Tafuta

Papa Benedikto XVI  wakati wa ziara yake ya kitume Nchi Takatifu mnamo tarehe 15 Mei 2009. Papa Benedikto XVI wakati wa ziara yake ya kitume Nchi Takatifu mnamo tarehe 15 Mei 2009.  (ANSA)

Hayati Papa Mstaafu Benedikto XVI:ziara ya Nchi Takatifu ilikuwa hija halisi

Katika Misa ya kuombea hayati Papa Mstaafu Benedikito wa Kumi na sita,iliyoadhimisha katika Kaburi Takatifu huko Yerusalemu,Padre Patton alisema kwamba"kwa kutazama yeye tunatambua kuwa maisha yetu yote yanapaswa kuweka kiini kikuu cha Kiristo.Inatosha kusikia hata maneno yake ya mwili aliyosema'Yesu ninakupenda'."

Na Angella Rwezaula; – Vatican.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Baba Mtakatifu  Mstaafu Benedikto XVI  iliadhimishwa mnamo tarehe 10 Januari 2023 kwenye Makaburi Matakatifu mjini Jerusalem, ambayo iliyoongozwa na Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, Askofu Mkuu Pierbattista Pizzaballa. Kati ya waliohudhuria ni wawakilishi wa Makanisa mbali mbali, Dini ya Kiyahudi na Kiislamu, mamlaka za kiraia na wajumbe wa mabalozi walioko Nchi Takatifu.  Msimamizi wa Nchi Takatifu Padre Francesco Patton, ndiye aliyetoa mahubiri yake  huku akirejea ziara ya kihistoria ya Papa  Mstaafu Benedikto XVI katika Nchi Takatifu mnamo mwaka 2009.  Akichukua baadhi ya maneno kutoka katika hotuba za Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikito XVI, Padre Patton alisema kuwa, “Hiyo haikuwa ziara ya heshima  tu bali ilikuwa ni hija halisi ambayo alitaka kuonesha ukaribu na jumuiya ndogo ya Wakristo wa eneo hilo kwa kuwahimiza Wakristo wasihame na wabaki waaminifu katika mizizi yao.

Katika hija hiyo, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikutana na Mapatriaki na Wakuu wa Makanisa dada kwa njia ya maelewano  na kidugu. Alikutana kidugu na mamlaka ya kidini ya Wayahudi na Waislamu, pamoja na mamlaka ya kiraia ya Jordan, Israeli na Palestina. Pia alitembelea pia shughuli   nyingi za kijamii ili kuelezea ukaribu wake kwa watu maskini na wahitaji zaidi. Kwa upole ambao daima ulimtofautisha au kumfafanua, alijaribu kupanda amani na kukaribisha majadiliano. Wakati wa ziara yake, Papa Mstaafu Benedikto XVI alizungumza juu ya Yerusalemu, akitumaini kwamba inaweza kweli kuwa mahali pa mkutano na sala kwa watu wote na akakumbusha wito kwa ulimwengu wote kuhusu Jiji hilo, Takatifu na linalopendwa na Wayahudi, Wakristo, Waislamu na wengine wenye mapenzi mema. Hasa kwa sababu hiyo alizungumza nao maneno ambayo yana maana kubwa zaidi katika ulimwengu wa leo hii tunamoishi.

Padre Patton katika mahubiri hayo aliongeza kusema kuwa ni maneno yaliyosemwa ili kuwaonesha hao wanaoishi hapo njia ya kutembea kwenda mbele. Papa Mstaafu Benedikto aliwakumbusha kwamba, hasa kwa kadiri ya wito wake, Yerusalemu 'lazima pawe ni mahali pa kufundisha ulimwengu wote, heshima kwa wengine, majadiliano na kuelewana; mahali ambapo chuki, ujinga na woga unaowachochea vinashindwa na uaminifu, uadilifu na kutafuta amani vinachanua. Kwa njia hiyo alisisitiza kwamba pasiwe na nafasi ndani ya kuta hizo kufungwa, ubaguzi, vurugu na ukosefu wa haki.

Waamini wa Mungu wa huruma wanastahili wawe Wayahudi, Wakristo au Waislamu, kwanza kuendeleza utamaduni huo wa upatanisho na amani, hata hivyo mchakato unaweza kuwa wa kuchosha na wa polepole na mzigo wa kumbukumbu za wakati wa zamani zinaweza kuwapo. Kwa kutazama mchakato wa  safari ya uwepo wa Papa mstaafu Benedikto XVI na pia kutazama maneno ya mwisho aliyozungumza kwamba “Bwana, ninakupenda,” ni wazi kuelewa kwamba hata katika maisha yetu lazima kuwe na ukuu wa upendo. Na tunaelewa kuwa ili tuweze kupenda tunahitaji kuchota mara kwa mara kutoka katika uhusiano na Yesu, alihitimisha mahbiri yake Padre Patton, Msimamizi wa maeneo matakatifu ya Nchi Takatifu.

Misa ya kuombea hayari Papa mstaafu
17 January 2023, 15:35