Tafuta

Ni vema tukakumbuka na kuuzingatia daima mwaliko tunaoupata kutoka katika Neno la Mungu: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6). Ni vema tukakumbuka na kuuzingatia daima mwaliko tunaoupata kutoka katika Neno la Mungu: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6).  

Ujumbe wa Noeli 2022 Kwa Familia ya Mungu Inayojali na Kuwajibika

Askofu mkuu Nkwande anaialika familia ya Mungu inayojali na kuwajibika kuhakikisha kwamba, inajikita katika malezi na makuzi ya watoto. Anatoa angalisho kuhusu madhara ya matumizi ya katuni kwa watoto na kwamba familia zijitahidi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha malezi bora yanayopania kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Familia Takatifu!

Na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, - Jimbo kuu la Mwanza.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, - Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, anapenda kuialika familia ya Mungu inayojali na kuwajibika kuhakikisha kwamba, inajikita barabara katika mchakato wa wazazi na walezi, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto. Anatoa angalisho kuhusu madhara ya matumizi ya katuni kwa watoto na kwamba, familia zijitahidi kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu katika malezi na makuzi ya watoto wao, kila mwanafamilia ajitahidi kutekeleza wajibu na majukumu yake, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha malezi bora yanayopania kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni vema wanafamilia wakakumbuka na kuuzingatia daima mwaliko wanaoupata kutoka katika Neno la Mungu: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6). Wapendwa familia ya Mungu, ninawatakia heri na baraka tele kwa Sherehe ya Noeli. mTunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia fursa ya kuiadhimisha Noeli ya Mwaka huu 2022. Tunaiadhimisha sio tu kama tukio la kihistoria, bali la kiimani. Noeli ni sherehe yenye ujumbe wa Ukombozi wa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Ni sherehe inayohuisha ndani yetu amani, furaha na matumaini mapya, kwani kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu anajidhihirisha kwetu na anafanya makao kati yetu (Mungu pamoja nasi/EMMANUELI) na hivi kuurudishia hadhi na thamani ubinadamu wetu. Aidha, ni sherehe inayotupa mwaliko wa kujali na kutimiza maagizo ya Mwenyezi Mungu juu ya kuujaza na kuulea ulimwengu kwa kusisitiza malezi bora ya watoto wetu.

Wazazi na walezi wawajibike vyema kwa malezi na makuzi ya watoto wao
Wazazi na walezi wawajibike vyema kwa malezi na makuzi ya watoto wao

Tunapoisherehekea Noeli ya Mwaka huu wa 2022 ninapenda kuwaalika tutafakari zaidi juu ya wito na wajibu wa kila mmoja wetu wa kutoa malezi bora kwa watoto wetu. Tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya “Mtoto Yesu” aliyezaliwa na kupokea malezi bora, ni fursa ya kujihoji ni kiasi gani nasi tumetimiza wajibu huu muhimu. Kwa bahati mbaya, ziko nyakati nyingi ambapo tumeshindwa kuwa walezi wema na hata kuruhusu dhambi kutamalaki. Kama tunaamini kwamba Mungu ni yule yule, jana, leo na hata milele (Ebr. 13:8), ni lazima tufikiri mara mbili. Kama Mungu aliwakasirikia watu wa Sodoma na Gomora hata akawanyeshea kibiriti cha moto (Mwa. 19:1-29), hawezi kubadilika leo na kukubali mambo yanayolenga kupyaisha “usodoma na ugomora.” Kwa hiyo, ni hakika kwamba kama hatawanyeshea waovu kibiriti cha moto sasa, mwishoni mwa historia wakati wa kuuhukumu ulimwengu taabu yao itakuwa pale pale. Wapendwa familia ya Mungu, malezi ya watoto imekuwa ni changamoto kubwa leo kuliko zamani; pengine ni kutokana na kutekwa na utandawazi na matumizi mabaya ya uhuru wetu. Mahangaiko ya maisha ya leo, (kutokana na kujitafutia riziki, ajira na biashara) yanapelekea wazazi na walezi wengi kushindwa kutimiza wajibu wao wa kutoa malezi bora ya kiimani na kiutu. Ikumbukwe kwamba, kuelimisha akili pasipo kuuelimisha moyo na dhamira ni sawa na kazi bure. Ni wazi kwamba tunahitaji elimu ya darasani na inayopatikana vitabuni, lakini tunahitaji pia kujisimamia kama wanadamu ili kuushinda uovu unaojipenyeza kwa kupitia tabia ambayo daima hatuijifunzi kwa mtaala darasani bali kwa njia ya uhalisia wa maisha. Ni kwa kutegemea Neema ya Mungu, usimamizi makini na ujasiri wa kukemea maovu, ndipo tunaweza kustawi katika tabia njema iliyojisimika katika haki, upendo kwa wote na maisha ya ushuhuda kwa wengine juu ya kweli za Kimungu.

