Mtakatifu Yohane Bosco Baba, Mlezi na Mwalimu wa Vijana wa Kizazi Kipya
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Yohane Bosco, Padre, Baba, Mlezi na Mwalimu wa vijana wa kizazi kipya, anakumbukwa na kuadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari. Ni Padre aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa vijana waliokimbilia mjini Torino, Kaskazini mwa Italia kutafuta fursa za ajira baada ya kutokea kwa Mapinduzi ya Viwanda wakati huo. Kwa kusoma alama za nyakati, akaanzisha mahali pa kuwakutanisha vijana, akawapatia malezi, makuzi na majiundo makini ya kitaaluma na huo ukawa ni mwanzo wa Vituo vya michezo na malezi ya vijana Parokiani “Oratorio”. Mtindo wake wa elimu na makuzi kwa vijana ukawa ni dira na mwongozo wa Mtakatifu Francisko wa Sale, Muasisi wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican. Kila mwaka tarehe 31 ya mwezi Januari Kanisa linafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, Mtakatifu ambaye aliyatoa maisha yake, vipaji vyake, akili zake kwa ajili ya vijana, kama yeye mwenyewe alivyowahi kusema “Kwa ajili yenu nasoma, kwa ajili yenu nafanya kazi, kwa ajili yenu naishi, kwa ajili yenu nipo tayari hata kutoa maisha yangu” (Katiba ya Wasalesiani n. 14). Katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo wa II uliojulikana kama “Iuvenum Patris” aliowaandikia wasalesiani wote katika maadhimisho ya miaka 100 tangu kifo cha Mtakatifu Yohane Bosco, Baba Mtakatifu alimtambua kama “Baba na Mwalimu wa Vijana.”
Mtakatifu Yohane Bosco alizaliwa mnamo tarehe 16 Agosti 1815 na Baba Francesco Bosco na Mama yake Margherita Occhiena, huko Castelnuovo ya Asti, leo hii panaitwa Castelnuovo Don Bosco, Torino Italia. Baba yake alifariki mnamo mwaka 1817 wakati Yohane Bosco akiwa na miaka miwili. Mama yake alijitahidi kuwatunza na kuwalea yeye na kaka zake wawili katika malezi bora. Kufariki kwa baba yake akiwa na umri mdogo kulimfanya Yohane Bosco ajisikie kujitoa zaidi na kuwa baba wa vijana wengi walioteseka na waliokosa mahitaji maalum katika jamii. Akiwa na umri wa miaka 9 Yohane Bosco alipata ndoto ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni kama ufunuo wa utume wake kwa vijana. Ndoto hii ilimpatia mwelekeo maalum wa maisha yake na ndipo baadae aliamua kufuata wito wa upadre na hatimaye kuanzisha shirika kwa ajili ya vijana maskini na wahitaji katika jamii. Mtakatifu huyu ambaye msemo wake maarufu ni “cheza, imba, ruka lakini usitende dhambi” hata baada ya kuwa padre aliendelea kujikita katika kuwatafuta vijana hasa waliokuwa katika hali duni ya maisha; aliwatembelea vijana magerezani na kusikiliza matatizo yao kwa lengo la kuwapa ushauri wa kubadilika ili wawe “Wakristo Wema na Raia Hodari”.
