Tafuta

Kristo Yesu ndiye kiini cha maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Kristo Yesu ndiye Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria. Kristo Yesu ndiye kiini cha maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Kristo Yesu ndiye Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria. 

Ujumbe wa Noeli kutoka Kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni WCC: Msiogope!

Katika hali ya umaskini huo, utukufu wa Mungu ulionekana na kuwa ni: chemchemi ya huruma, umoja, upatanisho na upendo kwa watu wote sanjari na kazi yote ya uumbaji. Ujumbe wa Noeli kwa 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Msiogope.” Huu ni wakati kwa waamini kuwa ni vyombo vya haki na amani, daima wakitambua kwamba, wao ni mahujaji wa haki, upatanisho na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu ndiye kiini cha maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Kristo Yesu ndiye Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwake Bikira Maria katika hali ya unyenyekevu na umaskini mkubwa. Wachungaji waliokaa makondeni ndio mashuhuda wa kwanza wa tukio la kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu. Katika hali ya umaskini huo, utukufu wa Mungu ulionekana na kuwa ni: chemchemi ya huruma, umoja, upatanisho na upendo kwa watu wote sanjari na kazi yote ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuilinda na kuiendeleza. Ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2022 kutoka katika Baraza la Makanisa Ulimwengu, WCC unanogeshwa na kauli mbiu “Msiogope.” Huu ni wakati kwa waamini kuwa ni vyombo vya haki na amani, daima wakitambua kwamba, wao ni mahujaji wa haki, upatanisho na umoja. Usiku ule wa manane Malaika alipowatokea wachungaji kule kondeni, waliogopa sana, lakini “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.” Lk 2:10-12. Malaika wanatangaza ukuu na utakatifu wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Leo hii kinachowaogofya walimwengu ni woga wenyewe unaowanyima usingizi kutokana na athari za mabadiliko makubwa ya tabianchi; Kuyumba kwa uchumi Kitaifa na Kimataifa na hivyo fursa za ajira kutoweka kama ndoto za mchana, kiasi cha watu ndani ya familia kuwa na wasiwasi kwa ajili ya mustakabali ya watu wao kwa siku za mbeleni.

Hofu ya vita, njaa, magonjwa na umaskini vimetanda duniani kote.
Hofu ya vita, njaa, magonjwa na umaskini vimetanda duniani kote.

Baraza la Makanisa Ulimwengu, WCC, linasema kwamba, watu wa Mungu wanahofu na wasiwasi mkuu katika maisha yao kutokana na vita, kinzani na mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na biashara haramu ya silaha na matumizi yake. Bado kuna sikika mahubiri ya chuki na uhasama kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani badala ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu. Bado kumeenea nadharia ya njama za silaha za nyuklia duniani; uvunjwaji wa haki msingi za binadamu pamoja na vitisho dhidi ya demokrasia ya kweli. Pamoja na vitisho na hofu zote hizi, lakini ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2022 ni huu ni “Msiogope.” Fadhila ya imani, matumaini na mapendo thabiti kwa Mungu na jirani ziwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye siku moja ataweza kutekeleza ahadi yake ya amani, ustawi na maendeleo kwa watu wote wa Mungu. Hata leo hii, bado Malaika na wingi wa jeshi la mbinguni, wanamsifu Mungu wakisema “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Lk 2:14. Hii ni changamoto kubwa kwa Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya: upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano.

Majadiliano ya kidini yanogeshe haki, amani na maridhiano kati ya watu
Majadiliano ya kidini yanogeshe haki, amani na maridhiano kati ya watu

Hawa ni watu kutoka katika makabila, lugha, jamaa na tamaduni mbalimbali, wanaopania kusimama kidete kwa ajili ya kusaidia upyaisho wa ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hawa ni watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya mifumo yote ya ubaguzi na hofu ya wageni “Xenophobia”. Hawa ni wandani wa hija ya haki, upatanisho na ushirikiano. Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanapoupokea ujumbe wa Noeli, Roho wa Bwana anawataka wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu wanaoishi nao na kuwazunguka. Baraza la Makanisa Ulimwengu, WCC linahitimisha ujumbe wake Noeli kwa mwaka 2022 kwa kusema kwamba, huu ni wakati wa kunogesha mahusiano na mafungamano ya tunu msingi za maisha ya kifamilia, kijamii, kikanisa, Kitaifa na Kimataifa, ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaozalisha chuki, uhasama, tabia ya kutaka kulipiza kisasi na baadhi ya Mataifa kutaka kujimwambafai. Katika ile Noeli ya Kwanza, Mwenyezi Mungu aliwatembelea waja wake kwa njia ya Neno wake, Kristo Yesu, ili aweze kuwapatanisha wote na Mwenyezi Mungu, ili waamini nao waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa kweli. Huu ni wakati kwa waamini kuwa ni vyombo vya haki na amani, daima wakitambua kwamba, wao ni mahujaji wa haki, upatanisho na umoja.

Makanisa: Amani 2022

 

27 December 2022, 11:18