Noeli ijikite katika fadhila za Kimungu
Noeli ijikite katika fadhila za Kimungu

Ni ukweli usiopingika kwamba, watoto watakaozoeshwa mabaya sasa watazeeka nayo kama ilivyo kwa wale watakaozoea mema wanavyoweza kuzeeka nayo. Ndiyo maana, kwa kuwaepusha watoto na maovu ambayo wanaweza wakakua nayo, tunaalikwa kufuatilia tabia na makuzi yao kwa uangalifu mkubwa zaidi sasa tangu katika familia, shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari na vyuo, ili wasizame katika tabia zisizofaa, hususani mitindo ya kisasa ya kujamiiana pamoja na nadharia ya jinsia kwa ujumla, maana mambo tayari yameanza kuharibika. Ni vema tukakumbuka na kuuzingatia daima mwaliko tunaoupata kutoka katika Neno la Mungu: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6). Wapendwa familia ya Mungu, tukitazama jamii yetu leo, kwa sehemu kubwa watoto wameachwa wajiongoze wenyewe. Kwa mfano: wanatembea usiku bila udhibiti wa wazazi na walezi, wanaruhusiwa kwenda kwenye majumba ya starehe, wanaishi kwa kubembelezwa hata kama wamekosea na kuruhusiwa kutumia vitu vya kisasa kama simu na TV bila uratibishi wa wazazi na walezi wao. Maisha na mahangaiko ya wengi leo, yamepelekea kuwaacha watoto wao na uhuru usiokuwa na mipaka. Mbali na kulelewa kwa muda mrefu na watu wasiokuwa wazazi wao, upo pia mtindo wa kuangalia KATUNI. Kwa bahati mbaya, katuni zimechukua nafasi ya wazazi kwa watoto wengi na hata kugeuka kuwa mwalimu wa tabia na maisha yao. Watoto wengi wameachwa ili wapende katuni zinazobadili tabia na maelekeo yao. Katuni nyingi zinawaandaa watoto kuwa na tabia zisizo nzuri. Watoto wa hivi, wenye kupenda katuni za ajabu hawaandaliwi kuwa wakombozi wa jamii wanazoishi na hawatakuwa na majibu ya mahangaiko ya wazazi, ndugu wala jamii zao. Niseme tena waamini: KATUNI nyingi katika mitandao na Chaneli nyingi za TV ni mbaya. Zinatuandalia watu wa ajabu na waovu huko mbeleni.

Watoto walindwe na kuelimishwa katika njia bora zaidi.
Watoto walindwe na kuelimishwa katika njia bora zaidi.

Hivyo, ninapenda kutoa wito kwa wazazi na walezi wote kutenga muda wa kuziangalia kwanza katuni hizo na kujiridhisha juu ya maudhui yake kabla ya kuwaonesha watoto. Aidha, ninawasihi sana muwafundishe watoto juu ya kutawala matumizi ya muda tangu wakiwa wadogo; badala ya kuangalia katuni kwa muda mrefu, watenge pia muda kwa ajili ya SALA na kushiriki kazi nyingine ambazo zinawajenga zaidi. Wapate muda wa kujisomea na kujifunza vitu vizuri. Daima familia zetu ziwe ni shule ya imani, maadili mema na uwajibikaji na wazazi muwe na muda wa kutosha kuwa karibu zaidi na Watoto wenu. Kwa ajili ya malezi bora ya watoto wetu, tunaitwa kwa namna ya pekee kujifunza kutoka kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu waliomtunza Mtoto Yesu, na hata Wachungaji na Mamajusi wa Mashariki (wataalamu wa nyota) walipokwenda kumtafuta Mtoto Yesu ili wamwone, hawakumkuta ameachwa peke yake, hawakumkuta Mtoto ametelekezwa; Maria na Yosefu walikuwepo daima (Lk. 2:16; Mt. 2:11). Hata Herode alipopanga kumuua Mtoto Yesu, Maria na Yosefu walikimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto (Mt. 2: 13-15). Tofauti na leo, watoto wanaingia kwenye hatari za kimwili, kiroho na hata kimaadili lakini wazazi wanashindwa kuwaokoa na hatari za namna hiyo. Hata Yesu alipopotea kwa kubaki Hekaluni, wazazi walihangaika kumtafuta na kumfuatilia mtoto wao (Lk. 2:41-52). Wazazi wengi wa leo wana muda kidogo sana na watoto wao na wengine hawana kabisa. Wengi hawapo nyumbani kutwa nzima na wanarudi usiku na hali hii inajirudia wiki na hata miezi. Watoto katika mazingira ya namna hii, WAMETELEKEZWA. Krismasi ni sherehe inayotukumbusha kuwapenda, kuwajali, kuwalinda na kuwatunza watoto wetu kwa kuwarithisha tunu bora, imani hai na tabia safi, ili wawe hodari, imara, wenye upendo wa kweli kwa Mungu na kwa wanadamu wenzao na bidii katika maendeleo ya familia na taifa letu.

Wazazi na walezi wazingatie malezi bora kwa watoto wao.
Wazazi na walezi wazingatie malezi bora kwa watoto wao.