Aliweza kuanzisha kikundi cha vijana alichokiita Oratori na mwanzoni kabisa aliweza kuanza na kijana mmoja tu aitwaye Bartolomeo Garelli tarehe 8 disemba 1841. Alifanya yote haya kwa lengo la kuwasaidia vijana kwa mafundisho na kuwarudisha katika maisha ya uadilifu na ya kiroho. Mnamo mwaka 1859 Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco lilianzishwa rasmi na Don Bosco mwenyewe, na leo shirika hili lina wasalesiani elfu 14 wakiwemo mapadre na mabruda katika mataifa 134 duniani na kila mwaka zaidi ya wanovizi 450 huweka nadhiri za kwanza. Pamoja na kuanzisha Shirika la watawa wa kiume, Mtakatifu Yohane Bosco akishirikiana na Mtakatifu Maria Domenica Mazzarello mwaka 1872 walianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, ili walee wasichana kwa roho ileile aliyokuwa ameanzisha. Kauli mbiu yake ilikuwa “Nipe Moyo mengine yote chukua” (Da mihi animas, cetera tolle) kwa namna hii Mt Yohane Bosco alipenda vijana wake wamjue Mungu na mwisho wafike mbinguni. Kwa kutimiza nia yake hii ya kutaka vijana wamkabidhi mioyo yao, ndipo akaja na mfumo maalum kwenye malezi ya vijana wake, uliojulikana kama Mfumo Kinga ambao ulitokana na upendo wake wa kutaka kuziokoa roho. Huu ni mfumo ambao unamfanya mtu afuate sheria zilizowekwa kwa kuongozwa na upendo ili aweze kuelewa taratibu. Mfumo huu uliundwa na nguzo tatu yaani Upendo, Akili na Dini.
Tunaposheherekea sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco tunaendelea kukumbuka ule utamaduni ambao yeye mwenyewe aliuanzisha wa kutoa ujumbe au kaulimbiu (Strenna) kila mwaka kwa vijana wake na kwa familia nzima ya wasalesiani. Ujumbe huu uliokuwa kama zawadi na tunu uliowaongoza katika maisha yao ili kutafakari yale wanayopaswa kuishi katika shirika na Kanisa zima kwa ujumla. Hivyo utamaduni huu umeendelea hata kwa warithi wote wa Don Bosco na ndio maana hata mwaka huu, yaani mwaka 2023 Mkuu wa Shirika Pd. Àngel Fernàndez Artime anatoa ujumbe kwa vijana na familia nzima ya kisalesiani unaombatana na kaulimbiu (strenna) isemayo: “Kama Chachu katika familia ya binadamu leo. Kipengele cha walei katika Familia ya Don Bosco.” Kumbe ni mwaliko wa makundi yote katika familia ya Wasalesiani, kuanzia watoto, vijana, watawa wote (mapadre, mabruda na masista) wa Shirika la wasalesiani wa Don Bosco na Walei kwa namna ya pekee kuwa chachu katika ulimwengu wetu wa leo kama Kristo anavyotueleza katika Injili ya Mtakatifu Luka: “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.” (Lk 13,21). Mfano wa chachu umetumika na Yesu kufananisha na ufalme wa Mungu. Chachu ni kiungo ambacho hutumika kwa kiasi kidogo sana kwa ajili ya kubadilisha ule unga na kuwa katika hali ya kuumuka. Ndio mwaliko huu ambao Mkuu wa Shirika anauleta kwa kila mmoja katika familia nzima ya Wasalesiani wa Don Bosco, hasa walei, watawa na vijana wote kuwa chachu katika ulimwengu, kwa kueneza Neno na Ufalme wa Mungu. Na kufanya hivi kunahitaji ushirikiano wetu.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican. Chachu hufanya kazi kimya kimya bila kelele yeyote. Mara nyingi mchango wetu katika jamii au ile bidii ndogo tunayoifanya huonekana ni kidogo sana, huonekana na mapungufu mengi sana, lakini ni muhimu sana mbele za Mungu. Hatutakiwi kupima matokeo ya jitihada zetu kwa kuweka thamani ya vile tunavyojitoa kwakuwa Mwenyezi Mungu ndie sababu yetu ya mwisho. Hatutakiwi kuwa ni wenye kuonekana wazuri mbele ya macho ya wanadamu, lakini kuonekana wazuri mbele ya macho ya Mungu. Mungu ndiye pekee anayeweza kuongoza jitihada zetu na kule kuwa kwetu chachu katika unga, ili mkate wa ulimwengu, mkate wa Ufalme wa Mungu uweze kukua na kuwa wenye radha nzuri. Mkuu wa Shirika Pd. Àngel Fernàndez anatukumbusha kuwa ni jukumu letu sote kujenga na kustawisha familia ya wanadamu. Hatutakiwi kuacha mpaka kesho lile zuri tunalopaswa kufanya leo, tukumbuke kuwa familia ya wanandamu ina uhitaji mwingi sana: uhitaji wa amani, upendo, haki, ukweli na undugu, uhitaji wa kutunza mazingira na zaidi ya yote uhitaji wa Mungu. Kumbe tunaitwa kuwa chachu katika hii familia nzima ya wanadamu, katika huu ulimwengu wa leo. Ndicho kile ambacho alikifanya Don Bosco kwa vijana wake. Siku moja wakati wa kuadhimisha sikukuu ya Somo wake na Somo wa Jiji la Torino yaani Mtakatifu Yohane Mbatizaji tarehe 24 Juni 1855, Don Bosco kabla ya siku hiyo, yaani usiku wake, aliwaambia vijana wake “kesho mnataka kunifanyia Sherehe na nawashukuru sana.
