SECAM:Kundi la wataalam katika kikao cha II cha kazi ya Sinodi kibara!
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Katibu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM), kwa kushirikiana na Initiative for African Synodality (ASI), yaani Mpango wa Sinodi kwa ajili ya Afrika, wanayo furaha kuwatangaza wote juu ya mkutano wa kundi la wataalam kutoka bara la Afrika kwa ajili ya kikao cha kazi ya pili ya Sinodi ya kibara kuhusu Sinodi, inayofanyika kuanzia tarehe 23 Januari hadi 25 Januari 2023 katika Jumba la AFRICAMA, jijini Nairobi, Kenya. Mkutano huo unafuatiwa na sehemu ya kikao cha kwanza kilichofanyika mjini Accra, nchini Ghana kuanzia tarehe 6 hadi 9 Desemba 2022, ambapo timu ya Bara ilitafakari kuhusu Hati ya Hatua ya Mabara (DTC) iliyoandaliwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Vatican. Kutokana na mktadaha huo katika kikao cha kwanza, timu ya bara iliithamini hati hiyo (DTC) katika muktadha wa masuala yaliyojitokeza kutoka katika makanisa kwenye ripoti za kikanda na kufafanuliwa rasimu ya waraka wa kisinodi wa bara la Afrika. Kikao hicho cha Pili kwa maana hiyo ni njia ya kusikilizana na ya Roho Mtakatifu, ambayo itashuhudia timu ikijitolea katika: kufafanua upya hati ya sinodi ya bara la Afrika na ufahamu mpya unaotoka katika Makanisa mahalia; na kujadili mpango unaowezekana wa mkutano wa Sinodi ya Bara la Afrika uliopangwa kufanyika Juma la kwanza la mwezi Machi 2023 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Hata hivyo kabla ya mkutano huo, kilifanyika kikao kwa njia ya mtandao ambacho kiliwaleta pamoja Makatibu wakuu kutoka mabaraza ya Maaskofu wa Kanda mbali mbali za mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu ambayo yanaunda Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM). Viongozi wa Kanisa walishirikishana baadhi ya changamoto na matokeo yaliyopatikana katika Afrika kwenye mchakato wa sinodi. Wakati wa hatua ya pili ya mchakato wa sinodi, Kanisa hata hivyo linawaalika mabara mbalimbali kuendelea kupambanua na kusikiliza sauti ya Roho kwa kutumia Hati ya kitendea Kazi kwa ajili ya Hatua ya Kibara. Akizungumza wakati wa kikao mtandaoni ambacho kilikubaliwa na sekretarieti kuu ya Roma na SECAM, Askofu Luis Marín de San Martín, wa Shirika la Mtakatifu Augustino(OSA), ambaye ni Katibu Msaidizi wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi alibainisha kwamba kanda ya Afrika inapaswa kutambua kipengele cha tofauti za kiutamaduni katika mchakato wa sinodi hasa wanaposikilizana wao kwa wao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Na hii kwa kuongeza alisema na kama vile Neno la Mungu lilivyo jikita ndani yake katika historia, hivyo hivyo hata mchakato wa Sinodi unahitaji hatimaye kuchukua maamuzi ambayo yanatambua na kurutubishwa na tofauti za kiutamaduni za Afrika na mabara mengine. Na utofauti huo wa kiutamaduni utalitajirisha Kanisa la ulimwengu wote.
Katika kuwasilisha kwa waandishi wa habari juu ya tafakari ya kwanza ya awamu ya mwisho ya hatua ya bara kwa Makatibu wakuu wa Sinodi ya Afrika, walieleza changamoto ambazo karibu zinazofanana kwa bara zima. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA), Padre Anthony Makunde, kuhani wa Tanzania, alisema kuwa: “Mchakato wa usikilizaji unafanyika katika mazingira ya mchanganyiko wa jamii, hivyo eneo hilo halina mazingira ambapo hata kama Wakatoliki ni wengi lakini kuna mchanganyiko wa madhehebu”. Akitaja maeneo mengine yenye changamoto, Padre Makunde alisema imani za kijadi bado ziko hai katika nchi mbalimbali, hivyo kuwashawishi wasikilizaji, na idadi kubwa ya nchi zina migogoro ya kisiasa inayoambatana na misimamo mikali ya kidini ambayo imekithiri katika mabaraza mbalimbali. Zaidi ya hayo, Padre Makunde alibainisha kwamba: “Kanisa linapaswa kufanya zaidi kuimarisha dhana ya Kanisa kama familia ya Mungu kwa kurejea kwenye misingi ya ndoa na maisha ya familia, kwamba kuna wasiwasi juu ya hali ya kuishi pamoja na kuwa na uhusiano wa kimapenzi bila kuoana, kuoa mapema, ndoa za mitala na kulazimishwa na ndoa za utotoni.”
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mnamo Jumanne, tarehe 17 Januari 2023, walibainisha kwamba Kanisa Barani Afrika liliweka nuru juu ya utume na uinjilishaji na juu ya uhusiano na mashirika ya kiraia, hasa na utamaduni, siasa na haki na hitimisho lilionesha hitaji la kuwasindikiza watu ili kwamba Kanisa linaweza kuchangia maendeleo ya jamii. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikutano baina ya Kanda za Maaskofu wa Kusini mwa Afrika (IMBISA), Padre Rafael Baciano Sapato alisisitizia juu ya kuimarisha sura ya familia barani Afrika na juu ya utamaduni wa kiafrika. Kwa mujibu wake alisema kuwa: “sura tuliyo nayo katika eneo letu bado ni Kanisa kama familia. Tuna matumaini kwamba mchakato huu utaimarisha sura ya familia, kwa kuwa kila mtu anazingatia sinodi. Kwa maana hiyo “tunahitaji kwenda mbele katika suala la utamaduni. Hadi sasa tunatambua kwamba elimu ya kiutamaduni inahusiana zaidi na liturujia, lakini kuna mambo mengine ya imani yetu ambayo yamejikita katika utamaduni wetu,"aliongeza kusema kuhani wa Jimbo la Lichinga nchini Msumbiji.
Katika kikao hicho kwa njia ya mtandao kilitanguliwa na mkutano wa kwanza wa bara ambao ulifanyika jijini Accra, Ghana kabla ya ule wa pili ambao unaendelea nchini Kenya kuanzia tarehe 23-25 Januari 2023 na hatimaye Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, litaadhimisha Sinodi kwa Kanisa la Bara la Afrika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Machi 2023 huko mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Mkutano wa mwisho wa Sinodi ya Bara la Afrika na Madagascar (SECAM) utajumuisha wajumbe 155: wanawake walei 27, wanaume26, wasichana 16, wavulana 16, waseminari 5, wanovisi 5, mabruda 8, watawa 12, mapadre 18, maaskofu 15 na makadinali 7.
Katika hilo Awamu ya Pili ni muhimu sana katika mchakato wa utambuzi wa dhana ya Sinodi, jinsi ambavyo Kanisa linatembea katika umoja na kudadvua avipaumbele vya Makanisa mahalia, ili hatimaye, kuweza kupata mang’amuzi ya pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikishano na mshikamano wa udugu kati ya watu wa Mungu. Katika milenia ya tatu, Kanisa litambua vema juu ya uwepo wa shida, changamoto na mivutano inayosimikwa mizizi yake katika tamaduni pamoja na historia za watu mahalia. Na ikumbukwe Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi katika ngazi ya Kimabara ilianzia mwezi Septemba 2022 ambayo itahitimishwa kabla ya tarehe 31 Machi 2023.