Tafuta

2022.12.Pango la kuzaliwa kwa Bwana mjini Vatican. 2022.12.Pango la kuzaliwa kwa Bwana mjini Vatican. 

Ujumbe wa Amani ya Noeli kutoka CCEE:Njia ya Mungu sio nguvu wala ubinafsi

Sikukuu ambayo ina umuhimu fulani kwa wengi,iwe ni imani ya Kikristo au la. Kwa wengine,hata hivyo ni nyakati za kujaribiwa sana.Kwa mfano tunafikiria hasa mateso makubwa ya watu Ukraine na wale waliolazimika kukimbia kutoka nyumba zao ili kutafuta hifadhi kutokana na uvamizi wa kikatili wa kijeshi ulioanzishwa sasa ni zaidi ya miezi tisa iliyopita.

Na Angella Rwezaula; – Vatican.

Wakristo  ulimwenguni kote  kwa sasa wanajiandaa kuadhimisha noeli, sikukuu ya matarajio, upendo, matumaini na amani. Sikukuu ambayo ni ya umuhimu fulani kwa wengi, wawe wa imani ya Kikristo au la. Kwa wengine, hata hivyo, hizi ni nyakati za kujaribiwa sana. Kwa mfano tunafikiria hasa mateso makubwa ya watu nchini Ukraine, na wale ambao wamelazimika kukimbia kutoka katika nyumba zao ili kutafuta hifadhi kutokana na uvamizi wa kikatili wa kijeshi ulioanzishwa sasa ni zaidi ya miezi tisa iliyopita. Umwagaji damu unaoendelea nchini Ukraine ni jeraha la wazi la ubinadamu ambalo vivuli vya giza vya vita vimeendelea kuenea, na kuhatarisha kuongezeka zaidi. Ni kutoka katika ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya maaskofu barani Ulaya katika kuelekea maadhimisho ya Noeli 2022. Ujumbe huo unaongozwa na kauli mbiu kutoka kifungu ncha Injili ya Luka kisemacho:  ‘Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani amani kwa  watu wenye mapenzi meema ( Lk. 2:14 )

Mada kuu ni amani duniani kwa wote waliojaribiwa

Katika ujumbe huo wa Noeli ambao unajikita katika mada kuu ya amani viongozi hawa wanabainisha kwamba :“kwa habari ya watu wa Mungu waliojaribiwa, pia kwetu leo, kuna ahadi ya tumaini: ‘Watu walioishi gizani wameona nuru kuu’ ( Mt. 4:16 ), ‘kwa maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu; mwana tuliopewa, naye 'ataitwa Mfalme wa Amani' (Isa. 9:6). Njia ya Mungu sio nguvu na ubinafsi. Kinyume chake, inahusisha ukaribu na huruma. Tunaposoma katika Maandiko, Mungu hakujidhihirisha kwa nabii huyo si katika upepo wenye nguvu, wala katika tetemeko la ardhi wala katika moto, bali katika ‘kimya tupu’ (1Fal. 19:11-12) na ‘Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu' (Yohana 1:14), kama alivyofanyika zawadi kwa wanadamu katika mtoto mdogo na dhaifu Yesu Kristo. Kwa kuzingatia sikukuu ya Noeli inayokaribia, wamebainisha kuwa kama sisi viongozi wa Makanisa yetu tunawaalika watu wote kusali kwa namna ya pekee kwa ajili ya amani nchini Ukraine.

Amani ilete faraja kwa mama na watoto wao

Amani ya Kristo na ilete utulivu katika kunguruma kwa silaha na faraja kwa akina mama wanaowalilia watoto wao (rej. Mt. 2:18), ambao walilazimika kufa kwa sababu ya ubinafsi fulani. Aziunganishe familia na jamii nyingi ambazo zimesambaratishwa na chuki na vurugu. Wakiwa wameteswa na baridi, njaa na woga, mtu yeyote asijisikie ameachwa, na wale wote wanaokimbia vitisho vya vita na wapate kukaribishwa kwa uchangamfu. 

Mapendekezo kuelekea amani tu

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaua wakisukumwa na mateso ya kutisha ya mwanadamu na kuongozwa na fadhila za hekima, uadilifu na busara, wavamizi waache uhasama ili pande zote kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa zijitokeze kwa mazungumzo na majadiliano ya mapendekezo mazito kuelekea amani tu. Ujumbe wa Noeli ututie moyo sisi sote kutafuta upatanisho na amani, ili badala ya kuta za mifarakano na kutojali, mbegu ya kuheshimiana, mshikamano na udugu wa kibinadamu ipandwe na kulishwa mioyoni mwetu.

17 December 2022, 16:22