NIGERIA:Habari za kuuawa kwa Padre Isaac Achi jimboni Minna
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Kwa mujibu wa polisi wa nchi ya Nigeria wamebainisha kuwa Paroko wa Parokia, Padre Isaac Achi alikufa kwa kuchomwa moto uliosababishwa na majambazi waliojaribu kuingia katika makazi ya Parokia ya Mtakatifu Petro na Paulo, huko Kafin-Koro, Jimbo katoliki la Minna Mkoa wa Paikoro, wakati Paroko msaidizi wake Collins akidaiwa kupigwa risasi mgongoni wakati akijaribu kukimbia na sasa amelazwa hospitalini. Kwa sasa wameanzisha uchunguzi ili kuwakamata washambuliaji.
Kabla ya mapambazuko ya Dominika 15 Januari 2023, asubuhi, katika eneo hilo nchini Nigeria, kundi la majambazi lilivamia makazi ya Parokia ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro na Paulo, huko Kafin-Koro, katika jimbo la Minna, mkoa wa Paikoro na kumuua Padre Isaac Achi na kumjeruhi mshiriki wake Padre Collins katika mgongo wake kwa risasi alipokuwa akijaribu kutoroka. Vikosi vya ulinzi na usalama vilipowasili, wavamizi hao waliiacha nyumba hiyo kwa kuichoma moto na hivyo kusababisha kifo cha Padre Achi.
Akithibitisha kutokea kwa shambulio hilo la kikatili na la kusikitisha lililotokea majira ya saa 3 asubuhi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Jeshi la Polisi katika Jimbo hilo, Bwana Wasiu Abiodun, alisema kuwa majambazi hao walijaribu kuingia kwenye makazi hayo, lakini walishindwa na kuwasha moto kuichoma nyumba, na wakati huo huo Paroko aliuawa kwa kuchomwa moto. Timu za mbinu za kipepelezo za polisi za Kafin-Koro, kwa mujibu wa Abiodun, alithibitisha kuwa zilitumwa mara moja kwenye eneo la tukio, lakini majambazi hao walikimbia kabla hawajafika.
Mwili wa Padre Isaac ulipatikana, na wakati huo Padre Collins alipelekwa hospitali kutibiwa. Kulingana na tovuti ya Jimbo katoliki la Minna ni kwamba alikimbizwa na kulazwa hospitalini kwa haraka. Naye Bwana Ogundele Ayodeji, Kamishna wa Polisi, wa Serikali alituma kikosi cha kulinda eneo hilo na juhudi zinaendelea kuwakamata washambuliaji, huku uchunguzi wa shambulio hilo la kusikitisha ukiendelea.