Tafuta

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Familia, msingi wa malezi bora ya kikristo. Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Familia, msingi wa malezi bora ya kikristo. 

Sikukuu ya Familia Takatifu: Msingi wa Malezi Bora ya Kikristo, Kijamii na Kiutu!

Mtakatifu Yohane Paulo II: Kuhusu: Wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu, alisisitiza umuhimu wa familia katika malezi ya watoto na ujenzi wa Kanisa na taifa kuwa; Familia ni kitalu cha kanisa na jamii kwa ujumla. Ili jamii na Kanisa lifanikiwe ni lazima kuwe na msingi mzuri katika familia ambayo ndio inaathiri tabia, mwenendo na maisha ya wanajamii kwa ujumla.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ambayo tunaiadhimisha katika Jumapili katika Octava ya Noeli au tarehe 30 Desemba kama katika Octava hakuna Jumapili. Itakumbukwa kuwa kiini na mwanzo wa sherehe hii ni 1921 ambapo Baba Mtakatifu Benedikto XV, alitangaza kuwa jumapili katika oktava ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, au tarehe 30 desemba itakuwa ni sherehe ya Familia Takatifu. Katika sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Familiaris consortio” akieleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu, alisisitiza umuhimu wa familia katika malezi ya watoto na ujenzi wa Kanisa na taifa kuwa; Familia ni kitalu cha kanisa na jamii kwa ujumla. Ili jamii na Kanisa lifanikiwe ni lazima kuwe na msingi mzuri katika familia ambayo ndio inaathiri tabia, mwenendo na maisha ya wanajamii. Mtakatifu Yohane Paulo II pia katika mahubiri yake ya 2 Septemba 1990 katika viwanja vya Jangwani Dar es salaam kwenye misa ya upadrisho alipoitembea Tanzania 1990 alisisitiza kuwa; “Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai. Familia ni Kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala. Familia ni shule ya uaminifu na upendo. Familia ni shule ya utii na kuaminiana na Familia ni shule ya huruma”. Mtakatifu  Yohane Paulo II aliendelea kusisitiza kuwa; Familia Takatifu ni ile ya kumpendeza Bwana, ni familia inayodumu katika pendo la Mungu, imejaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu.

Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa
Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa

Familia ya Yesu, Maria na Yosefu inawekwa mbele yetu kuwa mfano wa familia zetu ambayo inatuonyesha namna zinavyoweza kuiishi vyema furaha ya upendo katika familia na tiba kwa zile zilizojeruhika kwa kukosa upendo kama anavyosisitiza Papa Francis katika Amoris laetitia. Ndiyo maana, katika hitimisho la barua yake ya Familiaris consortio, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Lengo kuu hasa la kuadhimisha Sikukuu hii ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu ziwe ndani mwao daima, zaidi sana kujifunza na kuiga mfano bora wa hii familia kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo akisema; “Ee Mungu, umependa kutuonyesha mifano bora ya Familia Takatifu. Utujulie kwa wema wako tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia Takatifu katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo”. Tunaomba fadhila ya upendo ambayo ni kiini cha furaha ya familia kama maneno ya mwanzo katika barua ya kichungaji ya Papa Francisko juu ya maisha ya familia yanavyoashiria; Amoris letitia yaani furaha ya upendo. Kwamba katika magumu yote; upendo unaleta furaha.

Ni neema na baraka za Mwenyezi Mungu, kusherehekea Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa
Ni neema na baraka za Mwenyezi Mungu, kusherehekea Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa

