JUGO MEDIA NETWORK Dar es Salaam Yapata Tuzo, Yapongezwa kwa Uinjilishaji Kiganjani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jamii inahitaji vyombo vya mawasiliano ya jamii, vyenye uwezo wa kujenga madaraja ya kuwaunganisha watu. Vinahitajika vyombo vya mawasiliano vyenye nguvu ya kuvunjilia mbali kuta zinazoonekana na zile zisizoonekana, lakini bado zinawatenganisha watu. Jamii inahitaji vyombo vya mawasiliano vitakavyowasaidia watu na hasa vijana wa kizazi kipya kuunda dhamiri nyofu, yaani uwezo wa kupambanua mema na mabaya, kwa kuangalia ukweli wa mambo bila kupindisha pindisha. Watu wa Mungu wanahitaji vyombo vya mawasiliano ya jamii vitakavyosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; maridhiano ya kijamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jamii inawahitaji wadau wa mawasiliano watakaosimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya mawasiliano bora ya jamii, dhidi ya watu wachache wanaotaka kuharibu sheria, kanuni na taratibu hizi kwa mafao yao binafsi. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia washiriki wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki, “Catholic Press Association, CPA” kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 2 Julai 2020. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau katika sekta ya mawasiliano ya jamii, kuungana na kushikamana wao wenyewe, kwani Kanisa linathamini sana mchango wa vyombo vya upashanaji habari. Hii inatokana na ukweli kwamba, ndani ya Kanisa, waamini wote wamebatizwa katika Roho Mtakatifu na wote wanajenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
Ni katika muktadha huu, kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anachangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa njia ya weledi unaofumbatwa katika ukweli na katika upendo, ili hatimaye, Kanisa liweze kukua na kushamiri katika Kristo Yesu. Wanahabari wa kweli wasiokuwa na hila ndani mwao ni wale wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao, kama mtu binafsi, jamii na familia kubwa ya binadamu katika ujumla wake. Hawa ni watu wanaozama katika shughuli zao, ili kushuhudia ukweli wanaotaka kuutangaza. Mawasiliano yanabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, linalowashirikisha waja wake amana na utajiri wa Kimungu, ili hata wao, waweze kuwashirikisha wengine, amana na utajiri huu. Baba Mtakatifu anawaombea wadau katika tasnia ya upashajjaji habari wote karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa na: busara, hekima, uelewa wa kutosha, ili hatimaye, waweze kutoa ushauri mwema. Wawe ni vyombo vya faraja na matumaini kwa watu wanaotafuta ukweli kwa wote. Huu ni mwaliko wa kuvunjilia mbali saratani ya mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki na amani; hali ya kutowajali na kuwathamini wengine; mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na familia ya binadamu.
Kwa njia ya sadaka na majitoleo yao katika kazi, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wawasaidie jirani zao kuweza kutafakari matukio mbalimbali ya maisha kwa macho ya Roho Mtakatifu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa Katoliki wajitahidi kuzungumza lugha inayopania kukuza na kudumisha ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wawe mstari wa mbele kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii kutokana na hali na mazingira yao. Wawe ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti; watu wanaohitaji huruma na hatimaye, kuweza kueleweka. Amewataka wadau wote kuendelea kuungana pamoja katika sala na utume huu nyeti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni katika mazingira na hali kama hii, tarehe 18 Januari 2023, Askofu Msaidizi Stephano Musomba, OSA, wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewawezesha Vijana wa Jugo Media Network kwa kuweza kupata Tuzo Maalum kutoka kwenye Kampuni ya Youtube Marekani baada ya kuvuka kiwango cha wafuatiliaji 100, 0000. Jugo Media Network ni chombo makini cha uinjilishaji kupitia mitandao ya kijamii, kilichoanzishwa na Ibrahim Gores kwa kujikita katika uinjilishaji na utamadunisho, ili furaha ya Injili iweze kuwafikia wengi.
Lengo ni kuwawezesha watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania kuboresha maisha yao kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu, Ibada, maisha ya sala na shuhuda za tunu msingi za Kiinjili kupitia mitandao ya kijamii. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi Januari mwaka 2023, Jugo Media Network imeweza kuwafikia watu wa Mungu zaidi ya milioni 27 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ndiyo maana Jugo Media Network inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 4 iliyopita. Jugo Media Network imeanza kutanua huduma yake kwa kufungua Ofisi ndogo na kuwa na Mwakilishi Jimbo Katoliki la Morogoro. Lengo kuu ni kuendelea kutanua huduma katika majimbo mbalimbali kupitia mpango mkakati wa kazi wa mwaka 2023 hadi 2026. Hii imekuwa ni siku ya kutoa vyeti vya shukrani, kuzindua Mfuko Maalum wa Jugo Media Network, Bodi ya Wadhamaini pamoja na kuwasilisha Mpango Mkakati wa Kazi kuanzia Mwaka 2023-2026. Itakumbukwa kwamba, Jugo Media Network wamekuwa ni wadau waaminifu wa Radio Vatican kwa kurusha taarifa na matangazo yake kwa kutumia YouTube. Wameendelea pia kurusha Katekesi za Baba Mtakatifu Francisko zinazotolewa kila Jumatano, bila kusahau matukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.