Tafuta

Urithi mkubwa kutoka kwa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC ni: Unyenyekevu, moyo wa furaha na upendo wa udugu wa kibinadamu. Urithi mkubwa kutoka kwa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC ni: Unyenyekevu, moyo wa furaha na upendo wa udugu wa kibinadamu. 

Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC , Kuzikwa Rakwaro, Kenya: Urithi Anaowaachia Ivrea SRS

Urithi mkubwa kutoka kwa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC ni: Unyenyekevu, moyo wa furaha na upendo; Udugu na moyo wa shukrani kwa matendo makuu ya Mungu katika maisha. Sasa aendelee kuwahamasisha watu wa Mungu kuwasha taa ya: imani, matumaini na mapendo. Kifo katika ujana, kiwakumbushe watu udhaifu wa maisha ya mwanadamu na tumaini kwa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawahimiza waamini kutafakari juu ya umuhimu wa kushiriki katika Fumbo la Pasaka na hatimaye, waweze kuingia katika heri, maisha na uzima wa milele. Hii ni kwa sababu maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mama Kanisa anawaombea waamini marehemu ili watakaswe, ikiwa wanahitaji kutakaswa, kabla ya kupokelewa mbinguni, wakae na watakatifu, wakati miili yao inapobaki ardhini ikingojea kurudi kwa Kristo Yesu, Ufufuko wa wafu na uzima wa maisha ya milele.

Fumbo la Kifo liwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Fumbo la Kifo liwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo

Ndiyo maana Mama Kanisa anatolea sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili kuwakumbuka na kuwaombea marehemu, pia Mama Kanisa anasali na kuwaombea marehemu kusudi wapate msaada wa maisha ya kiroho, na waamini wanaokuwa bado hai wapate matumaini ya maisha na uzima ujao huko mbinguni. Hayati Papa Benedikto XVI aliwahi kuwakumbusha waamini kwamba, Kristo Mfufuka, daima yuko pamoja na waja wake katika hija ya maisha yao hapa duniani, tayari kuwashika mkono na kuwainua na kwamba, yuko tayari kuwaokoa mahali popote pale, wanapoweza kuteleza na kuanguka, yuko pamoja nao, hata wakati wa kifo, ili kuwasindikiza huku wakiwa wepesi, ili kuwakirimia mwanga wa maisha ya uzima wa milele! Ni katika muktadha huu, Masista wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea maarufu kwa jina la “Masista wa Ivrea,” Jumanne tarehe 17 Januari 2023, huku wakiwa wameungana na umati wa watawa, mapadre na watu watakatifu wa Mungu katika ujumla wao walikusanyika kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria in Trastevere” Jimbo kuu la Roma, kumshukuru Mungu na kumsindikiza katika uzingizi wa amani, Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC aliyefariki ghafla tarehe 3 Januari 2023 mjini Roma.

Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Monsinyo Marco Gnavi, Paroko wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Trastevere.” Katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa kusali na kumwombea Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC ambaye katika maisha na utume wake, alijitahidi kupandikiza mbegu ya: upendo wa udugu wa kibinadamu katika unyenyekevu; akatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zilizomwezesha kujenga urafiki na maskini, wanyonge na watoto. Fumbo la kifo limefika katika ujana, ndiyo maana majonzi ya watu wa Mungu yamekuwa ni mazito sana. Huu ni mwaliko wakati huu wa kipindi hiki cha maombolezo kuwa ni watu wa shukrani na kutambua umuhimu wa zawadi ya uhai kutoka kwa Mungu, ili kuendelea kujibidiisha katika maisha na huduma, kwa kutambua kwamba, hapa duniani, binadamu wote ni wasafiri na wala hawana makao ya kudumu. Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC kabla ya kufikwa na mauti, alibahatika kwenda kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kutoa heshima zake kwa Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022 na kuzikwa kwenye Makaburi yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 5 Januari 2023. Alibahatika kufanya tafakari kuhusu utukufu wa Mungu kwa Mtumishi wake aliyelala kwenye usingizi wa amani, akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC katika maisha na utume wake, alijitoa sadaka kwa ajili ya utukufu wa Mungu kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Akaonesha umuhimu kuwa ni vyombo vya huruma, upendo na msamaha ili kujenga na kudumisha urafiki na mafungamano na Kristo Yesu.

Sr. Rose alibahatika kutoa heshima zake kwa Papa Benedikto XVI
Sr. Rose alibahatika kutoa heshima zake kwa Papa Benedikto XVI

Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC atakumbukwa “kwa tabasamu lake la kukata na shoka”, ushuhuda wa maisha na utume wake. Urithi mkubwa kutoka kwa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC ni: Unyenyekevu, moyo wa furaha na upendo; Udugu wa kibinadamu na moyo wa shukrani kwa matendo makuu ya Mungu katika maisha. Sasa aendelee kuwahamasisha watu wa Mungu kuwasha taa ya: imani, matumaini na mapendo. Kifo katika ujana, kiwakumbushe watu wa Mungu udhaifu wa maisha ya mwanadamu na umuhimu wa kumtumainia Mungu daima. Awe ni mfano wa shukrani kwa Fumbo la Ufufuko, wito na maisha yake. Baada ya kumaliza mwendo wa maisha yake hapa duniani, sasa apokelewe mbinguni na kuwekwa miongoni mwa watakatifu wa Mungu, ili wote waweze kushiriki utukufu wa Kristo Yesu. Masista wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea, ndugu, jamaa na watu wote wa Mungu wafarijike kwa sala na sadaka ya Misa takatifu kwa ajili ya kumkumbuka, kumwombea na kumsindikiza Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC katika usingizi wa amani, AMINA.

