Ujumbe wa Noeli Kutoka kwa Viongozi Wakuu wa Makanisa Uingereza na Wales: Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtoto Yesu ndiye kiini cha Sherehe za Noeli, asaidie mchakato wa kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, ushirikiano na mshikamano katika familia na jumuiya mbalimbali za waamini! Amani na matumaini ni fadhila zinazoibuliwa katika Sherehe ya Noeli. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Matumaini hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821.
Viongozi wakuu wa Makanisa ya Uingereza na Wales katika Ujumbe wao wa Noeli kwa Mwaka 2022 wanasema, Kristo Yesu alizaliwa katika mazingira magumu, tete na hatarishi, kiasi hata kingeweza kuwakatisha tamaa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, Mtu wa haki, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Rej Lk 2: 11. “Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe.” Lk 2: 6-7. Hofu na mashaka vikatoweka, furaha, amani na matumaini vikarejea tena. Watu wengi bado wameathirika na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za dunia; Umaskini, Njaa na Magonjwa ya Mlipuko bado yanaendelea kuwa ni tishio kwa usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu, kiasi kwamba, hali ya maisha ya watu inaendelea kuwa duni, lakini gharama ya maisha, inaendelea kupanda kwa kasi.
Uingereza na Wales bado wanaendelea kumwombolezea Malkia Elizabeth II aliyefariki dunia hivi karibuni. Pamoja na hali tete na ugumu wa maisha, lakini bado watu wanaendelea kuonja cheche za: Imani, Matumaini na Mapendo; kwa kumshukuru Mungu kwa sadaka na maisha ya Malkia Elizabeth II; Upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi; kielelezo kwamba, Uingereza na Wales zinataka kuwa ni Madhabahu na Nchi ya Amani, Utu na Heshima ya Binadamu na kamwe, Noeli isifunikwe na malimwengu na hivyo kuigeuza Sherehe hii kuwa na mwelekeo zaidi wa kibiashara na hivyo kupoteza maana yake halisi. Viongozi wakuu wa Makanisa ya Uingereza na Wales katika Ujumbe wao wa Noeli kwa Mwaka 2022 wanahitimisha kwa mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, na hivyo kujitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kujenga Jumuiya ya waamini inayosimika maisha yake katika: Imani, Matumaini na Mapendo kwa Mungu na jirani.