Tunapoongelea familia ni vyema tukafahamu maana halisi kadiri ya mpango wa Mungu kama walivyosisitiza na kufundisha Mababa Askofu wa Tanzania katika ujumbe wa kwaresma wa mwaka 2019, mwaka wa familia Tanzania kuwa Familia Kanisa la nyumbani na ni Shule ya Imani na Maadili. Katika ujumbe huu Mababa Askofu wakifanya rejea katika Maandiko Matakatifu waliweka mkazo kuwa Familia ni muungano wa Mume na mke, unaofungamishwa na upendo na tunda litokanalo na Upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi; Baba na mama. Familia ni mpango wa Mungu (Mw. 1:26-28; 2:24). Tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji ili tunu ya uhai iendelee kuwepo duniani. Kumbe familia ni wito wa kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Kumbe, familia ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi kwa njia ya sala, nyimbo na Sakramenti.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua Bin Sira (YbS 3:2-6, 12-14) linasema; “Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto.” Familia ya Kikristo inatakiwa ijengwe kwa mahusiano mazuri kati ya wanafamilia yaani wazazi na watoto wawe na wajibu na ari ya kudumisha amani na mapendo wakistawisha tunu za kikristo, kimaaadili na kiutamaduni. Familia ya Nazareti ni mfano mzuri wa kuigwa. Katika Somo la pili la Waraka wake kwa Wakolosai (Kol 3:12-21), Mtume Paulo anatuasa kwamba kwa kuwa tumekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, tujivike moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, tukichukuliana na kusameheana zaidi ya hayo yote tujivike upendo ndio kifungo cha ukamilifu. Hizi ndizo zilikuwa tunu za familia takatifu. Familia ni mahala pa msingi pa kuujenga utu wa mtu kwa ajili ya kanisa na jamii na hivi ndio chanzo au chimbuko la “Uhai na Mapendo” Katika Injili ya Mathayo (2:13-15, 19-23); tunasikia simulizi la Familia Takatifu kukimbilia Misri na baadae wanaenda Galilaya na matukio yote mawili yanaongozwa na ujumbe wa Malaika anaupokea Yosefu katika ndoto kwa unyenyekevu na utii. Tendo hili linatukumbusha kuwa kuzaliwa kwa Kristo Mkombozi ni mwanzo wa taifa teule jipya, mfano wa taifa la Israeli. Katika familia, baba na mama ni viongozi wanaotakiwa kushikana mikono ili waishi vyema hapa duniani kwa furaha, amani na upendo wakijiimairisha katika taabu na mahangaiko ili mwisho wafikishane mbinguni kama mwili mmoja. Ndipo hapa tunaona baba ana wajibu mkubwa kwa mama na vivyo hivyo mama kwa baba lakini pia wazazi kwa mtoto na watoto kwa wazazi.

Watoto ni zawadi safi kutoka kwa Mungu
Watoto ni zawadi safi kutoka kwa Mungu

Baba kwa hakika ni nguzo ya familia inayohakikisha ulinzi ustawi, mahitaji na maendeleo ya kweli ya familia yanapatikana. Kwa kuonyesha upendo, Baba anapaswa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu familia yake, kujibidisha kumcha Mungu na kuwapa watoto wake malezi bora hasa muda wa kukaa nao na kuwafundisha tunu zilizo njema. Yosefu mwenye ni mfano halisi katika hilo. Ni ukweli usiokanika kwamba, Mama ni jiwe la msingi la familia katika kulea watoto, kulinda tunu za familia yaani utu, kazi, upendo, umoja, nidhamu na amani. Mama mwema wa familia siku zote anapaswa kumheshimu mme na watoto wake, kumcha Mungu na kupigania ustawi na mafanikio ya familia yake kiroho, kimaadili na kiuchumi. Huyu ni mke mwema na si mwanamke tu. Watoto ni zawadi ya Mungu katika Fanilia, ni vyema basi kumtukuza Mungu kwa kuwalea vyema katika maadili mema ya jamii, kumwogopa Mungu na siku zote kuwarithisha tunu za kiutamaduni na kidini. Waswahili wanasema; “kuzaa si kazi, kazi ni kulea” - hakika ni kweli. Basi watoto pia wana wajibu wa kuwaheshimu wazazi wao ambao ni wawakilishi wa Mungu duniani ili waishi vyema kama Yesu na wakue katika kimo na hekima na katika uzee wao wawaheshimu na kuwatunza.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani.
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani.

Yesu mzaliwa ni mfano halisi wa watoto ambao kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francis katika Chritus vivit  yaani Yesu anaishi akisema; Vijana mwigeni Yesu mkakue vyema na kukomaa katika maisha kiakili, kiroho na kimwili. Tunapoadhimisha sikuuu hii ya familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ikiwa imejazwa na upendo na uchaji wa Mungu, tuiangalie, tujifunze na tukaziishi tunu za hiyo familia ili tuendeleze familia zetu kiroho na kimwili na tutibu familia zile zilizojeruhika kwa kukosa upendo wa kweli na kukosa uchaji wa Mungu. Tuige mfano wa familia takatifu ili tujenge familia bora ambazo zitakuwa paradiso ndogo hapa duniani. Hili linawezekana kwani mfano tunao na njia tunayo, kazi kwetu kuangalia na kuishi. Familia takatifu itusaidie kuilinda imani yetu na matendo mema katika familia tuishi kwa amani na furaha na mwisho tuufikie uzima wa milele. Lakini katika yote yatupasa kukumbuka kwamba hakuna familia yeyote itakayosimama imara, kufanikiwa na kudumu kama haina upendo wa kweli na Mungu hayuko katikati yake.

30 December 2022, 18:10