Sr. Palma Porro, aliyewahi kuwa Mama mkuu wa Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingizwa dhambi ya asili wa Ivrea na Mlezi wa Wanovisi kwa miaka mingi, katika mahojiano maalum na Radio Vatican amemwelezea Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC kwamba, alijitahidi kumwilisha ndani mwake tunu msingi za maisha ya Kiinjili; alikuwa ni shuhuda na chemchemi ya furaha, amani, sadaka na majitoleo; alikuwa ni mchangamfu na mcheshi. Masista wa Ivrea kama urithi wao kutoka kwa Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, muasisi wa Shirika; wameachiwa: Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Fumbo la Ekaristi Takatifu na Msalaba kama nyenzo msingi za maisha na huduma ya Injili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC alijitahidi kumwilisha karama ya Mwanzilishi wa Shirika, Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, aliyepambana kwa imani thabiti dhidi ya umaskini wa hali, mali na utu. Alikuwa na imani thabiti kwa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, Mama wa Yesu na Mama wa Kanisa: Chemchemi isiyokauka ya: imani, neema na matumaini. Ni mang’amuzi ya maisha ya mwanamke ambaye hakuogopa kupenda. Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, Dada wa upendo alikuwa huru katika kusema “Ndiyo” kwa Bwana, kwa ajili ya utumishi wa upendo kwa Mungu na kwa jirani. Baada ya taratibu zote kukamilika, Mwili wa Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC, utasafirishwa kwenda Nairobi, Kenya na baadaye mazishi yatafanyika Rakwaro.

Sr. Rose amesindikizwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu.
Sr. Rose amesindikizwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu.

Kwa upande wake Sr Priscila Isidori, SCIC anasema, Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC alikuwa ni: Mcheshi, mfurahivu, aliyewajali na kuwasaidia watu; alikuwa na moyo wa upendo na ukarimu. Alibahatika kuwa na karama na mapaji mengi aliyoyatumia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Alikuwa na bidii ya masomo, akawasha taa ya matumaini na tegemeo kwa Kanda ya Malaika Mkuu Mikaeli inayoundwa na watawa wanaotekeleza utume wao nchini Kenya na Tanzania pamoja na Shirika katika ujumla wake, mintarafu Sheria za Kanisa. Mauti yamemfika baada ya kumaliza kuandika kazi yake na kabla ya kuitetea. Sr. Margaret Adhiambo Onywera, SCIC, anasema, Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC alikuwa ni mnyenyekevu, mpole wa moyo na mnyofu, mtaratibu pasi na makuu; alibahatika kuwa na kipaji cha elimu na kwa hakika alikuwa ni mwimbaji mzuri; mtu mwenye uso na tabasamu ya furaha; mpenda amani na utulivu, mshauri na mchangamfu. Kwa upande wake, Mheshimiwa Connie Nkatha Maina, Kaimu Balozi wa Kenya nchini Italia, kwa niaba ya Balozi na wafanyakazi wote wa Ubalozi wa Kenya wanapenda kutoa salam za rambirambi kwa Masista wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea, ndugu, jamaa na watu wote wa Mungu kutokana na msiba huu mzito. Katika kipindi hiki, watu wa Mungu kutoka Kenya wanaoishi nchini Italia, wameonesha ari, na moyo wa umoja na upendo wa kindugu kwa kuiishi falsafa ya harambee kwa vitendo, kiasi cha kuchangia kwa hali na mali, ili kufanikisha kusafirisha mwili wa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC hadi Nairobi, Kenya na hatimaye, huko Rakwaro kwa mazishi. Wanawashukuru wakuu wa Shirika kwa kuridhia ombi la familia la kutaka Marehemu Sr. Rose azikwe nyumbani kwao. Hii imekuwa ni faraja na heshima kubwa kwa watu wa Mungu nchini Kenya. Sasa wajiandae kuupokea Mwili wa Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC kwa imani, matumaini na mapendo makuu, ili aweze sasa kupumzika kwa amani.

Wamemsindikiza kwa machozi ya matumaini, imani na mapendo
Wamemsindikiza kwa machozi ya matumaini, imani na mapendo

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Sr. Rose Atieno Jonyo, SCIC alizaliwa tarehe 12 Februari 1978 huko Suba, Mkoa wa Nyanza Kusini, kwenye mwambao wa Ziwa Victoria nchini Kenya. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa, tarehe 12 Juni 2010 akaweka nadhiri za kwanza huko Rakwaro, nchini Kenya. Alitekeleza utume wake kati ya vijana na watoto wadogo Veyula, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, Eldoret na Macalder nchini Kenya na baadaye Ihumwa kwenye shule ya Wayesuit, Jimbo kuu la Dodoma. Tarehe 8 Desemba 2017 akaweka Nadhiri zake za daima kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria in Trastevere” Jimbo kuu la Roma. Mwaka 2018 akaanza masomo ya Sheria za Kanisa, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Akiwa katika maandalizi ya kutetea kazi yake katika ngazi ya uzamili, ghafla, akakutana na fumbo la kifo, tarehe 3 Januari 2023 ili kukutana na Kristo Yesu, aliyempenda, akamkomboa kwa mateso na kifo cha Msalaba na kumwita kushiriki katika huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na furaha kwa watu wa Mataifa. Yaani! Apumzike kwa Amani.

Marehemu Sr. Rose
18 January 2023, 13:54