Wapendwa familia ya Mungu, wito na wajibu wa kutoa malezi bora kwa watoto wetu ni wetu sote. Noeli ya mwaka huu wa 2022 itukumbushe tena juu ya utume huu muhimu sana. Kila mmoja kwa nafasi yake anaalikwa awe macho na ajione anawiwa kutimiza kiaminifu yale yanayompasa: Wazazi muwe macho kwa sababu Mungu amewapa ninyi nafasi maalumu katika jamii ya watu kwa kuwashirikisha katika kazi ya uumbaji. Mnao wajibu msingi na dhamana ya kuwalea watoto wenu katika maadili mema ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu, mila na tamaduni za kuzitambua na kuziheshimu tofauti za kijinsia. Himizeni juu ya misingi ya utu na kupinga yale yote yenye sura ya unyama! Ninyi wenyewe onyesheni mifano bora ili Watoto wetu waige. Wasaidieni walimu mashuleni na hata majirani ili nao wajiamini katika kulea Watoto. Kuna hatari ya walimu kuogopa kulea ipasavyo sababu wazazi wanaweka masharti yasiyosaidia kutoa malezi bora. Nanyi Walimu muwe macho maana kwa nafasi yenu mnapaswa kuwafundisha watoto maadili mema. Kamwe msiisaliti dhamana yenu ya ualimu na kuwaacha watoto wakajizoesha maovu, hususan ile tabia ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile na kwa watu wa jinsia moja. Tayari taabu imengia katika shule zetu kwa ngazi zote na hata kujipenyeza kwa watu wenye ndoa halali. Msiruhusu msingi wote ubomolewe kwa njia ya katuni. Aidha, kataeni mitaala inayoelekea kubariki maovu haya. Muwe mashujaa kuukataa uovu. Walezi na wakubwa wengine wote mnatakiwa pia muwe macho. Ninyi wenyewe mna watoto, na watoto wa watu wengine ni watoto wenu pia. Ya kwamba watoto wa wengine ni watoto wenu pia ni uelewa wa tangu jadi. Wazazi wasipokuwepo, ninyi mnasimama mahali pao. Msiwaache watoto wajilishe kwa vitabu, picha na katuni zisizowajenga kiakili na kimaadili. Watoto wa wengine wakiharibika watawaharibu na wenu pia.

Viongozi wawe watetezi wa tunu msingi, utu na heshima ya watoto wadogo
Viongozi wawe watetezi wa tunu msingi, utu na heshima ya watoto wadogo

Viongozi wa Serikali na Wanasiasa mnapaswa kujipa moyo na kusimama imara katika kulinda na kutetea tunu njema za taifa letu. Kwa ujasiri mpinge mila potofu na malazimisho yanayoweza kuletwa toka nje, yanayotujia kwa kujua au kwa kutokujua. Huo ndio Ukoloni mamboleo unaolenga kututawala kifikra na hata kimwenendo. Uduni wetu wa kiuchumi usitufanye tuwe wanyonge mbele ya wenye nguvu wa dunia hii. Kamwe tusiruhusu wimbi la soko huria likatufanya tukawa jalala la kila bidhaa zikiwemo katuni zisizofaa, biashara ya ngono na misaada ya hovyo. Tujiamini, tupeane shime na hata ikilazimu tusukumane kwa upendo ili kuweza kujenga taifa lenye maadili mema na linalozingatia misingi ya utu. Tukiyatenda haya vema, tutalinda heshima yetu kama waafrika na watanzania mbele ya macho ya ulimwengu na kuwa funzo kwa wale wasiotutakia mema. Hatimaye tutapata maendeleo ya kweli na halali. Sisi, viongozi wa dini ni sauti ya wasio na sauti. Ni wachungaji wa jamii zote. Lazima nasi tuwe mstari wa mbele na jasiri katika kuonya, kukemea na kufundisha. Huu ndio wakati ulioaguliwa katika Agano Jipya kuwa mbaya - wakati wa watu kujichagulia walimu na kufungua masikio yao wasikie yale tu ambayo wanayapenda hata yakiwa maovu (2Tim. 4:1-5). Ndio wakati watu wanapokataa ukweli na kujikunyata katika hadithi za uongo. Hivyo, tuongozwe daima na dhamiri zetu kufundisha yaliyo kweli, ya haki na manufaa kwa taifa la Mungu. Wapendwa familia ya Mungu, Noeli iwe kwetu sherehe yenye maana, inayotujenga katika fadhila kuu za Kimungu, yaani Imani, Matumaini na Mapendo. Tumfungulie Kristo malango ya mioyo yetu, aongoze uhuru wetu ili nia yetu iwe sawa na nia yake (Wafilipi 2:5-11). Mwisho, ninawatakia tena Heri na Baraka za Noeli. Ninawaombea ili mwaka mpya 2023 uwe wa mafanikio, furaha na kukua katika imani na uwajibikaji kwa Kanisa na taifa letu. Amani ya Kristo iwe nanyi daima.

Noeli isimikwe kwenye fadhira za Kimungu
Noeli isimikwe kwenye fadhira za Kimungu

+Renatus Leonard Nkwande

ASKOFU MKUU WA MWANZA.

Ujumbe wa Noeli 2022
24 December 2022, 15:58