Kwa upande wangu nataka niwape zawadi ambayo kila mmoja anatamani. Hivyo ningeomba kila mmoja wenu achukue karatasi na kuandika ile zawadi anayoitaka. Mimi sio tajiri, lakini msiponiomba jumba kubwa la kifahari, nitafanya yote kuwaridhisha.” Alipokweda kusoma kile walichoandika vijana wake alikutana na vitu vya kushangaza. Mmoja wa vijana wake aliomba pipi na chokoleti. Mwingine aliomba apatiwe mbwa mdogo ili aweze kupeleka nyumbani. Mwingine akaomba tarumbeta. Don Bosco alipofungua ile karatasi ya Dominiko Savio alikutana na maneno matatu tu: “Nisaidie kuwa Mtakatifu.” Don Bosco akamwita na kumwambia: “wakati mama anapotengeneza keki, anachanganya vitu tofauti kama vile: sukari, unga wa ngano, mayai, hamira (chachu)… kuwa mtakatifu unahitaji pia kuchanganya kwa pamoja vitu tofauti, navyo ni: kuwa na Furaha, kutimiza wajibu wako wa masomo na sala, kutenda mema kwa wengine.” Kumbe hata sisi tunapofanya mambo haya matatu (kuwa na furaha, kutimiza wajibu wetu na kutenda mema kwa wengine) tunakuwa chachu katika ile sehemu na katika yale mazingira ambayo Mwenyezi Mungu ametuweka. Don Bosco alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika malezi ya vijana, na yote haya yaliwezekana kwakuwa aliweza kuwashirikisha walei wengi katika utume wake. Mtu ambae alikuwa karibu sana ni mama yake mpendwa Mama Margherita ambae alikuwa pia ni mama wa vijana wote wa Don Bosco.
Tunayo mifano mingi pia ya walei ambao ni Watakatifu, kama Mtakatifu Artemide Zatti aliyetangazwa kuwa Mtakatifu miezi michache iliyopita, aliyefanya utume wake kama mlei kwa kuleta upendo na furaha kwa watu wake waliokuja kutibiwa hospitalini; Zafferino Namuncura na Laura Vicunà, Albert Mavelli na Dominiko Savio. Wote hawa wanatuonyesha ni kwa jinsi gani tunaweza kuendelea kufanya kazi katika Ufalme wa Mungu katika hali yeyote ile ya maisha. Ni walei wangapi ndani ya familia ya Wasalesiani katika yale mambo madogo wanayoyafanya wanakuwa chachu katika ulimwengu wa leo? Wanaojitoa katika malezi na elimu kwa vijana kupitia mfano wa Mtakatifu Yohane Bosco? Mlei ni Mkristu ambae anatakatifuza ulimwengu kutoka ndani, anayefanya kazi katika uumbaji na katika kujenga ule Ufalme wa Mungu usioonekana kama chachu. Ewe kijana mpendwa, ewe padre, ewe mtawa, ewe Baba na Mama wa familia, ewe mwalimu. Tujiulize ni sehemu gani ambayo tunayo katika uhalisia huu wa Ufalme wa Mungu? Kama Mtakatifu Yohane Bosco alivyojitoa katika maisha yake na kuwa Baba na Mwalimu wa Vijana, vivyo hivyo nasi pia tunaalikwa katika hali yeyote ile ya maisha yetu kuwa chachu katika familia ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Nawatakia Sherehe njema ya Mtakatifu Yohane Bosco.