini katika nyanja ya umma.

Kwa hivyo Papa Benedikto XVI alipenda kuwaalika wote , kila mmoja katika nyanja zake za ushawishi, ili kutafuta njia za kukuza na kuhimiza majadiliano kati ya imani na hoja katika kila ngazi ya maisha ya kitaifa. Yeye alikuwa na uhakika kwamba katika nchi hiyo pia kuna nyanja nyingi ambazo Kanisa na mamlaka za umma zinaweza kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya raia, kwa kuzingatia desturi ya kihistoria ya Bunge hilo  la kuomba mwongozo wa Roho kwa wale wanaotaka kuboresha hali ya maisha ya wanadamu wote. Ili ushirikiano huu uwezekane, taasisi za kidini, zikiwemo zile zinazofungamana na Kanisa Katoliki, hazina budi kuwa huru kutenda kulingana na kanuni na imani zao maalumu , zinazoegemezwa katika imani na mafundisho rasmi ya Kanisa. Kwa njia hii haki hizo za kimsingi zinaweza kuhakikishwa, kama vile uhuru wa kidini, uhuru wa dhamiri na uhuru wa kujumuika. Malaika wanaotutazama kutoka kwenye nafasi nzuri sana ya Jumba hilo la kale linakumbusha utamaduni wa muda mrefu ambao Bunge la Uingereza limesitawisha. Wanakumbusha kwamba Mungu anatuangalia daima, ili kutuongoza na kutulinda. Na wanatuita kutambua mchango muhimu ambao imani ya kidini imetoa na inaweza kuendelea kutoa kwa maisha ya taifa”.

Sala ya Kiekumene Uingereza kuombea Papa Benedikto XVI
25 Januari 2023, 15:13